BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 6

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*

_Hakuna kisichowezekana kabisa duniani.. Kule kukifikiria kit utu hata kisichokuwepo ni dalili kuwa kuna nafasi ya kukifanya kiwepo. Lakini, kuna gharama katika kile unachotaka kiwezekane. Ni pale tu tunapoogopa gharama za kuvifanya vitu viwezekane, au tunapozikwepa gharama hizi tunaanza kuzuia yale yanayowezekana kufanyika. Mfano, hata wewe unaweza kuwa mtu bora wa kuwaonyesha wengine njia ya kupita. Lakini ni wengi wamekusa njia kwa kuwa, mara zote umekuwa ukifikiria gharama utakazohitaji kufikia lengo lako._

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA SITA*

_Alifika darasani_

“Good afternoon” Alisalimia darasa lenye wanafunzi 38 wa mwaka wa tatu na wa mwisho wa masomo yao yatakayowawezesha kupata shahada ya kwanza ya uhasibu. Wachache waliitikia kwa kusimama kwa kusitasita na kabla hata hawajafikia nusu ya kusimama, Clifford aliupunga mkono kuwaashiria wakae.

“Well well… CR I asked you to collect your papers from my office earlier. Hope that you did..” Aliongea huku akimsogelea kiongozi wa darasa ambaye mara moja aliitikia
“Yes sir”. Mwanafunzi mmoja ambaue tayari alikuwa akijishughulisha kuunganisha computer ya Clifford na projector ili kuanza kipindi alijibu.
“Hamjafanya vizuri sana kwenye test ya mwisho. Sijui ni wapi hapakueleweka vizuri. Nitajaribu kuwa na nafasi jumamosi hii ili kama kuna yeyote ambaye anahisi hakuelewa nionane naye. Next week tutaandaa Markup test kwa watakaohitaji. Otherwise leo tutaenda hatua moja mbele.. We’ll be talking on ‘Cost accumulation for inventory valuation and profit measurements’.
“Well then.. At the end of today’s session, you will be able to…..”

Ufundi ukaanza. Kurasa ziliendelea kupepea katika ubao maalumu ulionururishwa na mwanga wa kifaa kile maalumu kilichokuwa kikichukua maandishi kutoka katika computer huku hapa na pale Clifford akiendelea kuusulubu ubao mwingine wenye rangi nyeupe kwa kalamu maalumu ili kuelezea vema zaidi yale aliyokuwa anayaelezea kwa ufasaha mkubwa.

Mwanafunzi mmoja aliyekuwa amekaa katikati ya wengine alikuwa ametumbua macho kwa umakini, hapa na pale akiukunja na kukuna kichwa chake. Ni wazi kuwa alikuwa akijitahidi kusikiliza na kuelewa kile kilichokuwa kinafundishwa bila mafanikio. Clifford ni kama aliliona hilo na hapa na pale akawa anapunguza mwendo wa kufundisha na kurudia rudia baadhi ya vipengele. Darasa zima likawa limechangamka na ni wazi kuwa walikuwa wanaanza kuelewa kwa ufasaha kile kilichokuwa kinafundishwa.

_“Now please… Can someone here differentiate a payroll and a labour cost accounting?”_ Aliuliza kwa utulivu Clifford huku akitabasamu kirafiki na kalamu yake akiiweka juu ya meza. Nusu ya darasa mikono ikawa juu.. Hakujali sana, akasimama akimtazama mwanafunzi yule aliyeonekana kujawa na hofu wakati wote.

“Neema… Can you?”
“Eeeh.. Sorry sir.. Can you repeat the question?”
“Neema.., _Can you please, and kindly, tell the difference between payroll and labour cost accounting?”_ Aliuliza Clifford huku kwa mara nyingine tena akitabasamu, akijipindapinda mbele na nyuma kwa mbwembwe, wakati huu macho yake akiwa ameyakaza kwa Neema.

“N…. No.. Sir… I can’t”. Alijibu Neema kwa huzuni huku nusu ya macho ya wanafunzi wenzake yakiwa yamemwelekea.
Aibu iliyochanganyika na hofu vilimjaa.

“Well well… Lets try something different then… Can you briefly remind us all Material Recording Procedures in a well defined store?”

_“Material recording what in a well defined what?”_ Alihoji Neema huku akianza kuonekana kutokwa na jasho kwa mbali. Zaidi ya nusu ya darasa wakacheka kwa nguvu. Hata Clifford naye alijikuta akicheka huku akitikisa kichwa. Hakuonekana kusikitika hata kidogo. Akarudisha kurasa nyuma na kukifikia kile alichokuwa amemuuliza Neema. Akarudia kukifundisha taratibu huku macho yake yote mawili yakiwa yamemuelekea Neema. Alitumia dakika ishirini akirudia rudia huku akitoa mifano mingi zaidi. Wengine wakaonekana kuchoka kwa kuelewa zaidi na hapa na pale wakawa wanajibu haraka hata kabla Clifford hajauliza.

