Maoni TANZANIA

Neno la Leo: Sitaki Kusema Huu ni Wazimu; Hivyo, Sisemi!

Na. M. M. Mwanakijiji

Nashukuru Mungu mimi siyo mtu mwingine. Siyo kwa ajili ya majivuno kama yule mtu wa kwenye Injili ila tu kwamba, kuna baadhi ya vitu najua katika akili yangu timamu na katika mazingira tuliyonayo haya siwezi kuvisema hata kama naweza kuvisema nikiamua. Yaani, kuna baadhi ya mambo baada ya kuyafikiria sana na kuona jinsi yasivyo na maana naona hayafai kutamkwa kutoka katika kinywa changu hivyo nayaachilia tu yapite. Hivyo, kuna baadhi ya mambo ambayo kwa kweli kabisa najua siwezi kuyasema hata nikilazimishwa sana na kubembelezwa kwa nyimbo za taarabu.

Najua unaweza kujiuliza ni mambo gani ambayo siwezi kuyasema. Sasa ukiniuliza hivyo ina maana itabidi niyasema na mimi nimesema siwezi kuyasema! Lakini kama kijiji kizima kikiitisha kikao chini ya mwembe na kuniuliza “ah kwanini usiyaseme tu ili tujue” naweza kufikiria sana na kuamua kuyasema labda kwa kumnong’oneza mtu aliye karibu yangu ili yeye ayaseme kwa niaba yangu ili sauti yangu isisikike kuyatamka mambo hayo.

Kwa mfano, moja wapo ya mambo ambayo ningeweza kuyaita ni wazimu uliopitiliza – yaani wazimu ulifika halafu ukapitiliza – basi ni hili jambo la “magenius” fulani ati kuzuia watu wasichangie damu kama namna ya kuonesha kwao kuguswa na tukio lililomgusa Tundu Lissu. Yaani, kama ingekuwa wazimu unateleza basi umeteleza pale ulipofikiria unaweza kuishia basi haukuishia hapo ukapitiliza!

Hivi, mtu anapoamua tu katika kizunguzungu cha ulevi wake wa madaraka kwamba hataki tu watu wajitokeze au kukusanya kuchangia damu kwenye kile kichwa chake kuna vitu gani atakuwa amejiambia kabla ya kufikia uamuzi kama huo? Ni lazima kuna kitu hakiko sawa. Kuna habari ya kimataifa leo kutoka Afrika ya Kusini ambapo jamaa mmoja ameuawa na polisi baaday a kumkuta akiwa anamla mwanamke mmoja aliyemuua; yaani anamtafuna kwa meno kama yuko kwenye sherehe! Sasa mtu kama huyo ni lazima ujiulize kuwa ndani ya fuvu lake ambapo inadaiwa kuna kile kinachoitwa “grey matter” huyu mwenzetu ya kwake itakuwa inafanya kazi kwa namna gani? Au inawezekana imesimama kabisa na kuona mwili wa mwanadamu mwenzake kama kuku wa Salanda?

Sasa mtu mzima na akili zake timamu anaweza vipi kwa mfano kuzuia watu kwenda kujitolea damu sehemu mbalimbali wakati kila siku watu wanakufa kwa kukosa damu au kuwepo kwa upungufu wa aina fulani ya damu na hivyo mahitaji ya benki ya damu ni makubwa sana. Miezi kadhaa nyuma nilijiandikisha kutoa damu kwenye taasisi ya Msalaba Mwekundu lakini sikuweza kutimiza ile mihadi. Juzi wamenipigia simu kuniuomba kama naweza kwenda kujitolea damu tena hata kwa kunipa kajizawadi ka dola 25 ya usumbufu! Sasa hawa walio daraja la kwanza wanavyojua uzito wa watu kujitolea damu na wanatafuta watu wanaojitolea hivi kwanini sisi wengine tuone kama ni wakati wa kumkomoa fulani?

Sasa hili kwa kweli nisingetaka kulisema kwani kwanza limeniondoa ile ladha ya kulisemea kwani haiingii akili mtu akaamua kukataza watu kwenda kuokoa maisha ya mtu na mtu huyo bado akawa timamu kichwani – haijalishi sana kama amevaa suti au la! Upande mwingine hatuna budi kuwapongeza watu wote ambao wamejitolea damu hadi hivi sasa na wale wote ambao walionesha nia ya kufanya hivyo.

Kinachoudhi ni kuwa kweli kuna mtu anafikiria hiyo damu inayochangwa kweli ingepelekwa Nairobi kumsaidia Lissu? Kwani wameambiwa Lissu anahitaji damu zaidi huko? Ni wazi tu kuwa wanaochangia damu wanafanya hivyo kuonesha mshikamano lakini damu wanayochangia kwa kiasi kikutwa itatumika katika mahospitali ya maeneo yao kuokoa maisha ya watu wengine. Sasa hili ubaya wake ni nini? Oh kwa vile wamesema wanamchangia “Lissu”? Kwani Lissu peke yake katika taifa zima anahitaji msaada wa damu? Kuna Lissu wangapi kila siku wanapoteza damu? Au labda waamue kutunga jina la kuwa wanamchangia damu “Petero” ndio wataruhusiwa?

Ila la kuangalia sana ni kuwa kama kiongozi wa kisiasa anapigwa na kujeruhiwa na watu wanakimbia kutoa damu ambayo labda hawakuwahi kufikiria kuitoa hadi mtu wanayempenda ameumizwa, itakuwaje kama “evil genius” mmoja akaamua kuwa hili la kuumiza watu wanaopendwa linafanya watu wachangie damu na hivyo kila mwezi akaamua kumpopoa mmoja? Wazo linatisha hili!

Sasa kwa vile sikutaka kusema jambo lolote wacha ninyamaze; nisije kuambiwa nimewaita watu wana wazimu, sijui “magenius” sijui madudu gani. Wala sisemi na niliyemnong’oneza akisema nilichosema namruka vile vile. Na sitaki mtu aniulize nasema nini kuhusu wale wanaouziwa kufanya maombi ya Lissu – kana kwamba wana ukiritimba na Mungu – na wale wengine wanaouziwa kufanya albadiri sijui na vitu gani vingine. Kwani mtu akisema anaenda kuomba ina maana anaenda kumlazimisha Mungu akubali? Mmh.. haya ngoja niache nisije kuanza kusema mambo mengine ambayo sikutaka kuyasema bure.

Na kwa vile sitaki kusema basi sisemi na mkinilazimisha nagoma!

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(168)

About the author

bongoz

2 Comments

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  • Duh!
    Hii ni kali,ila kiukweli nchi hii ni yetu sote,hii tabia ya watu fulani kujiona wao ndiyo wana hati miliki ya kuwaamulia wengine hata vitu vya haki za kikatiba mwisho wake tutaishia kubaya!

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available