Simulizi

Riwaya: SIKU YA MKOSI -1

Na. M. M. Mwanakijiji

Kanusho: Simulizi hili ni la kubuni; mfanano wowote na mtu au matukio halisi, mahali majina na hali mbalimbali ni ya kinasibu na matokeo ya ubunifu wa mtunzi. Riwaya inavyotokea hapa ni kwa ajili ya majaribio; baadhi ya mambo yanaweza kubadilika litakapotoka kwenye kitabu. Nitakuletea mwendelezo wa simulizi hili kila Jumanne.  UKIONA MAKOSA YOYOTE YA MTIRIRIKO WA MAWAZO NIJULISHE. MMM

 

SURA YA 1

Siku ya mkosi haiji na mmoja. Siku yangu ilianza kwa jina langu kuwa miongoni mwa majina yaliyotajwa kama waliotumbuliwa na Waziri mara baada ya serikali mpya kuingia madarakani. Nilipolala jana yake nilikuwa miongoni mwa watu wazito kwenye mojawapo ya taasisi nyeti zilizo chini ya Wizara ya Fedha; unaweza kuniita kuwa nilikuwa miongoni mwa ‘vigogo’ au ‘vingunge’. Usiku ule ulikuwa ni kama siku nyingine zilizopita; nilienda kulala nikiwa na mipango yangu mingine mingi tu ya kazi na ya kutumia nafasi mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza pale kazini kuendeleza maisha yangu, ya ndugu zangu na rafiki zangu. Nililala nikiwa na furaha na maisha yangu yakiendelea kung’ara. Sikutarajia kuwa asubuhi yake na siku nzima iliyofuatia ingekuwa ni siku ya kukumbukwa katika maisha yangu.

Asubuhi ya siku ile ya Jumatatu ilianza kwa dalili fulani hivi. Kwa vile sikuwa mtu wa kuamini sana katika mambo ya ushirikina baadhi ya dalili hizo nilizipuuzia kwani niliona kama bahati mbaya tu. Kwanza, niliamka na kukuta jenereta la umeme linaunguruma kuashirikia kuwa umeme wa TANESCO ambao tulikuwa tunaukopa Watanzania wengi ulikuwa umechukuliwa na wenyewe. Wakijisikia kuurudisha wataurudisha tu, nilijiambia.   Hilo halikunisumbua kwani pale nyumbani sikujali sana umeme huo. Ukiwepo nashukuru ukikosekana nasonga mbele.

Nilimuacha mchumba wangu Rita akiwa kitandani; alikuwa amechoka kwa kunichosha usiku uliopita. Labda na mimi nilikuwa nimemchosha pia; maana hayakuwa mapenzi yale ya usiku ilikuwa ni vurugu mechi. Nilijiona kama miongoni mwa watu wenye bahati sana duniani. Rita alikuwa ni mtoto wa Balozi wa Tanzania nchini China Dkt. Rose Kitangile Ericsson. Baba yake alikuwa ni Msweden aliyekuwa amefanya kazi Tanzania kama Mkurugenzi Mkazi wa SIDA miaka ya themanini na baadaye kuamua kuishi Tanzania baada ya mkataba wake kuisha. Aliomba uraia wa Tanzania miaka michache baadaye.  Walizaliwa wawili tu kwenye familia yake; yeye mkubwa na mdogo wake wa kike Marieta ambaye alikuwa anasoma huko Sweden.

Wakati naamka kitandani nilimuangalia Rita alivyolala na kujipongeza moyoni kuwa kwa hakika nilikuwa nimeopoa kweli kweli. Mtoto alikuwa ameumbwa akaumbika na kama mbinguni kuna malaika basi nina uhakika mmoja wao alitupwa duniani kama zawadi kwangu. Alikuwa amelala akiwa mtupu kabisa kajifunika shuka nyepesi ambayo ilimfanya aonekane kama picha nzuri ya kuchora ambayo mtu angeweza kuitundika ukutani kwa fahari. Ningekuwa mtu wa kuendekeza mambo hayo kwa kweli ningepiga simu kutokwenda kazini niendelee na sarakasi zangu. Kuna watu wanasema kiporo kitamu.

