BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 12 – Tamati

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*

_Si lazima uanze kila jambo likiwa katika ubora mkubwa. Hata magwiji wa elimu wanaamini kuwa, awali yaweza kuwa na changamoto zake nyingi tu. Lakini, daima lenga kuhitimisha kila jema unalolifanya kwa mafanikio makubwa. Azimia kuwa, ni muhimu kukamilisha kila unachokifanya kwa namna ambayo watu wote wataamini kuwa, daima ulikuwa ukilenga kufanikisha kwa mafanikio. Hatima nzuri sio tu inakupa moyo wa kuanza tena kwa nguvu, lakini inawajengea wengine Imani kuwa, misukosuko ya njiani haiwezi kuzuia mwisho Mwema wa safari!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*HAYA NDIYO NINAYOWAANDIKIA KATIKA KUHITIMISHA*

Jua liliwaka, likafika utosini…

Adhana ya alasiri ilimkuta Chiziza na familia yake wakiwa wamewasili jijini Mwanza, na wakafikia Charity Hotel. Ingawa alishawaeleza mkewe nab inti yake juu ya yaliyomkuta Clifford, bado yeye pia alitamani amwone Clifford na amweleze mwenyewe kwa kinywa chake Mwanzo mpaka mwisho wa kisa kile. Waliyozungumza asubuhi ile yalionekana kumuingia moyoni mwake na hapa na pale alitamani kumwona Clifford.

 

Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Chiziza alisikia uchungu usio wa kawaida!!

 

Naam.. Kikao cha kwanza kikakubaliwa kufanyika Charity Hotel. Wazee wale wale watano wakaongozana na Clifford hadi hotelini na baada ya hatua zote za utambulisho, mazungumzo yakaanza.

Wale wazee watano walikuwa wakimtumbulia macho Mzee Chiziza na familia yake kama vile walikuwa wakiwatoka sayari nyingine. Hapa na pale, walionekana wakinong’ona peke yao lakini ule ukali na uimara wa Chiziza uliwatisha! Ingawa hakuoneka kuwa mkubwa sana kuwazidi, alikuwa akiongea kwa mamlaka na kuhoji hapa na pale. Walizungumza kwa zaidi ya saa moja na hapo wakakubaliana kuanza safari ya kuelekea kwa mzee Masalu. Wakati huu, Clifford naye akaruhusiwa kuambatana nao!

Safari ya kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ikaanza. Njia nzima, wazee wale watano walikuwa wakikonyezana na kuzungumza kwa ishara, lakini ni kama kila mara Mzee Chiziza alikuwa akiwanyima uhuru. Mzee Upodo akanyanyua kinywa ili kusema jambo, lakini Mzee Tegu akamuwahi na kumkanyaga kwa nguvu huku yeye mwenyewe akipaza sauti na kuuliza.

 

“Vipi hali ya hewa ya Mjini bwana Chiziza.. Kule joto majira yote bwana” Alihoji Mzee Tegu.

“Ni ama wapumbavu au wasiojielewa tu wanaoweza kujiuliza na kujijibu wenyewe bwana mkubwa” Jibu rahisi lilimtoka Chiziza.. “Ni heri tu ungesema unaijua vema hali ya hewa ya Dar es Salaam na joto lake, tungekuelewa”. Chiziza alijibu huku akiangalia majengo mbalimbali nje ya gari waliyokuwa wamepanda.

Tegu akafikicha mikono na kuegamia kiti… Uso umemshuka na joto kali likimpita kwenye makwapa na sehemu nyingine muhimu.

Aliishiwa kauli!!

Kimya kikatanda hadi walipofika kwa Masagida Kaswalala Masalu..

***

Giza lilikuwa linaanza kubisha hodi kwa mbali, na nyumba ilikuwa na pilika pilika kiasi. Gari mbili zikawasili kwa pamoja. Moja walishuka Chiziza, Clifford aliyekuwa akiendesha, Tegu, Upodo na Claritha. Gari jingine wakashuka Mkewe Chiziza, Mzee Ng’wanzalima, Mzee Lasway, Mzee Makamba na Mzee Amri. Wajumbe wengine kutoka Singida walipaswa kufika baadae baada ya mazungumzo ya awali. Wageni wakapokelewa sebuleni, ingawa kila walikopita, miguno ilikuwa ikibaki nyuma huku wao wakisonga mbele.

