BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 9

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*

_Sio wote utakaokutana nao na kuwatendea mema watayakumbuka mema hayo maisha yao yote. Na tena, sio wote wote ambao utawaonesha ukarimu wako siku moja watakulipa kwa kukuonesha ukaribu utakapohitaji. Kukumbuka fadhila nacho pia ni kipaji, na sio wote wanacho. Lakini hii iwe tu ni sehemu ya wewe kujifunza kuwa, wajibu wako kwa wengine ni kuwatendea mema. Ukielewa vema hili na ukaanza kulitenda, dunia nzima itakuwa na binadamu wanaotendeana wema tu!! Kila jema linaanza na wewe!!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU TISA*

Masaa matatu yalipita.

Sasa mishale ya saa ilikuwa ikiwaaminisha kuwa, ilikuwa saa mbili na dakika kumi na moja za usiku. Clifford alishatembelea maeneo yote muhimu katika hospitali ile kuanzia vyooni, kwenye wodi za wagonjwa, sehemu za kuuzia vyakula, maegesho ya magari na hata nje kabisa ya geti. Sasa alishamaliza kote na ni sehemu moja tu ilikuwa imebaki ambapo alitamani sana kuingia.

Chumba kile alipoingizwa Neema wake.

Rafiki zake Laurent na Thobias walikuwa naye bega kwa bega, wakajadili kuhusu hili, likaisha, wakahamia kwenye lile, nalo likaisha, zikaja na mada zisizo na mvuto wowote, wakazimaliza. Sasa wote macho walikuwa wameyatumbulia kwenye korido ndefu ambapo ndipo alikokuwa amepelekwa Neema. Ni Mungu pekee aliyejua ni nini kila mmoja alikuwa akikiwaza kichwani mwake.

Naam..

Mlango ukafunguliwa.

Kijana mrefu mwenye sharubu nyingi na mawani kubwa akatoka akionekana kuchoka kwelikweli. Akavuta hatua haraka haraka kuelekea upande mwingine wa korido ile mbali na walipokuwa wamekaa Clifford na wenzake. Lakini hakumaliza hata hatua kumi, Clifford tayari alikuwa naye bega kwa bega.

“Yes Dr. Mark, poleni sana” Alimsalimu daktari yule ambaye alikuwa ameshakutana naye zaidi ya mara tatu alipomleta Neema kuhudhuria kliniki.

“Njema.. Oooh, bwana Cliff.. Twende ofisini mara moja” Alisema Dr. Mark bila ya kupunguza mwendo wala kumtazama Clifford usoni. Clifford alisimama ghafla na kumtazama Daktari yule ambaye hakugeuka nyuma. Alitazama ingawa hakumwona! Kisha akanyanyua tena hatua na kuanza kumfuata nyuma nyuma kama kondoo aliyekwenda machinjoni.

Tayari alishaanza kuwa na majibu mengi kwa swali moja, na yote yalionekana kuwa sahihi.

Walifika katika chumba kidogo ambacho Clifford alishaingia zaidi ya mara mbili wakati wa matembeleo ya kliniki, lakini chumba kilionekana kuwa kigeni kabisa kwake. Alihisi kukichukia na wala hakutaka kuwa pale muda ule.

Alimtaka Neema wake na mtoto wake awe amempakata mikononi akijaribu kucheza naye. Alikuwa akiyaona mashavu ya Neema katika uso wa mtoto wake. Alikuwa akiutazama uso wa kuvutia katika mtoto wake. Alitaka muda ule ule awe amemshika mtoto wake. Ni vipi sasa Dr. Mark anamleta katika hiki anachokiita ofisi huku hakina dalili yoyote ya kuwa na kitanda kitakachompokea Neema na mtoto wake watakapotoka huko walipo?

_“Enough Dr. Mark!! This isn’t a joke anyhow. Please speak out, how is my good wife and a baby? Are they fine? Is everything alright?”_ Aliuliza Clifford huku akionekana wazi kughadhibika hasa kwa kuwa, Dr. Mark aliendelea kujishughulisha na kifaa hiki au kile akimwacha Clifford akiwa amesimama dede!!

