SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Leo: Mdahalo wa “Seneta”, Kodi Kubwa na Hoja Zinazojadilika

Na. M. M. Mwanakijiji

Siku ya jana (Jumatano) kipande cha video (clip) kilikuwa kinasambaa kwenye mitandao ya kijamii kikionesha sehemu ya mdahao wa wanasiasa wa Marekani. Katika mdahalo huo ambao unaonekana ukifanyika chini ya Mwandishi Forrest Sawyer wa NBC. Katika mdahalo huo wa kugombea Urais inaonekana sehemu ambapo mmoja wao aliyetajwa tu kama “Seneta” akitolea mfano wa jinsi gani nchi za Kiafrika ziko katika hali mbaya na kwanini misaada ya kigeni haina uwezo wa kuzitoa nchi hizo katika umaskini wa kutupwa.

Seneta huyo alitolea mifano ya nchi za Afrika ya Kusini na Tanzania. Kwa Tanzania alitumia muda kidogo kuonesha tatizo la kodi jinsi lilivyokuwa na jinsi gani njia sahihi ya nchi hizi kutatua matatizo yake ni kupunguza ukubwa wa kodi mbalimbali ambazo ni mzigo mkubwa kwa makampuni na hazichochei ukuaji wa uchumi.

Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wamechukulia video ile kuwa ni ukweli na kuwa yaliyosemwea mle yawezekana yanahusiana na siasa zetu mwaka huu 2018. Nimeona nitoe maelezo machache kuhusiana na video yenyewe ili kwamba mjadala ufanyike kwa usahihi. Mambo kadhaa ya kuyafahamu.

 1. Video hiyo ni sehemu ya lililokuwo mchezo maarufu wa TV wa West Wing ambao ulichezwa katika kituo cha NBC. Onesho la mdahalo huo ambao sehemu ya video yake ndiyo imeibuliwa jana lilirushwa tarehe 6 Novemba 2005. Ilikuwa ni show ya Season 7, Episode 7 (S7E7).
 2. Wanaoonekana katika video hiyo ni waigizaji wa filamu na TV; anayeitwa “Seneta” na mwongozaji wa mjadala ni mwigizaji Alan Alda (akicheza kama Seneta Arnold Vinick) na pembeni yake akiwa mwigizaji Jimmy Smitts (akicheza kama Mwakilishi Matt Santos). Vinick akiwakilisha chama cha Republican na Santos akiwakilisha chama cha Democrat. Wote walikuwa wanataka kumrithi Rais Jed Bartlet (akiigizwa na Martin Sheen).
 3. Mwigizaji Alan Alda anajulikana sana kwa kucheza katika onesho la TV la MASH wakati Smitts anajulikana kama mpelelezi katika onesho la TV na NYPD Blue.
 4. Mwongozaji anayeonakana kumuita “Seneta” alikuwa ni mtangazaji wa kweli wa TV Forrest Sawyer.
 5. Mjadala ulihusisha mada nyingi zikiwemo suala la uhamiaji, kupunguza kodi, nishati, masuala ya elimu, afya, adhabu ya kifo na Afrika.
 6. Kilichowashangaza wengi ni kuwa Afrika ilijadiliwa katika mdahalo ule kwa karibu dakika kumi- video inaonesha tu sehemu kidogo ya mjadala huo.

Baada ya kusema mambo hayo na kuonesha kuwa video hiyo ni sehemu ya onesho la TV na kuwa wanaoonekana ni waigizaji, ukweli bado unabakia kuwa sehemu ya mjadala huo bado ina umuhimu wake na hoja zake zinajadilika. Nimesema hapo juu kuwa katika mdahalo ule Afrika ilijadiliwa kwa karibu dakika kumi ni vizuri kama watu wangepeta nafasi ya kuona sehemu nzima ya mjadala ule. Hata hivyo, kwa sehemu ambayo imeonekana ni vizuri kujaribu kutafakari mambo kadhaa.

 1. Mfumo wetu wa kodi una lengo gani hasa? Sote tunajua kuwa serikali ili ifanye kazi zake inahitaji fedha na namna ya kwanza na kubwa zaidi ya serikali kupata mapato ni kwa kupitia kodi.
 2. Ili serikali ifanye mambo makubwa na mengi zaidi – kujenga mashule, barabara, mahospitali, kutoa mikopo ya elimu n.k inahitaji fedha zaidi – yaani kodi zaidi.
 3. Hizi kodi “zaidi” nani anatakiwa kulipa? Katika mazingira yetu kodi inalipwa na wafanyakazi (wenye mapato rasmi), wafanyabiashara na wananchi wa kawaida. Sehemu kubwa hata hivyo ya kodi inalipwa na wafanyabiashara na wawekezaji (wa ndani na wan je).
 4. Mjadala wa kodi mbalimbali zinazohusiana na uzalishaji na uwekezaji ndio kwa kiasi unaibuliwa na video hii; ukweli wa hili bado haujabadilika. Ni kweli bado kodi ya makampuni iko kwenye asilimia 30 na haijashuka (isipokuwa kwa mtindo wa misamaha mingi ya kodi). Hoja kuwa nchi kama ya kwetu kuwa na kodi kubwa namna hii haitusaidii – ndio hoja ya “seneta”. Mifano ya nchi nyingine katika kodi hii (nazungumzia kwa ujumla wake na siyo exceptions mbalimbali zinazoweza kuwepo):
 • Fikiria kwamba Rais Donald Trump aliona jinsi gani kodi hii ilikuwa kubwa Marekani na akahakikisha inapunguzwa kutoka asilimia 35 hadi 21. Na hii ni nchi tajiri zaidi duniani!
 • Singapore kodi yao ni asilimia 17
 • Malaysia kodi hii ni asilimia 25
 1. Ikumbukwe kuwa kodi yetu hii inalingana na majirani zetu (Kenya, Uganda, na Rwanda). Msumbiji wako juu yetu (32%) Botswana (22%), Ghana (25%).
 2. Hoja ya kupunguza kodi peke yake haiwezi kuwa suluhisho la matatizo yetu kama mambo mengine yanabakia vile vile. Kuna mambo mengine ya kuangalia ikiwemo mifumo yetu ya sheria, upatikanaji wa nishati, usalama n.k Haya yote yanatakiwa yawemo kwenye mijadala inayohusiana na kuwainua watu kutoka katika umaskini.

Kwa ufupi video hii japo ni ya kufikiria (fictional) hoja zake zinachochea haja ya kuwepo mjadala mpana kuhusiana na sera za kodi na athari zake katika ukuaji wa uchumi. Mjadala ambao unahitaji pia kuonesha tofauti ya sera kati ya vyama vyetu vya siasa linapokuja suala la kodi. Hadi hivi sasa binafsi sijaona tofauti kubwa ya msingi ambayo inaweza kusimama kuonesha kuwa vyama vingine vya siasa vina sera bora zaidi ya kodi (iwe ya makampuni, ya mapato au nyinginezo) kiasi cha kuweza kuonesha kuwa sera hizo zitakuwa ni bora zaidi kwa uchumi na kwa maisha ya kila Mtanzania (au Watanzania wengi zaidi).

(116)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available