Kuna jambo halikuwa sawa hata kidogo..

Hata kidogo, Hapana!!!

Sebule pana ilikuwa tayari na watu nane.. Watu kumi wakazidi kuinyanyasa kwa kuingia na kusambaa. Ilikuwa ni bahati kubwa kwamba, Masagida Kaswalala Masalu hakujenga nyumba ile kichoyo.. Ilikuwa sebule pana iliyoweza kuwachukua wote ingawa wengine walilazimika kuketi kwenye mkeka uliokuwa chini.

 

Kimya kikuu kikatanda…

Alikuwa anangojwa baba mwenye mji, Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ili afike na mnakasha uanze.

Akafika!

Halafu!!

Kimya…

Kila mtu alibaki kimya…

Kioo kimoja kilikuwa kimesimama mbele ya kingine..

Kama vile walioambiwa na mtu, Mzee Chiziza na Mzee Masagida Kaswalala Masalu wakasimama na kutazamana.
Kilikuwa kituko cha mwaka!!

Alikuwa ni mtu mmoja aliyevalia mavazi tofauti… Walifanana kuliko mayai ya kuku wa kisasa yanavyoweza kufanana. Walikunja sura kwa pamoja, hapo wakazidi kuwashangaza waliokuwa wakiwatazama..

“Wewe … Ndiye mwenye nyumba?” Alianza Chiziza huku akimtazama vizuri mwenyeji wake.

“Naam.. Karibu.. Kwani wewe ni…” Alijibu Masagida Kaswalala Masalu

“Nimeuliza swali moja.. Ningependa lijibiwe kwanza” Chiziza alijibu haraka.

“Ndiye haswa.. Kwani wewe ni nani? Aliuliza tena Masagida..

“Mzee Chiziza.. Ni baba yake na …” Alianza Mzee Chiziza.

“Kuwa mstaarabu.. Habari za umezaa watoto wangapi nitakuuliza baadae” Masagida akajibu kwa haraka.

“Lakini.. Nahisi kama vile…..” Chiziza alianza tena, lakini akakatizwa.

“Kuhusu hisia zako tutaongea tukiwa na muda, keti tujadili uhalisia” Masalu alijibu huku akiketi.. “Nilikuwa na wazo.. Nadhani tuanze na…” Aliendelea Masalu, lakini naye hakumaliza.

“Habu tuachane na wakati uliopita.. Kama ulikuwa na wazo sio pahala pake hapa. Nadhani kama una wazo ndio tuanze nalo” Chiziza alisema huku akiketi.

Upodo, Makamba, Lasway, Tegu, Babudi na Ng’wanzalima waliangaliana kwa haraka. Hali ya sintofahamu ilikuwa imetawala.

Utambulisho ukaanza mara moja na baada ya utambulisho, mazungumzo yakaanza. Lakini hakuna aliyetaka kujadili kuhusu msiba kwanza. Wazee wale wawili wakawa ndio wa kuzungumziwa pale. Hata wao walionekana kuwa na sintofahamu, lakini upesi, Chiziza akasafisha koo lake na kujiweka sawa, kisha akasimulia.

***
*[Anasimulia Chiziza]*

Kwakweli nashindwa kuelewa ikiwa hiki ninachokipitia ni ndoto ama la, lakini naona kuna jambo fulani zito hapa. Mimi jina langu la kwanza ni Adolph.. Sijui ni nani hasa alinipa jina hili, lakini ninachojua ni kuwa, nilikuwa mtoto pekee wa Mzee Aidani Chiziza na mkewe Anastella. Mzee Chiziza alikuwa ni mfanyabiashara maarufu sana jijini Dar es Salaam, lakini hakuwa kuniambia hasa asili yake ni wapo ingawa baadae nilikuja kujua kuwa, alikuwa mgogo wa Dodoma.

 

Nilikuwa peke yangu nyumbani kwetu, na nililelewa kwa ukwasi kiasi kutokana na hali ya kiuchumi ya Mzee Aidani.
Hata hivyo, wakati nilipokuwa na akili timamu kabisa, mara kwa mara nilikuwa nikimsikia mama akilalamika kwa baba kuwa, kuna watu walikuwa wanamsema na kumcheka kuwa amebaki kuokotaokota watoto, lakini sikuelewa chochote. Wakati nilipofika darasa la saba, mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kizazi. Nikabaki na baba yangu ambaye alinilea kwa upendo mkubwa mpaka nilipoingia kidato cha kwanza.

