Maoni TANZANIA

Tahariri: Miili Iliyokutwa Ruvu Ifukuliwe; Ben Saanane Apatikane – Ni Ubinadamu Huu!

Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya ahadi za TANU ilikuwa ni ile iliyosema “Binadamu wote ni sawa” na pia “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”. Ahadi hizi baadaye ziliingizwa pia kwenye Katiba yetu kama sehemu ya Haki za Msingi (Bill of Rights). Kimsingi, kanuni hizi zinatuambia kuwa tunaweza kuwa na tofauti nyingi sana baina yetu, kuanzia zile za kidini, kisiasa, rangi, lugha, asili ya kitaifa n.k. Lakini mwisho wa yote sisi sote kama binadamu ni “sawa”. Usawa huu hauko katika masuala ya kisheria, hali, hadhi, ujiko, ukwasi n.k bali ni usawa unaotokana na ubinadamu wetu. Kwamba sisi sote kama binadamu tumeumbwa sawa na utu wetu wote ni sawa. Hakuna mwenye utu zaidi ya mwingine!

Taarifa za kupatikana miili ya watu saba ambao inadaiwa walikuwa wamefungwa kwenye viroba wakiwa na dalili za kuwa wameteswa au kuumizwa ni taarifa ambazo zinapasa kumshtua kila mtu anayejiona yeye ni binadamu. Katika usawa wetu wa kibinadamu tunajikuta tunaitwa siyo tu kuhoji lakini pia kupaza sauti kwa niaba ya binadamu wenzetu hao ili kutaka haki juu yao itendeke.

Bahati mbaya taarifa hizi pia zimehusishwa na kutoweka kwa miongoni mwa vijana wanaharakati Bw. Ben Saanane ambaye hajaonekana kwa muda sasa. Ninasema ni bahati mbaya kwa sababu Ben Saanane amekuwa akijihusisha na masuala ya kisiasa na hata ukosoaji wa viongozi walioko madarakani. Kutoonekana kwake katika kipindi kile kile ambacho miili hii imepatikana na kuzikwa kwa kile ambacho watu wanaona kama ni ‘haraka haraka’ kunawafanya watu wahisi labda kijana huyu ni miongoni mwa watu hao.

Binafsi naamini kwanza kabisa hata kama Ben Saanane angekuwa hajakosekana kama hivi na kama angekuwa anaendelea na shughuli zake bado kupatikana kwa miili hiyo kungetusukuma kutaka kujua ni nini kinaendelea, kwanini na na ni nani anahusika.

Kuna mambo kadhaa ambayo ni kweli. Kwamba, hao watu hawakujifunga wenyewe kwenye viroba lakini pia ni vigumu kuamini kama walijitumbukiza wenyewe wakiwa kwenye viroba kwenye mto Ruvu. Hili kimantiki haliwezekani. Ni wazi kuna binadamu wengine walihusika katika kufanya hili – la kuwafunga kwenye viroba na kuwatumbukiza mtoni. Na kama ni kweli watu hao walikuwa wameuawa kabla ya kufungwa au kutupwa mtoni basi ni wazi pia kuwa kuna watu walihusika na mauaji hayo.

Ni kwa sababu hiyo naweza kusema kuwa ni ukosefu mkubwa wa hekima na weledi kwa chombo chochote cha umma kutokufuata taratibu za msingi za kiutu za kushughulikia watu hao. Baada ya miili kukutwa ikielea jambo kubwa na la msingi kufanyika – kwa taratibu za kisheria na kawaida kabisa – ni kutaka kujua kwanza hao ni kina nani, walikufa vipi, na kwanini wapatikane eneo moja, na ni nani anahusika.

