MWANAKIJIJI Riwaya Simulizi TANZANIA

Siku ya Mkosi – 2

Vicent anaanza siku yake kati hali ambayo inaweza kuonekana ni ya kawaida. Anapofika kazini kabla siku haijaanza vizuri anaitwa kwenda ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Mipango. Endelea.

 

SURA YA PILI

Nilikuwa nimelowa jasho; mwili bado ulikuwa unatetemeka. Kila nilivyofikiria moyo ulinilipuka. Koo lilikuwa limekauka nikiwa na kiu ya pipa la maji. Nilikuwa nimetembea kwa mwendo wa haraka sana toka pale ofisini hadi makutano ya Barabara ya Maktaba na Bibi Titi Mohammed. Sikuwahi kutembea kwa haraka namna hiyo kama nilivyotembea hivyo tangu nilipokuwa shule ya Msingi Nyanguge miaka ile. Nilitamani kukaa chini kupumzika lakini sikuamini kama nilikuwa na muda wa kufanya hivyo. Toka ofisini barabara ya Madaraka hadi nilipokuwepo nilikuwa nimetembea kwa muda mfupi sana. Sikutaka kusimama pale; mfukoni nilikuwa na shilingi elfu ishirini tu. Nilikuwa na mamilioni benki na nikapata wazo la kwenda ATM yoyote iliyokuwa karibu nichukue hela kidogo kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Nilikata kushoto kuelekea barabara ya Morogoro. Nilikuwa na akaunti yangu mojawapo kwenye benki ya Barclays na lilikuwa ni kusudio langu kufika pale mara moja. Kelele za magari yaliyokuwa yanaenda huku na kule sikuzijali; mara mbili hivi nilijikuta narushiwa matusi na makonda wa daladala kwa sababu walinikosakosa.

Akili yangu ilikuwa inazunguka kuliko pia; bado nilikuwa katika hali ya kutoamini kwani yaliyotokea kama saa moja kabla niliona kama ni ndoto fulani ambayo ningeweza kuzinduka. Kwa kadiri nilivyokuwa natembea ndivyo nilivyojua kuwa sikuwa ndotoni; nilikuwa kwenye tukio lililokuwa linaendelea kutokea wakati ule.

Nilipoingia pale benki kitu cha kwanza niliomba chupa ya maji. Kabla sijaenda kwenye kaunta kujaribu kutoa hela kidogo. Nilitumia tai yangu iliyokuwa mfukoni kujipangusa uso wakati nakunywa maji. Nilisogea mbele ya kaunta ya dada wa benki na kumkabidhi kitambulisho changu pamoja na fomu ya rangi ya njano ya kuchukulia fedha. Alichukua vyote hivyo na kuanza kuingia kwenye mtandao wao kuangalia akaunti yangu na kunipatia fedha zangu.

Nilikuwa nimezama kwenye mawazo hata sikumuuona dada yule alipoondoka pale dirishani. Niligundua kuwa hakuwepo wakati namuona akija pale  dirisha la kuchukulia fedha na mtu ambaye nilimtambua kuwa ni menewa wa tawi lile la benki.

“Vipi kuna tatizo” niliwawahi kabla hawajasema kitu

“Samahani Vicent, kuna tatizo kidogo katika kuifungua akaunti yako” alisema Meneja ambaye nilikuwa nafahamiana naye kwa muda mrefu tangu nifungue akaunti yangu pale.

“Iddi, kuna shida gani ni kwa akaunti zote au yangu tu?” niliuliza kwa udadisi.

“Sasa hivi ni akaunti yako tu” alisema Iddi Mchonde. Mchonde alikuwa ni mtu wa makamu ambaye alikuwa amenyoa nywele zake zote kipara. Alikuwa mfupi na mwenye kitambi kidogo ambacho kama kitaachwa kinaweza kuwa ni shida mbele ya safari. Alivyonipa jibu hilo niliuma midomo yangu kutafakari kwa sekunde chache. Kabla sijasema lolote aliniwahi.

“Naomba uje ofisini ili tuweze kufuatilia makao makuu kugundua kuna tatizo gani” alisema.

Nilipiga hesabu za haraka haraka nikaona kuna mtego hapo. Nilishaona filamu nyingi ambazo zinatoa mafunzo ya vitu kama hivi; mara nyingi hakuna jema hapo. Mawazo yangu yalikatishwa ghafla baada ya kuona gari la polisi likiingia katika eneo la benki ile; meneja hakuweza kuona kwani ilikuwa upande ambao alikuwa ameupa mgongo.

