Ferdinand Phillips Maoni TANZANIA

F.M. Philip: Upatikanaji wa Haki Jinai Katika Tanzania

Utawala wa haki jinai(Administration of  criminal Justice) ni mfumo wa usimizi na utekelezaji wa sheria za  nchi  zinazohusu muenendo wa makosa ya jinai. Mfumo huu unajumuisha mambo mengi ikiwemo mfumo wa utendaji wa mamlaka zilizo na jukumu la kushughulika na masuala ya kijinai katika nchi hiyo, ambapo kwa nchi yetu ya Tanzania tunazungumzia jeshi la  Polisi kwa kiasi kikubwa,  katika maeneo ya ukamataji, uhifadhi wa watuhumiwa baada ya kukamatwa, mfumo wa kuwahoji watuhumiwa na upelelezi wa makosa ya kijinai kwa ujumla, uaandaaji wa hati za mashitaka, uhifadhi, usafirshaji na uharibuji wa vidhibiti baada ya shauri kuhitimishwa au kabla ya hapo, Mahakama ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kikatiba katika utawala  na utoaji wa haki nchini( Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ya 1977) na mamlaka zingine kulingana na aina ya kosa, kama PCCB na kadhalika.

Jinai ni nini ? Jinai ni tendo au matendo yanayofanywa au kuacha kufanywa na mtu au watu, ama taasisi (kupitia watendaji wake),kinyume cha sheria  ambazo zinaweka wazi kufanywa au kutokufanywa kwa matendo hayo kutamaanisha ni jinai kwa mujibu wa sheria hizo.Kosa la jinai huambatana na nia ou ya mtendaji wa kosa hilo, mfano  wa makosa ya jinai ni kama  makosa yaliyoainishwa katika sheria ya kanuni za Adhabu , makosa yaliyoainishwa katika sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa, sheria ya uhujumu uchumi, sheria ya utakatishaji fedha, sheria ya wanayama pori, sheria ya udhibiti wa madawa ya kulevya, na sheria zingine nyinginezo. Mtu yeyote anayetuhumiwa/kushitakiwa kwa kosa la jinai inachukuliwa kuwa ameikosea au ametenda kosa dhidi ya Jamhuri. Maana yake ni kwamba mtenda kosa au mtuhumiwa huwa anachukuliwa kuwa ameikosea jamii ya watu waliokubali na kupitisha sheria au taratibu zilizowekwa.

KANUNI KUU ZA HAKI JINAI

Utawala wa haki jinai kwa ujumla umejikita katika kanuni kuu zifuatazo:-

 1. Lazima kuwepo na sheria inayoainisha kwa uwazi kwamba matendo flani yanapofanywa na watu kuwa ni jinai(NULLUM CRIMEN SINE LEGE)
 2. Sheria hiyo lazima pia ianishe adhabu kwa matendo hayo ambayo ni makosa ya jina(NULLUM POENA SINE LEGE). Kanuni hizi mbili zimesisitizwa na maamuzi ya Mahakama ya Tanzania  katika shauri la  Peter thomasi dhidi ya Jamhuri, (1996) TLR 370.
 3. Wajibu wa kuthibitisha shitaka(ONUS PROBAND) dhidi ya mshitakiwa ni wa Yule anyelalamika, na kwa Tanzania ni Jamhuri, hivyo upande wa mashitaka unapaswa kuthibitisha shitaka lake dhidi ya mshitakiwa pasipo kuacha shaka. Katika shauri la  WOOLMINGTON  dhidi ya DPP(1935) AC 465, Mahakama ya juu ya nchini Uingereza ( House of Lords) “ilisema kwa msisitizo kwamba, upande wa mashitaka unawajibika kuthibitisha kila jambo ambalo linajitokeza katika shauri la jinai dhidi ya mshitakiwa iwapo wanahitaji mshitakiwa huyo akutwe na hatia “
 4. Mtuhumiwa atachukuliwa kuwa hana hatia mpaka itakapodhibitika hivyo( PRESUMPTION OF INNOCENCE). Dhana hii imezungumzwa pia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, kwenye Ibara ya 13(6)(b). Pia hili limesisitizwa pia katika shauri la WOOLMINGTON dhidi ya DPP(1935) AC 465.
 5. Mtu yoyote hatapelekwa gerezani pasipo kufikishwa kwanza Mahakamani( PRINCIPLE OF ARRAIGNMENT). Kanuni hii inataka kwamba, mtuhumiwa wa kosa lolote la jinai Lazima afikishwe Mahakamani, ahojiwe kuhusu uhusika wake katika kosa analotuhumiwa kutenda, ajibu kama anakubali kuwa alitenda kosa hilo au anakataa(PLEA). Hili limesisitizwa na Mahakama ya Tanzania katika shauri la NAUCHO OLE MBILE dhidi ya Jamhuri (1993) TLR.253, ambapo Mahakama ilisema kwamba” Mtu yoyote hatatiwa Hatiani kwa kosa lolote la Jinai bila kuulizwa na mahakama kuhusu uhusika wake kwenye kosa hilo na yeye kujibu  akiwa Mahakamani”

