SIASA TANZANIA

KKKT Laiwakia Serikali Mambo Saba katika Salamu za Pasaka

Na. M. M. Mwanakijiji

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanzania (KKKT)  limetoa waraka mkali wa kichungaji likilalamika na kuonesha mambo saba ambayo linaona yanaenda kombo katika siasa za Tanzania. Waraka huu umetolewa kama ujumbe wa salamu za Pasaka kwa waumini wa kanisa hilo na kwa taifa na unatarajiwa kusomwa katika makanisa mbalimbali ya Kilutheri kesho siku ya Jumapili ya Matawi tarehe 25 Machi, 2018.

Waraka huo ambao umetiwa saini na maaskofu ishirini na saba (27) wa kanisa hilo una kichwa cha habari Taifa Letu, Amani Yetu umekuja baada ya matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea na baadhi yakihusisha  wachungaji wa kanisa hilo. Hivi karibuni mchungaji mmoja wa kanisa hilo aliitwa na kuhojiwa na polisi baada ya kutoa kijitabu kidogo kikielezea hali ya kichungaji kwenye usharika wake hususan masuala ya sadaka. Kijitabu hicho kililaumu hali mbalimbali kama chanzo cha kushoka kwa mapato ya utoaji.

Mchungaji Fred Njama wa Usharika wa Karanga mjini Moshi katika Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT alitoa taarifa ya kichungaji kwa waumini wake wiki mbili zilizopita, taarifa ambayo inaonekana kugusa utendaji na mwelekeo wa siasa za Tanzania. Mchungaji Njama alinukuliwa kusema kuwa “Inavyoelekea uhuru umeanza kuminywa. Ulianza kwenye siasa, ukaja kwenye vyombo vya habari.”. Vile vile alinukuliwa kutoa mfano kuwa “takwimu za uchumi au chochote hata kama kina ukweli lakini utawala hautaki kusikia ukizungumzia hadharani au kwenye daladala ni kosa la jinai. Matukio ya miili kuokotwa yamezidi,matumizi ya risasi yameanza kuzoeleka kama kitu cha kawaida. Watu kupigwa risasi kwa walio wanasiasa na wasio wanasiasa yanafanya watu waishi kwa hofu.”

Mch. Njama aliposoma taarifa yake usharika wa Karanga, Moshi Tanzania.

Kufuatia taarifa hiyo Mchungaji huyo aliitwa na vyombo vya usalama na kuhojiwa kuhusu taarifa yake hiyo. Siyo tu aliitwa, lakini mchungaji huyo alitakiwa avichukue vitabu vyote ambavyo tayari vilikuwa vimesambazwa na vile vilivyoko kiwandani kurudishwa. Pamoja na hayo vyombo vya usalama vilidaiwa kufanya upekuzi katika ofisi yake. Hata hivyo, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuonesha kama kulikuwa na amri yoyote ya mahakama iliyotoa agizo hilo au alikuwa anatuhumiwa rasmi kufanya kosa gani. Viongozi mbalimbali wa mkoa waliotakiwa kutoa maelezo juu ya tukio hilo wote walionekana kama hawajui kilichotokea japo taarifa zilidai kuwa uamuzi huo ulitolewa na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika waraka wake wa salamu za Pasaka, KKKT limeanisha mambo saba ambayo limeyaona kuwa ni tatizo la msingi linaloendelea Tanzania. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na ujengwaji wa hisia ya hofu katika wananchi ambayo inatokana na kuongezeka kwa matukio mbalimbali ya utekaji, watu kupotea, matumizi ya silaha dhidi ya wanasiasa na matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya wananchi. Pamoja na hayo waraka umedai kuwepo kwa “mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi” pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

Jambo jingine ambalo linatajwa na kanisa hilo ni kile kilichodaiwa kuwa ni kutoweka kwa uhuru wa kujieleza. Waraka huu umejenga hoja kuwa wakati uhuru mbalimbali umeanza kuminywa basi kuna mwelekeo kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani. Hata hivyo, waraka huo haujafafanua ni kwa namna gani maaskofu wanafikiria uhuru wa kuabudu unaweza kuminywa.

Jambo la tatu ambalo maaskofu wameliona ni kile kinachodaiwa kutoweka kwa uwezo wa wananchi kuchagua viongozi wao bila kutumika kwa nguvu kubwa. Waraka huo mkali ambao bila ya shaka utagusa na unagusa hisia za watu mbalimbali ni kudai kuwa hivi sasa chaguzo “zote” zimekuwa zikigubikwa na nguvu kubwa sana ya kuhakikisha mgombea fulani anashinda.

Jambo la nne ambalo Maaskofu hao wakiongozwa na Mkuu wa Kanisa hilo nchini Dkt. Fredrick Shoo umedai kuwa uhuru wa mihimili mingine ya dola umeingiliwa kati. Mihimili ya Mahakama na Bunge waraka huo umedai imeanza kupoteza uhuru wake. Pamoja na mihimili hiyo waraka umedai kumekuwepo na udhoofishaji wa taasisi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja Serikali za Mitaa.

Jambo la tano ni madai mazito yaliyotolewa na waraka huo ni kuwepo kwa kila kinachoonekana shughuli za maendeleo kuelekezwa kwa minajili ya kiitikadi. “Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko” umesema waraka huo. Kauli hii inaweza kutafsiriwa na baadhi ya watu kuhusiana na madai kuwa Rais Magufuli anaonekana kupendelea watu wa Kanda ya Ziwa. Baadhi ya watu wamekuwa wakilalamikia jinsi ambayo baadhi ya watu ambao wanadaiwa kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za serikali ambao kwenye kanda ya ziwa watu hao wanaachwa kwenye maeneo hayo. Hilo linadaiwa kutokea huo Mwanza ambapo watu hao waliachwa kwa madai kuwa walimpigia kura Rais. Watu wa maeneo mengine kama Kimara huko Dar wameondolewa kwa nguvu wakati mazingira ya madai yao yanafanana na yale ya Mwanza au maeneo mengine ya kanda ya ziwa ambao watu wameachwa kuvamia maeneo ya serikali kwa amri ya Serikali. Rais Magufuli anatokea mkoani Geita.

Mambo mengine ni hisia ya kushamiri kwa chuki na visasi na udhalilishaji wa kauli njema ambayo Maaskofu wamedai inatumika vibaya. Waraka umedai kuwa utaratibu wa kulazimisha watu wahame vyama vyao na kujiunga na chama tawala umekuwa ukileta usumbufu mkubwa kwa wananchi pamoja na gharama kubwa za kurudia chaguzi mbalimbali. “Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani” umehoji waraka huo.

Haijajulikana jinsi gani waraka huo utapokelewa na serikali na kama huu ni mwanzo wa mgongano usioisha wa Kanisa na uongozi wa serikali.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(157)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available