BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 7

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*

_Kama vile nywele ziotavyo pasipo sisi wenyewe kujua mwenendo wake, au kama vile tunavyoendelea kukua pasipo kuweza kuamua ni kasi gani tuitumie, ndivyo hivyo mawazo yetu yanavyokua. Ujinga mdogo unaoupalilia leo unaendelea kukua taratibu, bila wewe kujua ni kwa kiasi gani unaongezeka. Tabia mbovu halikadhalika, hata kama ni kwa kiasi kidogo, inaendelea kukua taratibu taratibu tu. Ipo siku, kama unavyoshangaa nywele zako kuwa ndefu, utagundua kuwa, ujinga au tabia mbovu ulivyokuwa unavipalilia vinakudai uvifanyie sherehe ya kutimiza miaka hamsini!!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA SABA*

_Walikutana.. Wakapendana!!_

Wala haikuchukua muda mrefu baina ya Clifford na Neema kujenga ngome imara ya mapenzi baina yao. Walipendana kwa dhati na Clifford aliazimia kuwa, yule angekuwa mke wake wa ndoa. Lile doa ambalo liliingia katika maisha yake kwa mkono wa Nunu likaanza kufutika taratibu. Lakini sasa akaapa kuwa atakuwa makini. Alitaka kufuata taratibu zote za kitamaduni kumuoa Neema. Hakutaka tena kupumbazwa na jinamizi liitwalo ‘kupenda kwa dhati’.

Taalumua yake ya ualimu ikatumika kwa makini kabisa.

Kwanza, hakuwa kiherehere wa kumuhudumia Neema kwa kila kitu kama alivyodanganyika kwa Nunu. Alijibakiza kwa sehemu yake! Alikuwa mwalimu na msaada mkubwa aliopaswa kuutoa haukuwa fedha wala zawadi nyingine yoyote zaidi ya elimu. Wakaweka vikao, wakayaandika mapenzi yao katika karatasi na namna watakavyoyaficha ili yasije yakawaharibia machoni pa watu. Kila mmoja akapewa jukumu lake la kutimiza ili kulinda mapenzi yao.
Wakakaa macho…

Kila mmoja akiwa makini kabisa na mwenzake!!

Haikuwa ngumu kwa kuwa, pamoja na ule woga wake na aibu zake; aibu ambazo Clifford alizifananisha na zile za Nunu ingawa za Neema zilikuwa za dhati; Neema alikuwa msichana mwenye misimamo chanya na isiyotikisika. Mara kwa mara aliendelea kumzungumzia baba yake kuwa ni mtu mkorofi, na hii ikawa kete yake ya kujitunza vema. Alienda nyumbani kwa Clifford kwa machale sana, na popote alipokwenda, kwanza alitanguliza masomo na kisha mengine ndipo yakafuata.

“Utakapomaliza chuo.. Tutafanya mpango twende kwenu kwanza. Niwajue baadhi ya ndugu ingawa kwa kificho. Halafu sasa hapo nitakupeleka kwa Mzee mmoja anaitwa Chiziza. Unajisifia sana kuwa baba yako ni Mkali, ila kuna kiumbe kinaitwa Chiziza sina haja ya kuzisema sifa zake hapa. Utakapomuona ndipo wewe mwenyewe utathibitisha kuwa baba yako anaweza kuwa Malaika Mwema kabisa mbele ya Malaika mtoa roho aitwaye Chiziza” Clifford aliongea kwa utani akizichezea kucha za Neema baada ya kumaliza kumfundisha.

“Mh.. Karibu sana Kanda ya ziwa.. N’tafurahi ikiwa hilo litatimia. Mh! Sema watu watashangaa! Yani mwalimu kumuoa mwanafunzi wake???” Neema alisema kwa aibu..

“Kwani ubaya uko wapi? Tena ndio vizuri, tukizaa watoto nakuwa nawasimulia kuwa mama yenu alikuwa kilaza mimi ndio nikawa namfundisha” Alisema Clifford huku akianza kucheka..

“Cliff.. Cliff umeanza uchokozi.. Bwana mi staaaki.. Staki nakwambia, staaki.. Mi sio kilaza bwana, nilikuwa tu na hofu.. Na ukiwaambia mi nanuna” Alisema Neema huku akiigiza kununa. Uzuri wa binti yule wa kisukuma ukatutumka usoni pake! Akajidai kununa zaidi, lakini mikono iliyokuwa ikimfundisha muda mfupi uliopita ikawa ikimtambaa kila kona ya mwili wake.

