Maoni

MwanaKJJ Jumatano: Sababu 8 Kwa Nini Maandamano ya Mange ni Vigumu Kufanikiwa

Na. M. M. Mwanakijiji

Hakuna utata wala ubishi kuwa kama Mange kutikisa serikali ametikisa; hakuna utata kuwa kama kuwapa watu mshawasha, Mange amewapa watu mshawasha. Hata watu ambao miezi michache tu nyuma walikuwa hawamjui Mange sasa hivi jina lake linajulikana labda hata kwenye kona za miji na vijiji ambavyo havijawahi kusikia mtu anaitwa Mange Kimambi. Kwamba amefanikiwa kusababisha taifa kuzungumza hili halina shaka. Lakini je, maandamano aliyoyaitisha ambayo masaa machache kuanzia sasa yanatakiwa yafanyike na kurindika yatafanikiwa? Je, lengo lake kuu la maandamano hayo kweli linaweza kufanikiwa?

Naomba kupendekeza kuwa pamoja na kuangalia mambo yote – kama nilivyoonesha makala yangu ya jana – kama nikiulizwa nitabiri nini kitatokea kesho na kama kitafanikiwa jibu langu ni rahisi – Maandamano hayatafanikiwa. Kutokufanikiwa haina maana vijana hawana malalamiko halali na yanayojitaji kusikilizwa na Serikali na hasa na Rais mwenyewe. Yapo malalamiko na manung’uniko halali kabisa ambayo yanahitaji uzito unaostahili. Kamatakamata ya watu wanaompinga Rais, watu kutoweka, mashambulizi yenye mazingira ya kisiasa, watu kuwekwa ndani nje ya muda unaoruhusiwa kisheria, kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa kwa wengine wote isipokuwa Rais wakati Katiba inaruhusu n.k ni malalamiko ambayo hayawezi kudharauliwa au kutupwa nje kwa kudhania yataisha tu.

Kwanini Maandamano Hayatafanikiwa?

1. Lengo lake kuu la kuwahamasisha vijana kuandamana na kulazimisha Rais Magufuli ajiuzulu na hatimaye mama Samia Suluhu Hassan achukue nafasi ni lengo gumu, zito na ambalo ni gumu zaidi kuungwa mkono na wananchi wengi. Hili ni lengo ambalo linahitaji uwepo wa chuki kubwa sana dhidi ya Rais kiasi cha kwamba ashindwe kuungwa mkono na maelfu ya watu wengi sana kuweza kulazimisha ajiuzulu. Hili ni lengo lisilofikika. Njia pekee ambayo ni ya kawaida ya kuweza kumzuia Magufuli asiendelee madarakani ni kujipanga kuelekea uchaguzi wa 2020. Nje ya hapo ni vigumu kuona jinsi gani Magufuli ataondolewa nje ya taratibu za Kikatiba au Uchaguzi.

Sababu hii au lengo hili ni gumu kuliwekea mantiki. Tuhuma mbalimbali ambazo zinatolewa kuwa Rais aondolewe madarakani zinaweza kutafsiriwa kama ni vilio vya watu ambao walizoea maisha fulani na sasa mambo yamekuwa magumu na wanataka kurudi kwenye maisha yale ya awali.

2. Japo Mange ameweza kuhamasisha vijana kujitokeza kumpinga Rais Magufulu jambo moja hajaliweka kwenye hesabu ni nini kitatokea endapo vijana wengine wenye kumuunga mkono Magufuli wataitwa nao kujitokeza kuonesha kumuunga kwao mkono. Mfano mzuri wa kuzingatia hili ni jaribio la mapinduzi liliotakwa kufanywa dhidi ya Rais Erdogan wa Uturuki ambapo vikosi vya kijeshi vilijaribu kuasi lakini mara baaada ya Rais kujitokeza kwenye TV na kuonesha kuwa bado yuko salama na kuwaita mashabiki na wapenzi wake kujitokeza kumuunga mkono. Hadi hivi sasa nguvu inayoonekana ni ile ya kidola tu kushughulikia maandamano haya; lakini nguvu ya kisiasa ya maandamano pingani (counter demonstrations) haijaingizwa.

3. Japo hadi hivi sasa inaonekana ni kweli kuna hamasa ya vijana kujitangaza kuwa wataandamana kwa wale ambao tunakumbuka hamasa, hakuna kama hamasa ya Lowassa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015. Kama kulikuwa na wakati ambapo vijana waliohamasika kisiasa wangeweza kusababisha mabadiliko kweli kweli ilikuwa ni wakati ule. Hamasa ile ya mabadiliko ilizimwa kwa kiasi kikubwa na wazee na watu wazima. Hamasa hii pia inaweza kuzimwa na wazee na watu wazima ambao kwa sababu fulani hata kama hawafurahii yote yanayofanywa na Serikali ya Magufuli hawako tayari kuunga mkono Mange hasa kutokana na wengine wanavyoweza kuona ameendesha kampeni yake ambayo inaweza kuonena iliyopitiliza katika kuvunja heshima, uungwana. Kwamba, yale ambayo Rais Magufuli anadaiwa kufanya – kusema ovyo, ukali, lugha mbaya n.k – Mange mwenyewe anaweza kudaiwa kuwa anayafanya kwa watu wengine na hivyo kuonekana ni kama birika kukiita chungu cheusi! Hata kama lugha ya Mange ni lugha ambayo vijana wanaitumia miongoni mwao inawezekana isimfanye awe kipenzi cha wazee wengi na watu wazima.

