Simulizi TANZANIA

Kisa cha Kweli: Kijana Mchokozi na Kichaa Yule

Na. M. M. Mwanakijiji

Pale mtaani kwetu Nguvumali nje kidogo ya mji wa Tanga kulikuwa na kijana mmoja mchokozi sana. Lakini hili la uchokozi wake nitalisema baadaye kidogo. Upande wake mwingine kijana yule alikuwa anapendwa sana na watu wengi pale mtaani. Wengi walimuona kama ni kijana mwenye kusaidia sana watu wenye shida hasa wazee na kina mama. Wakati wowote mtu alihitaji msaada wa kubeba kitu Fulani au kushusha kitu Fulani kizito kijana yule alikuwa tayari kusaidia. Hakuna mahali ambapo alipita kijana yule bila kupewa hongera au asante.

Kama nilivyosema awali kuwa kijana yule alikuwa ni mchokozi sana. Na nitalieleza hili la uchokozi baadaye kidogo. Niseme tu kuwa tangu utoto wake kijana alikuwa na tabia Fulani hivi ya kupenda kufanya watu walie kwa ajili yake. Nakumbuka tulinunua kambwa kamoja kadogo tu na kalikuwa bado kanakunywa maziwa. Kambwa kale nilikapenda sana na kalikuwa kakipita kamenenepa kanalia lia tu. Kalikuwa kanakunywa maziwa kama kamerogwa. Kakishakunywa kanatembea ‘chapa –chupu, chapa- chupu” kwenye sakafu.

Kijana yule kumbe alikuwa anakereka kila akipita nyumbani akiona tunavyomfurahia mbwa wetu yule mpya – tulimuita Chui mbwa yule. Siku moja tulishindwa kumpata mbwa yule mtoto (puppy). Tulitafuta sana lakini hatukumuona na hatukujua alipotelea wapi. Mwisho wa siku watoto wakalia, na wakubwa wakahuzunika lakini tukaamini kuwa labda kuna mtu alimuiba.

Zilipita wiki nyingi tangu kupotea au niseme sahihi kutoweka kwa mbwa yule. Siku moja tukiwa tunapiga soga na kijana yule mtu mmoja alikumbushia kuhusu kimbwa kile. Kijana yule alianza kucheka sana, alicheka hadi machozi yanamtoka upande wa mashavuni. Tukamuuliza unacheka nini? Akasema tena hata bila kuvuta pumzi, “Nilikiua kimbwa chenu!” Akatuambia ati kilikuwa kinamkera kinavyotembea “chapa-chupu, chapa-chupu” na kitumbo chake. Hivyo alikikamata na kukiweka kwenye mfuko wa fertilizer akachukua rungu akaenda nacho kwenye shamba lililozunguka nyumba yetu akakapondelea huko na kukafukia! Akaendelea kucheka sana!

Tulihuzunika lakini wengine hatukushangaa. Watu walianza kuogopa kumkatalia kitu. Akitaka kitu inabidi umpe na usipompa atachukua kwa nguvu. Na hapa namaanisha kila “kitu”. Na kutokana na ugangwe wake huo kuna baadhi ya vijana wengine walianza kuwa nyuma yake kwani nao walikuwa wanafaidika. Alikuwa akienda mahali kundi linamfuata nyuma yake kwani nao walikuwa wanajua chochote atakachopata kijana yule na wao watapata. Wakati mwingine hata mechi zilipochezwa pale kwenye uwanja wa Shuley ya Msingi Majani Mapana ilibidi magolikipa waachilie magoli kijana yule alipofika uwanjani. Timu yake ilikuwa haifungwi, yaani mshambuliaji anaweza kufika hadi kwenye goli la timu ya kijana akampiga chenga hadi golikipa lakini akaamua kujikwaa au kulia “msuli” ili tu asifunge goli! Kumfunga goli kijana yule ilikuwa ni dhahama na taharuki!

NIkaja kugundua baadaye – kwa kadiri muda unavyoenda – kuwa kijana yule alikuwa anapenda sana kutesa watu na kusababisha huzuni huku wakati huo huo akitaka sana kupendwa na kukubaliwa. Sifa hizi mbili zilikuwa ni shida sana kuzioanisha. Nilipopata nafasi ya kwenda shule nikaja kujifunza kuwa watu wenye tabia hizi wanaitwa “sadists” yaani mtu anayefurahia na kujisikia kuridhika anapowafanya watu wengine wawe katika maumivu.

Nimesema kijana yule alikuwa mchokozi. Uchokozi wake ulitokana nay eye kupenda sana kuwachokonoa watu wengine kwa kijiti! Alikuwa anatembea na fimbo yake fulani ambayo alikuwa akimkuta mtu anamchokonoa nayo. Mwenyewe alifurahia kuona watu wanavyoruka kwa kushtuka wanapoguswa na fimbo yake ile iliyokuwa imechongwa mbele kama penseli. Watu walivyokutana naye ilikuwa ama waanza kumsifia na kumpongeza kwa kujikomba au wakae kimya na kujifanya hawamuoni. Na ole wako ujifanye humuoni, atakuchukonoa!

