SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Jumanne: Kuna Lawama kwa Rais, Lawama Rahisi na Lawama Halisi

Na. M. M. Mwanakijiji

Ni rahisi sana kumnyoshea Rais Magufuli kidole na kuseme ‘yeye alaumiwe’. Kwenye familia yoyote ile ambayo ina baba ndani, watoto wanapoanza kuugua, kuumia, kupigana, na kuanza kujikuta hawako salama ndani ya nyumba jamii na majirani watauliza kwanza “yuko wapi baba yao”. Kama inajulikana kwamba baba wa nyumba hiyo ni mlevi, au mtu asiyetulia nyumbani basi watu kwa haki watamnyoshea yeye kidole kwa matatizo yanayowakuta watoto wake. Na kama matatizo hayo yanafanya nyumba yake iwe mahali ambapo si salama basi baba huyo anaponyeshewa kidole anapaswa kujiuliza kama anatimiza majukumu yake sawasawa au la.

Bahati nzuri Rais Magufuli siyo Baba wa Watanzania na hivyo mfano wangu hapo juu unaweza usiwe moja kwa moja wenye kutosheleza. Hata hivyo, Rais ni zaidi zaidi ya baba wa familia ambaye ni mkuu wa nyumba moja; Rais ni mkuu wa familia ya Watanzania. Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “Tanzania ni ya Watanzania, na Watanzania ni Wote”. Kwamba, katika nchi yetu, tuko watu kutoka maeneo mbalimbali, makabila mbalimbali, historia mbalimbali na wakati mwingine hata katika makundi yetu madogomadogo bado tuna tofauti zetu nyingi. Kuna vijana, wazee, kuna kina mama na wapo kina baba, kuna wasomi, kuna wasi wasomi sana, kuna wenye nazo, na wasio nazo, na wapo wanaofikiria wanazo!

Katika tofauti zetu zote hizi, zikiwemo zile za rangi, dini, lugha na siasa bado sisi sote ni wana familia moja ya Tanzania. Nyumba yetu ni moja, ikiungua sote tunatakiwa kujitahi kuzima; tukiona mtu anaiunguza sote tunatakiwa kusimama na kumzuia mtu huyo asiunguze nyumba yetu. Lakini katika haya yote ni mkuu wetu wa nyumba ambaye hakujipa ukuu huo; bali amepewa kwa ridhaa ya wananchi wake basi anawajibika zaidi kuona kuwa nyumba yetu ni yote sote, na sote ni wote.

Lawama za Rais zipo; na zinamstahili.

Zipo lawama rahisi rahisi vile vile. Kwenye nyumba yetu ile ile ya mfano hapo juu, watoto waliokuwa na wenye familia zao na wenye maisha yao wanawajibika zaidi katika maisha yao kuliko watoto wadogo ambao wanaishi na wazazi wao. Mtu mzima ambaye matatizo yake yote anakimbilia kwa baba na mama, watu wataanza kumshangaa kama mambo yanayomkuta yeye mwenyewe hana uwezo wa kuyatatua kwa kiwango anachoweza. Mtu mzima anapokimbilia kwa wazazi wake, mara nyingi ni kwa ajili ya ushauri tu na siyo kwa ajili ya utatuzi; mwisho wa siku anawajibika kutatua matatizo yake na akishindwa, jamii haitolaumu wazazi.

Ni lawama rahisi rahisi kumlaumu mzazi kwa kila jambo baya linalowakuta watoto watu wazima na waliokomaa. Na wakati mwingine hata watoto wadogo (ukiondoa wachanga) wanaanza kubeba lawama (culpability) ya matendo yao wenyewe. Mtu kuwajibika kwa matokeo ya matendo na maamuzi ya maisha yake ni alama kuu zaidi ya kuwa mtu mzima. Mtu mzima ambaye anapenda kulaumu wengine tu hata kwa matatizo yake anaonesha alama ya kukosa ukomavu. Ni lazima mtu awajibike kwa tabia na maamuzi yake.

Hili ni kweli pia katika taifa. Wananchi ambao wanaangalia serikali kwa matatizo yao yote, au jamii ambayo imegoma kuwajibika kwa maisha yake ni jamii ambayo imegoma kukomaa. Sisi kama taifa tumefika mahali wapo baadhi yetu ambao wamegoma kabisa kukua; kwao kila tatizo ni la serikali, na kila shida ni ya Rais! Kuna wengine wangekuwa na uwezo hata matatizo yao ya ndoa wangependa yaundiwe Wizara ya Ndoa na Mahusiano!

Katika hili, watu wanatoa lawama rahisi rahisi kwingine kote isipokuwa kwao wenyewe au kwa watu sahihi. Ni rahisi zaidi na inamfanya mtu ajisikie vizuri kumlaumu Rais kwa matatizo ambayo  mfumo wetu umeyaweka nje ya Rais. Mojawapo ya shida kubwa iliyopo sasa na imekuwepo kwa muda mrefu na binafsi nimekuwa nikiliandika mara kwa mara ni shida ya kumfanya na kumfikiria Rais wetu kuwa ni Mfalme. Au kwa jinsi tunavyomlalamikia na kumtaja kuweza kumfanya hata yeye mwenyewe ajisikie kuwa na yeye ni mfalme kweli.

Lakini zipo lawama halisi.

Kuna watu, taasisi, na vyombo mbalimbali ambavyo vinastahili kubeba lawama. Kwa yaliyotokea Kinondoni kwenye uchaguzi mdogo na hata mauaji ya Binti Akwilina kuna watu wanastahili kubeba lawama na wanapaswa kubeba lawama. Wengi wamewataja watu na vyombo mbalimbali. Lakini sidhani kama tunaelewa uzito wa kuwabebesha lawama sahihi watu sahihi ili wawajibike au wawajibishwe kwa usahihi. Magufuli ana lawama zake, lakini kuna wanaobeba lawama zaidi.

Itaendelea kesho.

mwanakijiji@jamiiforums.com

 

(118)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available