Mpaka kipindi kinaisha, Neema aliweza kuyajibu maswali yale kwa ufasaha mkubwa huku akionekana kuchangamka zaidi ya alivyokuwa Mwanzo.

Kwa Clifford hii ilimpa moyo na akajikuta akiondoka darasani akiwa na hali nzuri zaidi. Alitamani sana anaowafundisha wamwelewe kwa kina, na hili alilitimiza kwa gharama yoyote ile.

Narudia hapa.. _“Gharama yoyote ile”_

***

Ilikuwa jumamosi ambayo walimu wengi waliitumia kupumzika na kufanya mambo yao nje ya chuoni, lakini haikuwa hivyo kwa Clifford Chiziza. Saa mbili kamili ilimkuta ofisini kwake akiwa anakabiliana na vitabu akijiandaa kuanza kuonana na wanafunzi wake wenye mahitaji muhimu na maalumu. Hakutaka amwache yeyote nyuma, hasa wale wa mwaka wa mwisho aliokuwa akiwafundishwa kwa namna ya kuwaandaa zaidi kuingia katika soko gumu la ajira.
Hamu hii iliongezeka kwa kuwa, ndio kwanza walikuwa wameingia mwaka wa tatu, na aliamini kuwa kama angewajenga vema Mwanzo kabisa mwa mwaka ule, huenda wangefanya vizuri na kusahihisha makosa yao yote ya nyuma.

Aliamua maisha yake apigane kufa na kupona kuandaa wasomi wa darasani na sio wahuni wanaosoma mtaani na kuwa waovu kama Nunu!!

Siku hii alikuwa na miadi na wanafunzi tisa ambao walijiandikisha siku moja iliyotangulia, huku wengine akiwatengea siku nyingine. Kama ilivyokubaliwa, saa tatu kamili walianza kuingia. Wapo walioingia wawili wawili na wengine mmoja mmoja. Mpaka kufikia majira ya saa saba, tayari alikuwa ameshaonana na wanafunzi nane ambao wote walitoka wakiwa na tabasamu huku wakiwa wamepewa kazi maalumu ya kufanya ambayo wangetakiwa kuikabidhi wiki iliyofuatia.

 

Kisha.. Saa saba na dakika kumi na nne, akaingia Neema.
Aliingia akiwa mnyonge na alionekana wazi kuwa na wasiwasi kama alivyokuwa wakati hajaelewa kule darasani.
“Good afternoon sir” Alisalimu huku akiangalia chini.
“’Afternoon Neema.. ‘Course you can sit down” Aliitikia Clifford. “Well.. Tell me Neema.. Muda mwingi unaonekana ukiwa na hofu sana.. Whats wrong with you?”

“Si…Sir… Sielewi. Yani najitahidi sana kuelewa lakini mara nyingi najikuta sikuelewi vizuri. Masomo ni magumu sana na baba hatanielewa nikifeli. Dady ni mkali sana, yani zile supplementary za last semester zilisababisha anipunguzie hadi kiasi cha matumizi. Anataka nifanye vizuri ili nisipoteze hela yake. Sijui nikifeli kama atanisamehe. Anaweza kunifukuza hata nyumbani kwake. Sidhani kama umewahi kukutana na mtu mkorofi kama baba yangu”. Neema aliongea huku akionekana wazi kulengwalengwa na machozi.

_“Ungemjua Mzee Chiziza ungenyamaza we binti.. Ila kwa kuwa humjui endelea kufikiri baba yako ni mkorofi”_ Clifford alijisemea kichwani kwake huku uso wake ukiumba lile tabasamu lake tamu. Kidogo Neema akaonekana kuanza kuzoea kuwepo pale.

“Sikiliza Neema… Unafeli kila mara unapokubali kuwa kuna kufeli. Forget about your father.. This is between your books, your lecturers and you. Huu ni muda wako wa kujithibitishia mwenyewe kwanza kuwa, You will make it. Yani una maanisha kuwa baba yako akikubali kukupokea hata ukiwa failure ndio utakuwa na furaha?” Aliuliza Clifford akiwa amemtazama Neema.

“Hapana.. Sipendi kufeli” Alijibu Neema kwa sauti ya chini.

“There you are.. That is what will take you through.. Jiambie ‘sitaki kufeli’, tena jikumbushe kila mara. Baba awepo au asiwepo, kataa kufeli.. Akulipie ada au asikulipie, kataa kufeli.. Anza kukataa sasa hivi kabla hatujafanya chochote.. Mkatae ‘kufeli’ na mambo yake yote, na fahari zake zote” Clifford alisema huku akiachia tena lile tabasamu lake.

