Ferdinand Phillips

Wajibu wa Makampuni kwa Jamii Wanapofanyia Kazi (Corporate Social Responsibility)

Na F.M Philip

Maendeleo ni jambo ambalo kila jamii inahitaji.Neno maendeleo kwa maana iliyo rahisi sana ni kitendo cha kutoka katika hatua moja kimaisha na kwenda kwenye hatua nyingine iliyo bora zaidi ya hatua iliyopita.Hii ni maana inayotumika sana katika kujadili maendeleo ya mtu mmoja mmoja katika jamii yetu au zetu kwa ujumla.

Kwa maana pana hasa pale tunapozungumzia au kulitazama neno maendeleo katika mtazamo wa jamii au jumia au nchi kwa ujumla, tunalihusisha neno hilo na upatikanaji wa huduma bora za jamii kama huduma bora za afya, miuondombinu bora ya barabara, umeme, maji, elimu bora, uwepo wa mazingira bora ya kuishi kwenye jamii,na kadhalika .Kwa ufupi tu sawa na kusema kwamba palipo na maendeleo, mfumo wa maisha katika jamii hiyo huwa umerahisishwa na kila huduma hupatikana kwa rahisi na haraka bila mikingamo yoyote.

Hivi tunavyozungumza Tanzania ni nchi inayoendelea, ni nchi yenye dira ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kwa maana nyingine ndoto ya Tanzania na watanzania wote ni kuona wanaishi katika nchi ambayo maisha yake yamewekwa katika mizania ya kuwa imeendelea.Tanzania inakuwa na matazamio ya kuwa nchi ya uchumi wa kati(2nd World Country) kwa kuwa inategemea sana uwekezaji katika sekta ya viwanda vikubwa na vidogo, uwekezaji katika uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia na mafuta, madini, biashara ya utalii na uwekezaji mwingine katika maeneo ya utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi.

Serekali ya awamu ya tano chini ya Mh Rais John Pombe Magufuli, imekuja na kauli yake ya “Hapa Kazi Tu” kama inavyoeleweka, lengo kuu ni  kuwahimiza watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla, lengo likiwa ni kufanya Tanzania kufikia kuwa nchi ya uchumi wa kati kama dira ya 2025 inavyoelekeza, na kama Mh rais alivyosisitiza katika kampeni zake wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi kwamba serekali yake itakuwa ni serekali ya viwanda.Kwa maana nyingine serekali hii itajikita sana katika uwekezaji wa viwanda, hivyo sisi kama watanzania tunatarajia uwepo ama ongezeko kubwa la uwekezaji kupitia makampuni mbali mbali ya ndani na nje ya nchi, na hapo ndipo hoja ya makampuni hayo kurejesha kiasi cha faida kitakachopatikana kutokana na uwekezaji wao katika ardhi ya Tanzania yetu kwa watanzania wenye ardhi yao inapopata nguvu kwa sasa.

WAJIBU WA MAKAMPUNI KATIKA JAMII (CORPORATE SOCIAL RESPONSIBILITY)

Falsafa ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii(Corporate Social Responsibility) ni  falsafa ambayo imekuwepo kwa miaka mingi sana katika  jamii ya mwanadamu, ni kwa zaidi ya miaka 4000 sasa. Msingi mkuu wa falsafa ama dhana hii ni kwamba mashirika ama makampuni  yanapaswa kuwajibika zaidi ya malemgo yake  ya kupata au kukuza faida katika biashara za mashirika hayo.Mfano mzuri upo katika sheria za kibiashara  za kiislam( Islamic law of Contracts and Business Transactions)  kwamba ni kinyume na ubinadamu au utu  kutoza riba iliyopitiliza katika mikopo.