UANZISHAJI WA SHAURI LA JINAI.

Utawala wa haki jinai kwa ujumla wake ni mchakato ambao unahatua mbali mbali mpaka haki hiyo inapokuja kupatikana. Hatua hizi huanza tu pale tendo au kosa la jinai linapofanyika na kutolewa taarifa katika mamlaka husika kama Jeshi la Polisi kwa makosa mengi hasa yale yaliyoainishwa katika Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 ya sheria za Tanzania. Katika makala hii tutajikita zaidi kuitazama sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, Sura ya 20 ya sheria za Tanzania, kama ilivyorejewa mwaka 2002. Sheria hii kwa ujumla ndio inayotoa utaratibu wa utawala wa haki jinai, kuanzia uanzishaji wa shauri la jinai, ukamataji, mpaka shauri linapofikia mwisho ikijumuisha na haki zingine kwa wahusika baada ya hukumu, kama rufaa.Hatua hizo ni kama zifuatazo;-

 1. LALAMIKO

Mchakato wa haki jinai huanza pale  lalamiko juu ya tukio la kihalifu linapofikishwa katika mamlaka husika. Kifungu  cha 128 (1)-(6) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, sura ya 20, kinatoa mazingira ambayo sheria hiyo  itatambua kuwa  utaratibu wa kuanzisha shauri la jinai umezingatiwa.

 • Lalamiko linaweza kufikishwa kituo cha polisi au mamlaka nyingine iliyo na dhamana katika kudhibiti uhalifu, mfano Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa yale makosa ya rushwa, kisha mtu atakamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama aidha kwa hati ya kumkata kutolewa au bila hati hiyo kutolewa.
 • Lalalmiko pia linaweza kuwakilishwa na mlalamikaji mbele ya Hakimu wa mahakama yenye mamalaka ya kusikiliza shauri hilo.Lalamiko hilo linaweza kuwasilishwa kwa mdomo ama maandishi, likiwa limewasilishwa kwa mdomo , basi hakimu atawajibika kuliweka katika maandishi na litasainiwa na mlalamikaji pamoja na hakimu aliyeaandaa lalamiko hilo na hati ya mashitaka itaandaliwa, hivyo mchakato wa haki jinai utakuwa umeanza rasmi.

Kifungu cha 129 cha sheria hiyo hiyo, sura ya 20, kinampa mamlaka hakimu kutoa amri ya kulikaa lalamiko au kutoipokea hati ya mashitaka ambayo kwa mtazamo wake haionyeshi kosa ambalo mshitakiwa ameshikiwa nalo. Kifungu hichi kinamtaka hakimu katika mazingira haya kueleza sababu za yeye kutoa amri  hiyo kimaandishi .

 1. UPELELEZI

Upelelezi katika utawala wa haki jinai husaidia katika kutambua ni kosa gani hasa la jinai liliotendeka, kuwabaini wahusaika, kubaini shitaka lipo kwa mujibu wa sheria gani na mwisho ni kutambua mahakama sahihi yenye uwezo na mamlaka kisheria kusikiliza shitaka linalokusudiwa.Upelelezi  kwa mujibu wa kifungu cha 52-59( sheria ya muenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania) kwa kawaida,hufanywa na Jeshi la Polisi au mamlaka inayohusika kutegemeana na kosa lilifanywa na mhalifu kama hatua ya awali kabisa. Upelelzi huusisha kuhuji mtuhumiwa, kukusanya vielelzo muhimu katika kuendesha shauri la jinai na nakadhalika. Upelelezi hulenga  kimsingi kutambua mambo makuu yafuatayo;-

 1. Tukio limetokea wapi
 2. Limetokeaje
 • Limetokea wakati gani
 1. Nani ni mhusika wa tukio hilo na kwa nini ametenda tukio hilo
 2. Tukio hilo limetokea lini na wakati gani

