TANZANIA

Serikali Yajitetea Mauaji ya Akwilini; Yatafuta wa Kumbebesha Lawama

Waziri wa Ndalichako wa kwanza kushoto, Naibu Waziri Masauni katikati na Msemaji wa Serikali. Picha na Michuzi Jr wa Michuzi Blog.
  • Wafuasi 40 wa Chadema Washikiliwa
  • Polisi 6  Pia

Na. M. M. Mwanakijiji

Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama jaribio la serikali kutafuta mchawi wa mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar-es-Salaam, serikali leo imetaka uchunguzi ufanyike na watu wote waliohusika kusababisha mauaji hayo wafikishwe kwenye mkono wa sheria. Hayo yamesemwa leo na Mawaziri kadhaa walipozungumza na waandishi wa habari katika kutoa pole na muongozo wa kuelekea kufuatia msiba huo uliolistusha taifa na kuongeza hisia za unyonge kwa watu wengi.

Katika taarifa yake kwa umma leo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Joyce Ndalichako amesema kuwa yeye mwenyewe na Rais Magufuli wote wamesikitishwa na kushtushwa na taarifa za msiba huo. “Napenda kutumia fursa hii kutoa pole sana kwa Familia na ndugu, jamaa, na marafiki wote wa Akwilini” amesema katika taarifa yake.

Hata hivyo, badala ya kunung’unikia kupoteza kwa uhai wa binti huyo ambaye alikuwa kwenye jitihada zake za kutafuta maisha Waziri Ndalichako katika taarifa yake ameonekana kusisitiza kuwa Akwilini alikuwa ni mkopaji wa Serikali. “Marehemu Akwilini alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya wanafuunzi wa elimu ya juu”. Haikufahamika mara moja kwanini Dkt. Ndalichako amezungumzia suala la mkopo alipokua anatoa pole zake.

Kauli yake nyingine ambayo inaweza kuwa imeacha ukakasi katika wachambuzi wa siasa ni ile ambayo inaashiria anailaumu CHADEMA kwa mauaji ya binti huyo. “Nawaihi sana Watanzania wenzangu tujiepushe kukiuka taratibu na miongozo inayookuwa inatolewa ikiwemo  na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusasbabisha maafa kwa watu wasio na hatia” amesema Dkt. Ndalichako katika taarifa iliyojaa makosa mengi ya kiuandishi na kisarufi na hivyo kuonesha tatizo la elimu Tanzania lipo hadi ndani ya wizara inayosimamia sekta hiyo.

Akwilini (pichani) aliuawa siku ya Ijumaa katika tukio ambalo limejaa maswali mengine na lisiloelezeka likaeleweka. Taarifa zinaonesha kuwa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo kukataliwa kupewa fomu kwa wasimamizi wake wa Uchaguzi wa marudio iliamua kufanya maandamano yasiyo rasmi kwenda kuweka shinikizo ili wasimamizi wake wapewe fomu hizo ambazo zingewaruhusu kusimamia uchaguzi mdogo Wilaya ya Kinondoni siku ya Jumamosi. Hata hivyo, maandamano hayo yalikutana na  ukuta wa polisi ambao waliamua kuyatawanya kwa kutumia nguvu na ni katika kutawanya huko risasi zilipigwa na moja ya risasi (haijajulikana kama ni zaidi ya moja) ilimpiga Akwilini aliyekuwa ndani ya basi katika shughuli zake (innocent bystander) ambazo hazikuhusiana na maandamano ya kisiasa wala uchaguzi.

Kwa mujibu wa Ndalichako, binti huyo alikuwa akipeleka barua “mahali alipokuwa anatarajia kufanya mazoezi kwa vitendo yatakayoanza 27/2/2018”. Pamoja na Akwilini kondakta wa basi ambalo Akwilini alikuwemo naye alijeruhiwa na risasi. Tukio hili limeonesha pia jinsi gani watu wetu wengi hawana ufahamu wa utoaji wa huduma ya kwanza na mfumo wetu wa uokoaji unavyosababisha watu wengi kupoteza maisha kwa kukosa huduma ya kwanza.

Viongozi wengine wa serikali waliozungumzia suala hilo leo ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Hamad Yusuph Masauni ambaye alisema  kuwa serikali itafanya uchunguzi na kuhakikisha kuwa wote waliohusika na tukio watachukuliwa hatua. Ameahidi uchunguzi huo utafanyika kwa haraka; japo hakutaja muda na na ni chombo gani ndani ya serikali kitafanya uchunguzi huo na hivyo kuweza kufanya uchunguzi usiaminike sana hasa kama utasimamiwa na chombo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambalo Jeshi la Polisi liko chini yake.

Yeye hata hivyo alienda mbali zaidi kuliko Ndalichako ameonekana kuanza kulenga pia viongozi wa siasa na kuhakikisha kuwa hata polisi nao watachunguzwa “Tutahakikisha hatua zinachukuliwa haraka kwa waliohusika na haku na ambaye ataachwa, kwe ofisa wa polisi au viongozi wa vyama vya siasa”. Kuna mashaka kama kauli yake ya “viongozi wa kisiasa” inawajumuisha viongozi wa Serikali ya chama chake au wanasiasa kutoka chama tawala.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limesema kuwa linawashikiliwa watu 40 ambao wanafikiriwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA pamoja na askari 6 ambao wanasadikiwa kurusha risasi kwenye tukio hilo. Hilo limesemwa na Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar-es-Salaam SACP Lazaro Mambosasa.

Kuanzia Jumatatu hii ZamaMpya itakuja na mfululizo wa siku tano wa makala zinazohusiana na hali ya kisiasa ya Tanzania na mwitikio wetu kama taifa.

 

(182)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  • Tulipokuwa tunamkosoa mtawala huyu wewe ulimtetea sana sasa nadhani akili yako imeanza kurudi kwenye ufahamu wake,hii mimi nafikiri ni wakati sasa umefika ukweli usemwe kwa ukamilifu wake.
    Askari aliyeweka silaha chini naona sasa umechukua silaha zako. Karibu kwenye uwanja was mapambano tuitafute haki.

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available