Niliamua kumshukuru na kumwambia kuna mahali ninaenda nitarudi tena baadaye labda tatizo litakuwa limetatuliwa. Sikutaka kupoteza muda nilibeba chupa yangu ya maji macho yangu yakiwa yanaelekea upande wa lile gari la polisi. Sikujua lilikuwa linafuata nini pale na sikutaka kujua lakini akili yangu yote ilikuwa inapiga ving’ora vya tahadhari. Nilitoka kwenye eneo la benki na mara moja kuchepukia upande mwingine wa jengo lile kuelekea barabarani ambako nilikuwa nimetokea. Nikashika tena barabara ya Bi Titi Mohammed kuelekea makutano yake na mtaa wa Uhuru.

Nilipofika kituo cha basi cha Baridi pale nikadandia kibajaji kuelekea mtaa wa Uhuru. Nilimuambia yule kijana anipeleke hadi tawi la NBC mtaa wa Samora. Akili yangu ilikuwa inaenda kasi sana; sikuwa nafikiria kitu kingine chochote isipokuwa uwezekano kuwa akaunti zako zote zinaweza kuwa zimepigwa stop na kama ni hivyo wapi nitaweza kupata fedha. Nilikuwa na kiasi kikubwa cha fedha taslimu nyumbani. Akaunti yangu nyingine iliyokuwa na fedha za Kitanzania ilikuwa pale; niliombea tu kuwa kilichonikuta kule Barclays kisirudie na kuwa  ilikuwa ni bahati mbaya tu ya mifumo yao na siyo kitu kingine chochote.

Dakika chache za kupishana na mabasi na magari ya kila namna nilifika pale NBC. Jambo la kwanza lililonishtua ni uwepo wa magari mawili ya polisi. Nilitembea mbali na pale benki nikiwa ninaangalia kwa machale. Kengele zangu za tahadhari ziliendelea kupiga kelele. Inawezekana hakikuwa kitu chochote lakini sikutaka kujaribisha kuona; nilijua natafutwa na wanaonitafuta wameamua kubana kila kinachoweza kubanwa kikabana.

Nilimwomba dereva wa bodaboda kuniteremsha makutano ya Azikiwe na Samora. Nilikuwa najisikia njaa maana tangu ile asubuhi nilipopata kifungua kinywa sikuwa nimekula chakula chochote na nilihitaji muda wa kufikiria vizuri nini cha kufanya. Hela kidogo niliyokuwa nayo mfukoni ingenitosha kwa chakula na labda ikibidi hata kujilaza kwenye hoteli mahali fulani. Lakini nilihitaji hela na mahali pekee nilipojua kwa uhakika palikuwa na hela taslimu ni nyumbani kwangu. Nilifikiria kuwa kama polisi walikuwa wananitafuta kwa hakika watakuwa wameshafika nyumbani kwangu au wananitegea nifike.

Katika kutafakari nini cha kufanya kati ya kumpigia simu Rita au mwenyewe kwenda pale nyumbani niliona lililokuwa salama zaidi ni kupiga simu nijue hali ilivyo pale nyumbani kuliko kwenda na kujikuta nimejiingiza mwenyewe mtegoni hasa baada ya yale matukio ya mapema mchana kwenye benki. Nilikuwa nafahamku kuwa polisi na vyombo vya usalama wanaweza kumfuatilia mtu kwa kutumia simu yake ya mkononi kwani teknolojia ya GPS ambayo simu zinatumia kuelekeza mahali inaweza pia kutumiwa kujua simu ya mtu iko wapi.

Nilitembea baada ya kushuka kutoka kwenye mtaa wa Samora hadi nilipofika Diamond Plaza; kulikuwa na mgahawa mmoja pale ambao nilikuwa napenda kwenda wakati wa mchana nikaingia kimya kimya kuagiza chakula wakati napanga mkakato wa nini la kufanya. Wakati nasubiria chakula nilichomoa simu yangu na kutoa sim card yangu pamoja na memory card nyingine ambayo ilikuwa na picha na video mbalimbali. Nilitoa betri kutoka kwenye simu kuhakikisha kuwa imezimika kweli. Nilifanya hivyo bila kuonekana na mtu yeyote na nilipomaliza kula tu nikaenda kutupa simu yenyewe kwenye pipa la takataka lililokuwa pale nje ya mgahawa; nilitupa betri baada ya kuvuka upande wa pili mtaa wa Mirambo kuelekea Barabara ya Sokoine. Nilitembea kwa muda kuelekea barabara ya Sokoine lakini muda wote ule akili yangu ilikuwa inazunguka kama pia kichwani mwangu, nilikuwa nahema, nimechoka lakini pia nikiwa nashuku kila gari lililopita karibu karibu yangu.  Sikutaka kusimama hadi nifike kwenye kituo cha mabasi Mwendokasi pale Mirambo inapokutana na ile ya Kivukoni. Sikuwahi kutembea maisha yangu yote kama nilivyotembea siku hiyo.

