BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 11

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*
_Mambo mengi yanayotuponza ni yale ambayo tunayafanya kwa kuwa ni ya hiyari. Kama mambo yote yanayotuzunguka yangalikuwa ni sheria, tena zisizotupa hiyari ya kuzitii ama la, huenda, narudia tena, huenda, kila kitu kingekuwa tulivu zaidi ya sasa. Lakini haiku hivyo. Tuna hiyari ya kuchagua katika kila kitu tunachokifanya. Mbaya zaidi, tuna hiyari ya kusema kweli au kuikataa kweli, na pale tunapoisaliti kweli na kuamua kuunda urafiki na uongo, tunajikuta kuwa, jambo dogo tunalolifanya kwa hiyari linajenga misingi ya matatizo makubwa yatakayotukuta kwa lazima!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA KUMI NA MOJA*

_Alfajiri ilifika.._

Kukapambazuka na kijua kikaanza kulimulika jiji la Mwanza.

Ni kama kila mmoja alikuwa akimtegea mwenzake aongoze njia.

 

Lakini ule utu uzima wao ukawasuta na kuwakemea. Wakainuka kwa pamoja, kisha wakaingia kwenye gari moja dogo wakiwaacha waombolezaji wengine wakiwa wamesambaa huku na kule. Wapo ambao toka walipofika walikuwa wamejikita katika ulevi na kupoteza mawazo, wengine walikuwa wamelala tu garini na wengine huku na kule wakijadiliana. Clifford yeye alikuwa amejikunyata garini akiwa mgonjwa wa ugonjwa ambao haujapatiwa damu ya kuponya wala kinga ya kuuzuia.

 

Ugonjwa wa hofu!

 

Wazee walishamwonya kabisa kuwa hata kama wangekubaliwa, asingepaswa kuonekana eneo la karibu na msibani kwa kuwa angezusha tafrani isiyo ya lazima. Kule kushindwa hata kushiriki kumzika Neema wake kulizidi kumpa homa isiyotibika.

Wazee watano wakafika kwa Mzee Masalu. Ile hali waliyoikuta tu kwanza ikaanza kuwatia ubaridi. Nyumba ilikuwa katika utulivu wake na hakukuwa na dalili yoyote ya kupokea mziba. Wakatazamana na kuulizana kwa kutumia macho, lakini hakuna aliyeonekana kuwa na jibu.

Wakafika na kugonga hodi!

Naam… Kidume cha futi tano unusu kikatoka kikiwa kimevalia suruali na shati huku kikiwa na kijitabu kidogo mkononi.

“Ohoooo… Bwana Tegu… Doh, Ng’wanzalima… Nawiwa nini nanyi hata mwanijia mapema yote hii?” Aliwalaki Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu huku akiwa na uso wake ule ule ambao hata alipotabasamu, ilikuwa ni vigumu kujua kuwa alitabasamu.

“Mgeni aambiwa karibu bwana, tena mwenyeji amwekee na kifua aangukiepo” Alijibu Tegu huku akitabasamu kwa kijilazimisha.

“Tangu lini Tegu akamwomba Masagida kifua aangukiepo? Tegu si wa kuangukia popote atakapo? Labda kama kuna kingine bwana” Alisema huku akijaribu kuwatazama wengine.

“Yapo mengi dunia ya leo bwana, na tena….” Alianza Ng’wanzalima

“Wala si mengi ya kuwakurupua asubuhi yote tena na wageni watu wazima kwangu. Kama ni posa jamani si mngeniarifu niwaandae na ndugu zangu? Au bado mnataka kuniletea huo utani wa msiba?” Alijibu Mzee Masagida huku sasa akiwa amesimama dede.

Hapo akakaribishwa Mzee Upodo. Akajitambulisha, yakafuatia maneno mawili matatu ya utani wa msukuma na mnyamwezi, kisha akaingia kazini. Itoshe tu kusema kuwa, Upodo alikuwa fundi wa kujieleza. Alipangilia kwa umakini mkubwa kauli zake, akayapekua vizuri maneno kabla ya kuyatoa. Akapanga semi na tamathali zake, penye kuweza kutumia neno la kinyamwezi au kisukuma akafanya hivyo. Jambo ambalo asiye mwerevu angetumia dakika mbili tu kulielezea, yeye akatumia saa moja na dakika kadhaa.

