Maoni MWANAKIJIJI SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Alhamisi: Magufuli Akipita Kwingine si Mkabila Tena…?

Na. M. M. Mwanakijiji

Rais Magufuli hatakiwi kwenda Mwanza, Shinyanga, Geita au eneo jingine lolote la Kanda ya Ziwa bila ya kuonekana anakupendelea na ni mkabila. Akipita huko, akifungua mradi wowote huko, au hata akienda kusalimia ndugu zake, anaonekana – kwa baadhi ya watu – kuwa anapendelea “watu wake”. Tuhuma hizi za kiongozi wa Tanzania kuonekana anakupendelea kwake siyo mpya sana kivile.

Kwa wanaokumbuka tuhuma kama hizi ziliwahi kutolewa na baadhi ya watu (inawezekana ni wale wale) wakati wa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete. Alipoanza kujenga kule Msoga, mara moja watu tulianza kuwa na mashaka na malengo yake na kuanza kuonekana anaanza kukujenga kwa vile ni kwao na anajiandalia mahali pa zuri pa kuja kupumzikia akistaafu. Ilipoanza kujenga interchange ya barabara ya ya Chalinze ikichepukia Msoga (kijijini kwa Kikwete) mara moja watu walianza kuhoji kama Kikwete anaanza kupendelea kwao.

Mtu mmoja akiandika mwaka 2013 kwenye JamiiForums alihoji hivi kuhusu hili “Tunajua kuwa Chalinze kuna foleni lakini nilitegea kuwa kama ni by pass iwe toka Msoga kuja Dsm bila kupitia Chalinze, kwa kuwa magari mengi yanapitia Chalinze kuja Dsm na siyo kwenda Moro. Kama Rais anakubali watendaji wake kumfurahisha kwa kutumia mabillioni ili barabara ya kitaifa ipite kijijini kwake tunapata picha gani? Nyerere angekubali hili?”

[​IMG]
Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo- Msata
Mtu mmoja naye akichangia kwenye mada hiyo alisema “Kikwete ni janga la taifa kwani amethamini zaidi vitu vinavyomnufaisha yeye binafsi, familia yake au watu wake wa karibu kuliko taifa zima. Bandari ya Bagamoyo ni miongoni mwa mambo ya ajabu kabisa kuwahi kufanywa na rais wa taifa hili.”.  Hili la bandari inawezekana liliacha ukakasi kwa wengi kwa kuona kuwa Kikwete alikuwa anajipendelea kweli kweli.

Ulikuwepo mjadala mkubwa kuhusu hili kwenye JF. Unaweza KUSOMA HAPA.

Hata Rais Mkapa naye alionekana kwa baadhi ya watu anatumia nafasi ya kupendelea “kwao”. Wakati wa Ujenzi wa lile linaloitwa “Daraja la Mkapa” kuna watu waliona pia kufanya kwake vile ilikuwa ni kuwasaidia watu wake wa Kusini.

Hata hivyo, sasa hivi ni Magufuli anayepata tuhuma hizi za ukabila na ushahidi unaotolewa ni vile vinavyoonekana “vimiradi” ambavyo haviingii akilini hasa kwenye mji wake wa Chato, Geita. Tayari baadhi ya watu wamelalamikia kuwepo taa ya kuongozea magari (kwa vile hakuna magari mengi – yaani hadi magari yawe mengi ndio taa ziongezwe), wanalalamikia kufungulia kwa ofisi mbalimbali kwenye makao makuu ya mkoa huo. Na hivi majuzi kumekuwa na kauli kali zinazomtuhumu Magufuli kuwa anapendelea kwao baada ya Benki ya CRDB kufungua tawi huko, na bila ya shaka hoja ya uwanja wa ndege wa Chato.

Hoja hizi zote zinaweza kuwa na mantiki na zinaweza kweli kuonesha kuwa Magufuli anapendelea kwao. Katika nchi zetu hizi kama Magufuli kweli anapendelea kwao hatokuwa Rais wa kwanza wa Kiafrika au duniani kufanya hivi. Wengi tunakumbuka jinsi Muammar Gaddafi alivyoujenga mji wa kwao wa Sirte, au alivyofanya Saddam Hussein alivyofanya kule Tikrit. Sadam aliijenga Tikrit na watendaji wake wengi walitoka eneo la huko kwao. Hata wakati wa Vita ya Iraq majeshi ya ushirika yalijipanga yakijua mwisho wa siku Sadam atarudi kwao na labda huko ndio itakuwa ni eneo la mwisho la kupigania. Alifichwa na watu wa kwake kwa karibu miezi sita akihama nyumba na nyumba hadi alipokuwa maili kama 15 nje ya Tikrit.

Kwa Afrika, mifano ipo ya watu kama Robert Mugabe. Kabla ya Anguko lake mwishoni mwa mwaka jana Mugabe alikuwa ameanza mipango ya kuhamisha makao makuu ya nchi hiyo toka Harare kwenda kwenye mji wake wa Zvimba (pichani chini) kilomita arobaini hivi Magharibi ya Harare, katika Jimbo la Mashonaland. Wengi hawakupendezwa na uamuzi huo kwani tayari mji huo mdogo ulidaiwa kupokea fedha nyingi za serikali kulinganisha na idadi yake ya watu au mahitaji yao.