 

 1. UKAMATAJI, UPEKUZI NA UPOKAJI MALI/VITU BAADA YA UKAGUZI WA MTUHUMIWA

UKAMATAJI

Baada ya lalamiko kutolewa katika mamlaka husika na wakati mwingine baada ya upelelezi kukamilika,  hatua  inayofuata huwa ni ukamataji wa mtuhumiwa au watuhumiwa wanaohusika. Kifungu cha 11(1) cha sheria ya  mwenendo wa mashauri  ya jinai, sura ya 20, kinatoa muongozo wa namna ya kufanya ukamataji, ambapo kinaeleza , kwamba mtu anaweza kukamatwa kwa kuguswa au kudhibitiwa kabisa na afisa wa polisi au mtu yoyote mwingine ambaye anatekeleza ukamataji wa mtuhumiwa.
Kifungu cha 19(1) cha sheria ya  mwenendo wa mashauri  ya jinai, sura ya 20, kinaeleza kwamba ikiwa mtuhumiwa anayetakiwa kukamatwa amejificha au inasadikiwa kuwa yupo  kwenye jengo au nyumba ambayo inatumika kwa makazi , basi polisi au mtu mwenye mamlaka ya kumkata mtuhumiwa analazimika kuomba ruhusa au kibali cha kuingia ndani ya jengo hilo kwanza, ili kumkamata mtuhumiwa huyo , na mtu anayeishi kwenye jengo husika au mwenye mamlaka na jengo hilo atawajibika kuruhu polisi kuingia na kumkata mtuhumiwa. Mwenye jengo hilo akikataa kutoa ruhusa hiyo, polisi wanayo haki ya kuunja na kuingia ndani ya jengo hilo. Pia kifungu cha 20 cha sheria hiyo hiyo kinamruhusu polisi au mtu aliyeingia kihalali kwenye jengo kumkata mtuhumiwa, halafu akazuiliwa kutoka kwenye jengo hilo, kuvunja na kutoka baada ya kumtia nguvuni mtuhumiwa.   Kifungu cha 19(3) cha sheria ya  mwenendo wa mashauri  ya jinai, sura ya 20, kinaeleza kwamba ikiwa ndani ya jejngo au nyumba hiyo anaishi mwanamke ambayekwa mujibu wa mila ama desturi  hapaswi kuonekana hadharani, afisa wa polisi ambaye anahitaji kumkamata mtuhumiwa kwa wakati huo, anapaswa amtaarifu mwanamke huyo juu ya haki yake ya kuondoka eneo hilo, na ampe nafasi mwanamke huyo aondoke kwenye eneo hilo kabla hajaingia ndani kutekeleza zoezi la ukamataji wa mtuhumiwa.

 1. WATU WENYE MAMLAKA YA KUKAMATA
  Wafuatavyo vimepewa mamlaka ya ukamataji:-
  i)Polisi(kifungu cha 11(1) na kifungu cha 14) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20
  ii)Mtu binafsi, kifungu cha 16 (1) na (2)cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20
  iii)Hakimu , kifungu 17 n1 18 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20
 2. II. AINA ZA UKAMATAJI

Ukamataji uko wa aina kuu mbili:-
i)Ukamataji wa kutumia hati ya kukamata.Hapa mtuhumiwa hukamatwa baada ya hati ya kukamata dhidi yake kutolewa na mamlaka yenye uwezo wa kufanya hivyo. Kifungu cha 13(1) (a) na (b) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20, kinnatoa mamlaka ya kutoa hati ya kumata.  kwa hakimu na maafisa watendaji wa kata au vijiji. Hati ya kukamata kisheria itatolewa pale tu kuna taarifa zimetolewa juu ya tukio la kihalifu kutendwa na mtu kwenye eneo ambalo mtoa hati hiyo mfano hakimu, ana mamlaka ya kiutawala kwenye eneo hilo. Pia hati ya kukamata hutolewa kwa kiapo, ambapo mtoa taarifa ataapa juu ya ukweli wa taarifa anazotoa  mbele ya hakimu kabla hati ya kukamatwa haijaandikwa,kama kifungyu cha 13(4) na (5) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 ya sheria za Tanzania inayolekeza. Kwa mujibu wa kifungu cha 112 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 ya sheria za Tanzania , kinaelekeza kwamba, hati ya kukamata inapaswa iwe na vitu vifuatavyo:-

