SIASA TANZANIA

Hawa Wawili Wanabeba Lawama za Kuvurugika kwa Siasa Tanzania

Jaji Kaijage anapata shida kusimamia uchaguzi Tanzania. Hata mdogo.

Na. M. M. Mwanakijiji

Nilivyoandika jana kuna watu wanaona sikusema kwa ukali sana. Wapo wanaosema naogopa kumnyoshea kidole Rais Magufuli kwa sababu nilimuunga mkono kugombea kwake kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015. Inachonishangaza ni kuwa hata watu wanaojua uandishi wangu wanafikiria kwa sababu fulani sijajiunga kwenye jukwaa la wanaotaka watafute uhalali wao wa kisiasa kwa kuonesha wanampinga Magufuli. Hili sina tatizo nalo na ndio maana ya uhuru wa fikra na maoni.

Hata hivyo, hatari ambayo ipo sasa kwa wanaharakati, wanasiasa, wanasiasa watarajiwa na watu wengine ni kuamua kufumba macho na kuwa wakali zaidi kwa kukosoa vitu na watu sahihi na kuwataka wawajibike. Rais Magufuli anabeba lawama zote za yale mambo ambayo yeye ndio mwamuzi wa mwisho na ambayo yanaweza kutatuliwa ama kwa ushauri wake au kwa maagizo yake rasmi (executive orders).

Kwa sasa, naamini kabisa siasa zetu zinaweza kubadilika kabisa, zikawa zakiungwana, zisizo na ulazima wa kumwaga damu na zisizojenga uhasama endapo vyombo hivi viwili chini ya viongozi wao wawili vitang’ang’aniwa na kulazimisshwa vifanye kazi yao inavyopaswa.

Hapa nazungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi la Tanzania. Hili ni wazi kwa watu wengi lakini labda uzito wake ndio wengi bado hatujaupata inavyopaswa na badala yake tunakimbilia kumdai Rais. Wapo watu wengi sana ukiwasoma pamoja na ujuzi wao wote na hata uzoefu wao wote, wanaonekana hawaamini kabisa wanapaswa kuving’ang’ania vyombo hivi viwili.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaundwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 74 na utendaji wake kazi unaongozwa na sheria na kanuni mbalimbali husika. Ni kweli kwamba, Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi huteuliwa na Rais; lakini hili si jambo geni. Nchi nyingi tu duniani tena za kidemokrasia zina mfumo ambapo Rais au Waziri Mkuu anateua wajumbe wa Tume za Uchaguzi. Suala kubwa kwa tume za uchaguzi si nani hasa anayeteua bali zaidi ni jinsi gani ziko huru kutoka kwa yule anayewateua.

Ni kweli kabisa, kwa mfumo wetu ulivyo, Tume ya Uchaguzi inamtegemea sana Rais. Hili hata hivyo, halimaanishi haiko huru kufanya kazi zake. Tatizo kubwa kwenye tume yetu ya Uchaguzi ni kukosekana kwa weledi (unprofessionalism) na hivyo kufanya kazi kinyume na kifungu cha 11 cha Ibara hiyo ya 74. Kiongozi yeyote wa tume (Mwenyekiti, Mjumbe au maafisa wa uchaguzi) wanaposikiliza, wanapofuata maagizo ya viongozi wa serikali au ya chama fulani cha kisiasa kama CCM kinyume na matakwa ya sheria na miongozo yao wanavunja Katiba.

Yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mdogo wa Kinondoni; chombo pekee kinachopaswa kubeba lawama zote za mapungufu yote yaliyotokea pale ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hii si mara ya kwanza kwa tume hii kuonekana inashindwa kuendesha uchaguzi kwa amani; na inaonekana kuzidiwa na misukumo na mihemuko ya kisiasa. Watendaji wake wanashinikizo kubwa la kusimamia haki na wakati mwingine inaonekana wanafanya kazi kwa woga au hofu fulani. Wapo waliojifunza kwa wenzao ambao waliwahi kuonekana kuadhibiwa au wengine kuzawadiwa.

Inawezekana vipi, tume miaka zaidi ya ishirini sasa ya kuendesha chaguzi mbalimbali bado inapata shida kuweka utaratibu mzuri kwa mawakala, wanasiasa, na hata kusimamia uchaguzi bila watu kuonekana wameonewa? Hivi ni kweli wote humo ndani ya tume hakuna mtu mwenye weledi na usomi wa kujaribu kutabiri (expect) matatizo mbalimbali yanayoweza kutokea kama jambo moja au la pili likitokea. Hivi ni kweli, tume haijaona jinsi gani masuala ya mawakala yanavyosumbua.