Kwa takribani miongo miwili iliyopita, falsafa hii imeshika kasi zaidi kujadililwa kulinganisha na vipindi vingine hasa katika jamii ya biashara. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa sana na kuongezeka kwa muingiliano kati ya serekali, biashara na jamii kwa ujumla. Katika miaka ya nyuma biasharana mashirika ya kibishara kwa ujumla,  yalikuwa yanahusika zaidi na matokeo ya kiuchumi(faida) katika maamuzi ya wenye mashirika hayo, hata hivyo, mazingira na mabaliko yaliyotokea katika mfumo wa maisha yetu hasa kizazi cha leo kinachohubiri masuala ya uwajibikaji na haki za binadamu, inasisititizwa kwamba, biashara haina budi kuakisi pia masuala ya kisheria, nidhamu ya bishara kwa jamii inayozunguka, utu na masuala ya kijamii katika uendeshaji wake.

Suala la  makampuni kuwajibika katika jamii (Corporate Social Responsibility) limekuwa likipigiwa kelele na wanazuoni wataalam na wa masuala ya biashara, sheria, uchumi na wanaharakati wa haki za binadamu kwa ujumla .Falsafa hii ilishika kasi sana mnamo mwaka 1953 pale mwanazuoni  wa kimarekani  Howard Bowen alipotoa andiko lake aliloliitaWajibu wa mfanyabiashara kwa Jamii(Social Responsibility of a Businessman)”  juu ya falsafa hii, maudhui makubwa ya mwandishi huyu katika andiko lake hili  ni kwamba maamuzi ya mashirika yafuate misingi na makubaliano yaliyo na faida kwa jamii yetu.

Hoja kubwa hapa ikiwa imejikita katika masuala ya kibiashara na ustawi wa jamii (business and social welfare) kwamba kama kampuni inafanya biashara katika eneo flani basi iwajibike kusaidia kwa namna moja ama nyingine kuiendeleza jamii ya eneo ambalo kampuni hiyo inafanyia shughuli zake,  katika kusaidia upatikanaji wa huduma za msingi za jamii na kuheshimu pamoja na kuendeleza  uwepo wa haki za msingi za binadamu, msingi wa hoja hii ni kwamba ustawi na ukuaji wa kampuni hiyo kwa ujumla au kwa kiwango flani unategemea sana ustawi wa hiyo jamii inayozunguka eneo la kibiashara la kampuni hiyo. Wanazuoni wengine wamekuwa wakidai kwamba, chini ya mwamvuli wa haki za binabadamu, jamii inayohaki ya kunufaika na faida inayopatikana katika biashara ama shughuli za makampuni yaliyopo kwenye maeneo yanayozunguka jamii hiyo kwa kuwa wanajamii ni washika dau(stake holders) katika uwekezaji wowote wa kampuni husika katika eneo lao.Je tunaposema uwajibikaji wa makampuni kwa jamii(Corporate Social responsibility) maana yake ni nini? na kwa nini nasisitiza kwamba maendeleo ya mtanzania wa zama hizi za Kazi tu na serekali ya viwanda yanategemea sana falsafa hii  ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii?

Uwajibikaji wa makampuni katika jamii ni kile kitendo cha kampuni kufanya maamuzi kwa hiyari yake yenyewe kuchangia katika maendeleo ya jamii na masuala mazima ya mazingira, kwamba jambo hili linahusiana na mambo machanganyiko yahusuyo utunzani wa mazingira, utawala wa rasilimali watu kwenye kampuni, masuala ya afya na usalama mahala pa kazi,mahusiano na jamii zinazozunguka kampuni yenyewe pamoja na mahusiano kati ya kampuni wasambazi wa bidhaa za kampuni hiyo pamoja na walaji(consumers) wa bidhaa za za kampuni husika. Maana hii inatumiwa sana ulaya na imetolewa na Jumuiya ya Ulaya (European Commission 2001).Wengine wanaeleza kwamba kampuni kuwajibika kwa jamii ni kitendo cha kampuni kuwa na utashi endelevu katika kuheshimu  maadili ya  biashara na kuchangia kwenye maendeleo ya kiuchumi huku ikisaidia katika kuboresha maisha ya watu, kuboresha hali ya waajiriwa wa kampuni hiyo na familia zao na pia jamii inayoizunguka kampuni hiyo, maana hii ni kwa mujibu wa shirika la bishara biashara kwa maendeleo endelevu duniani(World Busness Council for Sustainable Development). Wanazuoni kama Khuory na wengine(Khoury et al, 1999), wanaeleza kwamba kampuni kuwajibika kwa jamii ni mkusanyiko wa mahusiano ya kampuni ama shirika na washika dau wake, hii inajumuisha wateja waaajiriwa, jumuia(communities), wamiliki wa kampuni na wawekezaji katika kampuni hiyo kwa ujumla, serekali, wasambazaji na washindani wa kibiashara wa kampuni husika. Wanazuoni hawa wanasema, vigezo vya kampuni kuwajibika kwa jamii vinapimwa kwa uwekezaji ambao kampuni hiyo inaufanya kwa jamii inayoizunguka, wafanyakazi wake(employees), utunzani wa mazingira nakadhalika.