“Yes yes Clifford.. Just have a sit brother.. We need to talk” Alijibu Mark huku akijipangusa uso na kuiweka sawa mawani yake. “We need to talk? Talk on what you swine?” Alijisemea Clifford ndani ya kichwa chake. Akamtemea kohozi zito kimawazo na akajiapiza kuwa, hatazungumza tena na daktari yule akishatoka hospitalini na Neema wake na mtoto wao.

Akaridhika kiasi. Hasira zikampungua.

Akaketi kishingo upande huku akimtazama Dr. yule usoni. Alikuwa mbaya!!Alimchukia na kushangaa ikiwa ni yuleyule kijana mwenye sura nzuri ambaye alikuwa akimuhudumia mkewe! Akamtukana tena tusi la nguoni kimoyomoyo, akaridhika zaidi, akatulia na kumkazia macho.

“Kuna vitu inabidi tuviweke sawa…” Alianza Dr. Mark.

“Vitu gani? How much? Sema, pesa ngapi nikupe mwanaume? Sema upesi, au nikupe……” Kihoro kilikuwa kimempanda Clifford.

“Clifford you must learn to listern and listern good!” Mark alijibu kwa mkato kwa sauti ya upole lakini kwa mbali, ilionekana kuwa na msisitizo fulani unaolazimisha jambo fulani. Clifford akatulia tuli.

“Imekuwa ni ajabu kidogo. Mkeo alihudhuria kliniki zote na kila kitu kilikuwa sawa kabisa.. Hata wakati wa tembeleo la mwisho nilimpima mwenyewe na hali yake ilikuwa sawa na ingempasa ajifungue kawaida. Lakini tuligundua kitu tunakitita _“abnormal Presentation”_. Mkao wa mtoto haukuwa sahihi na wakati tunajiandaa kufanya upasuaji, kulitokea hali nyingine ambayo tunaiita _“Amniotic Fluid Embolism”_, ambapo katika namna isiyo ya kawaida, kuna fluid tunaiita _Amniotic Fluid_ ilianza kupenya kwenye mfumo wa damu, na fluid hii hupelekwa hadi kwenye mapafu na kusababisha hali tunayoiita kitaalamu _“Arteries contractions”_ and this is very…

“Dr Mark get to the business buda, get to the damn thing, tell me the fu.. Excuse me!!_.. Ningependa zaidi utumie lugha nyepesi tu, MKE WANGU NA MWANANGU WANAENDELEAJE? Achana na habari za amphibia, flomborism, autopia na mamalia, nitakuita wiki ijayo uje unifundishe nikiwa na kalamu na daftari. Nataka kujua hali ya Neema bana.. Amniotic arteries na Manini nini sijui huko utaniambia siku nyingine”. Alikuja juu Clifford.

“Clifford.. Wewe ni mwanaume, na unapaswa kujikaza. Mtoto ametoka salama na tayari wauguzi wanamuandaa. Lakini mke wako…. Neema ame…. Ametutoka Clifford. Haikuwa rahis….” Alisema Mark huku akijaribu kuiweka sauti yake kuwa ya kubembeleza.

Lile kofi la kisogo alilowahi kubamizwa na Martin Bazu likarejea tena kwa fujo kwenye mawazo yake, likambabatiza kwa nguvu. Lakini hili halikuambatana na maumivu, lakini madhara yalikuwa yaleyale. Na tena, Aliwaona akina Dr. Mark wanne wanaofana wakimtazama.

“Whaaaat?? Nini wewe? Unasemaje Mark? Neema ame.. Amefanya nini?” Clifford alishajikabidhi mwenyewe chini kwa kishindo! Hakuwa tena anajua kinachoendelea.

Vijana wa Kiswahili wangesema amekata moto!

***

Ulikuwa usiku wa hekaheka kwa Laurent na Thobias. Taarifa za kifo cha Neema ziliwatia ganzi na kule kupoteza fahamu kwa Clifford kukawaingiza katika tanuru ambalo halikuonekana. Walifuta jasho, wakapanda na kushuka. Haraka, mwili wa Neema ikaburuzwa kwa machela na kuingizwa katika chumba cha maiti. Shemeji ambaye walikuwa wakitaniana naye masaa kadhaa yaliyopita alikuwa kimya..

Kimya cha daima!!

