Maoni SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Ijumaa: Milioni Mia Saba si Haba na Wale Wanaobeza Vibaba!

Wawakilishi wa pande mbili wakitia saini makubaliano

Na. M. M. Mwanakijiji

Hawakutupeleka mahakamani. Hawakuamua kukusanya virago vyao na kuondoka na kufunga shughuli zao nchini kwa vile tumewakatalia kinachodhaniwa kuwa kilikuwa ni haki yao. Tuliambiwa hatukutakiwa kuwaambia “hapana” kwani wangekasirika; wangekasirika na sisi tungelipa! Tuliambiwa ilikuwa ni mwiko kuwakatalia wawekezaji wakubwa wa kimataifa na kwa vile wao ndio “wakubwa” basi sisi “wadogo” tulitakiwa tukubali tu kufanyiwa lolote, popote, vyovyote na yeyote.

Haubezwi Mchakato Tena Sasa Yanabezwa Matokeo

Leo kinachobezwa na ndugu zetu siyo mchakato tena; kinachobezwa siyo hatua za kulazimisha “wakubwa” kuja kuzungumza nasi kwa masharti yetu sisi wenyewe chini ya miembe yetu wenyewe. Kinachobezwa siyo kwamba hatukwenda kwenye mahoteli makubwa ya kimataifa na kukabishwa kwa mbwembwe kubwa huku tunaingizwa mjini. Hawabezi tena kuwa hatukwenda kwenye chumba cha hoteli kama ilivyokuwa kwenye Buzwagi na kuingizwa mjini. Kinachobezwa ndugu zangu ni matokeo ya mchakato huo ya kwamba mbona hayakuleta makubwa tuliyoahidiwa? Kwamba, tulisema tunadai matrilioni ya shilingi sasa mbona tumepewa karanga tu?

Bilioni Mia Saba si Haba

Kwanza ndugu zangu niweke jambo moja sawa sawa. Kuziita shilingi bilioni 700 kuwa ni punje tu ni kutokuwa wa kweli kwa uzito wa kiasi hicho cha fedha. Labda kuweza kuelewa kiasi hicho kinaweza kufanya nini kwenye sekta mbalimbali kunaweza kutusaidia kujua kama kweli hiki kiasi ni punje tu na cha kubezwa. Bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ni shilingi 1,115,608,772,090. Ni karibu trilioni 1.1. Fedha ambazo zimetolewa kama “kishika uchumba” (kuonesha nia njema) ni sawa na shilingi bilioni 700 ya fedha zetu. Hii ni sawa na asilimia 62.7 ya bajeti ya wizara ya Afya peke yake. Yaani, ni zaidi ya nusu ya fedha zote ambazo zimepangiwa bajeti kwenye wizara ya afya! Na wapo wanaosema ni za kubeza?

Labda mfano mwingine utasaidia. Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu kama ilivyosomwa na Dkt. Tizeba mwezi ilikuwa ni bilioni 267.865. Kiasi hicho ni kidogo mno kama alivyokosoa Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ambaye alifichua kuwa serikali kufika wakati ule wa bajeti ilikuwa imetoa asilimia 3.31 ya fedha za maendeleo zilizotengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo. Kiasi cha fedha ambazo zinabezwa na ndugu zetu hawa ni karibu mara tatu ya bajeti nzima ya Wizara ya Kilimo! Kweli ni punje za kupuuzia, na ni kiasi cha kubeza hiki?

Labda mfano mwingine utasaidia. Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka huu ni shilingi bilioni 623 kiasi ambacho kililalamikiwa Bungeni kuwa ni pungufu na kwa mara nyingine Zitto Kabwe aliikosoa kwa usahihi kabisa Serikali ya Magufuli ya kwanini kiasi hicho kimepungua hivyo ukizingatia kuwa hata fedha zilizokuwa zimeombwa mwaka jana na kuudhinishwa na Bunge ni asilimia 19 hivi ambazo zilikuwa zimepokelewa hadi wakati ule wa Bajeti kusomwa. Kiasi ambacho leo Serikali imekubaliana kupatikana kutoka katika majadiliano yake na Kampuni ya Barrick kufuatia ule mgogoro wa makinikia ni shilingi bilioni 700; hii tena ni zaidi ya bajeti ya Wizara nzima ya Serikali ya Muungano. Kweli hili ni la kubeza? Kweli hizi ni fedha za kupuuzia kwamba si kitu?