 

Pengo la mama yule halikuniathiri mimi peke yangu. Hata baba alionekana mara kwa mara akiwa na mawazo kupita kiasi na kuna wakati alikuwa akiniangalia kwa huzuni sana na kutoa machozi. Sikujua nini hasa kilimliza baba na kuna wakati mimi nami nilijikuta nikilia pamoja naye.

Siku moja usiku, baba aliniita na tuliongea naye kwa muda mrefu sana. Kwenye mazungumzo yake, alikuwa akiomba sana kuwa, siku moja nikiwa mtu mzima, niende nikaishi Mwanza. Sikuwa namwelewa kwa kuwa hakuniambia kwanini alitaka nifanye vile, lakini nilimkubalia na baadae akaniruhusu nikalale.

Siku iliyofuata, nakumbuka ilikuwa siku ya jumapili, nilimwamsha baba ilitujiandae kwenda kanisani kama kawaida yetu. Lakini baba hakuamka. Nikahisi huenda kule kuchelewa kulala kulikuwa kumemchosha, hivyo nikaamua kwenda peke yangu na kumwacha. Hata niliporudi, hali ilikuwa vilevile. Bado alikuwa amelala.

 

Baadae, iligundulika kuwa, Mzee Aidani alikuwa amefariki dunia. Nilihisi dunia nzima ikiniacha peke yangu!! Ingawa ndugu walikuja na kunifariji, sikuwa nimewazoea na sikuwahi hata siku moja kwenda kwa ndugu!!
Tukazika salama! Lakini baada tu ya mazishi, ndipo kikao cha familia kikaambiwa ukweli. Kwamba wakati mimi naletwa pale nyumbani, mama yangu hakuwa na mimba yoyote na baadae akasema kuwa amejifungua. Ndugu walipotaka sana kujua ukweli, baba yangu aliwajibu kuwa,nilitolewa kwenye kituo cha watoto yatima kwa kuwa yeye (baba yangu) na mama yangu walikuwa wameshatumia miaka ishirini ya ndoa bila kuwa na mtoto, na hivyo waliamua kupata mtoto hata kwa kuasili.

 

Niliumia sana siku ile!! Niliwaza sababu ya baba yangu kuniambia nije Mwanza. Familia ile ikanitenga, lakini sikuwa hata kwangu pia ilikuwa na nafuu. Sikutaka tena kuishi kinyonge. Nikaendelea kujibana bana pale nyimbani mpaka nilipomaliza kidato cha nne. Nafasi zikatoka na nikaenda jeshini, na tangu wakati huo, sikuwahi kujua habari zao tena!!!

Nilipokuwa jeshini, kuna bwana mmoja kutoka Mwanza alikuwa akipenda sana kuniita Teacher.. Siku moja nilipomuuliza, alinicheka na kuniambia.. “Mwalimu hata kama umekimbia chuo cha ualimu na kuingia jeshi, wewe ni mwalimu tu”..

Nilipuuza kauli ile na kuendelea na maisha yangu ya jeshi. Nikahitimu na kulitumikia jeshi hadi nilipostaafu kwa hiyari ili nifanye mambo yangu. Lakini maisha yangu yote, nimekutana na zaidi ya mtu mmoja ambao kila mara wanaishia kuniangalia sana na kuondoka bila kusema neno, au pale ninapowagombeza kwa kuniangalia ovyo!!
Sasa nashindwa kujua huyu aliyesimama mbele yangu leo ni nani hasa

***

Kikao kilizizima!

Kila mmoja mdomo ulikuwa wazi!!

Ni mtu mmoja tu ambaye alionekana kuwa na cha kusema lakini hata hivyo alikuwa na wasiwasi mwingi..

“Kwa kweli sijui kama hiki ninachokiona ndicho ama naota.. Lakini nakumbuka nilikuwa binti mwenye ufahamu wakati wifi alipokuwa mjamzito. Akiwa hospitali ambako alilazimishwa kwenda baada ya kanisa kujenga hospitali pale kijijini, kuna taarifa zilikuja kuwa wifi yetu ameleta mkosi nyumbani”.

