MAKALA Maoni SIASA TANZANIA

MwanaKJJ Ijumaa: Uteuzi wa Katibu wa Bunge ni Bunge Ndilo Lilivunja Katiba!

Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya mijadala iliyosisimua mitandaoni na katika jamii ni ule ambao ulisababishwa na uteuzi wa Katibu mpya wa Bunge uliofanywa na Rais siku chache zilizopita. Baada ya Rais kupangua baraza lake la mawaziri na kulipanga upya alitangaza pia kuwa ameamua kumteua Bw. Stephen Kagaigai (Kushoto kwa Spika) kuchukua nafasi ya Dkt. Thomas Kashililah (Kulia).

Mara moja hoja zilianza kutolewa kuwa Rais amevunja ‘sheria’ ambayo inamtaka kuteua mtu kushika nafasi hiyo baada ya kupokea majina matatu kutoka katika Kamati ya Utumishi ya Bunge. Sheria hiyo ya mwaka 2008 kifungu cha 7(3) kinasema kuwa “subject to Article 87 of the constitution,the Commission shall recommend three names of persons who are suitable for appointment to be the Clerk”. Kwamba, wa kuzingatia ibara ya 87 ya Katiba Tume itapendekeza majina matatu ya watu ambao wanafaa kuteuliwa kuwa katibu.

Ni kifungu hiki cha sheria ambacho wakosoaji wa Magufuli wamedai kuwa amekivunja kwani ameteua mtu (Kigaigai) bila kusubiri au kupokea majina matatu kutoka katika tume ya utumishi ya Bunge.

Je, ni kweli?

Naomba kupendekeza kuwa tukiisoma Ibara yote ya 87 ambayo ni fupi sana tunaweza kupata mwanga wa nani hasa amevunja Katiba. Kifungu hicho kinasema hivi:

(1) There shall be a Clerk of the National Assembly who shall be appointed by the President from amongst persons holding high office in the service of the Union Government.

(2)The Clerk of the National Assembly shall be the Chief Executive in the office of the National Assembly, and shall be responsible for the efficient discharge of the business of the Parliament in conformity with the provisions of this Constitution and of the relevant law.

Kwa ufupi kifungu hicho kinatuambia kwamba Katibu wa Bunge atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu ambao wanashikilia nafasi za juu katika Utumishi wa Serikali ya Muungano na kuwa Katibu huyo atakuwa ndio Afisa Mtendaji mkuu wa Bunge na kwamba atafanya kazi hizo kwa mujibu wa Katiba na sheria husika.

Kosa ambalo wakosoaji wa uteuzi huu wa Magufuli wanalifanya ni kuchukua matakwa ya sheria ya Uendeshaji wa Bunge na kuyalazimisha yakubaliane na Ibara ya 87 kifungu cha kwanza badala ya kujali kinachotakiwa kufanywa katika kifungu hicho cha kwanza.

Katiba haijasema uteuzi wa Katibu wa Bunge utatakiwa au utaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge. Uteuzi wa Katibu wa Bunge utafanywa na Rais na ni kwa sharti moja tu; kwamba huyo atakayeteuliwa atatoka miongoni mwa watu wenye nafasi za juu katika Utumishi wa Jamhuri ya Muungano. Katiba haijatoa NAFASI YOYOTE kwa Bunge kutunga mchakato wa kumpata Katibu huyo!

Sheria iliyotungwa na Bunge ilitakiwa ihusiane na utendaji na majukumu ya Katibu huyo tu chini ya kifungu cha pili cha Katiba kama kinavyotaka.  Kifungu hicho kidogo cha Ibara ya 87 kinasema “Katibu wa Bunge atawajibika kwa utendaji wenye ufanisi washughuli zote za Bunge kwa mujibu wa Katiba na sheria husika.”