Kitoto kichanga cha kike kilikuwa kikitumia mikono yake midogo kupangua hewa na kulia kwa bidii. Watawa wa kanisa katoliki ambao walikuwa wakiihudumia hospitali ile wakakanyakua juu juu na kukapeleka katika chumba maalumu na kuanza kukahudumia.

Ulikuwa ni uchungu usiovumilika kwa Clifford baada ya kupata fahamu. Alidumu katika hali ya kutokujitambua kwa saa moja na nusu ndipo alipofungua tena mboni zake na kuanza kuweweseka. Clifford alilia, akasimama, akakaa, akagaragara chini, akajipaka na vumbi, lakini sauti pekee aliyoisikia haikuwa ya Neema wala mwanae yule.. Sauti pekee ilitoka kwa Thobias aliyekuwa akitoa maneno yote kutoka katika biblia, tenzi za rohoni, katekisimu za kanisa na hata sala alizozifahamu yeye.

Zote hazikuwa na msaada wowote kwa Clifford.

Taarifa zikafika Singida mjini. Majirani, marafiki pamoja na jamaa wa karibu na Clifford wakayasikia yaliyomtokea. Usiku uleule, wakarudi mjini huku wakimwacha Neema akipigwa na ubaridi usiomithilika na kichanga kile kikiwa chini ya uangalizi wa wataalamu.

Usiku ule ule, tayari kikundi cha wanakwaya pamoja na majirani wengine wa Clifford walishafika nyumbani kwake. Nyumba ikaendelea kujaa kila baada ya dakika chache na mpaka kufikia siku iliyofuata asubuhi, tayari na turubai lilitundikwa juu ili kuwasitiri watu kwa jua. Clifford hakuwa na nguvu ya kuongea chochote. Alikuwa amejiinamia huku akiliona jinamizi kubwa la kifo likimjia na kumzomea. Ni wazee wachache na marafiki zake hasa wale wanakwaya waliokuwa wakishughulika kila kitu.

Hakika aliuona upendo wa watu kwake!

Lakini wote wale walikuwa wakihangaika bure tu. Hakuna hata mmoja kati yao aliyeonekana yuko tayari kumpa msaada wa kupata majibu magumu ambayo yalikuwa yakitembea kichwani mwake..
Angemweleza nini Mzee Chiziza?
Angemweleza nini Mzee Masagida Kaswalala Masalu?
Angempeleka wapi Neema?
Angempeleka wapi yule mtoto asiye na jina ambaye hata alikuwa hajamtia machoni?

Kamasi zilimchuruzika na wala hakuona umuhimu wa kuhangaika nazo. Alikuwa na mambo ya msingi ya kuwaza kuliko kuwaza zile kamasi na machozi yaliyokuwa yanamtoka bila kibali maalumu. Tayari alishaonekana kuchoka kuliko kawaida. Hakuwa mtu wa kuzungumza, na wote waliokuja kumpa pole aliwaona wanafki na wazandiki wakubwa.

Jua likawaka na kupunguza makali. Jioni ikafika. Wenye busara wakaona kimya, na kwa kuwa utu uzima wao ulishawakutanisha na mambo makubwa kuliko lile, wakaamua kuweka kikao kwa nguvu.
“Sasa Bwana Clifford.. Yaliyotokea yameshatokea. Neema ametutoka, Innallilah Wainai Lillah rajiun. Waislamu sisi tunasema Kul nafsin zakatul Maut, nadhani hana nanyi ndugu zetu katika Imani mnalikiri hilo, tumetoka kwake na kwake tutarejea”. Alianza kuzungumzwa Mzee Ibrahim Upodo, moja kati ya wazee ambao Clifford aliheshimiana nao mno pale Singida.

_“Acha uongo wewe.. Neema hajafariki”_ Clifford alisikia kitu kikimuwaka ndani yake, na kwa mara ya kwanza akamchukia Mzee Upodo. Bahati tu ilikuwa upande wake kwa kuwa maneno haya yaliishia katika kichwa chake tu. Mzee Upodo akaendelea.

