TANZANIA

MwanaKJJ Ijumaa: Serikali Inaweza Ku’cancel’ Oda za Bombardier?

Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya matatizo ya muda mrefu sana ambayo yamekuwa yakitusumbua sana kama taifa na hasa chini ya utawala huu wa Chama cha Mapinduzi ni tatizo la mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusiana na uwekezaji, biashara na mambo mbalimbali ya uchumi. Kuanzia sakata la IPTL hadi hiivi karibuni masuala ya manunuzi ya kimataifa hoja ya “mikataba” imekuwa ikija na kusimama na kusahauliwa tena kama watu tusiojifunza lolote kutokana na mang’amuzi ya nyuma (not able to learn from past experience).

Sakata la ununuzi wa ndege za kisasa kutoka Canada za Bombardier linaweza kutajwa kama mfano mwingine wa jinsi gani tumeshindwa kujifunza kutoka huko nyuma. Ndege zetu (tumeambiwa zimelipiwa taslimu) zinashikiliwa kwa sababu Serikali inadaiwa na makampuni mengine ya pembeni. Ndege zimekamatwa kwa amri ya mahakama na hatitoachiliwa hadi tuwalipe wale wanaotudai. Zimekamatwa kabla hazijakabidhiwa mikononi mwetu na zimekamatwa ikiwa ni kama kulishika taifa hostage (hostage taking).

Ni wazi kuwa wakati tunaamua kununua ndege hizi Serikali ilikuwa inawashauri wake na wanasheria mbalimbali ambao wanajua sheria za kimataifa na masuala ya biashara. Tulipoamua kununua ndege hizo kutoka Canada, tulikuwa tunajua tunadaiwa na makampuni mbalimbali (ni rahisi kuona haya kwenye mitandao ya mahakama za kimataifa za arbitration). Tulikuwa tunajua, au Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilipaswa kujua kuwa wanaotudai wana options gani katika kupata kile kinachodaiwaw kuwa ni chao. Kwamba, walikuwa na haki ya kisheria ya kukamata mali za Serikali kufidia deni.

Kama walijua hili, na bado wakaamua kwenda kununua hizi ndege huko Canada ni wazi kuwa wameonesha dalili iliyopitiliza ya incompetence! Kama hawakujua hilo bado wameonesha dalili ya mediocrity iliyovuka mipaka. Vyovyote vile ilivyo, katika mazingira ya biashara za kimataifa, haikupasa hata kidogo kujiweka katika mazingira haya kama vile ni watu ambao tunaishi kwa kudekezwa, kwamba kwa vile sisi ni Tanzania, na ni nchi maskini basi tutaonewa huruma!

Baada ya hilo kusemwa, hoja inabakia. Katika mkataba wa manunuzi ya ndege hizi (sijui kama ni mkataba mmoja au ni tofauti tofauti), je tuliweka vipengele vya kuhakikisha kuwa ni jukumu la Bombardier kuhakikisha kuwa ndege zetu zinakuwa mikononi mwetu? Au tuliwalipa tu tukijua kuwa tukishawalipa wao hawana Jukumu jingine lolote lile katika kuhakikisha kuwa mali yetu inatufikia?

Kuna mambo ya kujifunza:

1. Haikuwa busara wala makini kuamua kulipia mzigo mzima taslimu bila kuwa na namna ya kuhakikisha kuwa wanaotutengenezea wanatuhakikishia mzigo wetu unatufikia kabla hatujawapatia malipo yote ya mwisho. Ni watu wachache sana wanaoweza kuaminiwa kulipwa fedha yote kabla hawajakamilisha bidhaa au huduma wanayotakiwa kuifanikisha.

2. Ni vigumu sana kutenganisha kinachotokea dhidi yetu na tukio la serikali kukamata na kuzuia makontena ya makinikia na kusababisha hasara kubwa kwa kampuni ya Kikanada ya Barrick. Ukiniuliza mimi naweza kusema kuwa kilichotokea kwa Bombardier ni mwitikio wa Canada kuhussiana na sakata la Makanikia. Sitoshangaa – mjadala wa sisi kupatiwa Bombardier utakuwa unafungamanishwa na sisi kuachia makinikia ya Barrick. Sioni ni namna gani hivi viwili kwa watu ambao ni wabepari kama Canada wanaweza wasiviunganishe.