Hata hivyo, siku moja alitokea kichaa mmoja, sijui alitoka wapi lakini alikuja pale mtaani mwetu na kila sikua alikuwa anampaka yule bwana na kumuita kila aina ya majina. Jamaa alikuwa anakasirika na anawatumia watu wake kumuangushia kipigo kichaa yule. Nakumbuka siku moja walimsweka kwenye Landrover 109 na kwenda kumteremsha Kisosora karibu na maeneo ya Chumvini. Lakini kichaa yule akarudi na barabara hadi Magorofani pale tena hadi Nguvumali na kama alivyokuwa msahaulifu akamkuta kijana yule anapiga stori na washkaji zake. Kichaa alikuwa na fimbo na yeye kaichonga! Akamchokonoa nayo! Kijana aliruka, alikasirika na kutoa pumzi kama faru aliyekoswa na risasi! Walimpiga kichaa yule siku ile, na baada ya siku chache kichaa yule akatoweka!

Nilidhani ulikuwa ni mwisho. Wiki moja baadaye akatokea kichaa mwingine! Na huyu naye akaanza kumsema sana na kumkebehi kijana yule. Ni kama jamaa alikuwa kichaa-timamu hivi. Maana alikuwa anazungumza pointi sana. Nilikuja kugundua baadaye jamaa alichanganyikiwa alipoenda Urusi kusoma mambo ya Fizikia na mrusi mmoja alimzimia pisi ya sigara usoni. Jamaa alimtwanga Mrusi wa watu na kesho yake akarudishwa kwao Mabokweni! Hakuweza kuajiriwa mahali popote Tanzania hata shule ya vidudu hakuruhusiwa kufundisha akabakia kuwa mropoka hovyo.

Kijana yule akaanza tena kumfanyizia huyu kichaa. Siku moja kichaa yule alimkuta kijana anawatukana vijana waliokuwa wanajiandaa kwenda kazini kiwanda cha FOMA. Aliwabeza sana na kuwaita kila aina ya majina. Kichaa yule aliingilia kati na kuanza kumpaka na kumuita kila aina ya majina kijana yule na mara moja kijana yule akakasirika na kutaka kumshushia kipigo.

“Kabla hamjaanza kunipiga nataka niseme kitu halafu mnipige hadi mchoke” alisema kichaa yule huku akicheka.

“Wallahi, sema neno uone kama sitakivunja kibuyu kilichoko kwenye shingo yako” alisema Kijana yule mbabe!

“Sawa, sasa kabla hujavunja kibuyu” kichaa yule alidakia kwa kumkata maneno kijana. “Kama wewe hupendi maumivu kwanini unapenda kuwapa wengine maumivu, kama hupendi dharau kwanini unapenda kudharau wengine, kama hupendi kukejeliwa kwanini ukejeli wengine?” alisema kwa haraka haraka huku akijikunyata kusubiri kipondo!

Niliwaona wapambe wake wakiwa tayari kumtwanga na mimi nikaona niingilie kati, nikijua naweza kupata kipondo vile vile.

“Unajua anachosema ni kweli” nilisema. “Ukiwa unawachokonoa watu unaoamini wana ngozi laini wewe mwenyewe ni lazima uoneshe una ngozi ngumu ukichokonolewa” nilimuambia. Macho yake yaliwaka kwa hasira kwani hakutarajia mimi kusema kitu; lakini niliona ni lazima ukweli usemwe tu. Akaamua kunifukuza pale ati kwa vile tunaheshimiana.

Huku nyuma walimpiga kichaa yule na wakaenda kumfunga kwenye nyumba moja kule Msambweni. Jamaa akawa anataka kuendelea na vitendo vyake kama kawaida yake. Lakini kama vile laana ilikuwa inatafutwa, akatokea na kichaa mwingine. Wakamfanya hivyo hivyo, akatokea na mwingine, na kwa kadiri walivyodhani wamemzima mmoja wakaanza kutokea wawili, na kila walipowazima wawili walitokea wengine wanne.

Mwisho wa siku kijana yule akaanza kuzungumza mwenyewe kila anapokwenda, akasahau kuoga, akawa anavaa nguo chafu chafu lakini bado akiamini kabisa kuwa anastahili kupendwa na kuogopwa. Kutokana na ugomvi wake watu wakaanza kumuogopa na kumpa sifa za uongo ili tu asiwaletee ukorofi. Mwisho wa siku pale mtaani wote tulionekana vichaa ila yeye pake yake alikuwa timamu! Na watu ikabidi tuanze kumtendea hivyo hivyo, kuwa sisi wengine wote ni vichaa isipokuwa yeye.

Hadi siku moja aliposimama kwenye kioo na kujitazama.

Mimi baadaye nilihama mji kabisa na kwenda kuishi Arusha. Ila nasikia siku moja kijana yule alijitafakari na kutafakari kwanini yuko vile alivyo. Miaka mingi baadaye tukiwa wote wazima na familia zetu nilipata mawasiliano na “kijana” yule sasa akiwa mtu mzima tena akiwa na madaraka makubwa. Niliwaonea huruma watu waliokuwa chini yake. Barua yake ambayo hadi leo hii nimeihifadhi iliniliza kwani ilinifundisha kuwa siyo kila mwenye akili ni timamu!

Nikipata muda nitawarushia barua yake ile.

MMM

(165)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available