 

Akaweka kituo huku wale wazee wenzake wanne wakitamani wampigie makofi, lakini wakakumbika pale hawakuwa kilabuni wala kwenye minakasha ya gahawa. Walikuwa nyumba ya mfiwa, tena mfiwa asiye na uhakika. Wakaungana naye kwa kutikisa vichwa tu.

“Umemaliza maelezo yote mzee Upodo?” Alihoji Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu

“Naam.. Kwa tuo na kituo. Kama kuna lililobaki basi si la…”

“Sijauliza swali lingine, nadhani jibu lako la kwanza linatosha” Alijibu Masagida, kisha akawageukia wale wengine.

“Kuna mwenye maelezo mengine yanayokinzana na haya?” Alihoji.

“Hapana, Hapana bwana” Walijibu kwa pamoja kwa haraka kuliko walivyotaka.

“Vema sana. Hicho mnachokiita mwili wa Neema kiko wapi?” Alihoji tena

“Tumefika hapa jana usiku na tuli….”

“Nimeuliza swali moja tu.. Kiko wapi?” Akikatisha Mzee Masagida.

Jasho lilimtoka Mzee Upodo, akajiapiza kuwa angekuwa makini tangu muda ule kujibu maswali ya Mzee Masagida kama ilivyo kwa Mzee Chiziza.

“Penguin Hotel.. Ndipo magari ya waombolezaji yalipofikia kwa muda kuingoja alfajiri” Alijibu Upodo.

“Mzee.. Haya sasa, ngoja uone.. Kwanini mlifikia Penguin Hotel??” Akamkazia macho mzee upodo ambaye alikosa jibu la haraka.. “Ni wazi kuwa utajikuwa kuwa mlifikia hapo kuingoja alfajiri. Jifunze kuwa, kila swali unaloulizwa, toa jibu laka na uishie hapo. Acha kutoa majibu ya maswali ya kesho.. Utafeli” Mwalimu alirudi darasani, kisha kwa haraka akaanza kuongoza njia huku akisema

“Vema sana. Twendeni” Aliongoza Masagida na kuanza kuelekea kwa mguu kwenye njia iliyokuwa ikiiacha nyumba ile.

“Lakini Mzee… Kwanini… Sisi… Eeh, si tungekuja tu moja kwa mo….” Alijaribu kujieleza Tegu.

“Tegu.. Unajua vile tunaheshimiana Mzee mwenzangu. Hebu usicheze michezo ambayo hukujifunza ujanani ukiwa mzee.. Utajavunja mgongo ukose wa kukuokota.. Acha tuliocheza ujanani tumalizie uzeeni” Alimjibu na haraka akapotea machoni pao.

Waliduwaa!!

Kengele za hatari zikaanza kupiga makelele masikioni mwao.

***

Walirudi upesi Penguin Hotel na walipokuwa njiani, Mzee Upodo alimpigia simu Clifford na kumwomba atafute pahala pa kwenda kwa muda na awe mbali na pale kwa wakati ule. Walifika na kupokelewa na waliokuwepo lakini hawakusema chochote badala ya kuwaomba muda kidogo wa kujadili jambo. Lakini hawakutumia hata dakika kumi, wazee watatu wakawasili pale wakiongozwa na Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu.

 

Wazee wale wale watano wakawapokea na kuweka kikundi kidogo cha wazee pembeni. Wakajadiliana huku hapa na pale wakionekana kuvutana na kuelewana, na baada ya muda, vijana kadhaa wakaombwa kushusha jeneza lililokuwa limeuhifadhi mwili wa Neema. Wazee wale watatu wakaingia garini na kukaa huko kwa dakika kadhaa, na baada ya muda wakatoka. Kimya kikuu kilikuwa kimetawala na hakuna hata mmoja aliyezungumza na mwenzake.
Wakajadiliana tena kwa muda.

 

Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu akiwa na nduguze hawakusema neno. Wakaomba waende nyumbani kwa mazungumzo ya muda mfupi na kisha watatoa jibu.

