TANZANIA

MwanaKJJ Leo: Nani Amemzoea Nani; Maswali Potofu au Sahihi

Na. M. M. Mwanakijiji
Ukiangalia kwa karibu sana unaweza kuona kuwa kuna mambo yameanza kuzoeleka. Kama siyo mambo basi kuna watu wameanza kuzoeleka, na kama siyo watu basi kuna vitu vimeanza kuzoeleka. Au yote hayo. Tunapoanza kuingia katika nusu ya pili ya miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli kuna mambo yanahitaji kuangaliwa, kuhojiwa na hata ikibidi kuamuliwa kama ndivyo yalivyo au sivyo yanavyotakiwa kuwa.
Nikiangalia kwa karibu mwelekeo wa utawala wa Rais Magufuli kuelekea 2020 ni wazi kuwa kuna mambo yanahitaji kuulizwa – inaweza kuwa ni maswali sahihi au maswali potofu. Kama ni maswali sahihi au potofu ni jukumu la wengine kuamua lakini kwamba ni maswali ambayo yamejengeka katika fikra zangu hili sina shaka nalo.
Maguful Ameuzoea Urais?
Mojawapo ya mambo ya kwanza yaliyotokea mara baada ya Rais Magufuli kuapishwa ni hisia kuwa kuna utawala mpya nchini na kila mtendaji alitakiwa kuwa katika mkao wa mguu sawa. Nakumbuka pale alipotembea kutoka Ikulu kwenda Wizara ya Fedha na baadaye Muhimbili na hatua mbalimbali za awali za kuleta nidhamu kulivyosababisha watu kuhakikisha wanawahi makazini. Wengi tunamkumbuka bwana yule aliyekutwa ameenda kunywa chai wakati Rais anawauliza “huyu yupo wapi?”.
Watumishi wa umma walianza kujionesha kuwa mambo ya ‘kawaida’ hayapo tena. Wanaotakiwa kuwa ofisini saa mbili walianza kujitokeza saa moja asubuhi na wengine kwa mara ya kwanza walianza kwenda na vyakula vyao ili wasije kujikuta wako kwenye matatizo. Kulikuwa na harufu ya upya fulani hivi ambao ulileta matumaini. Mahospitalini watu walikuwa wanafurahia huduma na utu mpya ambao ulianza kuoneshwa. Mfano binafsi ni kuwa shemeji yangu mmoja alimpeleka mke wake Muhimbili kwa uchunguzi wa kawaida siku moja. Ilikuwa kawaida alipokuwa akimpeleka kabla ya ujio wa Magufuli alimshusha na yeye kwenda mjini kuendelea na shughuli zake hadi mida ya jioni ambapo alimfuata kwenda kumchukua. Hata hivyo, mara baada ya Magufuli kuingia na wakati ule wa upya alimpeleka na kabla hajapata mahali pa kuegesha gari lake kwa ajili ya shughuli zake nyingine alipigiwa simu kuwa mkewe tayari ameshaonana na daktari na kuandikiwa dawa na vipimo vingine; alitakiwa kwenda kumchukua. Hili lilimshangaza na kumtia moyo.
Sijui ni kwa kiasi gani hali hii bado ipo? Je, watu wameanza kuuzoea utawala huu na kuwa sasa mambo ambayo yalianza kuonekana ni hewa mpya yameanza kuwa kama kawaida? Ni kwa kiasi gani watendaji wanaendelea kuonesha mwamko wa kutenda mambo katika mwongozo mpya?
Nitatoa mfano mmoja ambao wengi wameujadili sana ulipotokea. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ya mwaka 2016/2017 ikiangalia kwa mara ya kwanza mwaka mzima wa Serikali ya Magufuli imetuonesha kuwa watu bado hawaogopi fedha za umma, hawajali taratibu za serikali na kanuni za kimataifa za uhasibu zinapuuzwa. Ripoti ile imeendelea kutuonesha ni jinsi gani sheria ya manunuzi bado inaonekana kama ni mapendekezo ya hiari na si matakwa ya lazima na matokeo yake bado tunakutana na vitabu vyenye kuota miguu kila wakaguzi wanapopita!
Nilitegemea sana watu wangejua jinsi gani fedha za umma ni chungu. Niliwahi kupendekeza miaka ya nyuma kuwa wakati ulikuwa umefika kwa kumpa CAG madaraka ya kisheria ya kumsimamisha afisa au mtendaji ambaye ofisi yake itaonekana na mapungufu fulani. Kwa mfano, CAG anapopita na kukuta ofisi haioneshi vitabu kwa ajili ya ukaguzi inawezekana vipi mtendaji akaendelea kukalia ofisi kama hata vitabu hajui vilipo? Au CAG anakuta ofisi imetumia bila maelezo au nje ya taratibu shilingi zaidi ya milioni 50 halafu mhusika bado anaendelea kukalia kiti cha uongozi? Kama Magufuli alivyosema fedha za umma ni sumu, mbona watu hawadondoki huku na kule na badala yake wanakaa bado ofisini mwaka mzima baadaye?
Ninaamini CAG anapaswa kuwa na nguvu ya kisheria ya kuweka Emergency Financial Manager (EFM) pale ambapo anakutana na mapungufu makubwa ya usimamiaji wa fedha za umma. Jukumu la EFM huyo likiwa kusimamia mahesabu na kuhakikisha kuwa taasisi husika inarudi kwenye taratibu zilizokubalika za usimamizi wa fedha za umma. EFM atakuwa na nguvu ya kumsimamisha au kumtimua na kumfunguilia mashtaka afisa yeyote atakayeonekana kuhusika na upotevu wa fedha za umma; kama fedha za umma ni chungu ni lazima ziwe chungu kweli kweli!