Image result for Zvimba

Hii ni mifano michache tu ya viongozi ambao wakiwa madarakani walitumia nafasi zao kunufaisha maeneo ya kwao au kuonekana wanafanya hivyo kwa gharama ya sehemu nyingine. Je, hili laweza kuwa kweli kwa Rais Magufuli vile vile?

Related image
Taa ya kuongozea magari, Chato.

Swali hili ni zito; Je, Magufuli anatakiwa asijali hali ya watu wa jimbo lake kabisa ili kuonesha kutolipendelea na hivyo hicho kiwe kipimo cha uzuri? Akienda likizo au kumtembelea mama yake na ndugu zake ni gharama gani itatumika kama ataenda kwa magari, huduma mbalimbali n.k? Inawezekana Watanzania wengi hawajaona faida ya Kikwete kwa mfano kutoka eneo karibu na Dar ambalo tayari lilikuwa na miundo mbinu ambapo Rais aliweza kwenda kusalimia kijijini na kurudi mjini siku  hiyo hiyo. Je, Rais akitaka kutembelea ndugu mgonjwa au kwa sababu fulani kwenda kwao iweje? Kwamba, asipoenda kutembelea kwao atakuwa anaonesha kupenda zaidi Watanzania kuliko watu wa kwao?

Uzito pia upo wa kuangalia swali hili kwa kuingiza kabila. Wengi tunajua kuwa sasa hivi kwa kiasi kikubwa hakuna mahali hasa kwenye maeneo makubwa ambapo unaweza kusema kuna watu wa kabila fulani peke yao. Kwa mfano, Bagamoyo hawaishi Wakwere peke yao; mafanikio yoyote ya Bagamoyo bila ya shaka yatachuja na kuwafikia hata watu wengine ambao si wa asili ya huko. Kujengwa Chato kunaweza kufanya eneo la Magharibi kuwa na miji mikubwa miwili Chato na Mwanza? Je hili ni jambo baya? kwamba kwa watu wa Magharibi maendeleo pekee yanatakiwa yawe Mwanza mjini tu?

Lakini hapa kuna hoja nyingine ya ndani zaidi; tayari tunamuona Magufuli akipita na kufungua miradi mbalimbali kwenye maeneo mengine ya nchi. Alikuwa Singida na leo nasikia anafika Morogoro na ameshaenda Dodoma. Je, huku kote anakopita anafanya hivi kwa sababu ya Wasukuma wanaoishi ndani ya miji hiyo? Kwamba hii reli ya SGR inayojengwa, barabara zinazojengwa na alizozisimamia wakati akiwa Waziri wa Ujenzi alikuwa anafanya hivyo akiwafikiria Wasukuma na watu wa Magharibi?

Hivi leo hii, akitokea na kutaka kutengeneza reli ya kasi (SGR) kwenda Tanga kutokea Dar ambayo inaaweza kusaidia zaidi kuunganika kwa kihistoria kwa miji hii miwili na hata kupunguza idadi ya watu wa Dar itakuwa ni kwa sababu ya ukabila? Au tuchukulia kwa mfano, ikaamuliwa kujenga barabara mpya ya kwenda Kusini (au kupanua ya sasa) anaweza kudaiwa kuwa ni ukabila?

Maoni yangu kwa kweli ni kuwa inawezakena baadhi ya watu kwa sababu wameamua kuwa wapinzani wa Magufuli basi wamejitoa kabisa ufahamu na hisia ya haki na hivyo chochote atakachofanya Maguful – iwe kwa kauli au kwa vitendo – ni lazima ichukuliwe kisiasa. Magufuli hata akisema utani (kwa baadhi yetu tunajua ana utani ule mkavu – rejea “walimia meno”) kwa wengine ni kama ameapa kufanya jambo kwa Biblia! Ni kwamba, watu wameamua kuondoa kabisa kumuelewa Magufuli kabisa na hivyo wanajikuta wanakwaza akicheka, wanakerwa akinuna, wanaumia akikaripia na wanachukizwa akisema jambo!

Swali linabakia hata hivyo, Magufuli anaweza kweli kufanya jambo lolote kuondoa hisia hii ambayo inaweza kujengeka hata kama haina msingi? Je, anaweza kupuuzia na badala yake anaweza akajikuta watu “wa kwake” wanaanza kuangaliwa kwa macho mawili mawili na kuanza kutengwa kama namna ya watu wengine kumlipizia kisasi? Je, anaweza kujikuta atakapoondoka madarakani “watu wake” wanaanza kutendewa kinyume kama kulipizwa kisasi? Lakini vipi kama anafanya yote kweli kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wote wa kila mahali bila kujali dini, kabila, rangi au lugha zao?

Sina majibu.

(200)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available