i) Iwe imetolewa na hakimu/jaji na ielekezwe kwa mamlaka ambayo itatekeleza ukamataji  mfano polisi
ii)Lazima iwe na mhuri wa  mahakama
iii)Iwe imesainiwa;
iv)Lazima iwe na maelezo ya mtuhumiwa k.m. Jina, kabila, dini n.k
v)Lazima iseme kuwa mtuhumiwa akamatwe na afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Hati ya kukamata mtuhumiwa hubaki kuwa halali  muda wote mpaka mtuhumiwa akamatwe au hati hiyo ibatilishwe na mahakama iliyotoa hati hiyo kama kifungu cha 112(3) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai kiliyoeleza.

ii)Ukamataji bila hati ya kukamata kutolewa. Mtu yoyote anaweza kukamatwa pasipo hati ya kukamata kutolewa dhidi yake. Mfano mtu anafanya tukio la kihalifu mbele ya afisa wa polisi, afisa huyo wa polisi anaruhusiwa kumkata mtuhumiwa huyo bila hati ya kukamata kutolewa dhidi ya mkamatwaji{kifungu cha 14 (a) mpaka (h) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20}. Mfano mwingine ni pale mtu anapofanya kosa la jinai mbele ya hakimu, hakimu anaruhusiwa kumkamata mtu huyo{ kifungu cha 17 na 18, cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20}.Mtu binafsi pia anaweza kumkata mhalifu anayefaya jinai mbele ya macho yake, mfano mwenye mali anapomkamata mtu ambaye anafanya uhalifu unaohusu uharibifu wa mali ya huyo {kifungu cha 16(1) na (2) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20}.

 1. C) Matumizi ya nguvu katika kufanikisha ukamataji:Sheria imekataza mtu yoyote awe afisa wa polisi au mtu binafsi kutumia nguvu zaidi ya inayohitajika katika kufanikisha ukamataji. Sheria pia imekataza utesaji wa aina yoyotye wakati wa utamataji. Sheria hiyohiyo inasisitiza kwamba, ukamataji lazima uzingatie utu na haki za mtuhumiwa kama mwanandamu. Ukamataji wa mtuhumiwa hautakiwi kufanyika katika namna amabayo inaweza kusababisha kifo au madhara yoyote ya kimwili kwa mtuhumiwa, labda idhibitike kwamba, kifo au madhara hayo  kwa mtuhumiwal ilikuwa ni jambo lisiloepukika katika harakati za kumkamata ( kifungu cha 21(10 na (2)). Kifungu cha 23(1),(2) na (3) cha sheria hiyo ya mwenenndo wa mashauri ya jinai, kinasisitiza kwamba, mtu anayetakiwa kukamatwa, lazima aelezwe sababu ya kukamatwa, isipokuwa tu katika mazingira amabayo mkamataji hawezi kumuleza mtuhumiwa sababu ya kukamatwa kwake aidha kwa sababu mtuhumiwa mwenyewe anaijua sababu ya kukamatwa kwake.

  UPEKUZI NA UPOKAJI  WA MALI  AU VITU VYA MTUHUMIWA

Inapotokea mtu akakamatwa kwa kutuhumiwa kutenda kosa la jinai na kuna sababu ya polisi kuamini kwamba anamiliki vitu ambayo vinahusishwa na kosa hilo la jinai alilotuhumiwa kutenda, mtuhumiwa huyo anaweza kupekuliwa(search) na vitu hivyo kupokwa(seizure) na mamlaka iliyompekua. Kifungu cha 24, 38  na 41cha sheria ya mwenenndo wa mashauri ya jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania kikisomwa pamoja na kifungu cha 42 cha sheria hiyohiyo, kwa pamoja, vifungu hivyo  vinatoa utaratibu wa upekuzi kwa watuhumiwa, upekuzi huo unaweza kufanyika kwa kutolewa hati ya upekuzi au bila hati ya upekuzi. Upekuzi wa mwili wa mtuhumiwa unaweza kufanyika pasipo uwepo wa hati ya upekuzi, lakini upekuzi kwenye makazi, au yombo ya usafiri kama gari na kadhalika, hati ya upekuzi ni muhimu kutolewa kabla ya upekuzi huo kufanyika. Hati hiyo ya upekuzi hutolewa na Askari Mfawidhi wa kituo cha polisi ambacho  mahali au chombo kinachoenda kupekuliwa kipo kwenye eneo lake. Hati ya upekuzi inaweza kutolewa  siku yoyote ikiwepo Jumapili isipokuwa utekelezaji wake ni katika kipindi cha kati ya machweo na mawio ya jua(sunrise and sunset) tu na sio masaa ya usiku. Hati ya upekuzi inaweza kutekelezwa masaa ya usiku, endapo tu kuna kibali cha mahakama kilichoombwa na afisa wa polisi kinachoruhusu upekuzi kufanyika  muda wowote ikiwemo usiku( kifungu cha 40 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20) .

