BURUDANI Hekaya

Simulizi Ya Maisha; Zawadi Ya Adhabu – 10

*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*

_Sio lazima ujichanganye na watu wote muda wote. Kila binadamu ameumbwa na namna fulani ya hali inayomfanya wakati fulani atake kuwa peke yake tu. Hii ni kawaida kabisa hata kwa sisi wengine, sio kwako tu!! Unapoona kuwa inakulazimu kujitenga na wengine, fanya hivyo. Lakini daima jijengee hali ya “kufikika”. Wafanye wengine wakuone kuwa mtu wanayeweza kumfikia katika hali walizonazo. Unapojenga aina ya kisiwa cha kukaa mwenyewe, kuna wakati unajitenga na fursa ambazo huenda hata wewe unazihitaji sana!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU KUMI*

_Hali sasa ilikuwa tete!!_

Kama Clifford alidhani alikuwa anaufahamu vema ukali wa baba yake, alikuwa amejidanganya vibaya sana! Mzee Chiziza alimsikiliza huyo wa kuitwa Upodo kwa umakini mkubwa tangu Mwanzo wa simulizi yake mpaka mwisho. Hapa na pale, Mzee Upodo alikuwa akitumia muda mwingi kuelezea busara za Clifford na namna alivyokuwa na heshima kwa watu anaoishi nao, na Mzee Chiziza alikuwa kimya tu akimsikiliza kwa umakini. Kwa mbali, timu ile ya watu wanne wakaanza kuhisi kuwa walikuwa wanaelekea kufanikisha jukumu lile kirahisi kabisa.
Mzee Upodo akamaliza.

“Umemaliza mzazi mwenzangu?” Sauti kavu ilisikika kwenye simu.

“Naam Mzee mwenzangu. Na nikaona hili nililete mimi kama…”

“Huwa napenda jibu moja kwa swali moja, huenda Clifford hakukueleza hilo. Msamehe tu, huenda hajakueleza mengi bado.. Nipe jibu la swali langu tafadhali” Sauti ile kavu na yenye wingi wa mamlaka ikamkatiza Upodo.

Wajumbe wale wanne wakatazamana, lakini haraka Clifford akatazama chini. Alishajua balaa linalokuja.

“Naam.. Nimemaliza Mzee mwenzangu” Upodo alijibu kinyonge.

“Sawa. Kwahiyo huyo bwana mdogo alikuwa akiishi na mwanamke, akampachika mimba na kuendelea kuficha akiamini kuwa baada ya kujifungua ndipo napaswa kupigiwa simu ili tu kutoa jina la mtoto, sio?” Aliuliza Chiziza.

“Eeeh.. Nadhani ndiyo ilikuwa maana yake, na huenda kulikuwa na….”

“Unaonekana nawe unaanza kuwa mzee mpumbavu mwenye kusahau sahau mambo. Nimesema swali langu moja huwa linahitaji jibu moja tu.. Hayo majibu yako yatunze, maswali yake ninayo pia” Hapa hasira zilionekana wazi wazi kwenye sauti ya Chiziza. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Mzee Upodo wala hakukasirika, alizidi kuwa mpole na uso wake kuwa makini zaidi.

“Nahisi hivyo bwana” Alijibu Mzee Upodo.

“Clifford ni mwalimu mzuri sana darasani. Naona amefika Singida amepata na wanafunzi wazee watu wazima ambao nao amewafundishwa somo linaloitwa “kuhisi”.. Kwahiyo utaacha muda gani “kuhisi” ili unipigie tuanze kuongea vitu halisi na sio hisia?” Aliuliza Chiziza huku akiweka msisitizo fulani kwenye baadhi ya maneno.

Clifford tusi zito likamtoka lakini jicho kali la mzee Upodo likamtuliza jazba!

“Mzee mwenzangu.. Lililopo mbele yetu ni tatizo kubwa, na wewe kama baba mzazi…” Upodo alijaribu kujitetea.

“Angalia bwana, nilisema nikiuliza swali lijibiwe kwa jibu moja, hayo maelezo kuna wakati ntakuja kuyahitaji halafu usiwe nayo bure. Jifunze kuwa na akiba ya maneno. Na kwa kukukumbusha tu ili usije ukakosea mara nyingine, Mimi sio “kama baba mzazi wa Clifford”, mimi ni “Baba mzazi wa Clifford”.

Simu ilikatwa!!!

Bumbuwazi ikatawala.

