KIMATAIFA TANZANIA

Mugabe Aachia Ngazi: Alikuwa Aondolewe kwa Mashtaka ya Kibunge

Robert Mugabe

Na. M. M. Mwanakijiji

Akijua kuwa wakati wake na zame zake zimefikia kikomo, muda mfupi uliopita Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameandika barua ya kujiuzulu kwa Spika wa Bunge la nchi hiyo ambalo lilikuwa limeanza utaratibu wa kikatiba wa kumuondoa Rais.

Baada ya miaka 37 ya kuiongoza Zimbabwe toka Uhuru Mugabe amejikuta katika shinikizo kubwa la kuachia ngazi hasa baada ya Jeshi kuingilia kati katika Operesheni ya Rejesha ambayo ilikuwa ina lengo la kurudisha utawala wa kikatiba. Uamuzi wa jeshi kuingilia kati na kumuweka kizuizini Mugabe wiki iliyopita ulilenga kuzuia uwezekano wa mke wa Mugabe Bi. Grace Mugabe kuchukua nafasi ya Urais kama urithi kutoka kwa mumewe.

Tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe lilipokelewa kwa shangwe na wabunge waliokuwa wamekutana ili kuanza utaratibu wa kibunge wa kumuondoa Rais baada ya hoja ya mashtaka mbalimbali kuwasilishwa Bungeni. Utaratibu huo (impeachment) kama ungeenda hadi mwisho ungemuondolea mafao mbalimbali Rais huyo na kufungua hata uwezekano wa kuja kushtakiwa. Kujiuzulu kwake kwa hiari kumeacha mwanya kwa Rais Mugabe kuendelea kupata mafao mbalimbali ya Urais.

Wananchi wa Zimbabwe katika miji yake mikubwa mbalimbali ikiwemo Harare na Bulawayo wamelipuka kwa furaha kufuatia Spika kutangaza maamuzi hayo ya Mugabe. Siku mbili tu nyuma (siku ya Jumapili) Mugabe alitarajiwa angejiuzulu lakini baada ya hotuba yake ya kama dakika ishirini hivi alionekana kugomea kuondoka huku akizungumza kuwa anaapanga kusimamia vikao vya chama kusikiliza kwa ukaribu matatizo ya wananchi na ya kuyatafutia suluhisho.

Hadi hivi sasa taarifa za kina  bado zinaendelea kutiririka kuelezea mwelekeo wa kisiasa wa Zimbabwe nchi ambayo ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi, ambapo ukosefu wa ajira ulifikia asilimia 90 na mfumuko wa bei ukiwe kwenye mamilioni ya asilimia.

Bado haijaeleweka sawasawa ni nani anachukua Urais katika kipindi cha mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo. Aliyekuwa Makamu wake wa Rais ambaye alimfukuza wiki chache nyuma na kusababisha jeshi kuingilia kati Bw. Emmerson Mnangagwa anatarajiwa kuwa mgombea wa Urais katika uchaguzi ujao.

(86)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available