TANZANIA

Mwanasheria Mkuu George Masaju Atumbuliwa; DPP Kufuatia?

Na. M. M. Mwanakijiji

Rais John Magufuli amemuondoa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Bw. George Masaju siku moja tu baada ya Rais Magufuli kulalamikia utendaji kazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu na ile ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Pangua hiyo pia imemhusisha Naibu Mwanasheria Mkuu Bw. Gerson Mdemu ambaye naye ameondolewa katika wadhifa wake.

Wote wawili Masaju na Mdemu wameteuliwa kwenda kuwa Majaji katika Mahakama Kuu ya Tanzania. Wakati huo huo kufuatia pangua hiyo Rais Magufuli amemteua Bw. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu. Kabla ya kuteuliwa kwake Bw.  Kilangi alikuwa ni Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino tawi la Arusha. Rais Magufuli amemteua Bw. Joel Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu akichukua nafasi ya Mdemu. Kabla ya kuteuliwa kwake Ngwembe alikuwa ni Mkurugenzi wa Sheria Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu Mafuta.

Akizungumza katika Siku ya Sheria Rais Magufuli alinukuliwa akilalamikia utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika kufuatilia kesi mbalimbali. “Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili, hivi sasa kuna kesi za Shilingi Bilioni 169.1 na Dola za Marekani Milioni 38.2 zinasubiri tu na nchi inakosa mapato” Alinukuliwa Rais Magufuli kusema.

Hata hivyo, haijajulikana kama mabadiliko haya yatakuwa na tofauti yeyote katika uendeshaji wa kesi, upelelezi na kufuatilia mashtaka mbalimbali nchini kwani hii si mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kulalamikia mifumo ya sheria nchini.

 

 

(309)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available