KIMATAIFA Maoni TANZANIA

Nini Maana Hasa ya Kufutwa kwa Uchaguzi wa Kenya?

Na. M. M. Mwanakijiji

Endapo Serikali ya Kenya ingefanya haraka haraka, pupa, au figisu figisu ya kumuapisha Uhuru Kenyatta baada ya uchaguzi Mkuu wa Augusti 8 mwaka huu basi wananchi wa Kenya wangeweza kujikuta wanaye Rais ambaye hakuchaguliwa katika uchaguzi uliokuwa huru, wa haki na wenye kuaminika. Maamuzi yaliyotangazwa leo na Mahakama Kuu ya Kenya yanatuambia tu kuwa bado Mahakama ndio njia sahihi Zaidi ya kutafuta haki na kuamua masuala ya uchaguzi kuliko kuingia mitaani.

Wakenya Walitengeneza Mfumo Wao

Kinyume na ilivyo katika Tanzania ambapo matokeo ya Uchaguzi wa Rais yakishatangazwa hadharani basi hayawezi kuhojiwa katika mahakama yoyote, nchini Kenya hali sivyo ilivyo. Kwao – na hii inatokana na masomo mabaya waliyoyapata kwenye uchaguzi wa 2007 na 2012 – wao waliamua kuweka namna ambayo itawapa watu wanaoona kuwa hawakutendewa haki kuweza kuleta ushahidi wao mbele ya chombo huru na hivyo kuondoa ulazima wa kulalamika au hata kukimbilia “kulinda kura”.

Mfumo wao wa uchaguzi hauna tofauti sana na wa kwetu ulivyo kuanzia upigaji kura na ujumlishaji matokeo. Tofauti kubwa iliyopo ni kuwa wenzetu waliamua kuweka namna ambayo uchaguzi unaweza kuhojiwa na hata kubadilitishwa endapo kuna kasoro kubwa ama za mchakato wenyewe au za matokeo yenyewe.

Hili ni somo ambalo siyo Tanzania tu inaweza kujifunza bali nchi nyingi za Kiafrika na nje ya Afrika zinaweza kujifunza. Kama Marekani walivyoweza kuamua uchaguzi wao wakati wa George W. Bush dhidi ya Al Gore kwa kwenda mahakamani leo Wakenya wameamua kuweka hisia zao zinazowagawa pembeni na badala ya kuamua kwenda mahakamani badala ya mitaani; waliamua kuwasha hoja za moto mahakamani kuliko kuchomeana nyumba za majirani zao!

Alama Sahii ya Utawala wa Demokrasia

Mfumo mzuri wa uchaguzi wa kidemokrasia ni ule ambao unaweka mazingira ya aliyeko madarakani kuweza kushindwa na kukubali kushindwa. Mfumo wowote ambao unaoonekana umetengenezwa ili kuhakikisha aliyeko madarakani haondoki hata kwa njia rahisi kabisa ya kujumlisha kura ni mfumo mbaya. Kwa Wakenya mabadiiko yao ya Katiba na sharia za uchaguzi yaliweka mazingira ambayo kama yangefuatwa hadi nukta yake ya mwisho basi mshindi angekuwa anapatikana bila lawama lakini endapo inatokea lawama (kama ilivyo sasa) basi ushindi unahojiwa na ama kuthibitishwa au kutenguliwa.

Na njia nyingine – kama tulivyoweza kujifunza kutoka Kenya – Tume ya Uchaguzi ni lazima uwepo uwezekano wa kushtakiwa endapo inafanya mambo vibaya. Katiba yetu kwa bahati mbaya inapiga marufuku kuishtaki Tume ya Uchaguzi kwa jambo lolote linalofanywa na tume hiyo chini ya Ibara 74(12). Kwa maneno mengine ni kuwa tume hata iboronge vibaya kiasi gani haishtakiki na hivyo inaweza kufanya mambo bila kujali matokeo (with absolute impunity). Kenya wametufundisha jambo zuri.

Raila na Uhuru Wote Mashujaa wa Demokrasia

Uchaguzi huu umetufundisha kuwa pamoja na tofauti zote za kisiasa, pamoja na ukali wote wa maneno, pamoja na uwezo wa kutumia nguvu – ama za umma au za dola – wanasiasa Raila Odinga na Uhuru Kenyatta watabakia katika historia ya Kenya kama kweli ni Mababa wa Demokrasia. Wameonesha kuwa wote wawili wanaweza kutulia na kutuliza vichwa vikali ambavyo labda vingetaka kutumia nguvu kidogo. Raila angeweza kuhamasisha wafuasi wake waende mitaani na kusababisha vurugu kama ya 2007 na Uhuru angeweza kutumia nguvu za dola kuzima upinzani na hata kutaka kuapishwa haraka haraka kama alivyofanyiwa Kibaki (aliyeapishwa usiku pale Ikulu)mwaka 2007.

