TANZANIA

Tafadhali Magufuli: Matatizo Haya Mengine ni Ya Kujitakia; Msimlaumu Zitto…

Zitto Kabwe

Na. M. M. Mwanakijiji

Kwa Mara Nyingine

Kwa mara nyingine tena tunashuhudia Serikali inakimbia kujitetea (on the defensive). Zinatolewa tuhuma, tena nzito lakini kwa mambo ambayo yanajibika vizuri. Mtu mmoja aliwahi kuandika kitabu cha “Lies, Damn Lies and Statistics”Alitumia maneno ambayo yananukuliwa toka kwa mwandishi Mark Twain. Katika andiko hilo alielezea jinsi gani namba zinaweza kutumiwa kusema uongo, kuchanganya watu na hata kufanya watu waamini kitu kisichokuwepo. Takwimu zinaweza kutumika kuthibitisha lolote lile.

Kwa mara hii nyingine tunashuhudia serikali inaonekana kukerwa, kusikitishwa na kushangazwa na jinsi gani watu wanahoji takwimu mbalimbali. Serikali inasikitika kwa sababu kina Zitto na wengine wanasema “mbona hizi namba haziingii kichwani”? Majibu yanayotolewa yanatolewa kujaribu kuelezea kwanini hizi namba ziingie kichwani; hata kama hazitoshi!

Sasa mwisho wa siku Rais anakasirishwa kwa nini watu wanaandika kwenye mitandao na kuhoji kwenye forum mbalimbali kana kwamba tatizo ni mitandao! Lakini hili ni tatizo la kujitakia kwa kweli kabisa; ni tatizo ambalo linaweza kuepukika.

CAG Anajua Kulikoroga

Ripoti za CAG zimekuwa ni mojawapo ya nyaraka muhimu za kitaifa ambazo zinawafikia wananchi bila kuchujwa. Matokeo yake wananchi wanapozisoma wanaona vitu ambavyo “haviingii kichwani”; wanaamua kuhoji. Kwa mara nyingine ripoti ya CAG inazua mjadala mzito na kwa mara nyingine CAG anachelewa kuweka sawa na kuacha mjadala huu uwe kama unga uliokandwa ukisubiriwa uumuke.

Serikali Haiwezi Kuendesha Nchi kwa Usiri

Serikali inajikuta inaanza kujitetea. Inanikumbuka wakati wa hoja ya ndege yetu ya Bombardier kukamatwa Canada. Hatukujua kuwa imekamatwa, hakukuwa na kiongozi yeyote aliyesema (kabla ya Lissu) kuwa tunadaiwa na ndege yetu inaweza kuzuiwa. Wakuu wetu wakaamua kulimaliza kimya kimya hadi lilipoibuliwa, na kuumbuliwa na Tundu Lissu. Watu wakamkasirikia Lissu kwa kutuambia kile ambacho wao walipaswa kuliambia taifa! Walikasirishwa kwa sababu Watanzania (wenye hela zao) hawakutakiwa kujua. Lissu aoneshwa kama ‘adui’!

Serikali inapojaribu kufanya vitu siri visivyopaswa kuwa siri itajikuta inaona imeumbuliwa wakati kama ingekuwa wazi mapema ingeonekana iko makini. Anayeficha maradhi wahenga walisema msiba ndio utamuumbua. Kama kuna tatizo ni bora zaidi kuliwahi na kuwaambia Watanzania mapema kuliko kuficha au kutokujali kuwaambia tukiamini kuwa hawatajua. Wakija kujua kwa njia nyingine tusiwakasirikie kwanini wameambiwa! Kama Mzazi hujakaa na watoto wako ukawaambia kuwa nyumba yenu imepigwa mnada usishangae watoto wakasikia mtaani na wakaja kukuhoji kwa ukali. Au tumesahau ya yule mtoto wa Bukoba hivi majuzi?

Hoja ya Trilioni 1.5 

Kwa mara nyingine tena, wakuu wote wanajua kilichotokea kwenye Trilioni 1.5. Hazikuibwa, hazikuwekwa kwenye akaunti maalumu ya Magufuli, hazikuliwa. Ni hela ambazo ama zimetumiwa vibaya (kama anavyodai Zitto Kabwe) au hazijafafanuliwa vizuri katika ripoti ya CAG – kama Naibu Waziri wa Fedha, alivyodai katika taarifa yake leo. Hakuna njia ya katikati.

Kwa mara nyingine, tunataka kumfanya Zitto awe adui kwa kuhoji ambacho serikali na CAG haikukifafanua au kuyaweka wazi mapema. Hivi, walitarajia watu wafanye nini? Kwamba, watu waangalie namba tu wasijumlishe wenyewe na kuzikokotoa? Kwamba kwa vile CAG kaandika namba basi watu wazimeze tu bila kuhoji? Hivi Mungu alitupa ubongo wa nini? Wanaotawaliwa ni wananchi, na wanaotawala ni wananchi; watawala wana ubongo na watawaliwa wana ubongo; bongo zikigongana ndio tunapata mtazamo mpana zaidi wa mambo.