Mzee Babudi na Laswai walitazamana, wakatikisa kichwa kwa pamoja. “Hivi baba yako ni kabila gani?” Aliuliza Mzee Babudi macho yakiwa yamemwelekea Clifford. Kabla hata hajajibu, Mzee Laswai akajibu kwa hasira.. “Huyu lazima atakuwa kabila mbovu tu.. Mali mbovu.. Mswahili sana huyu Mzee, doh”

“Tulizeni jazba, bado tuna nafasi kubwa kwenye hili. Hebu nipatie hiyo namba nimpigie kwa simu yangu, kuna jambo nimejifunza hapa” Upodo akapatiwa namba na dakika mbili baadae, alikuwa tena kwenye mazungumzo.

“Naam.. Nakupongeza kuwa kuacha kuhisi ndani ya muda mfupi tu. Haya sasa, hebu nieleze. Wewe ndiye uliyeyabariki hayo mahusiano ya huyo barazuli kuishi na mtoto wa watu, kumjaza mimba na kuendelea kuficha akiamini kuwa akishajifungua ndio anaweza kuwaambia wazazi wake?” Alikuwa ni Mzee Chiziza aliyeanzisha mazungumzo.

“Kwakweli hakuna mzee au mtu mzima yeyote anayeweza kubariki jambo kama hili. Kilichofanyika ni kosa na kilikuwa kosa tangu awali. Tatizo ni kuwa, vijana wetu kuna wakati wanafikiri kuwa wana dunia yao peke yao, na ni busara tukawaacha waamini hivyo. Lakini ni dunia hiyo hiyo inapowafunza, yatupasa tuwarudi na kuwakumbusha kuwa, njia uijuayo panapo mwanga huwezi kuiendea vema palipo na kiza” Hakukuwa na hofu wala mashaka yoyote katika sauti ya Upodo.

Alishaanza kuonesha ujabali wake!!

“Anhaa.. Kwa maana nyingine unamaanisha kuwa, Clifford, aliiona njia mchana wa jua kali. Akaipitia mara mbili mara tatu, na kiza kilipotua akajiaminisha kuwa njia ile anaifahamu vema, akafumba na macho kabisa na akapita tena, na mwishowe alipofungua macho amejikuta amepotea, sio?’ Alihoji Chiziza.

“Naam ndugu yangu.. Nadha…, Hapana, naamini kuwa kijana kwenye hili, sio kwamba tu amepotea. Lakini ametupoteza hata na sisi ambao inatulazimu sasa tumtafute, tumpate na kwa pamoja turudi hadi Mwanzo wa safari. Tumfundeshe tena namna ya kutembea gizani” Upodo alizidisha Kiswahili.

“Sasa mimi neno langu ni moja… Neno langu ni moja tu…” Alianza Chiziza.

“Naam”

“Na huwa nina utaratibu mmoja. Clifford atakueleza vema kama akiamua kufanya hivyo. Nikishafanya uamuzi juu ya jambo moja, natamani ufuatwe kama ulivyo, bila kupakwa rangi wala kupuliziwa uturi…, tuko pamoja?”

“Naam.. Nakusikiliza bwa’mkubwa”

“Na katika hili, neno langu ni moja. Na nikishamaliza tu kulisema, nitakata simu. Kama unatamani heshima yangu, usinipigie simu mpaka utakapolitimiza, tuko pamoja?”

“Eeeh… Nakusikiliza bwana, na naamini…”

“Achana na Imani yako bwana, nisikilize mimi. Kwanza usiamini usichokijua bwanaaa.. Nani vile ulisema?”

“Mzee Upodo”

“Ndio Upodo.. Usiamini usichokijua.. Sasa neno langu ni hili. Clifford, na mkipenda ninyi pia kushirikiana naye, malizeni huo upuuzi mliokuwa mnaulea pamoja. Kama mtazika, au mtaishi na maiti, au mtamrudisha mtoto wa watu kwao, hilo mimi sihusiki nalo. Sijafundishwa kusaidia watu wazima wanaochezea moto namna ya kuuguza majeraha yao, nilifundishwa kuwaelezea madhara ya moto. Huyo bazazi yalishamkuta makubwa, nikadhani amejirekebisha, na badala yake kaenda kuchuma makubwa zaidi. Sasa malizeni huo upuuzi, mkishamaliza tu, nipigie simu, nitakueleza nini kifuatacho. Nimekuheshimu sana kukupa nafasi hii, na sikumbuki mara ya mwisho niliitoa mwaka gani. Msiba Mwema”.

“Aah.. Lakini Chiziza… Unajua bwana hali iliv…..” Upodo alikuwa akiongea mwenyewe. Simu ilikuwa kimya. Tusi la kiarabu likamtoka kwa uchungu!

Kikao hakikuwa na maana tena, kikavunjika na wote wakaendelea kungoja majibu ya upande wa pili.

***

Ilikuwa rahisi sana kumpata Mzee Tegu ambaye mara moja aliwasiliana na mzee Masalu. Bila kukawia, Mzee Masalu akaungwa na waliokuwa Singida na mara moja mawasiliano yakawa baina yake na wao.