Hivi kwanini mawakala wa vyama vya siasa wanasubiri hadi siku moja kabla ya uchaguzi ndio wapate kukubaliwa? Kuna ubaya gani, kwa watu wenye akili timamu kusema tutengeneze utaratibu utakaohakikisha kuwa wiki moja kabla ya uchaguzi wowote – uwe mdogo au mkuu – kila chama kiwe kimeshapata kila kinachohitajika kuhakikisha kuwa mawakala n.k wanajulikana na wamepata utambulisho wote? Kwanini tusubiri hadi dakika za mwisho kama siyo kutengeneza mazingira ya watu kuonekaan wameonewa na kulazimisha watu wengine wajaribu kuweka shinikizo lisilo la lazima?

Leo hii tunawalaumu upinzani kwa kuandamana kudai mambo ya mawakala wao? Tuliwataka wafanye nini? Wakinge mikono na kuomba kama zawadi? Wote tumeona jinsi gani serikali na vyombo vyake vilivyotumiwa kwenye chaguzi hizi hasa Kinondoni; kweli kabisa tunataka Mahakama ndio ije baadaye kutengua uchaguzi huu huu halafu watu warudie tena kama vichaa wasiojifunza lolote? Binafsi naamini CHADEMA itakuwa na msingi mzuri tu wa kwenda mahakamani kupinga kuchaguliwa kwa Mtulia na sitoshangaa wakashinda! Lakini kwanini tufike huko?

Tatizo la utendaji wa Tume ya Uchaguzi ni kubwa mno, linatia aibu na linatufanya tujihoji kama tunaweza kuendesha uchaguzi sisi wenyewe bila kulazimisha uhasama, vurugu, na hisia za kuonewa. Niliuliza juzi; hivi kweli ni vigumu sana kwa Watanzania kuendeshsa uchaguzi kwa amani, kwa utulivu, na katika mazingira ya ushindani na siyo uadui? Kwanini tuendessha uchaguzi kama wale wengine wanaogombea wanatoka sayari ya Zebaki au Zuhura na hivyo hawastahili kabisa kuaminiwa au kupewa nafasi? Ni ukiritimba gani huu tulio nao kwenye fikra za kiutawala?

Hivi, kwa mfano CHADEMA wangeshinda Kinondoni katika mazingira ya uhuru, haki na usawa; hivi Kinondoni ingegeuka jangwa? Au wana CCM wa Kinondoni wangegeuka misukule? Si huyo huyoaliyegombea CCM alikuwa CUF na alishinda 2015 na Kinondoni watu waliendelea kuishi, kufanya shughuli zao na maisha yaliendelea? Au tu ni dalili kuwa inawezekana ipo haja ya kuanza kuandika tena na kusimuliza vile visa vya Ujinga wa Mwafrika? Kweli kabisa, tunashindwa kuendesha uchaguzi sisi kwa wasomi wetu, na watendaji wetu ambao waliapa kuendesha uchaguzi kwa haki na bila upendeleo wakizingatia Katiba?

Nani aliyesema kuwa tunahitaji amani zaidi siku ya kutumbukiza makaratasi kwenye masanduku kuliko mchakato mzima wakufikia siku hiyo. Kama uchaguzi ungekuwa ni kutumbukiza karatasi tu; sisi kampeni zinawekwa za nini? si lengo ni kushawishi watu kwa hoja. Sasa kama watu hawawezi kushawishi kwa hoja na badala yake wanatawaliwa na vihoja; kwanini isiamuliwe tu hakuna tena kampeni kama kampeni zinaudhi sana baadhi ya watu?

Matatizo yaliyomshinda Jaji Lubuva tunaona leo yanajirudia na kuwa ni magumu kushughulikiwa na Jaji Kaijage. Ina maana hawa majaji wanaweza kuwa ni mahiri wa sheria, lakini inawezekana ni viongozi wabovu. Kwanini mambo ambayo yanawezekana kama mtu akiwa thabiti yaonekane kuwa magumu hivyo? Kama wanaona hawawezi kufanya kazi bila kuingiliwa au mashinikizo mengine si waamue kujiuzulu  kuliko kujiabisha kwa kuendesha mfumo ambao unadharaulisha kabisa dhana nzima ya haki, usawa, na ushindani wa kisiasa? Yaani, kama marefarii wa mpira wa miguu wangekuwa wanapata shida kama hizi; kweli kuna mechi ingekuwa inachezwa? Kama refarii angesikiliza mashabiki na wamiliki wa timu, kweli wangeweza kuchezesha mchezo wowote?

Tatizo la pili; ni Jeshi la Polisi. Sijasema tatizo ni Askari Polisi. Nimesema Jeshi la Polisi. Suluhisho langu kuhusiana na hili hapo kesho, likipokelewa na wenye kupokea na wakalifanyia kazi nawahakikishia kwa asilimia 90 litabadili kabisa mahusiano kati ya Jeshi na vyama vya upinzani na litatengeneza mazingira mapya kabisa ya kisiasa.

Itaendelea Kesho

mwanakijiji@jamiiforums.com

 

 

(356)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available