3. Masuala ya manunuzi makubwa kama ya ndege kama haya ni lazima yafanywe kwa kuzingatia sheria za nchi na za kimataifa wakati wote na ni jukumu la viongozi wote wanaohusika (kuanzia Rais hadi mtumishi wa mwisho) kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zilizokubalika za kimataifa.

4. Ili kuondoa uwezekano wa mali zetu nyingine kukamatwa – na hili linawezekana mahali popote ambapo wadeni wetu wataweza kuwaka mkono wao – kuhakikisha kuwa tunalipa madeni yetu au tunafuata taratibu kuhakikisha kuwa njia zote za rufaa zimefuatwa na kuhakikisha kuwa kama tumeshindwa kesi basi tunalipa bila kukawia kuliko kujikuta tunajiabisha sisi wenyewe.

5. Kama makampuni yana haki ya kukamata mali za serikali, serikali zile vile zina haki ya kukamata mali za wadaiwa wake popote pale zilipo. Je, tuna watu gani, makampuni, au vinginevyo ambayo tunayadai na tumechukua hatua gani kuhakikisha na sisi wanatulipa. Katika ulimwengu wa kibepari, jibwa hula jibwa.

6. Kukamatwa kwa Bombardier zetu, wenye kubeba lawama zote kwa asilimia mia moja ni Serikali na si mtu mwingine yeyote. Kulaumu upinzani au mtu mwingine kwa kukamatwa kwa hizo ni kutokuwa wakweli kwa nafsi zetu. Zimekamatwa si kwa sababu Lissu au mtu mwingine yeyote aliwadokeza wadeni wetu; zimekamatwa kwa sababu tulikuwa tunadaiwa, tumeshindwa (hatukutaka kulipa) deni, na hatukufikiria kuwa mali zetu ziko katika hatari ya kukamatwa. Kimsingi, ilikuwa ni jukumu la AG aliyeondolewa (ambaye hakupaswa kupewa hata uhakimu wa kijiji) kulinda maslahi ya taifa kisheria. Zilikamatwa kwa sababu AG na timu yake walishindwa kufanya kazi yao.

7. Hakuna ubaya huko mbeleni kabla hatujaingia mikataba kama hii tuajiri wanasheria wa kimataifa na kuwaambia tunachotaka ni nini, hasa kama wanasheria wetu wameonesha gross incompetence katika kutekeleza majukumu yao.

8. Wanasheria hawawezi kusingizia au kulaumu viongozi wa kisiasa kwamba ushauri wao ulipuuzwa. Kama kuna mwanasheria yeyote kwenye ofisi ya AG au kwingineko alitoa ushauri wa kushughulikia masuala haya na akapuuzwa basi alipaswa kusesma hivyo na kuandika barua ya kujiuzulu akipinga (resign in protest), ili kuwe na rekodi ya kile alichosimamia.

9. Kama hatukuweka utaratibu wa kisheria katika mkataba wa jinsi ya kucancel oda zetu hizi bila kupoteza hela zaidi na kuhakikisha gharama inawarudia Bombardier wenyewe, shame on us!

Nje ya hapo, ni aibu sana kwa sisi leo hii kujikuta tunakwama tena kwenye mikataba ya manunuzi ya kimataifa kama watu ambao hawana uwezo wa kujifunza kutoka matukio ya huko nyuma. Nina amini tuna uwezo huo ni kuwa tu hatuamini tuna uwezo huo. Tunafikiria tunaweza kuonewa huruma kwa sababu sisi ni Watanzaia, tuna wajomba zetu huko! (nikitumia maneno ya Mwalimu).

Asiyejifunza kutoka historia, amejilaani kuirudia!

MMM

(295)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available