Siyo Kila Kitu ni Siasa

Sasa ninaelewa siasa na ninaelewa majadiliano. Siasa inawafanya wanasiasa kuangalia mambo kisiasa ili kupata alama za juu za kisiasa. Tukumbuke kuwa wale waliokuwa wanasema tutanyolewa hadi kucha walikuwa wanasema kama watu walioingiwa na hofu. Nakumbuka kuna watu walikuwa wanatuambia kabisa kwenye mitandao kuwa hatuwezi kuwalazimisha “wazungu” hawa na kwamba wazungu wana watu waliojipanga na wenye uzoefu mkubwa. Niliwabeza wakati ule watu hawa kwa sababu walikuwa na hisia za uduni (extreme inferiority complex). Hawa ni watu ambao mzungu akiwaambia kitu wao wanakubali tu na hawana ujasiri wa kusema “hapana” kwa sababu hawafikiri kabisa kuwa wazungu wanaweza kuwa matapeli na wanaweza kuwa wajanja sana kulinda maslahi yao!

Kilichokubaliwa ni Zaidi ya Fedha

Lakini ninafahamu kuwa habari nzima siyo hizo bilioni 700 tu; jambo kubwa limetokea jana katika mazungumzo tuliyoambiwa. Kilichotokea nyingine ni makubaliano ya mambo mbalimbali ambayo yalikuwa hayajawahi kufanyika huko nyuma. Wengine wanabeza hata haya na wanasema ni bure na kuwa hayawezekani. Hawa ni wale watu wa lile kabila la Wahatuwe! Ni watu ambao wanaamini kuwa hawawezi kufanya lolote, hawawezi kujenga hoja mbele ya wazungu, hawawezi kuwabana wazungu hadi wakabadilika rangi! Lakini ukweli – na mtasikia kwa watu wengine si muda mrefu – sehemu ya makubaliano hayo yalivyotangazwa kama yatatekelezwa ipasavyo yataleta heshima mpya kwa taifa na kwa Afrika kama siyo kwa nchi nyingine zinazoendelea. Uzoefu wetu wa kukaa mezani na makampuni makubwa kama Barrick na kuwalazimisha kuzungumza nasi kwenye uwanja wetu wa nyumba yatakuja kufundishwa kwa watu wengine na mataifa mengine. Si jambo dogo hata kidogo, na wala si la kubeza.

Ni lazima basi kutoa pongeze, pongezi zinapostahili. Ni kweli mtu anaweza kukosoa mambo fulani, lakini katika hili kwa kweli ukosoaji unaonesha tu ni kuwa ndugu zetu hawataki kumpongeza Magufuli kwa sababu wanadhania (kwa makosa) wakifanya hivyo basi watakuwa wamempa ‘kiki’ asiyostahili. Wanadhania kuwa wakisema kwa kweli hatua hizi zimeleta heshima kwetu kama taifa na zimetupa mahali pa kusimamia huko mbeleni basi kutamfanya Magufuli ajione ameweza. Lakini hili si lazima liwe hivyo, ukweli ni ukweli tu hata kama haupendezi. Sifuri jumlisha Tano ni ni Tano sasa huwezi kung’ang’ania iwe sifuri tu kwa sababu tano huipendi!

