SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Jumatatu: Kuna Kushinda na Kushindwa; CCM Imeshindwa kwa Kushinda

Mbunge Mteule wa Kinondoni, Mtulia

Na. M. M. Mwanakijiji

Katika michezo ya ushindani kuna kikomo ambacho mshindi anaweza kupongezwa kwa kushinda. Chelsea ikicheza na Arsenal (Gunners) au na Manchester United (Manu) kila mtu anatarajia kuwa mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa kwani kimchezo timu hizo tatu hazitofautiani sana. Moja ikiifunga nyingine mabado mawili bila au matatu kwa mawili hakuna anayeweza kushangaa sana japo inaweza kuumiza hisia za kishabiki za timu iliyofungwa.

Hata hivyo, mojawapo ya timu hizo ikicheza na timu ya Taifa ya Tanzania ikaifunga Tanzania bao moja bila, Watanzania wanaweza kushangilia kwa sababu “hawakufungwa mengi”. Lakini kama mojawapo za timu hizo ikaifunga Tanzania mabado nane katika mchezo kirafiki kabla hata ya muda wa mapumziko, kila Mtanzania hata walio mashabiki wa Chelsea, Arsenal au Manu watachukia kwani timu yao inafungwa si kwa heshima tena bali kwa mtu kujionesha ubabe. Lakini kama baada ya mapumziko timu hiyo ikaendelea kuchomeka mabao mengi kwenye timu yetu sidhani kama kuna Mtanzania atataka kubakia uwanjani; inawezekana watu kwa hasira wakaanza kurusha vitu uwanjani na wengine wanaweza hata kuingia uwanjani kutaka kuepusha udhalilishaji huo.

Kuna kushinda na kushindwa; lakini kupo kushindwa katika kushinda.

Michezo imewekewa kanuni mbalimbali kanuni hizo zipo zilizoandikwa na nyingine zinajulikana kwa wana michezo wote. Mojawapo ya kanuni isiyoandikwa kwa michezo mingi lakini inaheshimika na wanamichezo wote waadilifu ni kuwa hakuna ushindi wa furaha ambapo mshindi anamshinda mwingine ili kumdhalilisha. Mtu anashinda ili awe mshinde lakini bila kumvunja, kumharibu au kumfanya mshindani wake awe duni mbele zake.

Kitendo cha mchezaji au timu kucheza bila kumuumiza, kumdhalilisha au kumpigisha magoti mshindani au mpinzani wake kinaitwa “good sportsmanship” yaani “uanamichezo mzuri”. Bondia hapaswi kumpiga bondia mwenzie ambaye tayari amemtoa ‘knockout’; timu ya mpira wa kikapu haiwezi kuendelea kufunga vikapu wakati tayari inaongoza kwa vikapu 100 kwa 20; timu ya soka haifurahii kufunga mabado nane kabla ya muda wa mapumziko halafu ikataka kuendelea kufunga zaidi baadaye.

Ronaldo akimsaidia mshindani wake Messi kunyanyuka.

Kuna hata michezo ambapo mtu yuko tayari yeye ashindwe ili mpinzani wake asiumie au kudhalilika. Kuna visa vingi ambapo wachezaji waliokuwa katika nafasi ya kushinda walipoamua kuacha kushinda ili kumsaidia mwenzao aliyeumia au kuanguka. Nafahamu visa vya mtu ambaye alikuwa ashinde mbio zake lakini alipofika karibu yule aliyemfuatia akaanguka mita chache kabla ya utepe wa mwisho. Yule aliyekuwa anaongoza badala ya kukimbia kugusa utepe aliacha kukimbia akasimama kumsaidia mwenzake na kwa pamoja wakaelekea kwenye utepe.

Ndugu zangu, kuna kushinda na kushindwa; lakini kupo kushindwa katika kushinda.

Siasa zetu zimefikia pabaya. CCM inataka kushinda chaguzi ndogo, inataka kushinda viti vya udiwani, inataka kuendelea kushika madaraka. Inafanya hivi ili kushinda na kuangamiza kabisa ushindani dhidi yake. Wapo wanaoona hili sasa wakati wa utawala wa Rais Magufuli na kwa haraka wanamnyoshea Magufuli mkono. Wanaweza kuwa wako sahihi. Lakini kwa sisi tunaofuatilia siasa za CCM kwa miaka yote hii, CCM haijabadilika.

Yote ambayo tumeyaona Kinondoni hakuna jipya hata moja. Tuliyaona haya Igunga, tuliyaona Nzega, tuliyaona Tarime, tuliyaona Arumeru Mashariki, tuliyaona Babati, na tumeyaona sehemu nyingine nyingi tu ambapo zilihitaji kufanyika uchaguzi wa marudio. Tumeona watu wakiuaga, tumeona watu wakichinjwa, tumeona polisi wakitumika vibaya, tumeona jinsi gani upinzani unahitaji kupigishwa magoti ili tu CCM ishinde.

Binafsi sina tatizo kabisa na CCM kushinda kwani uwezekano wake kushinda bado ni mkubwa. Kina raslimali nyingi kuliko chama kingine chochote, kina wanachama wengi, kinaendesha serikali zote na kina uwezo wa kutumia mbinu nyingi halali tu kuweza kushinda. Kinachonitibua na hili si jipya sana ni kuwa bado kinataka kushinda kwa kuangamiza upinzani. Ni sifa gani ipo hapo? Ni sifa gani iko katika kushindwa huku kuna damu ya wapinzani wako, kuna damu ya raia wengine, kuna vurugu, kuna hofu, kuna woga n.k. Ni ushindi gani huu wa kujivunia? Ni kweli mtu anaweza akatoa pongezi kuwa ‘hongereni mmeshinda’; lakini wakati mwingine,

Kuna kushinda na kushindwa; lakini pia kupo kushindwa katika kushinda. Hivi, ni ugumu gani uliopo kwa CCM kushinda vizuri tu bila Watanzania kuona kama ni lazima kila mtu apige magoti na kutoa sadaka kwenye madhabahu ya CCM na asiyefanya hivyo basi ni Mtanzania nusu na asiye na mapenzi na Taifa lake? Tunawafundisha nini watoto wetu na vijana wetu kuhusu ushindani katika siasa?

Itaendelea kesho.

mwanakijiji@jamiiforums.com

(325)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  • Wameshinda kwa damu! Damu hizo zitashindana nao kama wataweza kuzishinda basi iwe juu yao! Vinginevyo damu hiyo iwe juu yao wote na watoto wa watoto wao kizazi hiki na hata vingine 3-4 vijavyo! Wananguvu, sisi tuna Mungu!

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available