Wakaondoka!!

Kimya kikatanda
***

Saa nne kamili.. Kimya!!

Saa tano kamili.. Hola!!

Saa sita kamili.., Hamna kitu!!

Saa nane na nusu, waapi!!

Tisa kamili, kumi kamili, kumi na nusu.. Malikiti!!!

Joto likageuka kuwa baridi.. Kila mmoja alitetemeka. Njaa iliuma lakini hakuna chakula kilichonunuliwa kikalika!
Macho ya watu wote yaliwaelekea wazee watano. Wao kwa wao pia, kila mmoja akimgeukia mwenzake, lakini kama vile walionong’onezana, kila mmoja akamgeukia Upodo!! Upodo yule mwerevu wa maneno ni kama alikuwa kwenye dunia ya peke yake huku wengine wote wakimtupia mawe.

 

Saa kumi na moja kamili, simu ya Mzee Tegu ikaita, na alipoangalia, herufi tatu zikajitokeza mbele yake zikimsanifu…

Mzee MKM!!!

“Masagida Kaswalala Masalu…” Alinong’ona huku akiipeleka simu yake sikioni.

“Halo Mwalimu” Alianza kusema lakini akagundua kuwa koo lilikuwa limekauka.. Akameza mate kwa nguvu ili kulilainisha lakini hakuwa na mate mdomoni. Akaishia kunong’ona tu.

“Hebu nizungumze na Upodo” Alisema mara moja Masalu. Mzee Tegu akatii na kumpa simu.

“Sasa bwana Upodo. Familia nzima imekutana na kujadili kwa kina. Ni kweli huo ni mwili wa Neema.. Hatuwezi kuutesa mwili wa binti niliyemzaa na kumlea kwa tabu kubwa kama Neem….” Ni wazi Mzee Masalu alikuwa akilia moyoni ingawa sauti yake ilijitahidi kubaki katika muhimili wake bila mafanikio.

“Sasa bwana.. Huyo kijana sijui Cliff nani huyo, mimi sina shida nae. Huenda kweli mwanangu ndiye alikuwa mbwa wa kujirahisi kwa wanaume.. Lakini nataka mnitendee heshima moja… Namtaka Mzee mwenzangu hapa.. Namtaka baba wa huyo kidume cha mbegu aliyenizalishia mwanangu na kupelekea kifo chake. Namtaka na huyo kiumbe aliyekuwa tumboni mwa Neema.” Alianza na kuendelea

“Nataka na taarifa ya daktari kuthibitisha kilichomuua Neema.. Vikipatikana hivyo hata sasa hivi, njooni na msiba tuzike. Pasi na hayo matatu, wala msijali. Nendeni makaburini, chimbeni, mfukieni Neema.. Ipo siku Neema wangu atarudi…” Alimaliza Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu na kubaki kimya kama vile aliyetaka kusika kutoka upande wa pili.

Damu iliwasisimka wale wazee!!

Ama kweli hili lilikuwa ni tukio la mwaka..

Mwili, upo, hii haina shaka.
Taarifa ya daktari na kibali cha mazishi, ipo, haina maneno!
Kichanga cha marehemu, hiki kipo pia.. Ila kiko mbali, ingawa kinaweza kuletwa..

Shida sasa…

“Chiziza” Alijisemea Upodo pasi na kujua kuwa simu bado ilikuwa hewani… Akaiweka mezani, akavua kikofia kidogo alichokuwa amekibandika kichwani, akakuna upara wake ulikuwa umezungukwa na mvi kwa mbali. Akashusha pumzi ndefu zilizotoka na aina fulani ya mlio kama wa vuvuzela.

Alichodhani kipo, sicho alichokikuta!

***

Simu ilipigwa..

Mazungumzo yakafanyika… Zulfa akaombwa asaidiane na kina mama wengine wawili, mmoja aliyekuwa rafiki mkubwa wa Clifford akifanya kazi kama muuguzi wa afya katika hospitali ya Mkoa wa Singida, kuwa wafanye juu chini kumchukua yule mtoto kule hospitali na kuja naye Mwanza upesi. Kazi ile ikafanywa kwa upesi na mpaka kufikia saa nne ya usiku, walikuwa wanaanza safari ya kutoka Singida kuelekea Mwanza.

