HABARI KUU SIASA TANZANIA

Maandamano ya Mange Yashindwa Kabla ya Kuanza; Atangaza Kwenda Likizo

Rais Magufuli akisalimiana na Rais wa SMZ Dkt. Shein leo Dodoma kwenye sherehe za Muungano. (Picha na Ikulu)

Na. M. M. Mwanakijiji

Kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na hasa kwenye Telegram vijana waliokuwa wanajiapisha kuwa hawatomuangusha mwanadada Mange Kimambi siku ya tarehe 26 Aprili walishindwa kujitokeza mitaani na kwenye makutano mbalimbali kuandamana. Toka asubuhi kwenye mitandao hiyo wanachama wake walikuwa wanategeana na kungojeana ili kuona nani atakuwa wa kwanza kunyanyua bango. Baada ya kuzimika kwa maandamano hayo ya Instagram, malundo ya lawama yameanza kutolewa huku wengi wakilaumu mkwara wa jeshi la polisi kwa siku mbili zilizopita kuwa umetishia watu. Hata hivyo, wengi wanashindwa kuelezea kama walitarajia nini kifanyike wakati lengo la maandamano liliwekwa wazi na Mange kuwa ni kumtoa Rais Ikulu? Ni nchi gani ambayo inaweza kulinda maandamano yenye kutaka kuelekea kuutoa uongozi halali madarakani kwa sababu tu watu wanadaiwa wanamchukia sana rais huyo? 

Pamoja na hilo mjadala mkubwa unaoendelea katika hali ya kujitafakari miongoni mwa mashabiki wa Mange ni juu ya maandalizi mazima ya maandamano hayo. Mange mwenyewe akiandika katika akaunti yake ya Instagram anakiri kuwa maandalizi ya maandamano yake hayakuwa mazuri kwani yalitoa nafasi kwa serikali kufuatilia kwa karibu na hatimaye kujipanga kwa ustadi mkubwa kuyadhibiti bila kurusha risasi hata ya plastiki.

Na ameonesha yeye mwenyewe kuumizwa na kile ameona kama kuingizwa mjini na Watanzania ambao walionekana kushabikia kweli na akawaamini. “Nimeumia kishenzi ila najikaza tu sababu I have to hold it together (inabidi nijikaze). Najua most of you are broken and I don’t want to add to that pain. Ila kihehere cha kujifanya nawajua sana kushinda Chadema wanavyowajua kimeniisha. Mbowe aliwastukia mapema akasitisha UKUTA mie nikaingia kichwa kichwa nikawaamini 100% kumbe bwana mnaongea tu ila vitendo ni zero….jamani mmeniacha uchi, wabaya wangu wanani cheka. Ntaweka wapi uso wangu?” ameandika Mange.

Kutokana na hili Mange ametangaza kuwa kuanzia sasa hatoposti tena malalamiko ya watu waliokuwa wanamtumia ili watu wakasirika na kuchoshwa kweli kweli. ” Ila matatizo na kero sitokaaaa kuposti tena. Sitokuwa sauti yenu tena. Yani sasa hivi inabidi muugulie matatizo yenu mpaka mzirai ili siku tukisema maandamano mnyanyuke kwa hasira zoooote.” amesema kwa uchungu kupitia akaunti yake ya Instagram.

Kwanini Maandamano Hayakuungwa Mkono wala Kujaribiwa?

Swali ambalo linaweza kuwa linawasumbua waliomuunga mkono Mange ni kwanini vijana ambao walijiapisha kutomuangusha Mange, walioapa kuwa “liwalo na liwe” watajitokeza kudai “haki” zao mbalimbali hawakujitokeza isipokuwa watu kama watatu tu nchi nzima?

Je ni woga? Sababu kubwa inayotolewa ni kuwa wananchi wengi wameingiwa na hofu na woga mkubwa na hawakuwa tayari kupigwa kipigo cha mbwa koko kama alivyotishia RPC Mambosasa wa Jijini Dodoma. Jibu la kuwa ni woga linaweza kuwa jibu rahisi zaidi lakini jibu lenyewe gumu kulikubali na labda lina ukweli zaidi ambalo sasa litakuwa limempa nguvu zaidi (emboldening) Rais Magufuli.

Hakukuwa  na Itikadi ya Kuwaunganisha Zaidi ya Matusi na Kejeli?

Kama waliokuwa wanataka kuandamana walikuwa wanajionesha kuwa wana ujasiri mkubwa na kuwa hawaogopi chochote ni kitu gani kilichowafanya wawe na woga tena? Ni wazi kuwa hakukuwa na kitu kinachowaunganisha kiitikadi wale waliotaka kuandamana. Mange hakuwa anaongoza mijadala yake kwa itikadi inayoeleweka; alikuwa anaonekana au kujionesha kuwa yeye alikuwa anamchukia Rais tu na kuwataka wengine wamchukie vile vile huku akitoa tuhuma mbalimbali nzito.