Baada ya upekuzi kufanyika ,na kukapatikana kitu chochote kinachohusiana na kosa aliloshitakiwa nalo mtuhumiwa, sheria inaelekeza kwamba, kitu hicho kitapokwa, na hati ya kupoka(seizure certificate) itajazwa na kusainiwa na mmiliki wa kitu hicho, pia mashahidi wanapaswa wawepo na wasaini katika hati hiyo na pia afisa wa polisi aliyefanya upekuzi huo naye atasaini kama kifungu cha 38(3) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai kinayoeleza. Vitu vilivyopatikana baada ya upekuzi wa mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria, vitahifadhiwa na Mahakama endapo mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani,kama  vielelezo katika shauri dhidi yake, mpaka shauri hilo litakapofika mwisho, hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 44(1) kikisomwa pamoja na kifungu cha 353 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania.Baada ya upekuzi kukamili, sheria inasisitiza kwamba, kila hati ya upekuzi iliyotolewa, irejeshwe mahakamani, na isainiwe na faisa aliyeeendesha zoezi la upekuzi  ikiambatanishwa  na maelezo yanayoonyesha wakati na  jinsi upekuzi huo ulivyofanyika.

 1. MUDA WA MTUHUMIWA KUWA CHINI YA UANGALIZI WA POLISI KABLA YA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Mtuhimiwa akishakamatwa, akapekuliwa na taratibu za kumfikisha kituo cha polisi kukamalika, hatua inayofuata ni kumfikisha mahakamani haraka inavyowezekana. Kifungu cha  30  na 32(1)  cha sheria ya mwenendowa mashauri ya jina, sura ya 20, kinataka mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya muda wa masaa 24 kama inawezekana kufikishwa makamani ndani ya muda huo, au apewe dhamana kama haitawezekana kufikishwa mahakamani ndani ya muda uliwekwa na sheria, isipokuwa tu kama kosa alilotuhumiwa nalo, halina dhamana.Dhamana hiyo inaweza kutolewa kwa kuwepo wadhamini au hata mtuhumiwa kujidhamini mwenyewe.

 1. MTUHUMIWA KUHOJIWA ANAPOKUWA KITUO CHA POLISI

Mtu anapokamatwa na kufikisjhwa kituo cha polisi kwa kutuhumiwa kutenda kosa la jina, sheria inaruhusu mtu huyo kuwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa kwa muda ambao sheria imeuweka. Mahojiano hayo hufanyika kwa lengo la kukusanya taarifa zinazohusiana na uhusika wa mtuhumiwa katika tuhuma zinazomkabili. Polisi anaruhusiwa kumuuliza mtuhumiwa maswali yoyote wakati wa mahojiano hayo kwa lengo la kupata taarifa muhimu kuhusu kosa alilotuhumiwa nalo(kifungu cha 48 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20). Mtuhumiwa anatakiwa kuhojiwa akiwa kituo cha polisi kwa muda usiozidi masaa manne  kuanzia alipotiwa nguvuni(kifungu cha 50(1) na (2) cha sheria ya mwenendo wa ashauri ya jinai, sura ya 20). Muda wa mahojiano unaweza kuongezwa kwa kipindi kisichozidi masaa manane ikiwa  afisa wa polisi (mfawidhi)nayepeleleza tukio au tuhuma zinazomkabili mtuhumiwa anayehojiwa kwa wakati huo ataona inafaa kufanya hio. Ikiwa muda wa mahojiano utaongezwa kuzidi masaa manne ya Msingi yaliyowekwa na sheria katika kifungu cha 50(1), mtuhumiwa anayo haki ya kujulishwa juu ya kuongezwa kwa muda huo wa mahojiano kati yake na afisa upelelezi akiwa chini ya uangalizi wa polisi kama ambavyo kifungu cha 51 (1)(a) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 kinavyoeleza.