Kwa ujumla, falsafa ya uwajibakaji wa makapuni kwa jamii(corporate social responsibility) inabeba maana nyingi na tofauti tofauti kulingana na watu , vitu na mahali ambapo dhana  hiyo inatumika au kutumiwa.Licha ya kuwepo kwa tofauti hizo za jinsi falsafa ya  uwajibikaji wa makampuni kwa jamii inavyoelezewa, maana zote zilizopo katika kuielezea falsafa hii, zinakubaliana katika imani moja kwamba makampuni yanawajibika kuutendea umma yale yaliyo mazuri na bora kwa maendeleo ya watu wa umma huo.Katika dunia yetu ya leo, dunia ya kisasa, inasisitizwa sana kwamba makampuni yawajibike kwa jamii kwa hiari kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa jamii inayozunguka makampuni hayo, kuwekeza katika miradi ya uhifandhi na utanzaji mazingira hasa kwa maeneo ya viwanda, mahusiano bora kwa washika dau wa makampuni hayo na mengineyo yaliyo na faida kwa jamii kwa ujumla wake.Kwa nini tuhahitaji falsafa hii  kufanya kazi kikamilifu kwenye Tanzania yetu ya leo?

Mabadiliko yaliyofanywa na Tanzania katika miaka ya 1980 na kuendelea mpaka leo hii, katika sera za uchumi wa Taifa hili, kwa kuleta suala la uchumi huria na kupunguza udhibiti wa serekali katika uchumi wa nchi ndio msingi wa kuzaliwa kwa dhana ama falsafa hii ya makampuni kuwajibika kwa jamii hapa nchini. Shughuli za kimaendeleo ambazo kiutamaduni zilikuwa zikifanywa na serekali mfano utoaji wa miundombinu ya msingi, utoaji na usambazaji wa huduma  za afya , elimu, maji, umeme na kadhalika, yote haya yamekasimiwa kwa sekta binafsi na asasi za kiraia pamoja na waendeshaji wa uchumi wa soko(market actors) baada ya mabadiliko hayo ya sera za kiuchumi kufanywa na serekali hapa nchini.Sekta binafsi imekuwa ndio mwajiri, mtoa huduma, mwekezaji na ndio wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi zinazoendelea, sera za kiuchumi katika nchi zinaziendelea ikiwemo Tanzania zinaitazama sekta binafsi kuwa kama kitovu cha uchumi katika kuondoa umaskini na ndipo msingi wa makampuni kuwajibika kwa jamii ya kitanzania unapopatikana katika Tanzania ya leo.Je serekali na mamlaka za Tanzania zifanye nini kuhakikisha kuwa falsafa  hii ya makampuni kuwajibika kwa jamii inawanufaisha wananchi?

