Dhima, Maono na Maadili ya Gazeti la Zama Mpya (GZM)

KANUNI ZINAZOTUONGOZA

Gazeti la Zama Mpya (GZM) katika msingi wake kabisa ni chombo cha kupasha habari. Hivyo, vyote ambavyo vitachapishwa iwe kwenye kurasa za gazeti, kwenye mitandao au kwa namna nyingine yoyote ni lazima kiwe kinachoendana na hadhi na maadili ambayo yanafanya chombo hiki kiendelee kuaminiwa. Kanuni hizi zina lengo za kuhakikisha kuwa sisi ambao tunawapa wananchi taarifa wenyewe ni lazima tuwe na msimamo wa kuweza kuaminika hasa tunapowasimamia wale wanaowahudumia wananchi katika nafasi zao mbalimbali.

NANI ANAHUSIKA

Kanuni hizi zinawahusu waandishi wetu wote wa vyombo vyetu vya habari vinavyomilikiwa na OZ Company. Hii ni pamoja na waandishi wa magazeti, wa radio, wa Televisheni na mitandaoni. Hii ni pamoja na waandishi huru (freelance) wanaochangia kwenye vyombo hivyo. Hii pia inawahusu waandishi na vyombo au vyanzo vingine vya habari ambavyo vingependa habari zao zitotolewe au kurushwa na vyombo vyetu vya habari. Wote hawa ni muhimu wasome na kuelewa kanuni hizi.

 1. USAHIHI (ACCURACY)

Lengo letu ni kuutafuta ukweli na kuupata popote ulipo. Hivyo, kuthibitisha (verification) madai mbalimbali ni jambo la msingi kwa kila mwandishi wetu. Hatupokei neno kwa sababu limetolewa na mtu mwenye madaraka tu bali tunataka kupata ushahidi wa hilo. Usahihi huu upo katika:

 • Kuripoti habari
 • Usahihi katika kutumia vyanzo na taarifa kutoka nje ya GZM
 • Kuwa sahihi katika kuripoti kwenye mitandao
 • Kuwa sahihi katika kutumia picha na video

 

 1. BILA UPENDELEO (FAIRNESS)

Kutoa habari bila upendeleo wa aina yeyote kwa kadiri ya uwezo wetu wote. Ili kufanya hivyo tutajitahidi kupata taarifa za pande zote muhimu katika habari hasa kwa wale ambao wanatajwa katika habari kwa mwanga mbaya au wanaokosolewa. Katika habari ambazo zina uzito mkubwa ni jukumu letu kuhakikisha kuwa taarifa zote muhimu na nzito zinapatikana. Hatutoi taarifa hata nzito kiasi gani bila kutoa nafasi kusikia maoni mengine ambayo yanaweza kuwa na uzito unaostahili kuwemo kwenye habari.

 • Hivyo, tutakuwa chombo kisicho na upendeleo:
 • Katika kutoa habari
 • Katika kutafuta na kuhoji wahusika mbalimbali
 • Kwa waandishi wengine
 • Matumizi sahihi ya vyanzo na habari mbalimbali

 

 1. UKAMILIFU (COMPLETENESS)

Tutatoa na kutaarifa habari kwa umma kwa ukamilifu wake wote unaowezekana. Hii ina maana kuwa pamoja na kuwa na taarifa nyingi ambazo tunaweza kuzitumia; tutatumia zile ambazo kwa kiasi kikubwa kabisa zinaweza kuelezea habari kwa ukamilifu wake wote (completeness). Hivyo, tutajitahidi kutoa taarifa kamilifu katika

 • Kuripoti matukio na habari
 • Katika mahojiano

 

 1. KUSEMA UKWELI (HONESTY)

Tutajitahidi kuhakikisha kuwa kile tunachoripoti tunakiripoti kwa ukweli bila kuweka uongo au kuongeza chumvi. Tutasema vyanzo vyetu vya habari na nukuu zetu mbalimbali. Isipokuwa katika mazingira ambayo maisha ya waandishi wetu au vyanzo vyetu vinaweza kuwa hatarini basi tutaficha baadhi ya taarifa na hilo wasomaji na wasikilizaji wetu wataambiwa na kwanini tumefanya hivyo. Tunakwepa kuweka vichwa vya habari vya kusisimua au vyenye kulaghai wakati taarifa ya ndani haiendani na vichwa hivyo vya habari. Hivyo tutasema ukweli:

 • Kwenye kuripoti habari mbalimbali kwenye vyombo vyetu vya habari popote
 • Katika kutambulisha vyanzo vyetu vya habari
 • Katika kufanya mahojianona watu mbalimbali
 • Katika kutumia taarifa na vielelezo mbalimbali

 

 1. KUWA HURU (INDEPENDENT)

Ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa chombo huru cha habari kinachoaminika na umma ni lazima kuhakikisha kuwa tunaondoa uwepo au mwonekano wa uwepo wa mgongano wa kimaslahi kati ya waandishi wetu na habari wanazoziripoti. Ni muhimu kuzingatia kuwa jukumu letu kubwa kabisa ni kwa umma na hivyo ni maslahi yao tu ndiyo yanatuongoza katika kutafuta na kutoa habari.

Kuepusha mgongano huu tutahakikisha kuwa waandishi wetu – hadi kwa wenza na familia zao wa karibu – hawawi sehemu ya mgongano wa maslahi katika habari na wakati wowote hilo linapotokea basi tunajitoa katika kuandika habari hiyo. Hivyo ili kuhakikisha uhuru wetu kama chombo cha habari katika taifa linalojaribu kujenga demokrasia tutahakikisha tunakuwa huru katika:

 • Kuondoa uwepo au mwonekano wa migongano ya kimaslahi
 • Mahusiano yetu na wafadhili au wanaotangaza kupitia vyombo vyetu vya habari
 • Kuamua ajenda yetu ya uandishi bila kushawishiwa na mtu au chombo cha nje
 • Kulipia gharama zetu – kutolipiwa au lipwa na wale tunaofuatilia habari zao
 • Kutopokea matangazo ya biashara toka taasisi za serikali isipokuwa kama sehemu ya huduma kwa umma (public service)
 • Zawadi zozote ambazo mwandishi amezipokea ni lazima azitangaze kwenye fomu maalum nakuhakikisha kuwa zawadi hiyo si jaribio la kununua uandishi wake au namna ya kuripoti habari fulani. Kutotangaza zawadi hizi ni kosa linalofukuzisha kazi mara moja.

 

 1. KUTOKUWA NA UPANDE (IMPARTIALITY)

Ili kuweza kuaminika na kuwa chombo huru kweli cha habari tunalazimika kuripoti habari zetu bila kuwa na upande isipokuwa ule wa haki, wenye kupinga ufisadi na unaosukumiza yale ambayo tunaamini ni mabadiliko yenye manufaa kwa wananchi na Taifa letu. Pamoja na hilo tunalazimika kujitahidi wakati wote kutoa habari na kuripoti habari bila kuchagua upande. Misimamo yetu ya upande yenye kuakisi msimamo wa kihariri wa gazeti itawekwa bayana kwenye tahariri ya gazeti.

 

 1. UWAZI (TRANSPARENCY)

Ili tuweze na kuendelea kuaminika tutaendesha utendaji wetu wa kuripoti habari kwa uwazi wote unaostahili. Katika kutimiza hili tutahakikisha kuwa wananchi na umma kwa ujumla unapata taarifa zote ambazo ni muhimu na ambazo zimechangia katika kuripoti habari husika. Uwazi huu utahusika katika:

 • Kufanya maamuzi mbalimbali ya kihariri
 • Kulinda vyanzo fulani vya habari – hakuna habari ambayo itachapishwa ikiwa na madai mazito lakini ikiwa na chanzo kimoja tu isipokuwa kama kuna ushahidi wa kutosha wa habari hiyo kupitia chanzo hicho
 • Vyanzo visivyotajwa vitaepukwa kwa kadiri inavyowezekana isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo na upo ushahidi wa kutosha wa habari hiyo kuaminika. Hata katika mazingira hayo vyanzo hivyo vitatajwa kwa kadiri inavyowezekana uhusiano wao na habari yenyewe.

