HABARI KUU SIASA TANZANIA

Tundu Lissu:”Lilikuwa ni Jaribio la Mauaji ya Kisiasa”

  • Azidi kuinyoshea kidole serikali
  • Ataka Serikali ya JPM Itengwe
  • Ahoji Bunge Kumtupa

Na. Mwandishi Wetu

NAIROBI – KENYA, Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhibu wa Upinzani Bungeni Bw. Tundu Lissu ameelezea tukio la jaribio la kuuawa lililomkuta miezi minne hivi iliyopita kuwa lilikuta ni tukio la jaribio la mauaji ya kisiasa. Akizungumza mjini Nairobi na vyombo vya habari jana katika matangazo yaliyorushwa moja kwa moja na baadhi ya vyombo hivyo Lissu amejielezea kuwa tukio la yeye kushambuliwa linahusiana moja kwa moja na ukosoaji wake wa Serikali ya Tanzania.

“Tangu mwaka 2010 na hata kabla ya hapo nimekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Tanzania” alisema Lissu akiwa amezungukwa na viongozi wengine wa CHADEMA na baadhi ya wanafamilia na kuongeza kuwa “tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015 nimekuwa mkosoaji mkubwa wa sera zake, matendo yake na wa serikali yake”.

Bw. Lissu amedai kuwa kwa maoni yake sababu ya yeye kushambuliwa katika jaribio hilo la mauaji ni huo ukosoaji wake dhidi Serikali na uongozi wa Rais Magufuli. Lissu amedai kuwa hadi hivi sasa siyo Magufuli mwenyewe wala Serikali yake ambayo imetoa taarifa yoyote rasmi hadharani juu ya shambulio hilo. Amedai pia kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania limekataa katakata kualika vyombo huru vya uchunguzi kama ilivyowahi kutokea huko Kenya miaka ya tisini ambapo mwanasiasa Robert Ouko aliuawa na mwili wake ukikutwa umechomwa moto maili kadhaa kutoka nyumbani kwake.

Akiongezea uzito wa tuhuma zake dhidi ya Serikali ya Tanzania na vyombo vyake Lissu amedai kuwa hadi wakati anazungumza na vyombo vya habari hakukuwa na mpelelezi yeyote aliyemfuata yeye wala dereva wake kuwahoji juu ya shambulio hilo wakati wao ndio mashahidi wa msingi kabisa wa tukio hilo. “Jeshi la polisi kwa maoni yangu halipelelezi tukio hilo; hawapelelezi kwa sababu wanajua ilikuwa ni a plan for a political assassination (mpango wa mauaji ya kisiasa)” alisema Lissu. Amedai mpango huo ulikuwa ni kumfanya aache kusumbua wale aliowaita kuwa ni “wakubwa wa Tanzania”.

Zaidi ya hayo Bw. Lissu alilinyoshea kidole Bunge la Tanzania na kudai kuwa Bunge lenyewe ambalo yeye bado ni mtumishi wake hadi hivi sasa halijagharimia sehemu yoyote ya matibabu yake kama inavyotaka Sheria ya Uendashaji wa Bunge ya mwaka 2008. Amedai kuwa hakuna kiasi chochote cha fedha kilichotolewa na Bunge kugharimia matibabu yake kama Sheria inavyotaka. Lissu amesema kuwa licha ya kuwepo mawasiliano kati ya familia yake na Bunge lakini hadi hivi sasa Bunge linaonekana linapiga “chengachenga” katika majibu yake. “Hawasemi hawatalipa, ila wanaleta chengachenga” amesema akiwa amekaa katika baskeli ya kiti cha wagonjwa.

Aliendeleza pia kutoa tuhuma dhidi ya Bunge na kudai kuwa hadi siku hiyo ya jana hakuna afisa yeyote wa Bunge ambaye amefunga safari kwenda kumuona. Amedai siyo Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, na Tume ya Huduma ya Bunge au afisa mwingine yeyote aliyeweza kumuona Zaidi ya miezi minne tangu tukio la jaribio dhidi yake kufanyika. “Kwa maoni yangu waliopanga mpango huu hawakuwa na mpango mwingine, wala Plan B kwani walijua huyu mtu ataenda kufa” alisema Lissu.

Lissu akizungumza kwa kujiamini na akionekana aliyepata nafuu amesema kuwa inapofikia wapinzani wa kisiasa wanaanza kuuawa ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati. Amevitaka yvombo vya habari vya ndani na vya nje kuanza kuihoji serikali na viongozi wake na kuamua kuacha kuwa kimya. Amedai matukio ya watu kupotea, kukamatwa wakati wa usiku na kuhojiwa kwa sababu ya kutoa maoni yao ni ishara mbaya kwa taifa. Ametaka Serikali ya Tanzania ifanywe kama fungo yule mnyama anayetoa harufu mbaya kama Afrika ya Kusini ilivyofanywa hivyo mbele ya jamii ya kimataifa wakati Nelson Mandela alipokuwa kifungoni.

Bw. Lissu akizungumzia hali yake amesema kuwa anaendelea vizuri na kuwa anaendelea na mazoezi na ameruhusiwa kutoka hospitali hiyo ya wagonjwa mahututi. Amesema pia kuwa madaktari wameamua kuacha risasi moja mwilini kwani kuitoa kungesababisha madhara Zaidi mwilini.

Wakati huo huo, Msemaji wa Serikali ya Tanzania akiandika kupitia mtandao wa Twitter amesema kuwa hakuna haja ya serikali kulumbana na Bw. Lissu na kuwa wanamwombea apone haraka. Hata hivyo hakujibu hoja moja kwa moja kama zilizyotolewa na Bw. Lissu na haijajulikana kama kuna kiongozi yeyote ambaye ataangalia hoja hizo na kuzitolea maelezo mustahiki.

 

(100)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available