Kwanza kabisa, Tanzania kama nchi inapaswa kutengeneza na kuiweka wazi sera yake ya makampuni(Corporate Policy) , kwa sasa Tanzania inatumia sana sera ya madini ya mwaka 2010 na sera ya Uwekezaji ya mwaka 1997 katika utekelezaji wa falsafa hii, hakuna sera madhubuti ya makampuni. Sera hii iitambue dhana hii na ionyeshe umuhimu wa utekelezwaji wa dhana hii kwa vitendo na makampuni yote nchi mwetu. Katika sera hii Tanzania ionyeshe moja kwa moja kwamba katika kuitekeleza falsafa hii ya makampuni kuwajibika kwa jamii, inafuata mlengo au mtazamo gani kati ya ile iliyopo kwa sasa.

Kimsingi dhana ya makampuni kuwajibika kwa jamii imebeba mitazamo au milengo  miwili ndani yake ambayo ndiyo inayoshindana kwenye kuitekeleza falsafa hii kikamilifu. Mtazamo wa kwanza ni ule unaojali faida zaidi kwa makampuni kuliko mengine(Profit maximization or the classical persepective on Corporate Social Responsibility), Wanaoiamini falsafa hii katika mlengo tajwa hapo juu, wanasema kwamba, kampuni inapaswa kuwekeza malengo yake na mipango yake yote katika kupata faida kwanza, ilimradi tu inafuata sheria zilizopo zinazoongoza uendeshaji wa makampuni katika nchi husika,hivyo makampuni yasibanwe na hoja zingine nje ya hilo la kutengeneza faida kwa wanahisa wake na kulipa kodi kwa serekali basi, huo ndio wajibu wa makampuni katika mtizamo huo wa faida zaidi kuliko mengine.mtizamo mwingine ni ule wa kijamii yaani (Social or the Stakeholder’s view), kwamba licha ya kupata faida, kampuni inapaswa irejeshe sehemu ya faida hiyo kwa jamii kama mdau wa mafanikio ya kampuni husika.

Faida hiyo itumike katika kuendeleza jamii katika nyanja mbali mbali, mfano kutoa ajira kwa wananchi, kusaidia katika miradi ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, kutoa huduma za jamii kama , elimu, maji, afya n.k, kwa kuanzisha miradi ya maendeleo katika eno ambalo uwekezaji wa kampuni hiyo unafanyika, kutoa fidia stahiki kwa wananchi wanaoumizwa na matendo ya kampuni katika uendeshaji wa shughuli zake, kampuni kujali walaji na watumiaji wa bidhaa zake kwa kuhakikisha zipo salama na katika ubora unatakiwa na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo. Kwa mtazamo wangu, naimba serekali ifuate mtizamo wa kijamii au wa washika dau(stake holder’s view) na kuufanya uwe ndio mlengo rasmi katika nchi yetu pale ambapo suala la muwajibikaji wa makampuni kijamii linapokuwepo. Faida kubwa juu ya mtazamo huu wa kijamii ukirasimishwa na kuwekwa katika sera ya makampuni, utazilazimisha kampuni zinazowekeza katika sekta yoyote nchini kutenga sehemu ya faida yao  kwa mwaka na kuirejesha kwa wananchi katika mfumo mwingine wa uwekezaji, yaani kuiwekeza faida hiyo katika miaradi ya kusaidia jamii inayozunguka eneo kampuni ilipowekeza.