Kwa kawaida sikuwa napata chakula cha asubuhi nyumbani kwani muda niliokuwa ninatoka nyumbani kwenda kazini ni mapema sana; nikishapiga mswaki na kuoga na kuvaa kujiandaa kwenda kazini nilikuwa nachukua glasi ya maji ya moto na kunywa kushtua tumbo kidogo. Siku hiyo hata hivyo, nilipochukua glasi kabatini kabla sijaishika vizuri iliteleza mkononi na kuanguka sakafuni; tena sakafu ya marumaru. Ilivunjika vipande vikubwa vitatu; na vipande vingine vidogo vidogo. Nilifyonza na kutukana kwa kimombo na kusikilizia kama nimemshtua Rita huko juu ghorofani. Sikusikia kitu. Nilichukua ufagio na kwa haraka nikafagia fagia na kuokota vipande vile vikubwa kuvitupa kwenye pipa dogo la takataka nikiwa nimefunga kwenye mfuko. Niliandika ujumbe mdogo na kuacha kwenye mlango wa jokofu kumtaarifu Rita kuwa ahakikisha anatumia mashine ya kuvuta vumbi kwani kulikuwa na vipande vidogo vidogo vya glasi pale chini.

Sikutaka kuchukua glasi nyingine; nilichukua ufunguo wa gari langu na mkoba wangu wa kazini ambao ulikuwa na nyaraka mbalimbali pamoja na Ipad yangu. Niliharakisha kutoka ndani ya nyumba yangu huku mawazoni nikianza kupanga siku yangu itakavyokuwa pindi nikifika kazini. Kabla sijavuka kabisa mlango nikakumbuka nimeacha simu yangu juu pembeni ya kitanda; nikaamua kuharakisha kwenda kuichukua. Na kama vile kulikuwa na njama imepangwa katika haraka yangu nikashindwa kukanyaga vizuri ngazi ya kwanza; nikateleza na kama nisingekuwa makini ningevunja pua hivi hivi. Nilijiwahi kushika chini na kujizuia kuumia. Nikashika kingo za ngazi vizuri na kupanda kwa heshima zote; na hata wakati wa kurudi nilidhamiria kuwa makini zaidi.

Niliingia kwenye gari langu wakati mlinzi akifungua geti kuniruhusu nitoke nyumbani kwangu. Mawazo yangu yalihamia barabarani wakati nakanyaga mafuta kuelekea kazini.  Nilikuwa naishi Masaki nyuma kidogo ya ofisi za Water Aid upande wa barabara ya Haile Selasie. Niliposhika barabara ya Haile Selasie sikufikiria kitu kingine chochote isipokuwa kusikiliza kipindi cha asubuhi kutoka EFM Radio.

>>>>>>

Nilipofika ofisini sikuhisi jambo lolote baya au kuwa na hisia yoyote kuwa kuna jambo baya linakuja. Ukiondoa Mkurugenzi Mkuu mimi nilikuwa ni mtu wa pili kufika ofisini siku ile. Kwa kawaida nilikuwa mtu wa kwanza kufika ofisini kila asubuhi. Ukiondoa sababu ya kukwepa foleni ya magari nilipenda kufika mapema ili kuweza kufanya kazi nyingi mapema ili mchana niweze kufanya mambo yangu mengine. Nilishakuwa na kawaida ya kutoka kazini majira ya saa nane hivi kuendelea na shughuli zangu; hakukuwa na mtu wa kuniuliza kwani nilikuwa msaidizi mkubwa wa Mkurugenzi lakini pia nilikuwa na watu chini yangu ambao walikuwa wanatekeleza majukumu mbalimbali pale ofisini.

Nimesahau kusema; nilikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu kwenye moja nyeti chini ya Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango.  Nilianza kupitia kazi mbalimbali ambazo nilikuwa nimeacha jana ikiwemo kupitia mafaili ya nidhamu ambayo yalihitaji kufikishwa kwa Katibu Mkuu baada ya Mkurugenzi Mkuu kuyapitia. Kulikuwa na baadhi ya maombi ya kusafiri kwenda nje ambayo nayo yalihitaji kupitiwa ili hatimaye tuweze kuyaombea kibali Ikulu. Niliendelea kuchambua na kuandika mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya Mkurugenzi Mkuu ili baadaye niweze kuyapitisha. Pamoja na hayo nilipitia taarifa mbalimbali za matumizi ya fedha kwa ajili ya hatimaye kuidhinisha madai mbalimbali ya watumishi ili wenye kustahili waweze kulipwa.

“Bosi, habari za asubuhi?” ilinishtua sauti ya Clara baada tu ya kufungua mlango. Japo nilikuwa natarajia wakati wowote angetokea lakini nilikuwa nimezama sana kwenye kazi zangu hata sikumsikia alipoingia ofisini. Clara alikuwa ni Katibu Muhtasi wangu na kabla ya mimi kuhamishiwa hapo kutoka Mwanza miaka mitatu nyuma alikuwa pia ni Katibu Muhtasi wa mtangulizi wangu.

