ELIMU MAISHA

Watoto Wa Kike Watakiwa Kutambua Ndoto zao.

Na Dotto Kwilasa

WAKATI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na mashirika ya kiraia yakipigana kutetea haki za mtoto wa kike, Kanisa katoliki pia linatambua utu wa mtoto huyo na kuchukua hatua stahiki za kumpatia elimu ili kumwezesha kujitambua na kujithamini.

Kwa kutambua hilo kanisa katoliki nchini ,mbali na kutoa huduma za kiroho ,limejikita kutoa elimu kwa mtoto wa kike kwa kuanzisha shule za sekondari nyingi takribani kila mkoa ili kuhakikisha kwamba elimu inakuwa kigezo cha kumkomboa mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kuikumbusha jamii kuwa mtoto huyo ana haki ya kupata elimu.

Miaka kadhaa iliyopita mtoto wa kike hakuwa na thamani katika jamii ,alidharauliwa kiasi cha kuharibu utu wake kwa kufanyiwa tohara na wakati mwingine alichukuliwa kama kitega uchumi kwa baadhi ya jamii na kusababisha watoto hawa kudharaulika na kukata tamaa ya kujishughulisha kiuchumi.

Katika ulimwengu wa sasa Mtoto wa kike yeyote Yule huishi katika ndoto zake kwa kutegemea kuwa atakapokuwa mkubwa atafanikisha ndoto zake kwa namna yoyote ili japo wakati mwingine ndoto hizo hazitimii kwa kutoelewa umuhimu wa ndoto zao au kukosa watu wa kuendeleza ndoto zao.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa  na gazeti hili umebaini kuwa mtoto anapokuwa mdogo huonyesha au huwa na hisia za kujifunza na kuchezea vitu vya ndoto zake ,mfano;unakuta mtoto anachezea magari muda mwingi kuliko michezo mingine inawezekana hiyo ndio ndoto yake na hivyo wewe kama mzazi ni jukumu lako kumsaidia kuienzi michezo yake.

Mwandishi wa habari hizi alipata fursa ya kutembelea shule ya sekondari ya wasichana ya AMANI inayomilikiwa na kanisa katoliki chini ya uangalizi wa masista waabuduo damu azizi ya yesu wilayani Manyoni Jimbo la Singida na kujionea jinsi ambavyo kanisa hili katoliki lilivyowekeza kumjenga mtoto wa kike kimaadili na kielimu ikiwa ni pamoja na kumfanya aishi katika ndoto zake.

Katika kuhakikisha kwamba mtoto wa kike anajithamini na kutambua ndoto zake ,hivi karibuni Mkuu wa shule hiyo Sister Frolida aliandaa mafunzo maalumu ya utambuzi wa ndoto zao  na kuishi nazo mpaka kufanikisha malengo yao hali itakayowawezesha kuishi kwa furaha na kujiamini.

Mafunzo haya maalumu yalifundishwa na wakufunzi mahiri ili kuwaaminisha watoto kuwa hakuna linaloshindikana chini ya jua kwa kumwamini mwenyezi Mungu ,na hivyo kuondokana na roho dhaifu ya kukata tama na kukubali kufanya mambo yasiyoendana na  Ukristo.

Mkuu huyo wa shule ya sekondari Amani,anaamini kwamba kila mtu ana ndoto yake kwa maana ya kwamba kila mtoto anakuwa anatamani kuwa mtu Fulani atakapo hitimu masomo yake kwa mfano;kuna wengine wana ndoto ya kuwa wajenzi,madaktari,wanasheria ,mafundi waashi ,nk.

Anasema kuwa ndoto hizi hufifia kwa baadhi ya wasichana kutokana na changamoto za kukatishwa tamaa na wanajamii au imani za kidini kwamba kazi Fulani inamfaa mtoto wa kiume ,au kazi Fulani haiendani na watoto wa kike na wakati Fulani kazi Fulani haziendani na dini husika.

Hali hii inachangia kuharibu huduma kwa wanajamii kutokana na kwamba mtu anakuwa yupo tayari kufanya kazi asiyoitaka ama kuipenda ili mradi aingize kipato bila kujali kuwa anaumiza wengine kwa kutokuwa na wito na kazi hiyo.

“Kuna watu wanafanya kazi bila matakwa yao ili mradi kupata kipato ,lakini ikumbukwe kuna watu wanaumia  kwa kuwa kazi nyingine zinafanywa bila wito,”amesema.

Anasisitiza kwa kutolewa mfano kuwa,unaweza kwenda hospitali ukakutana na Daktari au mhudumu wa afya akawa mkali na kuwatolea lugha chafu wagonjwa  ,wakati mwingine hata kudiriki kukataa kuwahudumia kwa wakati ,hatua hii inaonyesha wazi kuwa mtu huyu hakuwa na wito wa kuifanya kazi hiyo ila yupo hapo kwa maslahi binafsi.