Matokeo ya mtiririko wa uhamasishaji wa maandamano ulifanya iwe vigumu sana kwa taasisi huru na za kijamii kujitokeza kuunga mkono kama nilivyoonesha katika zile sababu nane za kwanini maandamano haya yasingeweza kufanikiwa. Ni mtu gani mwenye hekima, ni kiongozi gani wa kisiasa ambaye angeweza kujitokeza kuwaunga mkono? Ni nani angeweza kusimama na kusema anaunga mkono madai ya Mange kuwa Magufuli ni Mhutu, Mwizi, Muuaji, na kuwa anapaswa kuondolewa madarakani kwa shinikizo?

Na hili lilikuwa linaonekana katika video na jumbe mbalimbali zilizokuwa zinatumwa kwa Instagram ya Mange. Ni kwa kiasi gani hili liliwa turn off watu wengi na wenye heshima zao katika jamii ni vigumu kuamua. Lakini lugha hii ya mitaani na vijana inaweza kweli kuvutia vijana wa mitaani lakini inaweza vipi kuwavutia watu wazima na watu ambao wasingependa kuonekana wanahusishwa na maandamano yanaonekana hayana hoja na kama yanayohoja imejaa matusi ya nguoni ambayo magumu kuyatamka mbele ya watoto na watu wazima?

Mwitikio wa Serikali Ulitarajiwa

Hakuna ambaye hakutarajia mwitikio wa serikali na ni vigumu kusema kuwa ulikuwa ni mkali kuliko kawaida. Mwitikio kama huu umeshatokea huko nyuma kwenye baadhi ya mikoa tu. Hata hivyo, kutokana na oganaizesheni ya maandamano kitaifa, mwitikio wa polisi umekuwa wa kitaifa vile vile. Inawezekana kwa baadhi ya watu kuonesha misuli kwa serikali kulikuwa kukubwa na kwa kutia hofu lakini kwa wanaofuatilia masuala ya usalama mwitikio huu unaweza kutajwa kuwa ulikuwa “uliopimwa”. Japo watu wanaweza kudhani wameona askari wengi, ukweli bado ni kuwa wapo askari wengi zaidi waliokuwa kazini, kwenye vituo mbalimbali na kwenye majukumu mbalimbali. Fikiria kwamba, askari walioshiriki magwaride hawakuwa sehemu ya wale waliokuwa kwenye kudhibiti uwezekano wa maandamano. Ni wazi kuwa kilichotokea ni kuwa askari ambao walikuwa “off” siku hizi mbili siku hizo za “off” zilifutwa na kuwa kila askari alikuwa kazini au kuwa katika hali ya kusubiria (standby).

Nilielezea hili kwenye makala nyingine ile kuwa kutokuonekana kwa askari wa JWTZ mitaani kunaonesha pia ni jinsi gani serikali haikulipa uzito mkubwa sana kama wengi wanavyodhania. Kwenye maandamano ya UKUTA mwaka 2016 watu wanaweza kukumbuka jinsi gani CHADEMA walipotishia kufanya maandamano ya nchi nzima serikali ilichukulia kama tishio kubwa zaidi kiasi kwa namna fulani kulifanya jeshi lionekane katika ile operesheni yake ya kufanya usafi siku ile ile iliyopangwa kuwa ya maandamano. Safari hii hili halikuwepo kabisa. Kulikuwa na kujali (concern) lakini hakukuwa na tishio (threat).

Yawezekana watu wamesahau kabisa kuwa wakati wa Rais Kikwete mwaka 2012 Jeshi la Wananchi lilionekana kuranda mitaani Dar katika hali ya kuzuia maandamano yaliyokuwa yana lengo la kuishinikiza serikali kuhusia na Sheikh Issa Ponda. Kwa mara ya kwanza watu walishuhudia askari wa JWTZ wakipita kwenye magari yao ya dereya wakiongezea nguvu polisi. Ni wazi kuwa wakati ule kulikuwa na zaidi ya concern ya amani; bali kulikuwa na dalili ya tishio. Na hata hivyo, hilo lilifanyika Dar peke yake na siyo mikoa yote. Ni wazi na sahihi kusema kuwa mwitikio wa serikali safari hii ni chini ya ule wa 2012, kwani safari hii vikosi vya JWTZ havikuonekana mitaani kabisa.

Watanzania Waone Fahari kwa Vikosi vyao vya Usalama

Mojawapo ya mambo ambayo yanaonekana ni ya hatari ni ile hali inayoonekana ya kutaka kujenga uhasama kati ya raia na polisi wao. Kusema kweli kwa karibu nchi zote duniani polisi wana kazi ngumu sana ya kujenga uhusiano mwema na raia hasa kwa vile wao ndio watu wa kwanza ambao raia ama wanakutana nao katika majanga au wanawakimbilia na kukuta wanakosa haki mapema. Kutokana na hali hii mara nyingi watu japo wanatambua wajibu wa kazi za polisi lakini wapo ambao hawana amani na polisi na kuwachukulia kama sehemu ya mfumo unaowatawala kwani wanaonekana kama polisi kazi yao ni kuwatetea watawala au viongozi wa chama tawala cha kisiasa.

