SAYANSI & TEKNOLOJIA UCHUMI

Dangote Kujenga Kiwanda Kikubwa cha Mbolea Barani Afrika.

Na Sabina Wandiba

Wakati Tanzania ikivutana na kiwanda cha saruji cha Dangote kuhusu gharama za uendeshaji biashara, kampuni hiyo ya Nigeria imesaini makubaliano na OCP ya Morocco kuanzisha kiwanda kikubwa barani Afrika cha kuzalisha mbolea na kufanya biashara.

Kiwanda cha saruji cha Dangote cha Mtwara, kinachomilikiwa na mfanyabiashara tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote kimesimamisha uzalishaji kwa kile ilichooleza kuwa ni sababu za kiufundi, lakini kikaeleza bayana kuwa mazingira ya uendeshaji biashara nchini ni ghali.

Hadi sasa mvutano huo baina ya Serikali na Dangote umekwama katika gharama za nishati ya kuendeshea kiwanda hicho kilichopo Mtwara, kikijikita kwenye bei ya gesi na usafirishaji wa makaa ya mawe kama nishati mbadala.

Kwa sasa kiwanda hicho kinazalisha kwa kutumia nishati ya mafuta. Hata hivyo, Kampuni ya Dangote ilikubaliana na Kampuni ya OCP ya Morocco, ambayo inaongoza duniani kwa kusaka masoko ya malighafi ya fosfati inayotumika kutengeneza mbolea, kujenga kiwanda kwa ajili ya pembejeo hiyo.

Uamuzi huo unaiongezea nguvu sekta ya kilimo nchini Nigeria katika safari yake ya kuwa na uhakika wa chakula, gazeti la Vanguard la Nigeria limeripoti jana.

Ubia wa kampuni hizo mbili unategemewa kuanzisha jukwaa la pamoja Afrika na kuwa kinara wa uzalishaji mbolea duniani, imeeleza taarifa ya Dangote Group iliyokaririwa na gazeti la Vanguard.

Gazeti la Tribune pia la Nigeria limemkariri Femi Adesina, mshauri wa habari wa rais wa Nigeria, akiongea na waandishi kuhusu makubaliano yaliyohusisha nchi hizo mbili ambayo yalisainiwa juzi.

“Makubaliano mawili kati ya hayo yalihusisha mbolea ambapo uliomuhusisha Aliko Dangote ni wa
ubia na kampuni ya OCP Morocco katika kuzalisha mbolea kwa Nigeria na ukanda huu wa Afrika,” alisema mshauri huyo wa habari wa Rais Muhammadu Buhari.

“Wa pili ni wa Chama cha Wazalishaji Mbolea wa Nigeria (FEPAN) na OCP ya Morocco kuhusu kuchukua hatua za haraka kuingilia ugavi wa mbolea na uendelezaji wake.

Kampuni hiyo itasambaza mamilioni ya tani za mbolea mwaka huu kwa ajili ya kuuza kwa kwa bei nafuu kwa wakulima.”

Taarifa ya Dangote inaeleza kuwa ushirikiano huo baina ya kampuni hizo mbili utaisaidia Dangote kuchanganya madini ya phosphate nchini Morocco na gesi inayozalishwa Nigeria kuzalisha mbolea kwa ajili ya kuendeleza kilimo Afrika.

Gazeti la Vanguard linamkariri Rais wa Dangote Group, Aliko Dangote akisema makubaliano hayo yatasaidia juhudi za Nigeria katika kuwa na uhakika wa chakula, kuzalisha ajira na kutatua tatizo la watu kutoka vijijini na kuhamia mijini.

Dangote alisema kati ya dola 2.8 bilioni zinazotakiwa kuwekezwa, tayari dola 2.5 bilioni zimeshawekezwa kwenye mradi.

Mradi huo utaihakikishia Nigeria kuzalisha metric ton milioni 4.6 za mbolea ifikapo mwaka 2020 kutoka
metric tones milioni 3.6 zinazotarajiwa kuzalishwa ifikapo mwaka 2018.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza kazi Desemba mwakani. Kwa mujibu wa Dangote, mradi huo utasaidia serikali kuongeza mapato ya fedha za kigeni, kuzalisha ajira, kuongeza mazao ya kilimo kwa hekta na kuongeza mchango wa kilimokwenye Pato la Taifa.

Gavana Abubakar Badaru wa Jimbo la Jigawa, ambaye alishuhudia sherehe za utiaji saini, alisema makubaliano hayo yatazalisha ajira 250,000 mpya.

Rais Buhari na Mfalme Mohammed wa Morocco pia walisaini makubaliano mengine, yakihusisha kuimarisha ushirikiano katika uzalishaji bidhaa za mchanganyiko kwa kutumia malighafi kutoka nchi hizo mbili na masuala ya mazingira.

Pia walisaini makubaliano ya kuondoa malipo ya visa kwa viongozi na hati za kusafiria za kazi, huduma za usafiri wa anga baina ya Morocco na Nigeria, makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi, makubaliano katika kilimo na makubaliano baina ya mawakala wa nishati endelevu wa nchi hizo.

(38)

About the author

10cjlow1992

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available