Lakini watu hawaogopi au hawajioneshi kama wanaogopa au kujali tena kama Rais ni Magufuli. Rafiki yangu mmoja ameniambia sasa hivi “watu wanapiga kama wana akili mbovu”. Nilipouliza kwanini aliniambia kuwa kwa sababu watu wanajua sheria ya manunuzi haifuatwii kwa kiasi kikubwa. Viongozi kila mmoja anajiamulia kutoa tenda au kufanya mambo kwa jina la “kuharakisha maendeleo” na matokeo yake kanuni za manunuzi ya umma hazifuatwi.
Urais Umemzoea Magufuli?
Lakini jingine linaloweza kuwa linatokea ni kuwa mwanzoni Rais Magufuli aliingia kama mpya katika Urais. Alikuwa Waziri kwa muda mrefu lakini Urais ni ngazi nyingine kabisa. Aliingia na hamasa ya madaraka haya makubwa na hivyo alianza kuyatumia na katika kufanya hivyo alijikuta kweli ana madaraka makubwa sana. Matokeo yake? Yeye alianza kuuzoea Urais na hatima yake ni kuwa Urais umeanza kumzoea.
Hili ni swali lenye matatizo kidogo. Urais ni wadhifa uliowekwa kikatiba na unaongozwa na kanuni mbalimbali. Swali, je kanuni hizi zinamuwezesha au kumbana vipi Rais kutekeleza majukumu yake ya urais? Kama kanuni au sheria zinaonekana kumbana sana Rais kiasi kwamba anaweza kujikuta anafanya mambo kwa “prerogative” zake ni kwa namna gani anaweza kushughulikia vikwazo hivyo bila yeye mwenyewe kujikuta anaonekana kuvunja au kupindisha sheria?
Lakini Urais unaweza kumzoea Magufuli kiasi cha kumfanya aone ni mojawapo tu ya kazi za kawaida na uzito wa ofisi hiyo asiubebe ipasavyo. Kama Rais, Magufuli anajukumu kubwa la kuweka kwenye mizani matamanio, matarajio, ndoto, mipango na majukumu mbalimbali kama Rais wa wote na siyo wa kundi moja. Mojawapo ya mambo ambayo yanaweza kuonesha kuwa Urais umemzoea Magufuli ni fikra zinazoweza kuwa zimejengeka kuwa Magufuli ni Rais kwanza kabisa wa wale waliompigia kura (ambao hawezi kuwajua), halafu ni wa Wana CCM halafu ni wa wale wenye kumuunga mkono (bila kujali vyama vyao) n.k.
Ukikubali fikra hizi unawez kujikuta unadhania inampasa pia kutenda kwa mwelekeo huo huo. Hili hata hivyo limeshaonekana siyo kweli mara nyingi – ukiondoa wanasiasa wachache wanaolazimisha kuliona. Lakini, kuna jambo moja si la kukisia, vyama vya upinzani Tanzania havifanyi kazi zake kwa uhuru na haki ambazo zimeanishwa katika sheria na Katiba. Hili linawezekana ni kwa sababu ya kuona kuwa vyama hivi vinapotezea ‘watu muda’ na kuwa ‘siasa’ ziinachukua sana muda wa watu.
Sasa kama hili ni kweli – kwamba vyama vya upinzani zinapotezea sana watu muda wa kufanya kazi – njia sahihi kwa Serikali kushughulikia ni kupitisha mabadiliko ya Katiba na kutoka hapo sheria ili kuanisha ni katika mazingira gani vyama vya upinzani vinaweza kufanya kazi zake. Hili pia ni kweli kuhusiana na haki nyingine mbalimbali za kiraia (civil rights).
Tumeanza Kuzoeana?
Lakini pia kuna uwezekano watu wameanza kuzoeana na hivyo kuchokozana na kuzodoana kwa mtindo wa siasa zilizokuwa baada ya uchaguzi wa Rais Kikwete 2005. Kwamba, siasa zetu zimerudi katika kuendekeza “upande” huu na “upande ule”. Kwamba, upande mmoja unajitahidi kwa udi na uvumbi kutafuta kashfa na kuziibua kashfa mbalimbali ili kuonesha kuwa serikali ni ile ile. Upande mwingine serikali na chama chake nao wanajitahidi kwa kadiri wanavyoweza kuzima juhudi za upinzani ambazo zinaweza kuwapa upinzani ujiko. Matokeo yake, siasa zetu zimerudi katika kunyemeleana, kutegeana, kuumbuana na kuzodoana. Ukiangalia yanayoendelea Bungeni sijui kama unaweza kuwa umeona kuna tofauti kubwa kati ya siasa zetu za sasa na zile za 2005-2015.
Inawezekana tumerudi tulikokuwa bila kujijua; kwamba tuliko ndiko tulikokuwa, na tunakokwenda ndiko tulikoondoka, tulipo ndipo tuliposema tumeaga?
Matokeo yake, utaona hata mtaani watu wameanza kuzoeana kisiasa; hakuna ambaye anaonekana amesimama mahali bora zaidi kwa hoja. Tofauti ya utawala wa Magufuli sasa na ule wa Kikwete ni nini hasa? Nina wazo juu ya hilo pia na linaniacha na maswali mengine mengi, maswali ambayo yanaweza kuwa ni sahihi au potofu.
Ila haya ya leo sijui kama ni sahihi au potofu. Nani Amemzoea Nani?
Niandikia: mwanakijiji@jamiiforums.com

(128)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available