KIMATAIFA TANZANIA

Marekani Bado Yaongoza Matumizi ya Kijeshi Duniani

  • Yatenga mara 5 ya bajeti za China, Urusi na Korea Kaskazini Zikijumuishwa
  • Yaongoza kwa Meli za Kubeba Ndege
  • Trump Apanga Kuongeza Bajeti
  • Misri Yaongoza kwa Afrika

Na. M. M. Mwanakijiji

WASHINGTON, DC – Marekani bado inaongoza kwa kutumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha katika kuendesha jeshi lake kuliko nchi nyingine duniani. Marekani ikifuatiwa na Urusi, China, India na Ufaransa (katika tano bora) inatumia zaidi ya dola bilioni 590 kwa mwaka katika kutimiza mahitaji mbalimbali ya jeshi lake. Kiasi hicho pekee ni karibu na sawa na bajeti yote ya Tanzania (kwa fedha za sasa) kwa miaka kumi na mitano!

Fedha ambazo zinatumiwa na jeshi hilo zinatumiwa katika kuboresha zana za kivita, teknolojia na utayari wa kivita na hivyo kulifanya jeshi hilo pamoja na kuwa katika migogoro mbalimbali ya kivita duniani bado likiwa na hazina kubwa ya silaha na wapiganaji. Kinyume na fikra za watu wengi Korea ya Kaskazini inashika namba ya 23 kwa silaha za kivita duniani.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Global Firepower na matokeo yake kutolewa hivi karibuni Marekani inazizidi nchi za Urusi, China na Korea ya Kaskazini mara tano katika kiasi cha fedha zinazotumika. Urusi hutumia dola bilioni 45 wakati China inatumia bilioni 161 kwa mwaka. Hata hivyo, siyo tu fedha zinazotumika ndio kigezo bali pia aina ya silaha na uwezo wa silaha hizo unaangaliwa pamoja na vigezo vingine.

Marekani ina meli za kubeba ndege na helikopta (aircraft carriers) zipatazo 19 wakati China na Urusi zina moja kila mmoja na zinajipanga kuongeza miaka michache ijayo. Uwepo wa meli za aina hiyo unalifanya jeshi kuwa na uwezo wa kutumia ndege zake sehemu nyingine duniani bila kulazimika kutegemea viwanja vilivyoko ardhini na hivyo zinakuwa na uhuru wa kutua na kuondoka bila kutegemea sana uongozi wa ndege wa nchi kavu.

Marekani ina vifaru karibu 600 wakati Urusi ina vifaru vipavyo 20,000 wakati China nayo ina vifaru vipatavyo  6500. Ndege za kivita Marekani (13,700), Urusi (3800), China (3000) na India (2100). LInapokuja suala la askari China ina wapiganaji katika utumishi sasa hivi wapatao milioni 2.3 wakati Urusi ina wapiganaji 760,000, India ikiwa na wapiganaji 1.3. Marekani ina wapiganaji milioni 1.4. Idadi hiyo haijajumuisha askari wa akiba.

Ukijumlisha na idadi ya watu wote wanaoweza kuitwa kutumikia katika jeshi (hawa mara nyingi ni wale wote wenye umri wa miaka 18 kwenda juu ) China ina karibu watu milioni 750, wakati India ina watu milioni 600; Marekani ina watu milioni 150 wanaoweza kuitwa kutumikia jeshi (military manpower).

Hata hivyo, pamoja na uwezo huo mkubwa wa kijeshi bado Marekani haijapata majibu ya vita zinazohusisha mapambano yasiyo ya kimajeshi; ambayo yanahusisha wapiganaji wadogo wadogo na vita vinavyopigwana katikati ya miji (urban warfare). Vita za namna hii ndio zimekuwa zikiisumbua Marekani na hata nchi nyingine zenye majeshi makubwa kwani imeonekana kuwa na matokeo makubwa kama ilivyoonekana huko Fallujah, na Mosul Iraq ambavyo vikosi rasmi vya majeshi vinapambana na wapiganaji wenye itikadi za kidini kama za vikundi vya Daesh maarufu kama ISIS au vile vilivyokuwa vya kiongozi wa kidini Muqtadar al Sadr kutoka mji wa Sadr huko Iraq. Mapambano hayo yanalingana na vita vya msituni (guerilla warfare) kwa namna fulani ambavyo vimetumiwa na baadhi ya nchi za Kiafrika kupambana na vikosi rasmi vya serikali.

Kwa upande wa Afrika Misri inashika nafasi ya kwanza katika matumizi ya kijeshi  ikitumia dola bilioni 4.4 kwa mwaka ikifuatiwa na Algeria ambayo inatumia dola bilioni 10 wakati Ethiopia inafuatia ikitumia dola milioni 340 katika bajeti yake ya ulinzi. Nigeria inafuatia ikitumia dola bilioni 2.3 wakati Afrika ya Kusini inatumia dola 4.6. Ni wazi nchi ambazo zina migogoro ya kivita au zinazokumbana na changamoto mbalimbali za kiusalama ndizo zinajikuta zinatumia fedha nyingi zaidi.

Katika orodha hiyo Tanzania inashika nafasi ya 96 kati ya nchi 126 ikitumia zaidi ya dola milioni 200 kwa mwaka katika bajeti yake ya ulinzi.

(239)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available