“Nzuri tu Dada Clara” nilimjibu huku nami nikimjulia hali. Aliniambia tu kuwa amechelewa kidogo sababu ya mvua barabarani na mimi nilimwambia kuwa na mimi ilipiga vizuri tu wakati naelekea kazini. Alitaka kujua kama nilihitaji chai au kahawa asubuhi ile. Nilimwambia kahawa itatosha maana nilikuwa nataka nichangamke kidogo. Alienda sehemu yenye birika la umeme la kutengenezea kahawa na kufanya vitu vyake. Dakika chache baadaye harufu ya kahawa ilimtangulia alipoileta ofisini. Nilishukuru na nikampa maagizo kidogo ya vitu ambavyo nilitaka ashughulikie mapema kwani nilihitaji kumpatia Mkurugenzi ripoti saa nne kamili asubuhi. Niliendelea na kazi huku nikinywa kahawa yangu kavu taratibu.

Muda haukupita kwani ilipofika saa mbili hivi ofisi ilikuwa imeshachangamka na karibu kila mtumishi alikuwa tayari ofisini; japo wachache walikuwa wameanza kazi. Wapo ambao walikuwa wanapiga soga kidogo huku wakiwa wamekaa kwenye sehemu zao na wengine wakiwa nao wanakunywa chai. Miezi michache nyuma ilikuwa ni kawaida kwa lundo la wafanyakazi baada ya kujionesha kuwa wamekuja kazini walikuwa wanakimbia chini ambapo kuna migahawa kununua ‘chochote’ kabla ya kurudi kazini. Kazi hasa ilikuwa inaanza karibu saa nne asubuhi. Wengine walitumia muda mwingi wakiwa kwenye mitandao ya kijamii. Lakini tangu serikali mpya iingie madarakani hali ilikuwa inaendelea kubadilika taratibu; watu walikuwa wanaonesha kuheshimu kazi zaidi na hata labda kujionesha wanaheshimu kazi.

Nilitoka kwenye ofisi yangu na kutembea kidogo kusalimia baadhi ya wafanyakazi na ikawa kama ishara kwao kwamba ni muda wa kazi. Kila aliyeniona alijifanya anajishughulisha. Nilirudi ofisini kwangu. Kama saa tatu hivi na nusu Clara alichungulia kutoka kwenye ofisi yake ambayo inapakana moja kwa moja na yangu na kuniuliza kama nilikuwa na mpango wa kutoka.

“Hapana sitoki saa hivi hadi mchana” nilimuambia na kumuuliza “kwani vipi?”

“Hapana DG aliulizia tu”

Hilo lilinishtua kidogo, haikuwa kawaida kwa Mkurugenzi Mkuu kuniuliza kwani akitaka kujua nipo au vipi aliweza kunipigia extension yangu ya simu moja kwa moja.

“Kwani vipi?” nilijaribu kudadisi. Clara alinyanyua mabega yake juu kuashiria kuwa na yeye hajui.

Akili yangu ikaniambia labda ni kuhusiana na ripoti ambayo nilikuwa niwasilishe kwake au labda kuna kitu kingine maana wiki hizi tangu JPM aingie madarakani ofisi imekuwa hakukaliki. Niliangalia ripoti zangu zilikuwa safi, na mambo mengine ya mitkasi yangu nayo nilijua iko salama.

Hazikupita dakika chache simu yangu iliita na ilikuwa inaonesha ni kutoka ofisini kwa bosi.

“Vicent, acha yote unayofanya sasa hivi tunaitwa ofisini kwa Katibu Mkuu” alisema.

Moyo ulishtuka; kwa muda wote ambao nilikuwa pale ofisini nimekutana na Katibu Mkuu kama mara mbili hivi na mara zote hizo ilikuwa ni vikao vilivyopangwa. Lakini kuitwa moja kwa moja na Katibu Mkuu kulinifanya nishtuke.

“Sawa bosi, on my away” nilisema huku nikizungumza kwa sauti ambayo ilionesha kujiamini na kuwa sijali sana nani alikuwa ananiita. Nilifunga tai yangu vizuri na kuchukua jaketi langu nililokuwa nimeliweka nyuma ya kiti changu. Nilimuaga Clara kuwa nimeitwa kwa Katibu Mkuu pamoja na DG na Wakurugenzi wengine watatu. Moyo ulianza kunienda mbio.

(445)

About the author

bongoz

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available