Pili, pamoja na sera, serekali inahitaji kuwa na sheria rasmi juu ya jambo hili la makampuni kuwajibika kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii, india imefanikiwa kutengeza sgeria ya namana hii na ndio nchi ya kwanza duniani kufanya hivyo hadi sasa.Sheria hii itengezwe katika mfumo utakaolazimisha makampuni kutengeneza miradi ya maendeleo inayotokana na faida iliyowekezwa kwa jamii.  Miradi hii isimamiwe na pia iratibiwe na mamlaka za serekali kwa kushirikiana na asasi za kirai na wawekezaji husikaa kwenye eneo katika maeneo ambayo miradi hii itakuwepo.  Hivi sasa Tanzania haina sheria wala sera maalumu kwa ajili ya jambo hili  la makampuni kuwajibika kwa jamii, japo sera ya madini ya mwaka 2010, inatamka kwamba “Serekali itayataka makampuni ya madini kujihusisha na kutekeleza sera madhubuti za kuwajibika kwa jamii ama kuchochea makampuni ya madini kuhusisha jamii zinazozunguka katika kuweka vipaumbele kwenye miradi ya maendeleo na mambo ya kijamii wakati wa uhai wa uwekezaji wao”. Licha ya kuwepo muongozo huu kwenye sera hii ya madini na pia miongozo inayofanana na hiyo kwenye sera ya uwekezaji ya mwaka 1997, bado Tanzania haijanufaika na yaliyomo kwenye sera hizi kuhusu uwajibikaji wa makampuni kwa jamii kwa kuwa hakuna sheria maalumu juu ya jambo hili, makampuni yanaendesha mambo yao hasa kwenye suala hili  la uwajibikaji kwa jamii kwa kuzingatia sheria mbali mbali,ikiwepo Sheria ya Makampuni Na. 212/2002, Sheria ya Uhifadhi wa Mazingira Na 20/2004, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 kuhusu masuala ya ajira na mahusiano kazini, sheria ya Ushindani Na. 345, marejeo ya 2002, Sheria ya mauzo ya Bidhaa(Sales of Goods Act) Na. 214 marejeo ya 2002, sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, na sheria nyingine zinazohusiana na uwekezaji, biashara na mikataba, Sheria ya haki za msingi za mwanadamu(The Basic Rights and Duties Enforcement Act)  Na. 3/1994  na sheria zinginezo zinazohusu masuala yanayoendena na uwekezaji na haki za binadamu.Sheria hizi kimsingi zinamapungufu mengi kuhusiana na haki za jamii katika uwekezaji wa makampuni, na zinatoa uwanja mpana sana kwa makampuni kufanya yanavyotaka, na hivyo kuwakosesha wananchi fursa za kimaendeleo, hatimaye zinazusha migogoro mingi sana katika maeneo ya uwekezaji kati ya wananchi na wawekezaji, mfano mzuri ni mgogoro wa katika eneo la mgodi wa Nyamongo huko mkoani Mara.Hivyo ili jamii inufaike na uwekezaji kwenye eneo lake Tanzania inahitaji sheria hii itakayosaidia jamii kupata haki ya gawio la sehemu ya faida kwa lazima kutoka katika makampuni husika.Sheria hii ni mhuhimu sana ili kuondoa migogoro iliyopo katika maeneo ya uwekezaji kutokana na ahadi hewa ambazo wananchi wa maeneo hayo wanapewa na wawekezaji hasa wa kigeni pale wanapotaka kuwekeza kwenye maeneo yao, hii imethibitishwa na taarifa ya kiutafiti kuhusu Biashara na Haki za Binadamu inchi Tanzania iliyotolewa mwaka 2013 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LAHRC), ambapo tarifa hiyo iliweka wazi kwamba ahadi nyingi za wawekezaji kuhusu kusaidia jamii kutokana na uwekezaji wao hazitekelezwi.

Tatu, tunahitaji kuwa na mfumo mzuri na madhubuti wa usimamizi wa sheria(Proper Law enforcement mechanisim), kwa sasa sekta ya sheria na mfumo wa mahakama na usimamizi wa sheria nchini Tanzania upo dhaifu sana, sheria nyingi tulizonanzo haziakisi hali halisi ya matakwa na maisha ya mtanzania wa leo, mfano mdogo upo kwenye Katiba yetu amabapo bado Tanzania inatambulika kama nchi ya kijamaa wakati hali halisi ya maisha ya watanznia sio ujamaa, bali ni mfumo mwingine na ni serekali yenyewe imeuasisi mfumo huu ambao ni wa kibepari kupitia soko huria.Hivi karibuni, waziri wa Sheria na Katiba Dr. Harrison Mwakyembe alinukuliwa akisema kwamba sekta ya sheria inakabiliwa na changamoto nyingi ila kubwa kuliko zote ni “RUSHWA”. Ili sheria hii ifanye kazi tunahitaji mfumo madhubuti wa usimamizi wa wa sheria ili kuyabana ipasavyo makampuni na pia kuhakikisha miradi inayoanzishwa inakuwa ni kwa faida ya walengwa na watakaouhusika na ubadhirifu katika miradi hii kwa namna moja au nyingine basi sheria ichukue mkondo wake kwa kuwawajibisha mara moja.