“Tuliambiwa kuwa, amepata watoto wawili. Wazee walikusanyika na kuanza kupanga nini cha kufanya. Watoto hatukuruhusiwa kusogelea karibu na watu wazima walipokuwa wanajadili.. Lakini baadae, tulisikia kutoka kwa kina mama kuwa, watoto wale wangeuwawa baada ya kufika nyumbani” Alizungumza mama mmoja mtu mzima kabisa ingawa kwa mbali alionekana na nguvu kiasi”.

“Tulingoja wifi arudi na watoto wawili kwa kuwa hatukuwahi kuona watoto wawili wachanga kwa pamoja, lakini baadae alipokuja, haikuwa hivyo. Alikuwa na mtoto mmoja tu.. Basi ile habari iliishia pale. Sasa leo hiki nnachokona….” Alimaliza mama yule.

***

Mjadala uliendelea mpaka karibu saa sita usiku.. Ya Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu yalikuwa pasua kichwa. Kwanza kuna saa wao wenyewe walikuwa wakibadilikiana kupita maelezo.

“Nimeuliza swali Mzee, maelezo yako ni mazuri lakini siyahitaji” Chiziza alianza

“Swali la jibu hilo ninalo, tafadhali tunza jibu lako utalitoa baadae” Masalu naye akalipuka

“Nisikilize bwana, hata wanasayansi wanasema…” Alijaribu Masalu

“Achana na wanasayansi, nisikilize mimi” Chiziza akadakia!

Hata kama wasingekuwa mapacha wa kuzaliwa, tabia zao tu zilitosha kuwaita mapacha!!

***
Hakukuwa na namna tena.. Hakuna aliyekuwa na hasira kama awali..

Mwili wa Neema ulizikwa!!

Kila mtu alikuwa akiongea lake!

Juu ya nini kilitokea hata Chiziza na Masalu wakatenganishwa utotoni hakuna aliyekuwa na haja ya kukitafuta. Ukweli kuwa jamii nyingi zamani zilikuwa na utamaduni wa kuamini kuwa mapacha ni dalili ya laana ilijadiliwa, na kukawa na uwezekano kuwa, huenda wakati wakiwa hospitali pale, mtoto mmoja aliruhusiwa kuondoka na mama yake na mwingine akabaki na kutafutiwa malezi sehemu nyingine.

 

Hakuna aliyetaka kujua sana. Wazee wawili wakorofi walikuwa wamekutana, na kwa mara ya kwanza kwa ndugu zao, walionekana muda mwingine wakiongea na kucheka huku wakijitenga na watu wengine.

Damu nzito kuliko maji..

Halafu sasa kuhusu damu…

Ilishatokea.. Watoto wa ndugu wawili wamekutana na kuzaa mtoto.. Ndugu wawili waliopotezana wamekutana.. Alimuradi kila mtu alizungumza la kwake. Lakini ukweli ukabaki palepale.

Hakukuwa na haja ya DNA kupima undugu wa Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu!

Matanga yalivunjwa na taratibu za kumpa jina mtoto wa Clifford zikafanyika. Hakukuwa na jina jingine zaidi ya kumwita Neema, familia ikaridhia. Taratibu zote za kimila zikafanyika. Ndugu wakaitwa na wakatambuana. Wa kupigwa faini akapigwa na wa kusemwa akasemwa. Wakaonyana na kuwekana sawa, wakapena mikono na kubadilishana namba za simu. Wakapiga na picha za familia pamoja na “selfie”.

Chiziza akarejea Dar es Salaam akiwa na Amani ya kumjua ndugu yake.

Clifford alirudi Singida na kuendelea na majukumu yake kwa muda, kisha akaenda jijini Dar es Salaam kumsalimu Baba yake..

“Kijana… Nadhani sasa umejifunza nini maana ya ukali wangu juu ya maswala yahusuyo familia. Ujinga ulioufanya awali, na labda unaoendelea kuufanya hata sasa, wa kukutana tu na mwanamke na kuzoana ulitaka kuitoa roho yako. Lakini hakuna kosa kubwa kama kuishi na mtoto wa mtu bila kutoa taarifa kwa ndugu. Unaweza kuingia matatizoni mpaka ukahisi dunia hii ni chungu..” Mzee Chiziza alieleza.