E bwana ee.. Neema alisimama wima, akakunja ngumi moja na kuipigapiga kwenye kiganja chake cha mkono..
“Nakataa kufeli.. Nasema sitaki kufeli, na sitafeli.. Nitafaulu. SITAKI KUFELI”

_Shabash!!_

Tabasamu likachanua kwenye nyuso zao. Kipindi kikaanza. Walianza tangu somo la kwanza alilofundisha Clifford siku ya kwanza ya muhula ule. Akampitisha taratibu kwenye barabara pana ya taaluma, huku akimpa na mifano kedekede ya hiki na kile, hapa na pale akamruhusu kuuliza maswali ya uelewa, akayajibu kwa majibu rahisi lakini yenye maana kubwa. Hapa wakaenda mbele, pale wakarudi nyuma. Sehemu fulani wakasimama kwa zaidi ya dakika ishirini, wakarudia tena na tena, hesabu ndogondogo za mara kwa mara zikawekwa sawa na maelezo magumu magumu yakatafutiwa lugha nyepesi..

Yakaeleweka!!

Ni kule kuzama kwa jua ndio kuliwakumbusha kuwa muda ulikuwa umekwenda sana. Clifford akatazama saa yake. Saa kumi na mbili kasoro dakika chache, hakuhangaika kuzihesabu. Si Neema wala yeye aliyeonekana kuchoka. Neema alifurahia somo na Clifford alifurahia kazi yake inayomlisha na kumvalisha.
Jembe jipya lilikuwa limepata mpini imara.

Mpaka wanaachana majira ya saa kumi na mbili na nusu, Neema alikuwa na tabasamu pana lililoashiria kiasi alivyoelewa somo. Wakaagana na Neema akaelekea hosteli alizokuwa akiishi mitaa ya Sabasaba na Clifford akipanda bajaji na kuelekea mitaa ya Mwenge, Karakana alipokuwa akiishi katika nyumba kubwa aliyopanga zaidi ya mwaka uliopita alipohamia tu Singida.

Alikuwa na Amani kwa kazi aliyoifanya siku ile.

***

Hali ya kimasomo ya Neema iliimarika. Alikuwa akishiriki kikamilifu kujibu maswali popote yalipoulizwa kwa ufasaha mkubwa. Alijitahidi kuwa karibu na Clifford kama wanafunzi wengine, na mara kwa mara, hakusita kumfuata ofisini na kumwomba amwelekeze kile ambacho kilikuwa kikimshinda. Kuna wakati akawa anafundishwa hata yale ambayo darasani Clifford angeweza kuyasahau. Hii ikajenga urafiki hata wa nje ya masomo baina yao.

Kwa Clifford hili halikuwa na tatizo. Alipokuwa chuo kikuu cha Dar es Salaam, mara kwa mara alikuwa na utaratibu wa hata kualikwa kwenye sherehe za kuzaliwa za wanafunzi wake, au kualikwa kupata chakula cha mchana au usiku. Hii haikumpunguzia umakini wake wa kazi na badala yake, akajijengea heshima zaidi kwa kuwa, wanafunzi wale hawakumwomba upendeleo wowote katika masomo yao, bali walizidi kumtumia vema kuelewa kile walichokuwa wakifundishwa.

 

Neema naye akawa miongoni mwa wanafunzi wa Clifford walioondokea kuwa marafiki zake wa karibu.
Waliposhindwa kuonana chuoni kwaajili ya kueleweshana jambo fulani, wakakutana hata katika mikahawa nje ya chuo, barabarani au pahala pengine popote ambapo wangeweza kutimiza kiu yao ya kitaaluma. Kiu ya mwanafunzi kusoma na mwalimu kufundisha.

 

Hamadi! Neema akafika hata nyumbani kwa Clifford.

 

Kitabu kikasomwa kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho.. Mwalimu akafundisha na mwanafunzi akafundishika.
Lakini sasa, vitabu karibu vyote walishavimaliza. Mtaala wa muhula ule uliisha ndani ya muda mfupi tu. Wakasoma na magazeti, yakaisha. Hekaya za Zee la Kale na za abunuwasi, zikamalizika. Wasome nini sasa?

Wakakosa cha kufundishana.

Wakaanza kufundishana yasiyo kwenye mtaala.
Kizaazaa kikazaliwa, na kikaanza kukua…
Kikakaa, kikatambaa na kisha kikasimama kwa miguu yake…

_Ama kweli!!_

***

(78)

About the author

Paul Mpazi

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

Waandishi Makala

No recent posts available