SIASA TANZANIA

Kingunge Ngombale Mwiru – Aliishi na Kufa katika Imani

Na. M. M. Mwanakijiji

Msiba wa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru umekuja na kuacha pigo na simanzi kwa watu wengi ambao walimjua mzee huyu na kukumbuka mchango wake katika ujenzi wa taifa letu. Msiba huu ni pigo kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki lakini pia ni pigo kwa wale wote walioamini katika siasa kama nyenzo ya kuleta mabadiliko katika jamii. Mzee Kingunge alikuwa ni muumini aliyepitiliza wa siasa na matokeo ya siasa hizo.

Mzee Kingunge anakumbukwa kwa mambo mengi; ukiondoa kutuachia jina hilo la “Kingunge”. Anakumbukwa kwa wengi kama miongoni mwa wanasiasa ambao walikuwa hawana dini rasmi na kuonekana kama “mkomunisti” kweli kweli. Iliaminika na ilionekana mara nyingi mzee Kingunge akiapa kwa kutumia katiba tu bila kitabu chochote cha kidini. Hili lilimpa umaarufu kuwa Kingunge alikuwa haamini uwepo wa Mungu au hakuwa tu na dini.

Tangu kuelekea wakati wa uhuru, Kingunge akiwa kijana na baadaye Mzee Kingunge alikuwa anaamini katika siasa na uwezo wa siasa kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Ni kwa sababu ya imani yake hii aliaminiwa na viongozi mbalimbali wa taifa na kupewa majukumu mbalimbali ya kiuongozi. Uwezo wake wa kujenga hoja na kusimamia misimamo yake ulimtengenezea marafiki wa kudumu.

Kuwepo kwake katika siasa kwa muda mrefu kulimfanya ajulikane kama ni miongoni mwa wana CCM damu. Hata hivyo, alipoamua kuondoka Chama cha Mapinduzi na kuamua kujiondoa kuna ambao walishangazwa sana lakini kwa wale wanaomjua Kingunge hilo halikuwa jambo la kustaajabisha. Akizungumza na waandishi wa habari mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu alitangaza matatizo aliyoyaona katika chama alichoshiriki kukijenga na kusema kuwa kutokana na matatizo mbalimbali ambayo yaliifanya CCM isiwe CCM ile waliyoiasisi basi yeye alikuwa “anaachana” na CCM.

“Najua uamuzi wangu utawasumbua baadhi ya ndugu zangu, rafiki zangu, makada wenzangu, wazee wenzangu, ambao wengine tunawasiliana mara kwa mara na hata vijana. Lakini uamuzi wangu ni lazima niufanye vinginevyo mimi nitajisaliti mwenyewe” Alisema Mzee Kingunge. Aliongeza na kusema kuwa alishiriki katika kujenga misingi ya chama na kuhakikisha kuwa kuna demokrasia ndani ya chama. “Lakini demokrasia ndani ya chama inapigwa mateke” aliongeza Mzee Kingunge na kuwanyoshea kidole viongozi wakuu wa chama ambao walijitokeza wakati ule kudai kuwa mambo ndani ya chama yalifuata taratibu kitu ambacho kwa maoni ya Mzee Kingunge hakikuwa sahihi.

Kingunge katika mazungumzo yake yale alidai kuwa asingeweza kuwa kwenye chama ambacho hakiheshimu Katiba. Kwa hili Kingunge alikuwa anafanya lile lile la imani yake. Aliamini katika CCM, aliamini katika katiba ya chama hicho na aliamini haja ya kuwepo uwazi, kuheshimiana na kubishana bila kukashifiana. Ukiongoa Waziri Mkuu wa zamani Lowassa aliyeondoka baada ya kukatwa jina lake, Mzee Kingunge alikuwa ni mtu maarufu zaidi kuondoka CCM.

Kuondoka kwake CCM kuliipa nguvu Chama cha Demokrasia na Maendeleo na mzee huyo kutokana na imani hiyo alionekana kama mtetezi wa upinzani nchini na demokrasia na ameondoka akiwa amevutia hata wapinzani wengi kuamini katika maono yake.

Hata hivyo, funzo kubwa ambalo naweza kusema kuwa Mzee Kingunge amewaachia vijana na wazee, wana CCM na wasio wana CCM ni kuwa na msimamo katika imani ya kile unachokiamini hata kama kinaweza kukugharimu mambo mengi na makubwa. Mzee Kingunge kweli hakuwa tayari kusaliti imani yake na msimamo wake pindi alipouchukua; hakuwa tayari kufuata mkumbo wa wengi na upepo wa wengi zaidi.

Ametufundisha kuwa kweli siasa bado ni imani.

Apumzike kwa Amani.

Amina.

(186)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available