“Ni kweli baba.. Unakumbuka nilichokuambia mara ya mwisho kabla hujaja Mwanza?”

“Naam.. Nakumbuka”

“Naam.. Wakati wa nyuma, sikuwa nakuelewa vizuri ulipokuwa ukizungumza kama Baba.. Lakini sasa, najifunza kuwa, nitakapoamua kuoa, sipaswi tu kuangalia kuwa ni kiasi gani niko tayari kuoa peke yake, au watu wengine wananiambia nini kuhusu kuoa.. Napaswa kujichukulia kwanza kama Mume, lakini zaidi, bila kujali iwapo nina mtoto au la, nijichukulie kama BABA!!

“Sina sababu ya kukulaumu tena kwasasa.. Mpaka ulipofika, sina shaka kuwa umepokea adhabu.. Imekuwa ni adhabu ambayo kwa wakati huohuo imekupa zawadi. Kwa kumtazama mwanao Neema, mtazame pia kama zawadi ya adhabu kwako.. Na ikiwa utapenda kurudia tena makosa, tambua kuwa utakuwa hujajifunza chochote katika maisha yako, na hata Neema huko alipo atakutazama na kusikitika kwa kuwa, kifo chake kitakuwa hakijakufundisha chochote” Chiziza alimaliza…

***

Geti kubwa la nyumba ya Mzee Chiziza lilikuwa likigongwa kwa nguvu. Haraka, Clifford alinyanyuka kwenda kufungua huku kule kukatishwa mazungumzo na baba yake kulimkera.

“Nahisi kama Janeth ameenda kufungua, ama?” Alisema Mzee Chiziza huku naye akionekana kutamani kukaa karibu na mwanae.

“Achana na hisia mzee na rudi kwenye uhalisia, Janeth na mama wameenda mjini kitambo tu. Umekuwa msahaulifu tena?” Alisema Clifford huku akiufikia Mlango.

“Pumbavu kabisa. Clifford nitakupiga risasi we chalii” Chiziza alisema huku akisimama kwa utani.

“Nilikuuliza swali mzee, hilo tusi ungeliweka akiba, utalihitaji baadae” Clifford alibamiza mlango na kuelekea getini.
Alifungua mlango na kuchungulia nje.

Gari nyeusi ilikuwa imepaki ikiwa tupu ndani, huku mtu fulani akionekana kuanza kuondoka eneo lile.
“Oyaa.. Vipi? Nani?” Aliuliza Clifford..
Mtu yule akageuka na kumtazama kwa macho yaliyolegea na kuonekana kuchoka..

 

*Alikuwa NUNU!*

 

****MWISHO****

*Nunu atarejea. Na atakaporejea, kila chozi ambalo halikutoka mwanzo litadhihirika. Na maumivu yote yaliyopoa yatahuishwa, na kila kovu litafanywa donda bichi lenye kuuma Tena!!*

 

*_Mungu ni mwaminifu na kazi zake ni takatifu!_*

_Nakushukuru sana msomaji kwa kuwa sehemu ya kazi hii tangu Mwanzo mpaka kituo cha mwisho. Sijajua imekuwa ni safari ya aina gani kwako, lakini kwangu imekuwa ni neema ya nguvu ya Mungu kunipa nafasi ya kuyabadili mawazo yangu kuwa simulizi hii. Ni wazi umejifunza jambo. Lichukue na kulihifadhi moyoni. Kama halitakufaa siku ya mvua, litakusitiri siku ya jua. Na kama halitakunufaisha katika maisha yako, ligawe kwa mwenzako, huenda likawa ni Mwanzo mpya wa maisha ya mtu mwingine._

_Kipekee, asante sana pia kwa kuwa sehemu ya wasomaji wa kazi zangu kwa wakati wote. Hakika umefanyika kuwa zawadi kwangu na sababu ya kuendelea kukitumia vema kipaji changu. Naahidi kuwa, nitaendelea kuwa kisima kisichokauka cha simulizi na tungo zenye kujenga, kufurahisha, kufundisha, kusisimua na kipekee, kuyagusa maisha ya wengi zaidi_

 

*TIMOTHY PETER MSUYA KIRAKA!*

(241)

About the author

Paul Mpazi

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available