Afya & Mazingira MAKALA

Kupata Kinga ya PEP ya Virusi vya Ukimwi kwa Waathirika wa Ukatili wa Kingono

Na. Dkt. Joseph Ng’weshemi MD (ZAMAMPYA)

Utangulizi
Wanawake na watoto wamekuwa ni waathirika wakubwa wa ukatili wa kingono katika jamii nyingi ikiwemo Tanzania. Matokeo ya utafiti wa mwaka 2009 uliofanywa na UNICEF ikishirikiana na CDC pamoja na MUHAS nchini Tanzania na kuchapishwa mwaka 2011 ujulikanao kama “Tanzania Violence Against Children Survey, 2009” ulibainisha kuwa kila wanawake watatu kati ya kumi (27.9%) wenye umri kati ya miaka 13 mpaka 24 nchini Tanzania waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Ambapo pia asilimia 13.4% ya vijana wa kiume wa umri huo nao walitoa taarifa za kufanyiwa ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18.
Ukatili wa kingono ni mojawapo ya aina za ukatili wa kijinsia ambapo isipo dhibitiwa hupelekea athari kubwa kwa muathirika na hata kwa taifa zima kwa ujumla. Ukatili wa kingono una athari nyingi sana ikiwamo Kuambukizwa maradhi kama ukimwi, mimba zisizotarajiwa, maumivu ya kimwili na kisaikologia pamoja na unyanyapaa.
Makala hii inalenga kuongeza ufahamu juu ya uwezekano mkubwa uliopo wa kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi “VVU” kwa waathirika wa ukatili wa kingono na uwepo wa huduma hii katika vituo mbalimbali vya Afya nchini Tanzania, na pia kuongeza hulka ya kutafuta huduma hii miongoni mwa waathirika wa ukatili wa kingono.
Kinga ya Maambukizi ya VVU ni nini?
Kinga ya Maambukizi ya VVU ijulikanayo kitaalamu kama “HIV Post Exposure Prophylaxis” (PEP), ni kinga ambayo hutolewa mapema kwa kusudio la kuzuia hatari ya Maambukizi ya VVU. Kinga hii inahusisha kuanza umezaji wa dawa za kinga mapema iwezekanavyo (ndani ya masaa 72 “Siku tatu”) baada ya tendo moja la ukatili wa kingono ili kuzuia uwezekano wa kusambaa kwa VVU mwilini na hatimaye kuzuia maambukizi. Ukweli huu kuhusu Kinga ya VVU:-
• Ni huduma ya dharura ambayo hutolewa ndani ya masaa 72 na sio zaidi baada ya tendo moja la ukatili wa kingono. Kinga inapotolewa mapema kabisa ni bora zaidi kwa ufanisi wa kinga.
• Hutolewa kwa watu ambao hawana Maambukizi ya VVU kabla ya ukatili wa kingono, hivyo ni lazima kupima na kubaini hali ya Maambukizi ya awali kabla ya kuanzisha kinga. Endapo mwathirika wa ukatili wa kingono atakutwa na Maambukizi ya awali ya VVU hataweza kupatiwa kinga ya VVU.
• Itatolewa mfululizo kwa siku 28, na inaweza kusitishwa kabla ya siku 28 endapo mtuhumiwa wa ukatili wa kingono atathibitaka bila ya shaka kutokuwa na Maambukizi ya VVU.
• Hutolewa kwa muathirika wa ukatili wa kingono endapo hali ya Maambukizi ya mtuhumiwa wa ukatili wa kingo hajulikani.
• Huduma hii ya kinga ya VVU hutolewa katika vituo vyote vya Afya vyenye kliniki za kutolea tiba kwa waathirika wa VVU na Ukimwi “CTC” na pia baadhi ya kliniki za afya ya kinga ya mama na mtoto (PMTCT) nchini Tanzania.
Je ninaweza kutumia kinga ya VVU baada ya ngono isiyo salama?
• Kinga hii hutumika nyakati za dharura tu, kwamfano ndani ya masaa 72 baada ya ukatili wa kingono.
• Kinga ya VVU si chaguo sahihi kwa watu wenye mahusiano mengi ya kingono yasiyo salama na huweza kupelekea usugu wa matibabu ya VVU pindi tiba ya VVU inapohitajika.
• Njia bora za kujiepusha na Maambukizi ya VVU ni zile ambazo zina tukinga kwanza na Maambukizi (protect against exposure). Kama vile kushiriki ngono na mpenzi mmoja aliye salama, matumizi sahihi ya kondom, n.k.
Je nani wengine wanao stakili kupewa kinga dhidi Maambukizi ya VVU?
• Watumishi wa Afya ambao bahati mbaya wamepata ajali ya vifaa vyenye ncha kali ambavyo vina damu/vimiminika kutoka kwa wagonjwa.
• Watumiaji wa madawa ya kulevywa mara baada ya kuchangia sindano au uchangiaji wowote wa sindano usiokuwa wa hiari.

Kwakuwa ukatili wa kingono umekuwa ukiripotiwa kwa kiwango cha chini sana, hali hii imepelekea takwimu za kitafiti juu ya ukubwa wa tatizo hili kutofautiana kwa kiwango kikubwa. Idadi ndogo sana ya waathirika wa ukatili wa kingono inayofanikiwa kupata Kinga dhidi ya Maambukizi ya VVU inatokana na usiri mkubwa unaosababishwa na unyanyapaa kwa waathirika ambao wangeweza kuzuia kupata Maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Tusaidie wahanga wa ukatili wa kingono kupata kinga dhidi ya VVU kwa wakati.

Unaweza kuwasiliana na Dkt. Ng’weshemi kupitia # 0759344353

(901)

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available