Kwa upande wa mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo,Father Deus Mulokozi ambaye alikuwa na jukumu la kuwafundisha wanafunzi hao wa Sekondari ya AMANI juu ya utambuzi wa ndoto zao,anaamini kuwa ili upate kitu ni lazima uwe na ndoto nacho ,anazungumzia kuwa utambuzi wa ndoto unaweza ukaondoa unyanyasaji wa kijinsia pale msichana atakapo kuwa na malengo ya kujibu ndoto yake.

Anaizungumzia  ndoto kuwa ni picha inayofikirisha maisha ya baadae na kuchochea nguvu ya kufanya kitu kwa bidii,kusukuma na kuamsha ari ya matumaini mapya  ambapo jamii inapaswa kuheshimu mawazo ya watoto wa kike na kukithamini kile wanachokitaka ili kuleta maelewano na kuwafanya wengine kutokuumizwa kwa kupewa huduma na watu wasio na wito.

Anasisitiza kuwa kuna wasichana ambao husukumwa kutimiza ndoto za wazazi wao kwa maana ya kwamba,mzazi anamchagulia mtoto fani bila kujali kama anaimudu au anaipenda kwa kuwa tu amependezwa nayo na hivyo kumpa ugumu kiutendaji na kukosa furaha maishani.

“Imefikia wakati wazazi na walezi wanawachagulia fani watoto ,nawasihi wanajamii waheshimu mawazo ya mtoto wa kike kwa chochote anachokihitaji ili kuwaokoa watu wanaouumizwa kwa  kupewa huduma duni kutoka kwa watu wasiowaadilifu kwa kazi zao,”amesema Mulokozi.

Hata hivyo Padre Mulokozi anasema kuwa hii haimaanishi kuwa ukiipenda fani yako na kuitimiza hakuna changamoto,hapana ..changamoto ziko kila mahali isipokuwa zinatofautiana kwa kuwa utakuwa na uwezo wa kuzikabili na hivyo hutajiona mtumwa wa hiyo taaluma tofauti na unapolazimishwa kuishi katika ndoto za mtu mwingine hali hii hupelekea mtu kukimbia kazi na kujiona asiefaa.

Anasema kuwa imefikia hatua mtoto wa kike analazimika kuolewa katika umri mdogo  wakati mwingine na mtu asiyempenda na kunyimwa haki yake ya kupata elimu hali inayoonekana kuzorotesha matumaini ya kundi hili na wakati mwingine kujinyima haki ya kuzungumza na kusikilizwa na wengine.

Padre huyu anaweka wazi kuwa mtoto wa kike akipewa nafasi ya kutimiza ndoto zake anaweza akafika mbali zaidi na kumfanya ajitambue na kuifanya kazi ya ndoto zake kwa amani na furaha na kuwapa wengine amani hali anayoiita kuwa ni hitaji la kiroho.

“Mtoto wa kike ana haki sawa na watoto wengine ,hebu tuwaache watimize ndoto zao ili waishi vizuri na kuwapa wengine amani ya moyo hata waweze kufanya mahitaji mengine ya kiroho,”amesema.

Katika hatua nyingine mtetezi wa haki za wanawake  kanda ya kati Bi.Sarah Mwaga anapasha kuwa jamii inapaswa kulazimika kuendana na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia kuwa utu wa mwanamke ni sawa na utu wa mwanaume.

Japokuwa katika imani za kidini mwanaume anatazamwa kwa jicho la tofauti,jamii inapaswa kujua kuwa Mwenyezi Mungu hakumuumba mwanamke ili anyanyasike bali aishi kwa furaha katika nchi aliyotunukiwa na Mungu.

Anazidi kusema kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kujisikia huru hivyo dhana iliyojengeka katika jamii ya kumdharau mwanamke inabidi itokomezwe kwani watoto wote ni sawa wana haki ya kusikilizwa na kutekelezewa matakwa yao.

Pamoja na hayo anasema kuwa yeye binafsi asingepewa nafasi ya kutimiza ndoto zake asingekuwa hapo na kunogesha kuwa aliishi katika ndoto zake tangu akiwa mdogo hali iliyomfanya kutimiza malengo yake kwa urahisi japo kuwa changamoto ndogo ndogo zilikuwepo.

Shujaa huyu wa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake anatoa ushauri kwa mtoto wa kike kuzitumia changamoto zake kuwa fursa ya yeye kujituma kwa bidii na kuyakaribisha mafanikio ya kutimiza ndoto zake na kusema kuwa ni marufuku kukata taama .

“Ni marufuku kwa watoto wa kike kukata tamaa kwani ni dhambi.Mtoto wa kike ahakikishe anatumia changamoto anazokutana nazo na kuzigeuza kuwa fursa kwake ili kuyakaribisha mafanikio ya malengo yake,”amesema Sarah Mwaga.

MWISHOO…

 

(114)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available