4. Mange amesema wazi na mara kadhaa kuwa lengo lake siyo kuiondoa CCM madarakani bali kumuondoa Rais Magufuli. Na kwa vile amesema maandamano haya yasihusishwe na vyama vya kisiasa jambo hili japo linaonekana ni zuri lakini vile vile ni kikwazo cha kufanikiwa kwake. Uchaguzi wa 2015 waliomfuata Lowassa aliko walikuwa wana lengo la kutaka kuiondoa CCM madarakani. Hawakumpinga Magufuli kama Magufuli tu bali walimpinga kwa maoni yao kwa sababu ulikukuwa ni mwendelezo bado wa utawala wa CCM. Hivyo CHADEMA na UKAWA waliwakilisha chama mbadala; je maandamano haya ambayo yanatakiwa kuwa makubwa yanata tu kumuondoa mtu bila kuiondoa CCM madarakani? Mara nyingi maandamano au mapinduzi yanayouondoa uongozi wa kidemokrasia HAYAACHI utawala umalizie muda wake; yanalazimisha kuitishwa kwa Uchaguzi mwingine ili uongozi mwingine wa kidemokrasia uwepo. Je, wanaotaka kuandamana wanataka kuandamana ili CCM iendelee kuongoza hadi 2020? Hivyo, ajenda yenyewe ya lengo la maandamano imekosewa na ni ngumu kuungwa mkono na watu ambao hawaipendi CCM. Maandamano haya yangeweza kupata nguvu kama yangefanyika 2020 kama ingetokea Bunge linabadilii katiba kuondoa ukomo wa vipindi ili kumruhusu Magufuli kugombea bila ukomo. Katika mazingira hayo hata sisi wengine ambao tulimuunga mkono atakuwa ametupoteza na bila ya shaka itakuwa ni hoja nzito ya kuipinga.

5. Kukosekana kwa uongozi unaoongoza maandamano hayo nchini na hivyo kuyapa sura ya kuwa yanaongozwa na watu walioko Tanzania na ambao kama ikitokea yapambe moto wanaweza kuitwa kuwa sehemu ya majadiliano ni ngumu. Ikitokea kweli maandamano yafanyike kwa kiasi kikubwa na serikali inataka kukutana na viongozi wa vijana hawa ni nani atakayejitokeza kusimama na kuwa msemaji wao? Je, Mange akiitwa aende Tanzania kuzungumza na serikali jinsi ya kusitisha maandamano atakuwa tayari kwenda? Je, serikali itamruhusu kama akitaka kwenda mwenyewe kuwasaidia vijana badala ya kwenda Washington DC tu? Kama kiongozi wa vijana hawa ni umbali gani yuko tayari kwenda kuonesha kweli anawaunga mkono na yuko tayari kuwaongoza? Kukosekana kwa Mange mwenyewe au watu ambao ni wawakilishi wake kuongoza maandamano yeye akiwa “uhamishoni” kunafanya yawe magumu kufanikiwa kwa lengo lile la kwanza hapo juu.

6. Siku iliyochaguliwa kufanya maandamano haya inawezekana kuonekana ni nzuri kwani inagongana na siku kuu. Hata hivyo, siku hii ni mbaya kwa sababu siyo siku ya kazi. Maandamano yote duniani yenye kusumbua serikali ni yale yanayotokea siku ya kazi na kuingilia shughuli mbalimbali za kazi za kila siku. Kwa vile maandamano yanatakiwa kuanza Alhamisi basi kwa upande wa serikali kimkakati inahitaji hadi Ijumaa tu kuyazima (kama yakifanikiwa kuendelea usiku). Siku nyingine mbili za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) zinatosha kabisa kwa nchi kuwa pacified (kutulizwa). HATA HIVYO:Endapo kweli itatokea maandamano yahimili siku ya Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili na yaelekea kuingia siku ya kazi Jumatatu – natabiri mapema kabisa TUTASHUHUDIA WAZIRI MKUU akijiuzulu kuinusuru Serikali ya Magufuli na pamoja na hilo italazimisha mabadiliko makubwa kwani. Hii ni licha ya hoja ya 8 hapa chini.