Demokrasia ni pamoja na kujua kushindwa kwa heshima na neema (defeat in grace and honor). Nina uhakika hata uchaguzi ukirudiwa katika mazingira ya uwazi Zaidi na usahihi Zaidi yeyote kati yao atakuwa tayari kukubali kushindwa na mshindi akashinda vizuri tu.  Na nina uhakika endapo Uhuru atapoteza marudio ya uchaguzi na akakubali atapata heshima kubwa ndani ya taifa lake na historia itamhukumu vizuri Zaidi labda kuliko kiongozi mwingine wa serikali ya Kiafrika katika miaka hii ya siasa za upinzani.

Changamoto Iliyobakia

Kusema ukweli matatizo ya Kenya yangeweza kutatuliwa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa hasa kama kungekuwa na utaratibu huru wa kupata na kutangaza matokeo bila kutegemea Tume peke yake. Tatizo hili tuliliona Tanzania katika uchaguzi wa 2010 na ule wa 2015 ambapo kama Kenya na nchi nyingine bado hatumaini kama watu wengine wanaweza kupewa namba zile zile na wakaweza kuzijumlisha na kupata majibu yale yale labda hata kwa haraka kuliko kwa kusubiri ukiritimba wa Tume ya Uchaguzi.

Vyombo vya habari vinapaswa kuruhusiwa kufuatilia na kupokea matokeo ambayo yametangazwa majimboni na kuyajumlisha mbele ya hadhara na hivyo kuwa na majibu sawasawa. Kwa wanaofahamu kanuni za hesabu ambazo wengi tunajifunza mapema sana shule ya msingi ni kuwa haijalishi mpangilio wa namba za kujumlisha unaweza kuanza na yeyote na majibu bado yakawa yale yale. Hivyo, 2 + 6 + 8 + 5 = 21 ni sawasawa kabisa na 5 + 2 + 6 + 8. Hivyo kama watu wote wanapata namba zile zile kutoka majimbo ya uchaguzi haijalishi wapi unaanzia kujumlisha mwisho wa siku ukijumlisha majimbo yote namba za kura ni lazima ziwe sawasawa. Huu ni ukiritimba wa mwisho unaopaswa kuondolewa Kenya na Tanzania na nchi nyingine ambazo haziamini watu wanajua kujumlisha!

Vyombo vya habari, taasisi binafsi na vyama vya siasa viruhusiwe kujumlisha namba zao kwa kadiri wanavyozipata na hivyo itaweka msukumo kwa tume za uchaguzi kuhakikisha zinajumlisha hesabu sawasawa. Itakuwaje kama taasisi nyingine zote zilizofanya majumlisho kwa uhuru bila kuwasiliana ziweze kupata jumla inayolingana ya kura halafu Tume ije na namba nyingine!?

Wakenya Wako Kumwanya!

Sasa hakuna shaka yoyote kuwa ndugu zetu Wakenya wako juu! Wako juu kwa sababu wameweza kufanya lile ambalo wengi inawezekana walidhania haliwezekani. Wameweza kutuonesha kuwa uchaguzi siyo mwisho, kutangaza matokeo siyo mwisho, na kinachodhaniwa kuwa ni mwisho siyo mwisho. Mwisho ni haki kutamalaki.

Swali kubwa ni je, Tanzania na viongozi wake watakuwa na ujasiri wa kuhakikisha demokrasia inatamalaki? Je, tuna viongozi wenye ujasiri wa kuangalia mfumo wetu na kuutengeneza ili hatimaye na sisi tusije kulazimika kwenda mahakamani au mitaani kutafuta mshindi wa Urais? Je, tunaweza kujifunza namna ya kuendesha uchaguzi ambapo mshindi atapatikana katika mazingira yaliyo huru wazi, na yenye kuaminika?

Swali hili labda linaweza kujibiwa ndani ya miaka hii mitatu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020. Labda na sisi tunaweza kuwa kweli vinara wa demokrasia na viongozi wetu wakatukuzwa kwa kuonesha ukomavu na uthubutu wa kiuongozi.

Kwa sasa Wakenya wamekwepa risasi ya kuweza kuwa na Rais ambaye uchaguzi wake ungeweza kuwa na giza la kuaminika kama kweli alipatikana kihalali au la. Siku sitini zijazo zitatuonesha kama Kenya inaweza kurudia uchaguzi katika mazingira ya ufanisi uwazi, haki, usawa na yenye kuaminika na hivyo kumpata Rais ambaye kweli ataakisi matokeo ya uchaguzi na sauti za wananchi wa Kenya kwa kupitia sanduku la kura.

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com

 

(114)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available