Maoni TANZANIA

Kamba Aliyoachiwa Makonda Itamning’iniza Mwenyewe?

Na. M. M. Mwanakijiji

Hakuna namna tena. Paul Makonda atajiuzulu au atafukuzwa na haitaishia hapo. Kwa muda mrefu kuna watu wamekuwa wakiamini kuwa Makonda ni kiongozi mwenye nguvu  sana na kuwa alikuwa ana uwezo wa kufanya lolote, popote na kwa yeyote. Watu waliamini kuwa  Makonda anapendwa sana na anapendwa sana na Rais Magufuli kiasi kwamba yumkini hata yeye mwenyewe alikuwa anaamini kuwa anapendwa sana.

Wapo waliofikia mahali pa kumuita “mwana mpendwa” ambaye “Magufuli amependezwa naye”.  Kuanzia sakata la Warioba hadi hili la Makontena hakukuwa na shaka kuwa Makonda alikuwa anaonekana kama “mtu maalum” ambaye hakuna jambo baya analoweza kufanya ambalo linaweza kumfanya apoteze upendo ule.

Hata hivyo inawezekana bahati yake inaweza kuwa inafikia kikomo sasa. Makonda ameenda kugusa kisichogusika; ‘kodi’. Nchi yeyote ile haiwezi kuendelea isipokuwa kwa kukusanya kodi. Na kodi siyo hiari; kodi ni lazima kwani bila kodi hakuna kinachoweza kufanywa na serikali. Hili la kodi siyo suala la Magufuli wala nini; Nyerere alilieleza hili vizuri sana huko nyuma. Bila kodi hakuna namna ya kuendesha nchi. Misaada inaweza kusaidia nchi kwa kiasi lakini nchi haiwezi kutegemea misaada; ni lazima itegemee kodi.

Sasa Makonda katika kutumia hoja ya misaada ametaka kukwepa kodi. Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mipango akainua mapembe na habari za ndani ni kuwa alikuwa tayari kujiuzulu siyo kwa kutishia tu lakini kwenye kile kitu ambacho huwa nakisema mara nyingi ni “kujiuzulu kupinga” (resigning in protest). Huwa nasema kuwa inapotokea viongozi hawakubaliani na maamuzi ya juu yao na kuwa hamna namna ya kusuluhisho na inahusisha mambo makubwa basi hakuna jinsi ni lazima yule anayepinga ajiuzulu na aseme kwanini amejiuzulu. Dkt. Mpango aliashiria juzi alipofanya ziara kuangalia ya Makontena msingi wa kanuni za kujiuzulu kwamba 1. kodi ni lazima ilipwe kwa vitu vyote vinavyotakiwa kulipiwa kodi na 2. Ni waziri wa Fedha peke yake ndiye mwenye madaraka ya kuamua masuala ya kodi.

Makonda alikorofisha wengi hasa kauli yake kuwa eti makontena yale yakipigwa mnada basi atakayenunua atalaaniwa na Mungu. Labda ni ujana au kiburi lakini vyote viwili vinaweza kumfanya akose hekima na hata baada ya watu kushtuka hakuwa mwepesi kuomba radhi. Alitegemea atalindwa tena kwa vile anapendwa sana.

Leo Magufuli kafanya kile ambacho wale ambao tunamjua tunaju ana uwezo wa kukifanya; kwake hana anayempenda sana kuliko Tanzania. Magufuli hana mti mtakatifu usiokatwa. Makonda amepewa kamba na Magufuli alikuwa anasubiria aone kama “kijana wake” anahekima ya kujua ni mambo gani hayana mzaa.

Binafsi naamini kuwa anguko la Makonda limetarajiwa. Kwamba, kuna siku atakanyaga visivyokanyagwa na hakuna atakayemuonea huruma au kukimbia kumsaidia. Kama atanusurika kwa hili – kwa kulipa kodi – labda atakuwa amepata ujumbe mkali kutoka kwa Rais. Lakini kama atajiuzulu au atafutwa kazi ni lazima sheria imfuate hadi mwisho wake. Kama ametumia nafasi yake vibaya na madaraka yake vibaya anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria liwe somo kwa wengine wote wanaodhania kuwa “wanapendwa sana” kuliko Tanzania.

Na liwe somo pia kwa vijana na wote wengine wanaotamani au ambao wameingia kwenye nafasi za madaraka. Angalieni kamba mliyopewa.

Mtajining’iniza nayo wenyewe. Na mafuta yenu manono; mtakaangiwa kwayo.

 

MMM

(209)

About the author

bongoz

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available