Maoni SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Ijumaa: Kuvuja kwa Pakacha na Tatizo la Pakacha la Jirani!

Na. M. M. Mwanakijiji
Nilisimuliwa kisa hiki nikiwa maeneo ya Maramba huko Muheza Mkoani Tanga mwanzoni mwa miaka ya themanini. Ni kisa cha mchuuzi wa maembe ambaye alikuwa ananunua maembe kutoka kwa wakulima mbalimbali na kuyapeleka Makorola mjini Tanga ambapo alienda kuyauza kwa jumla. Yule bwana alikuwa ni mchuuzi maarufu na mkubwa kwani akinunua maembe anajaza matenga mengi tu na kuyabeba kwa magari ya Landrover 109 ya nyakazi zile. Hii ilikuwa ni kabla ya kuja haya 110 na Discovery.

Hakuwa peke yake kwani pia kulikuwa na mchuuzi mwingine mdogo ambaye ilikuwa sana shida kwake kupata maembe na hivyo alikuwa anasarandia sana matenga (mapakacha) ya yule mchuuzi mkubwa hasa anapoyatoa kwa wakulima. Aliweka watu wake kila alipoweza kuweza kutoboa matenga yale na kuiba maembe ili na yeye aweze kujaza matenga yake na hatimaye naye apate nafasi au kajinafasi ka kwenda kuuza huko Makorola Tanga au sehemu nyingine yoyote ambapo watu wanahitaji maembe.

Kweli alikuwa anafanikiwa mara moja moja kuvujisha matenga ya mchuuzi mkubwa. Katika simulizi lile niliambiwa kuwa mchuuzi yule mdogo kila alipopata maembe kutoka kwenye tenga la mchuuzi mkubwa alifurahia sana na kujitapa sana kwa watu kuwa ametoboa tenga na amemtia hasara mchuuzi mkubwa. Watu walikuwa wanamuambia labda siyo hasara kwani “kuvuja kwa pakacha ni nafuu kwa mchuuzi”.

Mchuuzi yule mkubwa yeye hakuona shida sana kwani alijua habari za mchuuzi yule mdogo na hakuhangaika naye sana. Hakuhangaika naye sana kwa sababu haikumtia hasara. Haikumtia hasara kwa sababu mchuuzi mdogo hakuvunjisha yale maembe makubwa, yaliyonona, matamu na yenye harufu ambayo unaweza kuivuta hata ukiwa ndotoni. Alichoweza kuvunjisha yalikuwa ni maembe yaliyoanza kuooza, na ambayo yalikuwa yanafuatwa fuatwa na inzi na wadudu wa kila namna. Maembe yale yaliyobonyea bonyea japo yalionekana kama yameiva na yana harufu nzuri kama yale mengine ukweli wake ni kuwa yalikuwa yemeanza kuharibika na yasingekaa muda mrefu na hivyo yalihitaji kuuzwa kwa haraka.

Mchuuzi mkubwa alichosema ni kuwa kuvujishwa kwa maembe yake kulimletea wepesi zaidi wa kuweza kujaza maembe mengine mazuri zaidi. Hakukumtia hasara zaidi bali kulimpa nafasi ya kutengeneza faida kwani maembe mengi mabovu, yaliyoanza kuoza na yaliyopasuka pasuka yalikuwa tayari yalikuwa yamechukuliwa na yule mchuuzi mjanja ambaye naye alikuwa anatafuta nafasi.

Hasara kubwa aliipata mchuuzi mdogo kwani licha ya kupata maembe mabovu, alitumia gharama kubwa wakati mwingine kunyemelea maembe yale mabovu, kuharibu tenga za mchuuzi mkubwa na baadaye kusafirisha maembe yake kule kule Makorola lakini pia akakosa soko na kujikuta akiuza maembe yake kwa bei chee mno na wakati mwingine alijikuta akimbembeleza mchuuzi mkubwa kuyanunua!

Ndugu zangu, kuondoka kwa Nyalandu hakujanipa tatizo kabisa. Sababu alizozitoa za kwanini ameondoka sina shida nazo kwani zinadai ameonesha msimamo fulani. Na kama nilivyowahi kusema huko nyuma kuwa yeyote anayepingana na Magufuli ndani ya CCM au serikalini yampata kujiuzulu sina tatizo kwa Nyalandu kuchukua ushauri huo. Sijasema “kila anayetofautiana na Magufuli” kwani kutofautiana ni msingi wa uongozi mzuri, demokrasia na chanzo cha kupata mawazo mbadala. Nimesema “wanaopingana” kwa maana ya kwamba hawakubaliani kinachofanywa na Magufuli na serikali yake.

