TANZANIA

Tahariri: Serikali Isiache Ihusishwe na Jaribio la Mauaji ya Lissu; Ijisafishe!

Na. M. M. Mwanakijiji

Haijalishi nani amefanya, haijalishi nani amedhaniwa kufanya, na haijalishi nani anaweza kuwa amefanya. Kwamba, jambo hili limefanyika inatosha kabisa kuwafanya watu wote wenye kuheshimu utu wa mwanadamu kulaani kwa maneno yote yanayowezekana jaribio la kiwoga dhidi ya maisha ya Mbunge wa Singida Mashariki, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani Bungeni Bw. Tundu Lissu.

Shambulio hilo la risasi zaidi ya ishirini kwa mtu ambaye hana silaha, na hana ulinzi wa kutosha ni wazi halikuwa la kumtishia tu bali lilikuwa na lengo la kuondoa uhai wake mchana kweupe na bila kujali matokeo yoyote kwa watakaofanya. Tukio hili limefanyika tayari kukiwa na hisia ya kuongezeka kwa vitendo vya mauaji yasiyoelezeka na matukio ambayo yanaashiria kuwepo kwa mfumo mwingine wa kiutawala nje ya ule uliowekwa kikatiba na kisheria.

Sote tunafahamu kuwa tukio hili kwanza si la peke yake na siyo la kwanza la aina yake nchini. Tayari yameshawahi kutokea matukio ya mauaji ya watu mashuhuri nchini ambapo wahusika wake hawajaweza kufahamika hadi hivi sasa na kubakia kuwa ni “watu wasiojulikana”. Wiki chache tu zilizopita mmoja wa wanaharakati wa vita dhidi ya ujangili ambaye ni raia wa Uingereza aliuawa Jijini Dar-es-Salaam na hadi sasa hakuna taarifa zinazoeleweka za uchunguzi ulipofikia.

Miaka saba nyuma Julai 2010 mwanasheria mwingine mashuhuri na msomi aliyebeboa Profesa Jusa Mwaikusa aliuawa jijini Dar-es-Salaam mchana kweupe vile vile. Wakati ule watu kadhaa walikamatwa wakitajwa kuhusika na tukio lile.

Miaka mitatu baadaye mwanasheria mwingine na wakili mashuhuri Dkt. Sengodo Mvungi naye alijeruhiwa katika jaribio la mauaji na baadaye kufariki huko Afrika ya Kusini alikopelekwa kwa matibabu. Katika tukio lile watu wengine karibu kumi walimatwa na kufikishwa mahakamani.

Ni rahisi sana katika matukio ambapo wanasiasa au watu mashuhuri wanauawa au kujaribiwa kuuawa kuhisi moja kwa moja kuwa kwa namna fulani mkono wa serikali unahusika. Ni jambo la hatari na baya sana kwa serikali au vyombo vyake kudhaniwa kuwa vinaweza kutumia njia ya nje za kisheria (extra judicial) kushughulikia watu ambao inaona ni wana matatizo.

Binafsi, naamini – na tayari tumeona hili likitokea – serikali imekuwa ikitumia njia za kawaida za kisheria za kushughulika na changamoto na hoja za Tundu Lissu. Kwa baadhi yetu njia hizi tumeona si za lazima kwani kwa kiasi kikubwa hoja za Tundu Lissu zilikuwa zinaweza kujibiwa kisiasa na zimekuwa kujibiwa kisiasa. Na pale ambapo serikali imeona amevuka mpaka mara kadhaa wamekuwa wakimkamata na kumfungulia kesi. Inawezekana sasa hivi Lissu anashikilia rekodi ya kuwa Mtanzania mwenye kesi nyingi – za kushtakiwa na kusimamia kama wakili!

Ni kwa sababu hii wazo kuwa inawezekana kuna kuhusika kwa vyombo vya dola linatisha na linatulazimisha kutupa ukimya wa sekunde. Ni kwanini watu wanahisia hizo? Jibu kwa wengi ni kuwa tayari Lissu alishanyoshea mkono serikali na kudokeza kuwa anahisi anafuatiliwa na vyombo vya dola na alishatuhumu vyombo vya usalama kuwa kama kuna watu wametumwa kumfuatilia waache hivyo kwani tayari amewakaba. Vyombo vya dola havikusema maneno mengi ya kukanusha au hata kuonesha kuwa havihusiki; na inawezekana labda Lissu mwenyewe hakutoa taarifa polisi hasa kama inawezekana aliowadhania ni vyombo vya dola ni watu wengine wabaya.