Sijui ni kitu gani kilininong’oneza kuangalia upande wa pili wa barabara. Inawezekana ni mizimu, hisia ya machale au ni bahati tu; macho yangu yalimuona mtu ambaye ni kama nilikuwa nimemuona mara nyingi siku ile na sikumtilia maanani. Hata hivyo, kumuona tena pale kulinifanya moyo ushtuke kidogo. Alikuwa ni kijana hivi labda kama miaka ishirini na tano lakini siyo wa kuzidi miaka thelathini. Alikuwa amevaa suruali ya jeans na viatu vya raba za Nike. Alikuwa amevaa tsheti nyeusi na miwani ya jua. Kilichonifanya nimuangalie ni kuwa mtu huyo huyo nilimuona mara ya kwanza wakati nakimbia kutoka ofisini baada ya kufukuzwa kazi. Nilimuona tena wakati natoka benki ya ya Barclays na baadaye nina uhakika wa asilimia mia moja alikuwa mbele yangu wakati bajaji inanishusha pale Azikiwe na Samora.  Lakini kumuona kwangu tena umbali wa kama mita hamsini tu kulitokea si kwa bahati mbaya; macho yetu yaligongana kwa sekunde kadhaa na mara moja niligundua kuwa alikuwa ananitazama mimi.

Nilipoepusha macho yangu kujaribu kufikiria nifanye nini nilishtushwa na mlio wa gari lililofunga breki mbele yangu kabisa. Nilirudka pembeni kujaribu kujiepusha nalo nikidhani limekosea njia. Kilichofuatia kilitokea kwa haraka, sikupata hata muda wa kuufanya ubongo wangu ufuatilie kwa makini kwani pamoja na kukutwa na hofu ya ghafla, wazo la kuwa naelekea kufa lilinijia kwa ghafla vile vile. Sikujua ni nini kilitokea. Ninachokumbuka ni kuwa baada ya lile gari kufunga breki kitu pekee nilichoweza kukiona ni kuwa lilikuwa ni gari aina ya Toyota Landcruiser mpya kabisa ikiwa na vioo vilivyotiwa giza.

Mlango wa mbele wa abiria na ule wa nyuma wa upande wa kushoto ilifunga kwa wakati mmoja; watu wawili ambao walikuwa ni mapandakizi ya watu walitokea kwenye kila mlango na kabla sijajua nini kinafuatia mmoja alikuja nyuma yangu na mara moja nikahisi mdomo wa bastola.

“Ingia kwenye gari!” aliniamuru. Niliangalia kama kuna mtu yeyote ameona. Sidhani kama watu waliokuwepo pale walielewa nini kinatokea.

“Nimefanya nini kwani?” nilijaribu kuuliza huku nikijizuia kuingia kwenye lile gari. Ndipo yule mtu mwingine alipokuja mbele yangu na kunipiga ngumi tumboni iliyonifanya niiname kwa maumivu makali. Nilijihisi kutapika kwa ghafla. Kabla sijainuka wote wawili walinisukuma mzoba mzoba kuingia kwenye mlango wa nyuma wa abiria na mmoja akaingia upande wa kushoto kwangu. Wakati huo huo mlango ule wa abiria upande wa kulia nyuma ya dereva ulifungulia na yule jamaa niliyekuwa nimemuona mwanzoni; aliyekuwa amevaa suruali ya jeans na tsheti nyeusi aliingia na kufunga mlango. Jamaa mwingine aliyetoka upande wa mbele wa abiria naye aliingia kwenye kiti chake na mtu mwingine aliyekuwa dereva nilimuona akiondoa mguu wake kwenye breki.

Kabla sijafungua mdomo wangu; jamaa mwenye tsheti nyeusi alinichomeka sindano shingoni na mara moja nilihisi usingizi mzito ukinijia. Nilijaribu kufungua mdomo kupiga kelele sikuweza. Nilijaribu kujifurugusa sikuweza. Niiliishiwa nguvu. Nilijikuta napiga kelele moyoni tu.

“Mungu nisaidie”

(294)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available