Binafsi napenda kuipongeza Serikali kwa mwanzo huu wa kurudisha heshima ya taifa katika kusimamia na kulinda raslimali za taifa letu. Pongezi zinaenda mbele zaidi kwa timu zote ambazo zimethubutu kufanya mambo ambayo hayakudhaniwa kuwa yanawezekana kufanyika katika nchi yetu hii. Nina uhakika wakati ufike au utakapofika wajumbe wa tume ya majadiliano wajulikane wazi na kupewa heshima wanayostahili hasa kwa kuweza kusimama kidede na wakubwa hawa. Naogopa kudhania hata kwa mbali kama wapingaji wa yaliyotangazwa jana wangekuwa kwenye timu ya wajumbe taifa lingeambulia nini. Inawezekana wangebanwa na wazungu hawa wangekusanya mpira kwapani na kuondoka na kutuambia “tumeshindwa, wazungu wametubana sana”!

Kilichotangazwa jana ni jambo la kupongeza, siyo jambo la kuonea haya. Wengine wansema tulidai trilioni 400 na ushee na sasa tumepewa bilioni 700 tu kweli tushangilie? Ndugu zangu kuna msemo wa wahenga kuwa ndege mmoja mkononi ana thamani kubwa kuliko ndege tisa mtini! Na hata hayo madai yanaitwa madai kwa sababu hiyo; na imeelezwa vizuri jana kuwa hii si hatua ya mwisho. Sehemu kubwa ambayo inaonekana imebakia na labda itatuliwa muda si mrefu ujao ni suala la kodi. Kwa yeyote anayejua masuala ya kodi si mambo madogo. Serikali inaweza kudai lakini haina maana anayedaiwa hana haki ya kusema “hadaiwi chochote” au “hadaiwi kiasi chote hicho”. Baada ya Serikali kutoa madai yake tena wazi zile Barrick na Acacia walikuwa na haki ya msingi katika biashara kupinga (object) dhidi ya madai hayo na walikuwa na haki ya kutoa nyaraka mbalimbali ambazo zingepitiwa ili kuona ni madai gani ni ya kweli na yapi si ya kweli au yapi yanahitaji kupitia (adjusted). Lakini pia pande zote mbili zina haki ya kuangalia namna ya kutatua mgogoro wa kodi. Hata kwenye makampuni au wafanyabiashara wa kawaida si wana haki ya kuhoji (dispute) madai ya kodi na wakati mwingine madai yao yanabadilishwa au wanaweza wakatoa pendekezo (offer) la kulipa kiasi gani kwa mkupuo au kwa utaratibu fulani? Sasa kwanini tudhanie kuwa hilo haliwezekani? Yaani kwa vile tumesema tunadaia trilioni 400 basi ni lazima zilipwe zote na kiasi chochote chini ya hapo ni kuwa cha kupuuzia?

Hizi ni Zama Mpya

Ndugu zangu, hizi ni zamampya; ni zama ambazo baadhi ya vitu vinaenda kubadilika na ni vizuri watu wakae kujua vinabadilika. Wajue pia kuwa zama hizi bado zinatafuta mahali pake pa kushikilia. Kweli zipo hoja mbalimbali zinazoweza kutolewa kukosoa serikali na kwa haki kabisa serikali inapaswa kukosolewa. Kuna maeneo ambayo yanastahili kukosolewa na watu wanapaswa kukosoa. Lakini ni lazima na muhimu kukosoa kufanyike siyo kwa sababu ya chuki, hasira au ubaya fulani.

Hitimisho

Tunasubiria kwa hamu kuona hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa si kwenye madini tu bali kwenye sekta nyingine ili kuhakikisha Watanzania wanafaidika kwa kiwango cha juu kabisa na utajiri wa mali zao za asili; kwani wao ndio wawekezaji wakubwa kwenye jambo lolote linaloenda kufanywa. Kwani hakuna mwekezaji mkubwa kuliko mwenye raslimali zake. Ni lazima tujitambue hivyo, na ni lazima tujitendee hivyo. Tusijione kama siyo ‘wawekezaji’ na hawa watu wanaokuja na fedha ndio ‘wawekezaji’. Sisi ndio wawekezaji wakubwa; Tanzania ndio mwekezaji mkubwa zaidi.

Sasa kwanini tujione duni na kutetemeka mbele ya wawekezaji wadogo hata kama ni wazungu?

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(203)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available