TANZANIA

Zuma Ajiuzulu; Cyril Ramaphosa Rais Mpya Afrika ya Kusini

Ramaphosa akiwa Naibu Rais kushoto akiwa na Jacob Zuma

Na. M. M. Mwanakijiji

Baada ya kutii shinikizo kubwa ndani ya chama chake Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini hatimaye alitangaza kujiuzulu siku ya Jumatano na hivyo kusafisha njia kwa Rais wa ANC Bw. Cyril Ramaphosa kupitishwa na hatimaye kuapishwa kuwa Rais mpya wa Taifa hilo. Ramaphosa ameapishwa leo baada ya Bunge la nchi hiyo kumpitisha kuwa mgombea pekee wa Urais na hatimaye kumpigia kura ya kuwa Rais mpya wa nchi hiyo.

Rais Jacob Zuma alikuwa anakabiliwa na tuhuma mbalimbali tangu kuchaguliwa kwake na tuhuma kubwa zaidi zilimhusisha na kutumia nafasi yake ya Urais kujinufaisha yeye na marafiki zake wa karibu hasa familia ya kina Gupta, wafanyabiashara wakubwa nchini humo. Kwa miaka kadhaa kumekuwepo na majaribio mbalimbali ya kumuondoa Zuma madarakani bila mafanikio yoyote. Pamoja na njia hizo uchunguzi mbalimbali dhidi yake ulikuwa unafanyika na alitajwa kuhusika na mambo mbalimbali ya kifisadi lakini kesi karibu zote zilikuwa haziendi popote.

Hata hivyo, kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe miezi kadhaa nyuma kwa njia ya amani, wananchi wa nchi jirani ya Afrika ya Kusini nao walikuwa wameona kuna uwezekano wa kuweza kumuondoa Rais wa madarakani hata kabla ya muda wake endapo njia ya ushawishi wa watu na vyombo vyenye nguvu inaweza kutumika. Hata hivyo, tofauti na Zimbabwe ambako shinikizo kubwa lililetwa na jeshi la nchi hiyo huko Afrika ya Kusini hatimaye shinikizo kubwa lililetwa na Chama cha ANC ambacho ndicho kilikuwa kimemdhamini Zuma madarakani.

Wakati huo huo, Ajay Gupta mmoja wa watu wanaotajwa kuwa karibu sana na utawala wa Jacob Zuma ametajwa na kikosi maalum cha polisi cha kufuatilia uhalifu cha Hawks kama mtu anayetafutwa na Jeshi la Polisi baada ya kushindwa kujisalimisha mikononi mwa polisi kama alivyotakiwa.

Mwitikio wa watu mbalimbali nchini Afrika ya Kusini umekuwa chanya tangu Zuma ajiuzulu jana na Rais Ramaphosa kuapishwa leo. Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo Shirika la Utangaza la Afrika ya Kusini (SABC), wachumi wengi nchini humo wanaona kuwa Urais wa Ramaphosa unatoa nafasi mpya kwa Afrika ya Kusini kuboresha uchumi wake, kupigana na ufisadi na kushughulikia matatizo mengi ambayo yalionekana kushindikana wakati wa utawala wa Rais Zuma.

Wimbi la viongozi wa Afrika kuamua kuachia madaraka kwa sababu ya shinikizo la kisiasa halijakomea Afrika ya Kusini. Huko Ethiopia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bw. Hailemariam Desalegn (kushoto) ametangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo akidai kuwa kufanya kwake hivyo kutasaidia kutuliza hali ya kisiasa nchini humo na kurejesha demokrasia. Bw. Desalegn, amekuwa akihusishwa na udhaifu mkubwa wa kushughulikia matatizo ya kisiasa kiasi kwamba chini ya utawala wake mamia ya watu wameuawa na wengi wenye kushabikia upinzani wamefungwa jela. Majaribio ya kuachilia baadhi yao hayajatuliza upinzani wa kisiasa hasa katika maeneo ya Oromia na Amhara ambayo yanakadiriwa kuwa ni ngome kubwa ya upinzani. Chama kinachounda serikali kinatarajia kufanya uchaguzi wa mtu mwingine kuchukua nafasi ya Desalegn. Pamoja na mafanikio makubwa ya kiuchumi huko Ethiopia bado hali ya kisiasa na demokrasia ilikuwa imedumaa sana kiasi cha kuondoa umaana wowote wa mafanikio hayo.

Katika sehemu zote tatu, Zimbabwe, Afrika ya Kusini na sasa Ethiopia ni wazi kuwa mabadiliko ya kisiasa yalikuwa ni lazima yafanyike baada ya muda mrefu wa kuyapuuzia. Hata hivyo, katika nchi zote tatu bado vyama tawala ndivyo ambavyo vinapata nafasi ya kuunda serikali tena na hivyo upinzani haujapewa nafasi yoyote. Zimbabwe hata hivyo inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka huu na Afrika ya Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu mwakani. Uchaguzi Mkuu mwingine kwa Ethiopia ulikuwa ufanyike mwaka 2020. Hata hivyo haijajulikana kama Waziri Mkuu mpya atamalizia kipindi cha Desalegn au ataitisha uchaguzi mkuu mpya.

(32)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available