MWANAKIJIJI TANZANIA

MwanaKJJ Leo: Bundi CHADEMA? Lowassa Akutana na Magufuli Ikulu; Amsifia

Lowassa akizungumza na Rais Magufuli Ikulu leo (Picha na Ikulu)

Na. M.M. Mwanakijiji

Katika jambo ambalo limetafsiriwa na baadhi ya watu kama kuuchanganya upinzani leo Waziri Mkuu wa zamani Bw. Edward Lowassa amekutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar-es-Salaam kwa mazungumzo. Kufuatia mazungumzo hayo Lowassa alizungumza na waandishi wa habari na alimmwagia sifa Rais Magufuli na serikali yake kwa kazi nzuri inayofanywa. Maelezo yake hayakuelezea kama katika mazungumzo na Rais Magufuli kama Lowassa alizungumzia masuala ya haki za kiraia, masuala ya usalama na masuala mbalimbali ya kidemokrasia ambayo chama chake kimekuwa kikizungumzia sana siku za karibuni.

Kutokana na hilo baadhi ya viongozi wa Chadema na hata wanachama wa kawaida wameanza mara moja kumshangaa Lowassa kwa uamuzi wake wa kukutana na Magufuli na kummwagia sifa kama alivyofanya. Miongoni mwa viongozi walioonesha mwitikio wa kutofurahishwa na jambo hilo ni Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema. Lema akiandika katika ukurasa wake wa Twitter alisema hivi “Mh Lowassa umeikosea Tanzania kwa kauli baada ya kutoka Ikulu. Mema yapi umeyaona katika Serikali hii? Wakati Mbunge Lissu bado anauguza majeraha ya risasi, maiti zinaokotwa, Uchumi unaanguka, Benki zinafungwa, Demokrasia imekufa Bungeni/Nje ya Bunge na Sioi mkwe wako bado yuko Magereza”

Mwenyekiti wa CHADEMA naye Bw. Freeman Mbowe ambaye alifanya juhudi kubwa kumleta Lowassa ndani ya Chadema na hatimaye kutengeneza njia ya kumfanya kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015 ameonesha kushangazwa na kauli hiyo ya Lowassa. Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW Idhaa ya Kiswahili) Bw. Mbowe amesema kuwa kauli za Lowassa Ikulu ni zake binafsi na hazikuwa zinawakilisha msimamo wa chama.

Unaweza kumsikiliza Mbowe hapa: WhatsApp Audio 2018-01-09 at 11.01.42 AM

Wakati huo huo baada ya mkutano wake na Magufuli jioni hii taarifa zimekuja zinazoelezea kuwa Mzee Lowassa anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari kesho katika hoteli ya Serena. Haijajulikana anataka kuzungumzia nini hasa lakini kwa kuangalia wimbo wa kuhama Chadema unaoendelea sasa hivi na jinsi alivyogeuka na kuisifia Serikali ya Magufuli na kuacha kutetea misimamo ya Chadema wala ajenda zake hadharani hapo jana, ni wazi kuna uwezekano wa Lowassa kuamua kufanya mambo makubwa mawili.

Kuna uwezekano wa yeye kutangaza kustaafu siasa rasmi na hivyo kuamua kujivua nafasi zote za uongozi katika Chadema. Anaweza kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa wanasiasa vijana na wengine kuendelea kuijenga Chadema kuelekea chaguzi za 2019 na zile za 2020. Jambo jingine analoweza kulifanya atakapozungumza na waandishi wa habari ni kutangaza kukirudia chama chake cha awali cha CCM ambacho alichokulia na kukitumia kwa muda mrefu na ambacho kilimpa nafasi mbalimbali za juu uongozi nchini.

Endapo Lowassa ataamua kufanya hilo la kwanza ni wazi hilo la pili halitokuwa mbali; lakini kama ataamua kufanya hilo la pili ni wazi kuwa Lowassa atakuwa ameona kuwa hawezi kuendelea na siasa za upinzani kwani gharama ya kuwa upinzani ni kubwa sana na hakuwa tayari kuendelea kuilipa.

Kwa baadhi yetu ambao tumekuwa tunafuatilia siasa za upinzani hasa kufuatia Chadema kujivuruga kwa kumkumbatia Lowassa na kumtupa Dkt. Slaa kwa kejeli na dharau namna ile kuna somo ambalo viongozi wa Chadema watapaswa kuulizwa. Ni matumaini yetu endapo lolote litatokea kufuatia Lowassa kuamua ama kustaafu siasa au kujiondoa Chadema, wanachama na mashabiki wa Chadema watakasirishwa na uongozi wao na kutaka viongozi wote wa juu kuwajibika kwa kukivuruga chama.

Wakati umefika kwa wanachama wa kweli na wapinzani wa kweli ndani ya Chadema kuoneshwa kukasirishwa na uongozi wa chama cha kuanza kuoneshwa kukasirishwa na kutaka watu wawajibike kuanzia Mwenyekiti na Kamati Kuu nzima. Wasipoonesha hasira zao kwa viongozi wao na badala yake wakiendelea kumlalamikia Magufuli kwa kuvugura upinzani wataendelea kuwa kama mbuni aliyeficha kichwa chake mchangani na kama wale ambao wanazungumzia matatizo yote yaliyokuwemo ndani isipokuwa yule tembo aliyesimama pembeni!

Ni wakati wa malipo. Na alipo wataendelea kuwepo?

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(193)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available