Hata hivyo, sheria inamruhusu  afisa upelelezi katika kifungu cha 51(1)(b) cha sheria ya mwenedo wa mashauri ya jina, kupeleka maombi mahakamani ya kuongeza zaidi  muda wa mahojiano kabla ya muda wa msingi wa masaa manne kuisha au baada ya muda wa nyongeza wa masaa nane kuisha. Mtuhumiwa, kupitia mahakama baada ya maombi hayo kupelekwa na afisa upelelzi, atapewa haki ya kusikilizwa yeye mwenye au kupitia mwanansheria ambaye atamwakilisha katika maombi hayo ya kuongeza muda wa kuhojiwa dhidi yake, kama inayoelezwa na sheria katika kifungu cha 51(3). Kifungu cha 51(2) cha sheria hiyo hiyo, kinakataza afisa upelelezi  kuongeza muda wa mahojiano pasipo sababu za Msingi, na mtuhumiwa anayo haki ya kudai fidia endapo atahojiwa zaidi ya muda uliopangwa pasipo sababu za msingi za kuongeza muda huo kuwepo, na itakuwa ni wajibu wa mtuhumiwa kuthibitisha kuwa muda wa mahojiano uliongezwa pasipo sababu za msingi kuwepo.

Mtuhumiwa kabla ya kuhojiwa anapokuwa kituo cha polisi, anapaswa kuelezwa haki zake na afisa upelelezi anayemhoji lazima amwambie  jina na cheo chake,mahojiano yanapaswa kufanyika katika lugha amabayo mtuhumiwa anaielewa vyema na pia mtuhumiwa asihojiwe mpaka awe amepewa tahadhari kwamba, hawajibiki kujibu maswali atakayoulizwa na afisa wa polisi mpelelezi na pia anayo haki ya kuwasiliana na mwanansheria wake ili awepo katika mahojiano hayo, kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 53 na 54 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania. Kifungu cha 54(2) cha sheria hiyo kinampa haki polisi mpelelezi anayemhoji mtuhumiwa, kumzuia mtuhumiwa kuwasiliana na mwanansheria wake au ndugu zake, kama anaamini kwamba mawasiliano hayo yanalenga  kusaidia kutoroka kwa mtuhumiwa mwenza, endapo tuhuma zinamhusu mtuhumiwa zaidi ya mmoja au ikiwa mawasiliano hayo yanaweza kupelekea kupotea au kuharibiwa kwa ushahidi wowote ambao unaweza kujumuishwa katika shitaka dhidi ya mtuhumiwa anayehojiwa.

Wakati huo huo, kifungu cha 55 cha sheria ya wenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20, kinasisitiza kwamba, mtuhumiwa anapokuwa polisi kwa mahojiano au upelelezi, anapaswa aheshimiwe na utu wake ulindwe, akihitaji matibabu kama ni mgonjwa, polisi inapaswa kuhakikisha anapata matibabu hayo kwa haraka pasipo kucheleweshewa huduma ya kitabibu aliyoomba mtuhumiwa kupewa.

Ikiwa mtuhumiwa anayehojiwa ni mtoto, afisa wa polisi mpelelezi (mfawidhi) anayemhoji mtoto huyo aliye chini ya uangalizi wa polisi, atawajibika kuwataarifu wazazi ama ndugu wa mtoto huyo kwamba, mtoto husika yupo kituo cha polisi kwa tuhuma ambazo ametuhumiwa nazo na yupo kwa mahojiano juu ya tuhuma hizo, kama ambvyo kifungu cha 56(1) kinavyoeleza, huku kifunkidogo cha (2) kikieleza kwa mujibu wa sheria hiyo ya muenendo wa mashauri ya jinai, sura ya 20, motto ni mtu ambaye hajafikia umri wa miaka 16.

Mahojiano amabayo yatafanyika kwenye kituo cha polisi kati ya mtuhumiwa na afisa mpelelezi, lazima yawekwe kwenye maandishi( kifungu cha 57(1)-(4) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai), na pia mtuhumiwa asomwe maelezo hayo ndipo asaini na afisa mpelelezi asaini hati ya mahojiano baada ya mahojiano hao. Kama mtuhumiwa ameamua kuandika maelezo yake na kamtarifu afisa upelelezi juu ya maamuzi yake hao, basi apewe nyezo zitakazomwezesha kuandika maelezo yake kwa ufasaha kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha 58(1-3).

Makala hii itaendelea wiki lijalo

(137)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available