 

Mwili wa Neema ukashushwa na kupelekwa tena chumba cha maiti katika hospitali ya Rufaa ya Bugando ili usije kuharibika wakati ule wa sintofahamu. Waombolezaji wale wakagawana majukumu na namna ya kujikimu ikawekwa sawa, na ikaonekana kuwa, wengi walikuwa na ndugu, marafiki au jamaa pale Mwanza. Wakaenda kujisitiri huko.
Kazi ikabakia moja tu..

Kumshawishi Chiziza!!
Ee bwana wee!!

Upodo aliongea, Tegu akasema, Laswai akadakia, Ng’wanzalima naye akaweka neno, Makamba akaweka na uswahili kidogo, lakini ngoma ilikuwa inadundwa bila kutoa mlio. Mtu pekee aliyebaki kuwa na msaada akaonekana kuwa ni Clifford mwenyewe.

Usiku kucha wazee wale walifanya walichoweza lakini hakukuwa na matumaini. Asubuhi ya siku iliyofuata ikafika.
Siku ya nne tangu Neema aage dunia!!

Clifford alifanya maamuzi magumu!!

“Nataka niongee na Baba mimi mwenyewe, tafadhali wazee hebu niruhusuni” Alisema Clifford macho yakiwa mekundu kupita kiasi.

“Aah. Lakini Clifford, kwanini tusinge…” Aliingiliza Mzee Babudi

“Hapana.. Hebu tumpe nafasi.. Mwacheni ajaribu.. Damu nzito kuliko maji kumbukeni” Alishauri Upodo akiwa anaonekana mchovu kupita kawaida.

Simu ikapigwa, ikaita!!

“Shkamoo baba” Alisalimu Clifford akionekana kulemewa na machozi

“Ningekuwa namfahamu baba anayedharaulika kama mimi ningemtafuta ili tuunde umoja wa kina baba wapumbavu Tanzania” Alijibu Chiziza.

“Baba.. Sijawahi kuacha kukuheshimu Baba yangu” Alijieleza Clifford

“Iambie maneno hayo maiti ya huyo binti wa watu.. Iambie kuwa wewe Clifford, ulimuheshimu sana baba yako mzazi na ulimshirikisha hata juu ya mpango wako wa kuoa.. Iambie, iambie baradhuli mkubwa weye…” Chiziza alinguruma.

“Siwezi kushindana na wewe hata kwenye ujinga baba yangu.. Hata kwenye kuchezea matope ni wewe ndiwe ulikuwa mwalimu wangu, siwezi kukushinda. Wewe umenizaa na umenifikisha hapa nilipo. Kujifunga mkanda na kutaka kushindana na wewe ni kuiambia dunia kuwa elimu yangu haijawahi kunisaidia. Ujanja wangu kwako ni upumbavu mtupu, na hamna chochote kinachonifanya kuwa bora kuliko wewe baba angu” Clifford alisema huku chozi likimtoka.

 

Kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake, alikuwa amemjibu mzee Chiziza jambo na kisha mzee huyo akaacha kusema. Ikamlazimu kuendelea.

“Mimi ni mtoto mjinga ambaye daima sitakua mwerevu mbele yako. Baba, si kwamba dunia nzima ina akili kama ulivyo wewe. Mimi ni mtoto, na huenda hata wewe hungependa kunikumbatia chini ya mbawa zako daima. Kuna wakati unaniacha niende huku na kule kuokota okota kama kifaranga. Si yote ninayokutana nayo yanafanana na yale unayonipa wewe baba. Sio akina baba wote wana busara kama za kwako. Lakini ni wewe wa kunifanya nijione niko salama tena baba yangu. Hata pale kila mtu anaponifungia mlango, nakuwa na Imani kuwa upo mlango mmoja ambao haujafungwa. Na mlango huo ni wewe baba” Clifford machozi yalikuwa yakimtoka.