 

 1. KUPUNGUZA MADHARA (MINIMIZING HARM)

Mara nyingi taarifa za habari zinaweza kusababisha madhara kwa wahusika mbalimbali – iwe ya kisaikolojia, kazi, maisha au vinginevyo. Kutokana na ukweli huu taarifa zetu zitahakikisha kuwa zinajitahidi kwa kadiri ziwezavyo kupunguza madhara kwa vyanzo vyetu na wale ambao wanatajwa katika habari mbalimbali. Kutokana na hilo, ili kupunguza madhara:

 • Tutatumia lugha inayokubalika kutambulisha makundi mbalimbali; hii ni pamoja na kutumia lugha ya staha yenye kuheshimu utu wa mtu. Hii inahusisha pia lugha katika masuala ya ngono, utupu, matumizi ya nguvu, vifo n.k
 • Hatutataja rangi, kabila, dini ya mtu kama namna ya kumtambulisha isipokuwa kama vitu hivyo vinahusiana na habari husika
 • Mahali ambapo chanzo cha habari kinaweza kikawa sehemu ya mjadala tutahakikisha chanzo hicho kinaelewa matokeo ya taarifa yake kutumika na awe tayari kutoa ruhusa yake kutumiwa kwa habari hiyo (informed consent)
 • Tutalinda watoto wanapokuwa sehemu ya habari kwa kuhakikisha kuwa picha zao zinatumika kwa staha, kutowataja katika habari zinazohusu ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia na hatutatumia picha ambazo zinawaweka watoto katika hali ya masuala ya kingono. Mara zote tutawasiliana na wazazi au walezi kabla ya kuzungumza na watoto ili kupata kibali na wazazi/walezi hao watakuwa sehemu ya mazungumzo na mtoto yeyote.

 

 1. UTAFUTAJI NA UPATAJI HABARI (METHODS OF NEWS GATHERING)

Katika kutafuta na kupata habari tutatumia njia za wazi, bila ulaghai na zenye kuweka wazi waandishi wetu kama waandishi wa habari. Katika kutafuta na kupata habari hizi tutahakikisha kuwa tunakuwa wa wazi isipokuwa pale ambapo kwa sababu ya maslahi makubwa kabisa ya umma kupata habari hiyo haiwezekani kwa njia hii. Kutafuta habari kwa njia nyingine yeyote kunahitaji kibali cha Mhariri Mtendaji. Pamoja na hayo:

 • Tutajitambulisha mara zote tunapoenda kutafuta habari kuwa ni waandishi wa habari na si vinginevyo
 • Waandishi ni lazima waheshimu sheria husika katika kutafuta habari
 • Inapotokea mwandishi wa habari anapewa habari ‘off the record’ ni lazima apima na kuona umuhimu wa kulinda chanzo hicho na makubaliano hayo yanamfunga mwandishi huyo na chombo hiki cha habari kutomtaja mhusika
 • Hatulipi ili kupata habari
 • Haturuhusu vyanzo vya habari kupitia habari zetu kabla ya kuziweka mbele ya umma katika vyombo vyetu vya habari
 • Tutatunza kumbukumbu za mazungumzo na mahojiano yetu na vyanzo mbalimbali kwa ajili ya rekodi

 

 1. KUWAJIBIKA (ACCOUNTABILITY)

Pamoja na kuwa katika uandishi wetu tunataka watu wawajibike sisi wenyewe vile vile tunapaswa kuwajibika. Hivyo, ili kuhakikisha kuwa tunawajibika na tunaweza kuwajibishwa:

Tutafanya masahihisho ya makosa yeyote ambayo tutayaona na mara moja. Makosa ya taarifa kwenye mtandao yatasahihishwa kwa kuongeza taarifa katika habari kuwa imefanyiwa masahihisho na ni masahihisho gani

Kwenye makosa ya mambo yanayofahamika na kukubalika gazeti litatoa nafasi ya kusahihisha, kutoa nafasi ya jibu kamili au kuomba radhi inapobidi.

 

 1. UBORA (EXCELLENCE)

Katika kazi zetu zote tunatarajia kuandaa taarifa katika ubora wa hali ya juu kabisa ambao unapita vyombo vingine vyote vya habari. Hii ni katika uandishi, matumizi ya picha, michoro, sauti na video na katika masimulizi.

Hizi ni kanuni zinazotufunga na wakati wowote mwandishi wetu ana mashaka na hajui afanye nini ni vizuri kuwasiliana na Mhariri wake kwa maelekezo zaidi.

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available