KIMATAIFA TANZANIA

Kashfa ya Ngono: Maaskofu 34 wa Chile Waandika Barua za Kujiuzulu

Na. Mwandishi Wetu

ZAMAMPYA – Maaskofu 34 wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Chile wamejiuzulu leo mbele ya Baba Mtakatifu Fransisko jijini Vatican kufuatia kuibuka kwa kashfa ya ngono ambayo maaskofu hao walishindwa kuishughulikia katika majimbo yao mbalimbali. Maaskofu hao walituhumiwa na Papa mwenyewe kuwa walishindwa kushughulikia ipasavyo tuhuma mbalimbali za udhalilishaji wa kingono uliofanywa na makasisi (mapadre) wa Chile kwa miaka mingi ya nyuma na kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha wa jinsi gani baadhi ya maaskofu walijitahidi kuficha au kutoweka uzito unaostahili tuhuma hizo mbalimbali.

Baada ya tuhuma mbalimbali kuibuliwa Baba Mtakatifu Fransisko aliunda timu ya uchunguzi iliyoongozwa na Askofu Mkuu Charles Scilcuna wa Malta na Padre Jordi Bertomeo wa Hispania. Uchunguzi wao hawa ulianzia baada ya tuhuma dhidi ya Askofu Juan Barros wa jimbo la Osorno ambaye aliteuliwa kuongoza jimbo hilo mwaka 2015. Askofu Barros alituhumiwa kuficha matukio ya udhalilishaji wa ngono uliodaiwa kufanywa na Padre Fernando Karadima.

Padre Karadima aliondolewa katika kaza za kichungaji mwaka 2011 baada ya Baraza la Mafundisho na Imani la Papa kumkuta na hatia na hivyo kutaka aondolewe kwenye huduma hiyo mara moja. Maaskofu wengine watatu nao walituhumiwa kujua vitendo vya Padre Karadima lakini walivifumbia macho. Maasofu hao ni Askofu Andrés Arteaga, Tomislav Koljatic na Horacio Valenzuela.

Wakati wa ziara yake nchini Chile mwezi Januari Papa Fransisko mwenyewe alimtetea Askofu Barros akidai kuwa tuhuma dhidi yake zilikuwa hazina ushahidi wa kutosha. Hata hivyo, baada ya kupokea ripoti ya kina ya Askofu Mkuu Scilcuna na Padre Bertomeo Fransisko aliomba radhi kuwa hakuwa na taarifa sahihi wakati ule na kufuatia hilo alitaka kukutana na maaskofu wote pamoja na wahanga wa vitendo hivyo vya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto wadogo.

Baba Mtakatifu aliwaandikia maaskofu wa Chile barua kali akiwatuhumu kujua vitendo hivyo na kujaribu kuficha na hata kuharibu nyaraka mbalimbali za ushahidi pamoja na kuwahamisha mapadre kutoka jimbo moja na shule moja kwenda nyingine ambako huko nako walikuwa bado na nafasi ya kufanya kazi na watoto wadogo.

Baba Mtakatifu Fransisko katika barua yake ameelezea kuwa matatizo mengi ambayo yameonekana kufuatia uchunguzi huo yametokana pamoja na sababu nyingine mafunzo ya seminari ya mapadre ambapo baadhi ya mapadre mashoga walipata nafasi ya kufundisha seminarini na wengine kuanza kuwaharibu waseminari.

Papa amesema kuwa mojawapo ya matatizo ni kuwa maaskofu waliacha kumuweka Yesu kama msingi wa huduma yao na badala yake walijiweka wao kama msingi na hivyo kumpoteza Yesu kama msingi wa huduma yao ya kinabii. Papa amesema kuwa haitoshi tu kuwaondoa watu kwenye nafasi zao bali ni lazima kwenda mbali na ndani zaidi kuweza kupata mzizi wa matatizo haya. “Itakuwa ni makosa makubwa kudhania kuwa kuwaondoa watu tu kwenye nafasi zao bila kukigusa chanzo kutaondoa matatizo haya; itakuwa ni kujiongopea” amesema Fransisko katika barua yake iliyorushwa na kituo cha TV13 cha Chile Mei 17.

Maaskofu hawa 34 wote waliwasilisha barua zao za kujiuzulu mmoja mmoja mbele ya Papa Fransisko na wote wanasubiri kama Baba Mtakatifu atakubali kujiuzulu kwao mara moja tena kwa pamoja au atafanya kwa kupitia mmoja mmoja au mpaka atakapoteua maakofu wapya.

(107)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available