 

“Anhaaa.. Kwahiyo unafanya upuuzi wako kwa vile unajua kuwa Mzee Chiziza ataelewa tu, si ndio? Sasa imekula kwako fala wee.. Malizia mwenyewe ujinga uliouanza, fisi maji wewe” Alijibu Chiziza lakini ni wazi kuwa , hakuwa na hasira kama awali.

“Hapana baba.. Hapana hata kidogo. Kama leo nikiulizwa nimtaje baba aliye bora kuliko wote duniani, bado Mzee Chiziza anabaki kuwa the best. Ni wewe uliyenizaa na kila kitu chema ninachokifanya kimetoka kwako. Haya mabaya yooote ninayoyafanya nakiri tu kuwa nimetoa kwingine, lakini sio kwako baba yangu. Mimi sit u fisi maji.. Ni zaidi ya hata hayawani wote wa mwituni, majini nan chi kavu” Alijieleza Clifford.

“Acha kuniremba hapa. Kila mtu anakosea duniani..” Chiziza alijibu. Ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake Clifford kusikia kauli ile kutoka kwa Chiziza!!! Damu ikamsisimka. Bila kujielewa akajikuta akisema.

“Umesema sawa baba, daima najua kuwa kila mtu anakosea. Lakini napiga magoti yangu mbele yako leo baba, sio ili kuanza kukumbushana kuwa nani alikosea wapi, na kwanini. Leo hii, kuna baba ambaye mtoto wake yupo kwenye jokofu kwa siku ya nne leo. Kuna baba ambaye yeye pia anajua kuwa kila mtu anakosea, na anaugulia kifo cha mtoto wake.. Sitaki awepo baba mwingine atakayeumia kwa kupoteza mtoto wake Mzee Chiziza!” Clifford alisema kwa utulivu uliowatisha wenzake.

Hewala!!

Wazee wale nywele za shingo ziliwasimama!! Hakuna hata mmoja aliyetegemea kauli nzito kama ile kutoka kwa Clifford. Mzee Upodo akafuta chozi!

“Kwahiyo unanitisha kuwa nawe unaweza kufa sio? Unataka ujiue ili nami niwe baba mwingine anayelilia mtoto sio?” Sauti kavu ya Chiziza ilihoji.

“Hapana baba.. Siwezi kukutisha kwa kujiua hata siku moja. Nikifa leo ili kukukomoa, sitakuwa nimejifunza chochote. Kama niliwahi kukuita baba kwa kumaanisha, nadhani wakati huu nakuita baba nikiwa namaanisha mara mia zaidi. Sikuwahi kujua jukumu lililopo mabegani mwa baba. Wakati huu ninapoongea na wewe, na mimi ni baba. Nami ni baba wa mtoto mmoja. Kuna kiumbe sasa kinaniangalia na kusema “baba, baba”. Nitakuwa baba wa ajabu zaidi duniani kama nitakiacha kiumbe hiki kiendelee kuchekwa na dunia wakati mimi baba yake nikiwa hai!” Alimaliza Clifford.

Halafu…

Kimya!!!

“Mwili wa marehemu mmeuhifadhi wapi?” Katika hali isiyo ya kawaida, Mzee Chiziza alibadili uelekeo wa mazungumzo baada ya kimya kifupi.

***

Ndani ya dakika arubaini, Mzee Chiziza, Mkewe pamoja na dada mkubwa wa Clifford aitwaye Claritha ambaye kwa bahati tu alikuwa jijini Dar es salaam kibiashara walikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege ili kuelekea jijini Mwanza.
Joto lilirejea.

Taarifa ilitolewa kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu juu ya ugeni ule ili taratibu za msiba zianze mara moja. Kweli kabisa. Nusu saa tu tayari nguvukazi ilikuwa ikishambulia majukumu kama mchwa. Ilipangwa kuwa, siku hiyo jioni kifanyike kikao kikubwa cha familia zote mbili na kuweka mambo sawa, na panapo majaliwa, kesho yake mazishi yafanyike.

Naam..

Walikuwa wakimngoja Chiziza…

Na wakati huo, kumbe walikuwa wakingoja kizaazaa kingine cha karne!!

Ama kweli likiandikwa, litatimia!!

***

(183)

About the author

Paul Mpazi

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available