Vyovyote vile ile ilivyo ni wajibu wa serikali kujisafisha na kuonesha kuwa katika nchi yetu sasa hivi hakuna sera ya mbwa kala mbwa! Siyo maslahi ya Rais Magufuli kuonekana kama Rais ambaye ameanza kushindwa hoja za maneno na sasa serikali yake inataka kuingia kwenye hoja za damu. Siyo sahihi kwa serikali na vyombo vyake ambavyo mara nyingi imedai kuwa na “intelligensia” inayokataza mikutano ya vyama vya upinzani lakini inakosa inteligensia ya kufuatilia watu ambao wana uwezo wa kumwaga risasi ishirini mchana kweupe na wakatokomea bila kufahamika.

Ninaamini, ni muhimu kwa serikali na vyombo vyake vyote kuhakikisha kuwa waliohusika na tukio hili wanafahamika na kukamatwa na kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayazoeleki kwani tayari kuna hisia kwa baadhi ya watu kuwa tunaweza kuanza kuonekana kwa matukio ya namna hii.

Lakini vile vile ni wajibu wa vyama vya upinzani na hasa chama kikuu cha upinzani kuhakikisha kuwa kinatoa ulinzi kwa viongozi wake wakuu na hasa watu kama Lissu ambao tayari wameonekana kutishiwa maisha. Na hili linawezekana kwa viongozi hao kuwasiliana na Jeshi la polisi ili kutoa taarifa za kuwepo kwa ulinzi kwa viongozi wao, ulinzi ambao wa watu wenye silaha. Inasikitisha katika nchi ambayo tayari tuna harakati za kila namna viongozi wa namna hii hawapewi ulinzi wa watu wenye silaha. Na hata kama hakuna watu wenye silaha CHADEMA inapaswa kutoa ulinzi wa karibu kwa viongozi wake kuanzia sasa mara moja ili kuhakikisha inakuwa vigumu kwa mtu kupanga na hata kujaribu kutekeleza tendo ovu kama liliojaribiwa kwa Lissu.

Kama nilivyosema, haijalishi nani amefanya, haijalishi nani anadhaniwa kufanya kinachojali ni kuwa jambo hili limefanyika na linapaswa kulaaniwa kwa lugha yote kali. Lakini, ni muhimu sana kujua nani amefanya tukio hili ili kuhakikisha kuwa wananchi bila kujali nafasi zao hawaanzi kuishi kwa hofu hasa kwa vile tukio hili siyo la kwanza la aina yake.

Ni muhimu pia kwa wananchi kuwa na utulivu na hekima ya kutafakari kwa kujiuliza swali la msingi hasa – ni nani angenufaika kama Lissu angeuawa? Huu ndio msingi wa uchunguzi. Japo wengi tayari wameshahitimisha kuwa “serikali inahusika” au kuwa ni “Magufuli”; kuna uwezekano mkubwa kuwa ambaye/ambao wangenufaika na Lissu kuuawa bila ya shaka siyo Magufuli. Ni maslahi ya Magufuli kuona kuwa Lissu hapatwi na janga kama kama hili. Wengine wanaweza kusema “vipi kama Magufuli hajali kama angenufaika au la?” Swali hili ni zito na jibu lake siyo rahisi lakini linaweza kufikirisha wengi.

Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa wahusika wanakamatwa mara moja ili isije kuonekana tukio hili ama lina mkono, baraka au maelekezo kutoka ndani ya serikali. Lakini kama jambo hili lina uratibu wowote kutoka kwa mtu yeyote (ndani ya serikali au nje yake), basi mtu huyo awe  pia na ujasiri wa kusimama hadharani na kusema kuwa aliagiza kufanyika kwa tukio hilo na hana majuto.

Tunamtakia na kumwombea uponyaji wa haraka Bw. Lissu ili arejee katika majukumu yake ya kulijenga taifa na kusimamia maslahi ya taifa.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

 

(1062)

About the author

bongoz

2 Comments

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available