Maelezo ambayo yametolewa yenye kuashiria kuwa hawa ni “wahamiaji haramu” yanazua maswali mengi zaidi kuliko yanayojibu. Kama Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Mwigulu Nchemba anajua kuwa hawa ni wahamaiji haramu basi ni muhimu kwenda mbele zaidi na kujibu maswali zaidi badala ya kuyaacha yaning’inie hewani kama mzoga uliooza. Yeye kama Waziri wa Mambo ya Ndani bila ya shaka atakuwa na majibu ya maswali yote haya. Hawa ni wahamiaji kutoka nchi gani na walijuaje? Je, ni kwanini waliuawa? Je, majina yao ni kina nani? Je, ni nani walihusika na ama mauaji yao au kuwatumbukiza mtoni?

Kama nilivyosema awali hawa ni binadamu; utu wao haujadiliki kwani binadamu wote ni ‘sawa’ na wote wana utu sawa. Hata adui bado ni binadamu. Hata mtu unayemchukia bado ni binadamu. Kanuni hii ya msingi iliyoliunda taifa letu haipaswi kupotezwa au kudharauliwa na yeyote.

Lakini swali la msingi na muhimu ni je Serikali iko tayari kuacha vyombo huru kufanya uchunguzi wa miili hiyo ili kujiridhisha kuwa hawa siyo Watanzania na raia wa Tanzania ambao wanalindwa na sheria mbalimbali za nchi yetu?

Binafsi naamini ili kuondoa hisia kuwa serikali ama inahusika – moja kwa moja au kwa namna moja – na tukio hili ni vizuri kwanza kabisa miili yote ifukuliwe, ifanyiwe uchunguzi wenye kushirikisha watu huru, na hatimaye taarifa itolewe (post mortem) ili kutoa wasiwasi wowote  ambao unaweza kuonekana umeingia kwa wananchi.

Lakini pia, ni jukumu la vyombo vyote vya serikali ikiwemo TISS, Polisi na vyombo vingine vya usalama kuhakikisha kijana Ben Saanane anapatikana kwani kutokupatikana kwake kunaleta ubaridi katika harakati za kisiasa nchini. Hii ni kwa sababu kama miili ya watu hao ni kazi ya kundi la kihalifu nchini na kutokujulikana au kupatikana kwa kundi hilo kunaweza kutumiwa kisiasa kuonesha kuwa serikali inaanza au taasisi zake zinaanza kufanya kile ambacho kimeshuhudiwa huko Burundi na Rwanda na kwenye baadhi ya nchi ambazo siasa zake hazijali sana haki za raia au zile haki za kibinadamu. Ni kwa maslahi ya serikali kumpata Ben Saanane.

Ni matumaini yangu, kuwa serikali yetu itafanya yote yanayopaswa ili kuondoa wingu la hofu ambalo linaweza kufanya watu wahofie serikali yao. Kupatikana kwa Ben Saanane na kufanyiwa uchunguzi kwa miili iliyopatikana Ruvu ndio njia pekee ya kuzidi kuonesha kuwa serikali ya Awamu ya Tano inajali wanyonge na wale wasio na watetezi hata kama watu hao ni wahamiaji au wanasiasa wa upinzani au wale ambao wanawakera au wanaoweza kuwaona kuwa ni maadui wao.

Nje ya hapo maswali yanayoulizwa sasa hayatakoma na yatapaswa kuulizwa na kutakiwa kujibiwa siku moja. Hata kama siku hiyo itachelewa. Na majibu yake yatakapopatikana wahusika wote bila kujali vyeo vyao vya sasa, hadhi zao za sasa, au kile wanachoweza kuamini kuwa ni kinga za sasa siku moja wataitwa kujibu mbele ya Watanzania, na mbele ya Mungu.

(64)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  • Mlikaa kimya wakati Ben alipojipa uhuru wa kumdhalilisha Rais. Mlikaa kimya alipojipa uhuru kumtukana kila aliyejaribu kujadiliana nae kuhusu jinsi alivyokuwa akimdhalilisha Rais. Leo mna “utu” nae? Alichezea wembe na sasa umemkata. Good riddance

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available