Afya & Mazingira TANZANIA

Shirika la Afya Duniani (WHO) Kuongozwa na Mwafrika kwa Mara ya Kwanza

Mkurugenzi Mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros FABRICE COFFRINI/AFP/Getty Images)

Mwandishi Wetu

GENEVA, USWISI –  Siku ya Jumanne Shirika la Afya Duniani (WHO) limepata Mkurugenzi wake mkuu mpya ambaye kwa mara ya kwanza anatokea Afrika. Dkt. Tedros  Adhanom Ghebreyesus kutoka Ethiopia alimshinda mpinzani wake kutoka Uingereza Dkt. David Nabarro katika raundi ya tatu ya upigaji kura kwa kupata kura za nchi 133 kati ya 186 zilizopiga kura. Uchaguzi ulifanyika mjini Geneva ambayo ni makao makuu ya shirika hilo. Mkurugenzi wa sasa anayemaliza muda wake ni Bi. Margareth Chan anayetokea Hong Kong. Dkt. Chan anamaliza muda wake mwezi Juni tarehe 30 ambapo Dkt Tedros atachukua ukurugenzi wa shirika hilo Julai Mosi.

Ushindi wa Tedros haukuwa rahisi kivile kwani pamoja na kuwa na uhakika wa kura karibu zote za bara la Afrika (kura 50) bado alipata shida kupata kuungwa mkono na baadhi ya nchi hasa baada ya tuhuma mbalimbali kuibuliwa dhidi yake. Bw. Tedros ambaye amewahi kuwa Waziri wa Afya wa Ethiopita amewahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na hivyo kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Ethiopita na ambaye rekodi yake ingeweza kuangaliwa. Baadhi ya tuhuma ambazo ziliibuliwa dhidi yake ni pamoja na kutumia misaada ya kigeni katika sekta ya afya kama silaha za kisiasa dhidi ya wapinzani wa serikali.

Katika ya wagombea wote watatu ni Dkt Tedros peke yake ambaye hakuwa na shahada ya udaktari wa binadamu, kwani shahada yake ni ya udaktari wa Falsafa katika Afya ya Jamii. Hii pia ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kuongozwa na mtu ambaye siyo daktari wa binadamu.

Ametuhumiwa pia kuficha kuibuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu wakati yeye akiwa Waziri wa Afya huko Ethiopia. Hata hivyo tuhuma hizo zilionekana kuwa zina lengo la kumchafua hasa baada ya mtoaji wa tuhuma hizo kujulikana kuwa alikuwa ni mshauri asiye rasmi wa mgombea wa Ukurugenzi wa WHO kutoka Uingereza Dkt. Nabarro. Nabarro mwenyewe alikanusha kumtuma mtu huyo kuibua tuhuma hizo japo alikiri kuwa alishawahi kuzisikia.

Katika mfumo wa kura za siri ambapo kila nchi ilikuwa na kura sawa; Tedros aliibuka kidedea na kusababisha mlipuko wa shangwe kutoka kwenye ukumbi hasa baada ya mwakilishi wa Ethiopita kutoka ndani na kupiga kelele kwa waandishi “Tumeweza tumeweza!” Dkt. Tedros anakuwa ni Mkurugenzi wa nane wa shirika hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1948 ikiwe ni mojawapo ya taasisi muhimu za Umoja wa Mataifa. Hii pia ni mara ya kwanza kwa mkurugenzi kuchaguliwa kwa kura za siri za wajumbe wote.

“Uchaguzi huu umeleta uwazi mkubwa kwa shirika na pia unampa uhalali zaidi Mkurugenzi” alisema Tedros baada ya kuchaguliwa kwake na kuongeza kuwa “nitatumia uhalali huu kuleta mabadiliko na mageuzi yanayohitajika katika taasisi hii nyeti ili kuweza kurejesha heshima ya kila mwanachama na kila mwananchi duniani”.

Katika kutekeleza majukumu yake mapya Dkt. Tedros ameahidi kuhakikisha kuwa WHO inaelekeza nguvu zake katika kuhakikisha kuwa afya duniani inapewa kipaumbele hasa kwa watu ambao hawana huduma nzuri ya afya hivi sasa. Amenukuliwa akisema kuwa haipaswi watu kufa au kupata huduma mbaya ya afya kwa sababu ni maskini tu.

(84)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available