Ni kanuni hii ya uongozi ambayo huwa ninairudia sana kuwa endapo kuna mtendaji au mwanachama wa ngazi za juu ambaye hakubaliani na Magufuli ndani ya CCM au serikali anawajibu wa kuandika barua yake ya kujiuzulu na katika barua hiyo ni lazima aeleze sababu ya kujiuzulu huko kama ni kutokana na kupinga jambo fulani au sababu nyingine. Ndio maana hata walipojiuzulu hawa viongozi wa Acacia kwa baadhi yetu tumeelewa kuwa wamefanya hivyo baada ya kushindwa kukubaliana na uongozi wao wa juu wa Barrick.

Tatizo langu kubwa hata hivyo ni kuwa Nyalandu kwa haraka amekimbilia CHADEMA. Ninachohofia sana kwangu ni kuwa japo kuna watu wanaweza kuchukulia kuwa CHADEMA imepata mwanachama “mwandamizi” kutoka CCM inawezekana chama hicho kikuu cha upinzani kikazidi kujimwagia matope mbele ya hadhara na kikajikuta kinazidi kupoteza mvuto kwa watu wa kawaida na badala yake kikabakia chama cha wenye sauti wachache wasomi (the elite vocal minority). Hii ni hatari ambayo baadhi yetu tumeanza kuiona tangu 2015 ambapo CDM iliamua kuchukua na kukumbatia viongozi ambao walionekana kuharibu wakiwa ndani ya CCM na kuwapa nafasi kubwa ndani ya chama hicho ikitegemea kufanya hivyo kutaipa ujiko zaidi mbele ya jamii. Hatari yake – naomba kupendekeza – ni kuwa CDM inajichimbia shimo ambalo itakuwa vigumu sana kwake kutoka.

Wasije kujikuta wanalalamikia Magufuli na serikali yake kwa kuminya siasa lakini wao wenyewe wakiharibu siasa zao za ndani.

Naomba kupendekeza kuwa ili kujikinga na kujiharibu (self-destruction) huko kunakokuja ni muhumu sana kwa CHADEMA kuweka utaratibu na kanuni zitakazoongoza upokeaji wa viongozi waandamizi wanaotoka CCM na hasa ambao wamewahi kutajwa kwenye kashfa mbalimbali. Ni kweli hili halikufanyikawakati wa ujio wa Lowassa kwa sababu zinazoeleweka lakini kwa sasa hakuna udhuru tena kwa chama hicho kukinga mikono na kupokea kila anayetaka kuja wakiamini kwa kufanya hivyo wanamuonesha Magufuli kuwa “anakataliwa” ndani ya CCM.

Wasipofanya hivyo, wanaweza kujikuta wanapokea kila mtuhumiwa, kila anayeharibu, kila anayeona “cha moto” na kila mwenye matatizo ambaye anaona hana chake tena na kukimbilia CHADEMA. Kwa wale ambao tumeiona CDM kwa muda mrefu ikiinuka na kuwa mtetezi wa wanyonge na kikijaribu kutengeneza dira ambayo iliwavuta watu wengi sana 2010 hadi 2015 tunazidi kupata wasiwasi kama CDM hii tuliyoiona miaka hii kumi hivi iliyopita itaweza kusimama tena 2020. Na sitoshangaa kuwa katika uchaguzi wa madiwani utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu pigo kubwa la kihistoria linaweza kuikuta CDM kiasi kwamba itatafutwa sababu nyingine yoyote kuelezea kuliko ile iliyoko mbele yao – kuchukua nyangumi waliokataliwa CCM na kuwaingiza kwenye bwawa la samaki na kuamini kuwa samaki watakuwa salama. Chui akiokoka, mbuzi wanashangilia kwa mbali.

Ni kweli kuvuja kwa pakacha ni nafuu kwa mchukuzi (mchuuzi), lakini pia inaweza kuwa faida kubwa kwake na hasara kwa anayeokota yaliyovuja!

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(172)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available