7. Kwa vile maandamano haya yanafanyika kwnye mtandao sana hasa Instagram, inawezekana mafanikio yake makubwa yakaishia huku huku kwenyee mitandao. Yanaweza kuja kubakia kuwa ni “maandamano ya Instagram”. Itakuwa ni hatua kubwa sana kwa watu kutoka kwenye mitandao kwenda mitaani; utamaduni huu ni mgumu na ni kikwazo kikubwa kifikra. Ni kweli baadhi ya nchi wameweza kujihamasisha kupitia mitandao kufikia kuwa na maandamano makubwa. Mifano ya Tunisia na Misri iko wazi. Lakini, mazingira ya nchi hizi zote kisiasa na kijamii ni tofauti sana na Tanzania kiasi cha kuweza kudhania yaliyotokea kule yanaweza kutokea Tanzania. Nina uhakika Watanzania wanaweza kujitahidi kubadilisha serikali kwa njia ya uchaguzi kuliko njia ya mapinduzi – iwe ya kijeshi au ya wananchi. Bila kuungwa na taasisi mbalimbali za kijamii ni vigumu kuona ni kwa kiasi gani yanaweza kufanikiwa. Namna pekee hili linaweza lisiwe kweli ni kama a. maandamano yanakolea na kuendelea kwa siku kadhaa na b. taasisi na asasi mbalimbali za kiraia (vikiwemo vyama vya kisiasa, taasisi za kidini n.k) zinajitokeza kuunga mkono na hata hapo bado kuna mambo mengine ya kuangalia. Angalia mfano wa DRC ambapo hadi mapadre walijitokeza kuandamana lakini Kabila yuko madarakani na tena wao Rais wao amekwepa kuitisha uchaguzi. Hali ya kisiasa ya TZ haijafikia hapo.

8. Jambo kubwa ambalo litasababisha maandamano haya yasifanikiwe; siyo kwamba yasianze lakini yakazimwa na nchi kutulizwa ni kama Rais ataamua kutumia nguvu za Mamlaka yake ya Wakati wa Dharua chini ya sheria ya Emergency Powers ya 1984. Ni kweli waandamanaji wamejipanga kupambana na hali ya kawaida ya vyombo vya usalama; kama polisi na maji ya washawasha, mikwara n.k lakini wengi hawajafikiria uwezekano wa Rais kuamuru nchi iingie katika hali ya hatari. Hili ni gumu sana kutokea kwani ni extreme measure (jambo la dharura sana). Hatujawa na hali rasmi ya hatari tangu wakati wa vita ya Kagera (kama kumbukumbu yangu uko sahihi) maana hata wakati wa kesi za uhaini sikumbuke kama kulitangazwa hali ya hatari. Na hata wakati wa vita ya Kagera hali ya hatari haikutumika katika uzito wake wote. Sasa kama kweli itatokea maandamano yakishindwa kudhibitiwa na polisi mara moja kiasi kwamba kuonekana polisi wamezidiwa nguvu basi JWTZ litaingizwa na kuituliza nchi. Kwa wale ambao tunafuaitilia siasa ujumbe wa uwezekano wa hili uko wazi kila siku mbele ya TV zetu.

Kwa sababu hizi saba, sioni namna gani maandamano haya yatafanikiwa kweli; yaani watu waingie mitaani na kulazimisha Rais Magufuli ajiuzulu. Sioni ni kwa namna gani maandamano haya yanaweza kuwa yakudumu zaidi ya siku moja. Lakini kama nilivyosema jana, itakuwa ni makosa kupima mafanikio ya maandamano kwa kuangalia watu wangapi watajitokeza mitaani. Mabadiliko yoyote ambayo yamefanyika hadi hivi sasa na labda yanayokuja baadaye yakizingatia hisia za vijana hawa yanaweza kuwa ni mafanikio makubwa ya maandamano kuliko maelfu ya watu kujitokeza mitaani.

Vijana ambao watakuwa wamehamasika, itabidi Mange awahamasishe zaidi kujiandikisha kupiga kura ili nguvu na hamasa yao hiyo isiwe ya kwenye mitandao tu bali waende kwenye sanduku la kupiga kura kama vijana wenzao walivyofanya 2015. Nje ya hapo, njia hii ya mkato ya kujaribu kuleta mabadiliko naamini itakuwa ni ngumu sana kufanikiwa. Lakini hatuwezi kuwalaumu vijana kwa kujaribu.

Kama hawana njia nyingine salama, huru na ya kidemokrasia inayoheshimu utu wao na matamanio yao; kama hawana mtu anayewasikiliza na kuwakilisha mawazo yao; kama wanaona kuwa wanaachwa pembeni ya baraza la mafanikio; vijana hawa waende wapi? Christian Bella aliimba mojawapo ya nyimbo nzuri sana ambapo anahoji “sisi maskini twende wapi”? Kwa Magufuli changamoto kubwa siyo jinsi ataonesha na nguvu na madaraka, siyo jinsi gani anaonesha ni mkali na asiyetishwa; kibarua kigumu zaidi kwake ni jinsi anaweza kuonesha kuwa anajua, anajali, na anasikiliza sauti ambazo ni ngumu wakati mwingine kuzisikiliza.

Maandamano haya yanaweza yasifanikiwe Aprili 26 kama ilivyotarajiwa na Mange na wanaomuunga mkono hata hivyo itakuwa ni makosa makubwa sana kudhania kuwa hayatajaribiwa tena, kwa sababu nzito zaidi; na itakuwa ni makosa ya kujutia kudhania kuwa hayatokuja kufanikiwa. Anayechimba shimo, huanza kwa kuchimbua padogo; kama kuchimbuliwa pameanza kuchimbuliwa.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

(472)

About the author

bongoz

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available