“Alhamdullilah Mwenyezi Mungu ameweka mkono mtoto amemnusuru. Kuna Ibra katika hili ndugu zangu.. Kuna mazingatio hapa na ni vema tukayashika na kuendelea kumcha M’nyaaazi Mungu mwingi wa reh’ma. Ni vema tukamshukuru M’nyaaz Mungu Subhannahu Wataalah wandugu. Lakini sasa, kule kwetu Tabora huwa tunasema Msiba haukosi pa kuingia. Na sasa kwetu umeingia. Nadhani labda kama umeshaongea na wazee ungetupa mrejesho ili walau tujue tunafanyaje bwana Clifford” Alimaliza Mzee Upodo na zaidi ya watu nane waliokuwepo pale sebuleni wakaafiki.

“Kwa kweli… Kweli sijui nianzie wapi.. Nashindwa… Nashindwa kujua ni balaa gani ili limenigongea hodi asubuhi na mapema.. Mi sijui kwakweli, sijui” Kilio cha kwikwi kikaanza kumtoka Clifford. Mzee Upodo akahisi kuwa lipo jambo, na upesi akawabagua waliopo pale ndani. Wakabaki wanaume wanne pekee, na haraka, Mzee Upodo kama vile ajuaye yanayomsibu Clifford, wala hakuhangaika kumbembeleza.

Akatoka nje na kuagiza vijana kadhaa kwenda huku na kule, wakati huo huo simu yake ikifanya kazi. Dakika arubaini baadae, sebule ile ikawa kama kikao cha ukoo. Wazee kadhaa wenye heshima pamoja na marafiki wa karibu zaidi wa Clifford wakawa wamekaa kwa kuelekeana, idadi yao ikiwa watu kumi na sita. Mzee Upodo ni kama vile alishajipachika cheo cha mwenyekiti na kila mara alikuwa akikagua kagua ili kujirishisha kuwa akidi imetimia, kisha sasa akafungua mjadala.

“Naam wazee wenzangu na vijana wangu wachache. Nimeona tuitane mara moja kuwekana sawa kwa yale yaliyompata kijana wetu. Nadhani wote hapa tunakiri kuwa huyu kijana amekuwa ni kijana wetu sasa. Heshima yake na utii kwetu vimempa jina jema miongoni mwetu. Huu ndio ujana wenye manufaa, pamoja na elimu kubwa aliyonayo lakini bado anatuheshimu sisi wazazi wake kwa kituo.

Sasa yamemfika mambo. Ana msiba. Ukimya wake tangu msiba ulipomfika umenishitua kama mtu mzima na nikaona muwepo watu wenye vifua ninaowafahamu. Tafadhali kama kuna anayejua hana msaada hapa, na labda nimemuita kimakosa, ajiondokee mara moja” Alianza Upodo na kimya kilipozidi kuzizima akaendelea.

“Haya bwana mkubwa.. Clifford, ulipojaliwa hayo maumbile hapo katikati ya miguu ulipewa na zawadi nyingine kubwa. Zawadi ya uanaume. Mwanaume si mtu legevulegevu, hata yamfike makubwa yepi, huangalia kwanza namna ya kuyakabili halafu ndipo aanze kulia. Sasa tumekutana hapa kusaidiana nawe kuyakabili hayo. Hebu funga fundo gumu kooni, kisha liteme hapa lililo moyoni mwako. Nakuapia hata liwe na uzito wa dunia, tutalibeba mabegani na kutembea nalo kwa madaha kabisa” Upodo alisema huku akiweka kifua mbele.

Ujasiri ukamuingia Clifford.

Kwa mara ya kwanza akatamani Upodo angekuwa ndiye baba yake mzazi!

_“Acha ujinga wewe, baba yako ni Chiziza…, Chizi Chiziza ambaye akisikia uliyoyafanya atakuachia laana ya kudumu”_

Ile sauti ikamjia tena lakini akaipuuza. Alifungua kinywa chake na kwa zaidi ya saa zima aliendelea kuwasimulia waliokuwa wakimsikiliza habari za Mzee Chiziza, kisha Neema na jinsi walivyokuwa wamepanga, na namna ujauzito ule ulivyowalazimisha kungoja, na juu ya uwepo wa Mwalimu korofi aliyeitwa Masagida Kaswalala Masalu ambaye wakati huo labda alikuwa akihangaika kumtafuta binti yake bila mafanikio kwa kuwa alikuwa na kawaida ya kuongea nae kila siku mara mbili au mara tatu.