Kule kununa kukabadilika, kukawa kuguna na kujipinduapindua kama joka lililoogeshwa mafuta ya taa. Kukuru kakara za hapa na pale zikaendelea. Vitabu vilivyowafanya wakajuana wakavisaliti, wakavisukuma kwa miguu mbali na upeo wa macho yao, navyo vikatii, hiki kikaangukia kule na kingine kikajificha chini ya uvungu kwa aibu. Hakukuwa na joto lolote lililowalazimu kupunguza nguo katika miili yao, lakini wakajikuta wakiwa uchi wa mnyama.

Mwalimu akawa mwalimu kweli, na mwanafunzi akabaki kukubali kila somo alilokuwa akifundishwa. Wakajikuta katika sakafu yenye marumaru zilizopoa kwa ubaridi mkali, lakini jasho likiwa limewaenea mwili mzima. Kwa dakika thelathini nzima hawakuwa kwenye dunia ya masomo ya kihasibu, bali pembezoni kabisa mwa dunia yenye raha na amani isiyoeleweka.

Huyu alikaa vile na mwenzake akaiga na kukaa vilevile bila yeyote kuwafundisha chochote. Baada ya “kuzozana” kule, aibu ikawarudia. Walikuwa uchi huku wakitwetwa. Kama vile waliopeana ishara, wakaamka kwa haraka na kukimbilia chumbani huku maungo yao nyeti yakipata shida ya kuogelea katikati ya hewa iliyokuwa ikiwazomea.

Wakajikuta bafuni wakiwa wamekumbatiana huku maji yakiisalimu miili yao. Waliporidhika na usafi ule, wakarudi chumbani. Hakuna aliyemuangalia mwenzake machoni ingawa Clifford alijikaza na kujaribu kumtazama Neema. Naye alipotaka kufanya hivyo, wote wakaangalia pembeni kwa pamoja.

Penzi likatunga tenzi!, Neema akalala kwa Clifford kwa mara ya kwanza!

***

Ikawa usiku, ikawa alfajiri.

Wiki zikageuka Mwezi… Wa kwanza na wa pili, kisha wa tatu.
Neema akamaliza muhula wa kwanza wa mwaka wa tatu, na ilimpasa kwenda kwao kwa mapumziko mafupi ya mwezi mmoja. Lakini angeendaje amuache Clifford wake mwenyewe? Haikuwa rahisi. Walishaamua kupendana na kuwa pamoja muda wote, ingawa kwa usiri ambao si Clifford wala Neema aliyeusaliti. Uongo ukatungwa, Neema yuko field Singida..

Hakwenda kwao!!

Zulfa, mkufunzi mwenza wa Clifford waliyekuwa wakitumia ofisi moja alihisi jambo, lakini haraka upepo ukageuzwa kisomi. Yeye mwenyewe alikuwa ni miongoni kati ya wanawake waliotamani kuwa karibu na Clifford, tena ukaribu wa kimapenzi. Hapa na pale alimualika Clifford nyumbani kwake na yeye kumtembelea, mara nyingine nyakati za usiku na kujibaraguza baraguza kuwa alikuwa na mambo ya kitaaluma ya kujadili.

Taaluma gani ijadiliwe baina ya Mhadhiri wa masomo ya Rasilimali watu na gwiji wa Uhasibu na usimamizi wa fedha? Alikuwa na lake jambo, na Clifford alishalijua, na hivyo haikuwa kazi ngumu kumkwepa.
Neema alishamtosha!

Likizo ambayo ilishamirishwa na harakati za kimapenzi pamoja na masomo hapa na pale ikaisha. Neema akarejea darasani na Clifford akarejea ubaoni. Vipindi vikaendelea bila matatizo. Kule kuonana kwao mara kwa mara hakukuathiriwa sana na ratiba ngumu zaidi ya masomo aliyokuwa nayo Neema, lakini ule uwepo wa Clifford ukamsaidia kwa kuwa alikuwa akipata pia muda wa ziada kusoma masomo ya ziada.

Masomo ya ziada chuo kikuu!!

Halafu sasa likazuka jambo!!!
Tena ghafla tu!!

***

Hakuwa na elimu kubwa. Kidato cha nne na kisha chuo cha ualimu, na kisha kurudi uraiani akiwa mwalimu aliyeipenda kazi yake kuliko chochote katika maisha yake. Alifundisha kwa makini masomo ya hesabu na lugha, na akawa kipenzi kwa wanafunzi wake kutokana na umahiri wake wa kufundisha masomo yale, hasa kwa darasa la nne na darasa la saba yaliyokuwa madarasa ya mitihani ya taifa. Shule ya Msingi Nyakato ndiyo iliyompokea na hapo ndipo makali yake yakaonekana.

Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu alikuwa mwalimu aliyeelewa maana ya ualimu! Alikuwa ni msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi waliopitia Shule ya msingi Nyakato. Mitihani yake ilijizolea umaarufu mkubwa Mkoani Mwanza na kanda nzima ya ziwa kwa kubeba maswali ambayo yangetoka pia katika mitihani ya taifa.

Mwanafunzi wa darasa la saba ambaye hajapata mitihani ya kutosha yenye herufi “MKM” hakujiona kuwa aliye tayari kufanya mtihani. Waliobahatika kufaulu na kujiunga kidato cha kwanza walikiri kuwa, nusu au robo tatu ya maswali waliyokutana nayo kwenye mtihani wa taifa, yalikuwa yamechukuliwa neno kwa neno, namba kwa namba kutoka kwa fundi yule ambaye hata shuleni walishazoea kumuita “MKM”.

Lakini pamoja na sifa isiyoisha ya umahiri wa kufundisha hisabati na lugha, Masagida Kaswalala Masalu alikuwa ni mwalimu aliyeogofya!! Kisingekuwa kile kipaji chake kisichoelezeka cha kufundisha, hakuna mwanafunzi ambaye angetaka hata kuwa naye karibu! Alikuwa ni mkali wa kupindukia na hakutaka kabisa urafiki usio na tija na yeyote katika maisha yake. Muda wote aliokuwa peke yake, alijitenga na dunia nzima na kuhangaika na madaftari ya wanafunzi wake tu!

Lakini hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Hatimaye akafunga pingu za maisha ya binti aliyekuwa muuguzi katika hospitali ya Bugando. Maisha yake yakaendelea huku ile sifa yake ya ukali ikifichwa chini ya ule mwavuli wa umahiri wake wa kufundisha pamoja na ule upole wa mkewe Beatrice Budodi. Mwaka wa kwanza na wa pili ukakatika, wakajaliwa mtoto wa kike waliyemuita Neema.

Neema akayamulika maisha yao! Ili kumlea vema, Masagida akazidisha juhudi mara dufu. Akafanya kazi kwa bidii zaidi na jina lake likazidi kujengeka. Hatimaye akapandishwa cheo na kuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakato.

Neema alipokuwa na miaka minne, mama yake akapata ujauzito mwingine. Furaha ikayafunika kabisa maisha ya Masagida. Alikuwa ni mwalimu mwenye furaha zaidi duniani. Miezi tisa ikatimia na mkewe akaingia kwenye chumba cha kujifungulia.

Haikuwa kama walivyopanga.
Haikuwa kama walivyotegemea.

Beatrice hakutoka chumbani mule akiwa hai. Mtoto alikuwa amekalia nyonga na hivyo jitihada za kujifungua kawaida zikagonga mwamba. Mama alikuwa ameshachoka sana wakati wataalamu walipoamua kumfanyia upasuaji! Walifanikiwa kumtoa mtoto mkubwa na mzuri wa kiume aliyekuwa na afya tele. Wakati wakilishona tumbo la Beatrice, walikuwa wakilishona tumbo la Maiti yake tu.
Beatrice mwenyewe alikuwa anayajongea malango ya muumba wake!

Alifariki dunia!!
Kifo chake kiliacha uwazi usiozibika katika maisha ya Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu. Kifo kilichomwacha na jukumu la malezi ya Neema aliyekuwa na miaka minne tu na mdogo wake wa kiume aliyemwita Machimu, akimaanisha Mikuki. Ni kweli kabisa mtoto yule alikuja kama mkuki ulioutoboa moyo wake na kuyachukua maisha ya mama yake.

Hakutaka kuoa tena..
Akaamua kuwalea watoto wake kwa mapenzi makubwa huku mdogo wake wa kike na ndugu wengine kadhaa wakimsaidia pale nyumbani.
Neema na Machimu wakakua katika upweke wa kumkosa mama yao. Kuna wakati sura ya aliyeitwa mama yao ilikuwa ikimjia Neema kwa mbali sana, lakini hakuweza kukumbuka chochote. Kwake yeye, baba yao mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ndiye alikuwa mama na baba. Ukali wake ukamjenga na kumuandaa vema kuwa binti aliyemfurahisha baba yake.
Kisha sasa, hili linatokea akiwa mbali na baba yake…

***

(112)

About the author

Paul Mpazi

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available