Binafsi naamini maelezo ya Serikali (ya leo) yanawezekana yanakaribiana na ukweli zaidi kuliko maelezo ya Zitto. Hata hivyo Zitto hajui fedha zimeenda wapi; hajadai zimeibiwa (madai haya ni ya wengine), hajadai Magufuli amezila au amegawa kwa washirika wake; hajadai zimeingizwa kwenye akaunti ya CCM au kwa ajili ya kampeni; anachouliza ni kuwa “hesabu haziingii kichwani”. Jibu la serikali kwa mara nyingine limechelewa; linakuja likiandamana na mikwara na vitisho badala ya shukrani. Kama Zitto asingehoji kwa ukali hivi, nani angetoa maelezo? Kama Zitto asingehoji hivi kwa ukali Rais Magufuli angeamuaje kuwahoji kina Prof. Assad na Waziri wa Fedha leo hadharani? Angewapigia simu vipi kupata maelezo?

Zitto anatakiwa ashikwe mkono na kupewa shukrani. Inawezekana Zitto anahoji kwa ukali kwa sababu za kisiasa – ilianzia kwa halmashauri yake kuwa mionngoni mwa halmashauri zilizopata hati chafu, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo akaondolewa kazini. Inawezekana hilo lilimuua. Akaamua kutaka kuonesha kuwa “uchafu” huu hauko Kigoma tu; hauko Ujiji peke yake; ni uchafu ulioko kwenye mfumo mzima wa serikali zetu (kuu na za mitaa). Inawezekana ukali wake umetokana na haya. Na hata tukikubaliana kuwa hii ndio sababu, bado Zitto yuko sahihi kuhoji!

Serikali Iwe “Active”

Kwa mara nyingine, Serikali inapaswa kuacha kuwa ‘reactive’ inayosubiri kutenda baada ya tukio (inayosubiri moto uwake ndio ikimbie na ndoo ya maji kuzima!); inapaswa kuwa ‘pro active’ (isiyosubiri) yaani inayowahi kutenda kabla ya tukio. Ukiona moshi una uamuzi wa kuwahi kuzima kabla miale haijaanza kuweka (proactive) au unaweeza kusubiri vianze kuungua uanze kujitahidi kuzima moto (reactive).

Ripoti ya CAG ilipotolewa na hoja ya Zitto ilipoibuliwa mara moja, Waziri na viongozi wa serikali walitakiwa kukaa chini na Mbunge huyu na kuhojiana na kupeana maelezo ya nini hasa kimetokea. Zitto kama mwakilishi wa wananchi ana haki ya kuhoji na wao Serikali iliyowekwa na wananchi wanapaswa kujibu! Si kwa vitisho bali hoja kwa hoja na siyo vihoja!

Kwa mara nyingine tena, Zitto anaibuka kama shujaa aliyejeruhiwa; shujaa ambaye ana chama kidogo zaidi na yawezekana kikiwa dhaifu lakini chenye kuthubutu. Udogo wa chama chake si udhaifu wa hoja zake. Ningekuwa naweza kupendekeza kumaliza hili ningewaita Zitto na Prof. Assad na Wizara wakae chini waje na maelezo ya kumridhisha Zitto na kwa niaba yake kuwaridhisha wale waliodandia treni la “IKO WAPI TRILIONI 1.5”. Inawezekana kabisa treni hilo lilikuwa haliendi popote lakini mlio wake unashtua! 

Magufuli Bado ni Mtu Sahihi

Ukiniuliza mimi hata hivyo bado imani yangu haijapotea. Sidhani kama kuna Rais yeyote au mtu mwingine yeyote anayeweza kufuatilia haya kwa ukali unaostahili kama Magufuli. Wale ambao wanataka Magufuli ashughulikie wasome alama za nyakati. Watu wasije anza kulia tena “dikteta kacharuka” Rais Magufuli atakapoanza kuwatia ndani na kuwatimua watu kazi sababu ya ripoti ya CAG. Hili lipo, linakuja, na litawashtua wengine. Sisi wengine hatutashtuka kwa sababu tunajua kama kuna mtu anaweza kuthubutu kumvika paka kengele mtu ni Magufuli.

Ni kwa sababu hiyo bado tunamuunga mkono. Ashughulikie na wafujaji na wanaotumia madaraka vibaya, ashughulike na vibaka wa urithi wetu na utajiri wetu. Ashughulike kwa ukali na wanaochezea fedha za umma kama wana akili mbovu. Hawa wanaohoji, hawa wanauliza wala wasimsumbue kwani wanamsaidia hata kama wanafanya hivyo kwa sababu nyingine. Lakini kusaidia wanasaidia.

Tukimalizana na Hili 

Tukimalizana na hili; kwa mara nyingine tujadili sasa ripoti ya CAG na yale makubwa yaliyoibuliwa ndani yake, yale ya ufujaji wa fedha za umma, yale ya kutozingatia sheria za manunuzi, yale ya matumizi mabaya ya madaraka, yale ya vitabu vya ukaguzi vyenye kucheza tiari bado, yale ya akaunti zenye miiba na yale yote ambayo yanatuonesha na kututhibitishia kuwa tatizo letu la matumizi ya fedha za umma bado lipo.

Kwamba, bado pamoja na jihada kubwa za kuisafisha nchi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavvyo na kuwa za moto hadi ziwatokee watu “puani” kama alivyodai Magufuli, bado Rais Magufuli anakabiliwa na tatizo kubwa sana la kusimamia fedha za umma. Siyo yeye kama yeye tu bali watu wa safu za chini bado hawaogopi fedha za umma. Na kama hawaziogopi ripoti ijayo ya CAG itakuja na mengine na mwaka mwingine tutarudi tena hapa hapa mwakani mwezi Aprili.

Tumegoma kujifunza, hatutaki kujifunza, ni wagumu kujifunza.

Au ni wepesi kusahau.

itaendelea: mwanakijiji@jamiiforums.com

(278)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available