Katiba haijaruhusu Bunge kutunga mchakato au namna ya jinsi ambavyo Katibu atapatikana kwani kifungu cha kwanza kiko wazi; Rais peke yake na bila kupokea ushauri au masharti kwa yeyote anapaswa kumteua Katibu wa Bunge. Kwa maneno mengine Rais Magufuli ametekeleza Katiba hadi nukta ya mwisho kwenye uteuzi huu.

Ili kuweka umuhimu wa hii tuangalie Katiba inasemaje juu ya uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu. Katiba katika Ibara ya 109 kifungu kidogo cha 1 inasema kuwa Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu watateuliwa na Rais kwa kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Katiba inamtaka Rais LAZIMA kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama kabla hajateua majaji wa mahakama kuu. Hili ni takwa la Katiba.

Mfano mwingine ni Tume ya Haki za Binadamu, Utawala Bora na Maadili. Katiba inasema kuwa makamishna wa tume hiyo na makamishna wasaidizi watatueliwa na Rais baada ya kushauriana na kamati ya uteuzi (nomination committee) – rejea Ibara ya 129 (3). Rais ni LAZIMA ashauriana na kamati ya uteuzi ambayo wajumbe wake wanatajwa kwenye kifungu kidogo cha 4 cha Ibara hiyo hiyo.

Uteuzi wa Katibu wa Bunge ni kama uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Attorney General – AG). Katiba katika ibara ya 59(1) inasema wazi kuwa Mwanasheria Mkuu atateuliwa na Rais. Kifungu kidogo cha 2 kinasema tu kuwa AG huyo atateuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma wenye sifa za uwakili na wawe na sifa hizo kwa zaidi ya miaka kumi. Utendaji kazi wake hata hivyo utaongozwa na sheria na Katiba (chini ya 3).

Kwa ufupi tunaweza kusema kwa uhakika wa kutosha kabisa kuwa Rais Magufuli hakuvunja Katiba. Ameitekeleza hadi nukta yake ya mwisho alipomteua Kigaigai kuwa Katibu wa Bunge. Sheria ya Bunge na hasa kipengele kinachoweka mchakato mwingine (contrary) na ule ambao Katiba imeweka kipengele hicho ni batili.

Hii ina maana ya kwamba, kama ningeombwa ushauri ningeshauri kuwa Bunge litakapokutana katika kikao chake kinachofuata kati ya mambo ya kwanza kufanyika ni kukifuta kipengele hicho (repeal) ili kumuacha Rais na uhuru wake wa kuteua Katibu wa Bunge.

Hata hivyo, kama wabunge wanaona – na binafsi sina tatizo nalo – kuwa ni vizuri kwao kusimamia uteuzi wa Katibu wa Bunge  basi waje na mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba waliyoapa kuilinda. Mapendekezo hayo yafanyia mabadiliko Ibara ya 87 (1) na waweke humo maneno yatakayowaruhusu wao kutungia sheria uteuzi wa Katibu wa Bunge.

Ilivyo sasa naomba kupendekeza kuwa ni Bunge ndilo lilivunja Katiba kwa kutunga sheria ambayo inapingana na Katiba na wakaifanya kuwa Sheria. Rais kwa kuangalia Katiba hakuna mahali popote ambapo pametoa mwanya wa yeye kumsikiliza, kusubiri au kupokea ushauri au mapendekezo yoyote kutoka kwa mtu au chombo chochote.

HOJA ZA KUJADILIWA:

Je, Rais anaweza kupuuzia sheria iliyotungwa na Bunge na kuridhiwa na Rais kwa kutaka tu kusimamia kilichomo ndani ya Katiba? Je, kwa kufanya hivyo hajavunja sheria hata kama hajavunja Katiba?

Je, Rais anapaswa kutii na kutekeleza sheria ambayo anaona inapingana na Katiba aliyopaswa kuilinda?

Je, Bunge linaweza kutunga sheria kutokana na madaraka yake kwa jambo ambalo Katiba haijaweka wazi kuwa linaweza kutungiwa sheria na Bunge hilo?

Nasimama kusahihishwa.

(niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com)

 

(378)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available