Mtazamo huu siyo sahihi. Ni mtazamo ambao kweli upo na inawezekana ni halali kutokana na mang’amuzi (experience) ya watu ilivyo na polisi. Lakini kuwachukulia polisi kama adui ni hatari kubwa sana kwa raia kuliko vinginevyo. Polisi ndio wanasimama kati ya utulivu na amani, kati ya usalama na vurugu, na kati ya sheria na ubabe. Hata vijana wote ambao tuliona wanataka kuandamana au kudai wataandamana wao wenyewe wakipata matatizo hawana pa kukimbilia isipokuwa polisi. Hata wanasiasa ambao wanalalamikia chama tawala na wanaona wanatendewa vibaya na serikali bado hawana pengine pa kwenda isipokuwa polisi.

Magari ya Polisi Shinyanga (picha na Kadama Malunde)

Ni haki basi na ni busara polisi wenyewe ni lazima waonekana hawaendeshi kazi kisiasa kwani kuaminiwa na raia kunaifanya kazi yao kuwa rahisi vile vile. Lakini polisi hawapaswi kufanya kazi ili wampendeze kila raia. Jukumu lao kubwa na la kwanza ni kuhakikisha wanalinda raia wote na mali zao na kuhakikisha kuwa katika mazingira ya kawaida kabisa nchi inakuwa katika hali ya utulivu na shughuli mbalimbali zinaendelea kama kawaida.

Nguvu Iliyoonesha Kuzuia Maandamano Ioneshwe Kulinda Maandamano

Kwa watu wengi waliofuatilia sakata hili zima; hoja kubwa ambayo inaonekana pia kuwa sahihi na halali ni kuwa polisi wameonekana kuwa na nyenzo, uwezo, muda, ujasiri, ujuzi, weledi na uzoefu wa kuweza kuzima maandamano kabla hayajaanza. Kama hili ni kweli, ni kitu gani kinaweza kuzuia polisi hawa hawa wenye hayo yote waonekane kushindwa kuyapa ulinzi maandamano ya watu kama elfu moja tu hivi? Kama wanaweza kujipanga vizuri hivi nchi nzima kuzuia maandamano ni kitu gani kinawafanya washindwe kutoa vibali na ulinzi kwa vikundi vya watu wachache wanaotaka kuandamana sehemu moja tu ya nchi?

Ni wazi kuwa polisi wetu wamejithibitisha kuwa wana kila kinachotakiwa kuweza kudhibiti maandamano yawe ya mtu mmoja sehemu moja au ya watu mamia sehemu mia! Wakati umefika naamini kwa Jeshi la Polisi na viongozi wa kisiasa kukaa chini na kuona ni kwa namna gani utaratibu unaweza kuwekwa kuhakikisha shughuli za vyama vya siasa zinafanyika kwa njia ya amani na kama kunatokea jambo ambalo linatishia amani, ni wazi jeshi letu la polisi lina uwezo wa kudhibiti mara moja kabla jambo hilo halijafika pabaya. Hili tumeliona na ni kweli.

Hatima ya Mange, Wamuungano Mkono na Serikali

Swali kubwa linalobakia na linalotokana na yote yaliyojiri hadi hivi sasa ni Mange na wanaomuunga mkono wanaenda wapi. Katika posti zake za leo pamoja na kuonekana kuumizwa moyoni Mange ameapa kutokata tamaa na hatowaacha waliomuunga mkono. Vijana wanaomba radhi kwa kumwangusha na kujitetea kwanini haikuwezekana kuandamana. Lakini swali lililoko ni je, Mange anaweza kufanya tafakari ya kwa namna gani yeye mwenyewe, ujengaji hoja wake, kauli zake zimeweza kuchangia kuwakatisha watu tamaa na kushindwa kuungwa mkono na taasisi muhimu au vikundi muhimu? Je, kama ataendelea na mwendo huu kuna uwezekano gani wa watu kufika mbali naye na kumuamini zaidi huko mbeleni? Kama ameamua kuongoza vijana hivi, je anataka kuishia kuwa mhamasishaji tu hivi au kuwa na matokeo ya kisiasa vile vile na ataweza vipi kuyafikia maelekeo ya kisiasa bila kukutana na vijana wanaomuunga mkono? Inawezekana akapanga siku moja – ikilazimu – kukutana na vijana hao nyumbani katika kuandaa jukwaa la kisiasa ambalo litakuwa na nguvu katika uchaguzi?

Haya ni maswali yanayobakia. 

Maswali mengine yamebakia kwa serikali kwa ujumla wake na kwa Rais Magufuli mwenyewe kama kiongozi wa Tanzania. Kuna lolote la kujifunza? Kuna lolote la kubadilisha? Kuna lolote la kuongezea? Jibu ambalo naamini ni sahihi ni kuwa Watanzania wengi kwenye siku ya Muungano wao, hawakuwa tayari kuitia dosari siku hii kwa maandamano au jaribio la kumuondoa Rais madarakani. Wanalipenda Taifa lao zaidi licha ya changamoto zao mbalimbali. Hata wale wanaotofautiana na Rais kwa kiasi kikubwa au serikali yake, wao pia hawakuwa tayari kugeuza Muungano kuwa Mchomano.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(352)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available