Serekali pia ili kufanikisha wananchi wanufaike na falsafa hii ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii, inapaswa kuwekeza sana katika elimu ya uraia, hasa maswala ya haki za binadamu na wajibu wa raia kwa nchi yao.Tafiti zinaonyesha kwamba, nchi zilizoendelea kama nchi za Ulaya na Amerika, wananchi wanamwamko sana na haki zao na hivyo falsafa hii imewasaidia sana katika kuyabana makampuni kutimiza wajibu wao hasa kaika masuala ya uhifadhi wa mazingira, haki za wafanya kazi katika maeneo ya kazi , kwa kupigania masalahi bora na hali nzuri ya mazingira ya kazi. Bila wananchi kuzitambua na kuzipigania haki zao bila hofu ni kazi bure, tutaendelea kusikia migomo viwandani na maeneo mengine ya kazi hivyo uzalishaji na biashara kwa ujumla kwa wawekezaji kuwa ngumu na hilo litafanya wao kupata faida kidogo na kutoirejsha kwenye jamii kwa kisingizio cha kuwa hawakupata faida.

Kwa ujumla, falsafa hii ya makampuni kuwajibika kwa jamii ni falsafa pana na inabeba mambo mengi sana, neno kampuni ama shirika kisheria linamaana pana, hata serekali yenyewe nayo na taasisi zake inakuwa sehemu ya maana hiyo maana ni “legal entity”, hivyo jambo hili halizungumziwi kwa upande mmoja tu kwamba ni kwa makampuni ua mashirika ya watu binafsi, bali jambo hili lipo hata kwenye mashirika ya kiserekali, asasi za kiraia, na kila taasisi ambayo inafanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi na imesajiriwa kisheria hapa nchini. Suala hili linaeleweka zaidi kama litatazamwa katika nyanja za haki za binandamu na utawala bora maana falsafa hii matokeo yake yapo katika kuwapatia wananchi haki zao katika jamii zao kwa ujumla. Kila mwananchi mategemeo yake ni maisha bora na ni haki yake ya msingi kabisa kuwa na tegemeo hilo halali kwa nchi yake.

Falasafa hii imekuja kulinda mategemeo ya wananchi na kuleta usawa kwa watu, kupunguza pengo kati ya wenyenancho(wamiliki wa makampuni na wafanya biashara kwa ujumla) na wasio nancho amabao ni wananchi wa kawaidia.Rai yangu kwa serekali ya awamu ya tano kwamba, iiitazame vyema falsafa hii na kuifanyia kazi hasa kwa kubana makampuni ya kibiashara ili yaisaidie serekali katika kufikia malelngo yake kwa kuwaendeleza wananchi kuliko hali ilivyo sasa ambapo uwekezaji kwa kiasi kikubwa haumnufaishi mwananchi wa kawaida katika taifa letu.Faida kubwa itakayopata serekali katika hili ni kupunguza utegemezi wa wananchi  kwa serekekali katika kubuni na kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao, na pia utegemezi wa serekali kwa wafadhili utapungua, amani itadumishwa kwani dhana hii ikisimamiwa vyema, itaondoa sana migogoro katika sehemu za kazi, migorogoro katika maeneo ya uwekezaji na itakuza mahusuano mema kati ya wananchi na wawekezaji, hivyo kuchochea maendeleo ya biashara nchini na pia kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Tanzania.

(120)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available