Mpaka anafika mwisho wa simulizi yake, sebule nzima ilikuwa imezizima kwa ukmya usiomithilika. Hakuna hata mmoja aliyenyanyua kinywa kuhoji wala kushauri.

Wote walikuwa wamesawajika!

“Mmmmh… Ama kweli ‘pachonge pangali panene’. Babu yangu aliwahi kunifundisha msemo huo miaka mingi iliyopita. Hiki kweli kizaazaa. Lakini bado sijaona dalili za kushindwa. Kwanza, nadhani wa kwanza kumuarifu habari hizi ni baba mzazi wa kijana. Mpigie simu Mzee Chiziza nami nitaongea nae taratibu na kwa kituo. Yeye akshatuelewa, nadhani tutakuwa na karata ya kwanza ya kututoa katika mtego huu” Alisema Mzee Upodo kwa kauli iliyokosa ule ujasiri wa awali.

“Halafu imekuwa ajabu kweli. Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu anayeongelewa mimi namfahamu vema sana. Mzee wangu aliwahi kufundisha naye pale Nyakato lakini yeye baadae akahamishiwa Geita. Nadhani naweza pia kumwomba baba yangu atusaidie upesi kuwasiliana na Mzee mwenzake ili walau tuone msimamo wake”. Joshua Tegu ambaye alikuwa rafiki wa Clifford akachangia.

“Unaona sasa Clifford? Haya mambo bwana ukikaa na watu wanayamaliza. Haya bwanaaa…. Nani vile?” Alihoji Upodo

“Tegu.. Tegu.. Mr. Joshua Tegu” Alijibu Tegu ambaye alikuwa mhandisi wa maji.
“Naam Tegu.. Hebu wewe na Mzeeee…. Makambaaaa, Nyonzo naaaa… Mmole.. Wewe, Makamba na Mmole chukueni jukumu la kuwasiliana na Mzee wako pamoja na kuhakikisha kuwa mpaka saa mbili kamili tunapata mrejesho juu ya huko nyumbani kwao marehemu kwa huyo Mzeeeee” Alisema na hakungoja mtu amkumbushe.. Alikuwa akipitia karatasi ambalo muda wote wa masimulizi alikuwa akiandikaandika mambo ya muhimu.
“kwa mzee Masalu”. Alimaliza.
“Mimi, Clifford, Mzee Babudiii.. naaaa…, nani mwingine jamani? Tujitokeze..”
“Mimi hapa” Aliitikia mtu wa makamo aliyekuwa ameegamia ukuta.

“Hewalaaa.. Mimi, Clifford, Babudi na Lasway tunajishughulisha na mawasiliano na Mzee Chiziza na upande mzima wa Clifford. Kama kawaida, mbili kamili tunakutana hapa kuweka vichwa pamoja tuone tumefikia wapi. Wengine wote tuliobaki, chini yaaaa… Oh, ndio.. Ningepitiwa hapa.. Chini ya Bwana Kimati.. Ambaye mimi napendekeza awe mwenyekiti wa kamati ya mazishi. Ninyi anzeni mipango mara moja. Wekeni sawa bajeti zote, angalieni kama tuna fedha ya kutosha na kila kitu kiwe sawa. Sisi tukija na majibu tu tunaendelea kutoka mlipoishia” Alimaliza Upodo na kuangalia kama kuna aliyekuwa na nyongeza.

“Sawa.. Mi nakubali. Na napokea jukumu hilo mara moja. Ila kwa kuwa shughuli hii itahitaji pesa, nashauri hapa kuwa mwenye nacho aanze kukiahidi au kukiweka kabisa mezani ili tujua tunaanzia wapi. Mimi nitachangia taslimu Milioni nne, na magari matatu” Alisema Kimati.
Hoja ikapita mara moja. Huyu akaahidi hiki na huyu kile. Ndani ya dakika tano tu, Milioni sita na nusu zikapatikana pale pale ingawa nyingine zikiwa ni ahadi. Kikao kikakamilika na watu wakasambaa wakikubaliana kukutana tena saa mbili na nusu.

Walikuwa na masaa mawili tu ya kufanya kazi ngumu kwelikweli!

Kazi ambayo hata hivyo…

Mh!!

***

(154)

About the author

Paul Mpazi

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available