Kwa zaidi ya dakika ishirini walijaribu kumuelezea kilichotokea lakini maswali mazito mazito yalikuwa yakirushwa mfululizo. Haraka wakaamua kumshirikisha na Clifford aliyekuwa ametoka kwenye kikao cha kuzungumza na baba yake. Akajieleza kwa kirefu kwa Mzee yule ambaye aliishia kuguna kila alipokuwa akisimuliwa.

“Kwahiyo wewe ulikuwa mwalimu wake wa chuo, sio?” Aliuliza Masalu

“Ndiyo baba”

“Na ulimpa mimba akiwa bado mwanafunzi hapo chuoni?”

“Lakini tulishaanza uchumb…”

“Unalikumbuka swali langu?”

“Ndio baba”

“Naomba jibu”

“Ndiyo, Neema alipata mimba akiwa anakaribia kumal..”

“Akiwa mwanafunzi, acha kuremba mwandiko, kumbuka unaandika imla”

“Nakubali baba, akiwa mwanafunzi”

“Maadili ya ualimu yanasema nini kuhusu mahusiano baina ya mwalimu na mwanafunzi?”

Jasho lilikuwa likimtoka Clifford. Aliona dalili za kupoteza kila kitu maishani mwake.

“Ni kweli si sahihi kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Lakini mimi na mwenzangu tulishakubaliana kufunga ndoa, na hata…”

“Wewe ndiye uliyemtafutia kazi chuoni?”

“Hapana baba, hakuwa anafanya kazi.”

“Jibu zuri kabisa. Wewe ndiye uliyemwambia anidanganye kuwa anafanya kazi ili uendelee kumlaza akiwa uchi kufuani pako, sio?”

Clifford angejibu nini sasa hapo? Alinyamaza kimya.

“Halafu.. Ni sheria ipi inamruhusu mwanaume kuishi na mtoto wa mtu kwa karibu mwaka mzima bila kutoa taarifa kwao? Au ndio ujana huo?”

“Tumekosea baba.. Tumekos..”

“Sema umekosea kijana, sema nimekosea”

“Nimekosea baba”

“Sawa.. Sasa mimi ninachojua, binti yangu Neema sio mjamzito wala hajafa. Yuko chuo cha uhasibu Singida akiwa anafanya kazi. Kama utamleta nimwone kuwa ndiye au siye hiyo ni juu yako, lakini binti yangu yuko hai!”
Simu ilikatwa!!

***

Saa mbili kasoro dakika nane wajumbe walikuwa tena pahala pamoja. Yaliyojadiliwa yakawekwa wazi. Kulikuwa na ugumu pande zote mbili, lakini unafuu ukaonekana upande wa Mzee Masalu. Ile kauli yake kuwa apelekewe mwaneye akamwone ilitafsiriwa na wazee kuwa ni kauli ya kiungwana na kishujaa. Huenda Mzee Masalu angeamini kuwa bintiye amefariki baada ya kumuona. Mipango ya kusafirisha ikaanza mara moja.

 

Kamati zikawekana sawa na marafiki wote wa Clifford wakawa tayari kwa safari. Mwili wa Neema ukaandaliwa na kurudishwa hospitali ya mkoa na mchana wa siku iliyofuata, kila kitu kilikuwa tayari. Pamoja na mchango wake katika kanisa, haikuwezekana kuwepo kwa ibada maalumu ya mazishi. Clifford alihesabiwa kuwa, kwa muda wote alishi suria, na kwa sheria na kanuni za kanisa katoliki, isingewezekana kuwepo kwa ibada ya misa takatifu. Zikasaliwa sala za hapa na pale, wanakwaya wakaimba na kuomboleza, na saa kumi kamili, safari ya mwanza ikawadia.

 

Gari sita zenye waombolezaji zikaanza safari, huku mkuu wa msafara akiwa Mzee Upodo huku akiwa bega kwa bega na wazee wenzake zaidi ya nane ambao wote waliamua kushiriki kukamilisha shughuli ile ambayo wangeendelea kuiwekea masihara, ingeweza kumwendea vibaya kijana wao Clifford. Tayari mawasiliano yote ya kumwomba Mzee Tegu awe Mwanza mapema ili kushirikiana na wazee wenzake kuupeleka msiba kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu yalikwishafanyika, na tayari Mzee Tegu alikuwa njiani kuelekea Mwanza.

 

Shughuli ilikuwa imepamba moto kwelikweli..

 

Ziliimbwa nyimbo, machozi yakatiririka, mafuta yakaungua, Mwanza wakatua. Saa sita na robo usiku, msafara wa magari ukawasili jijini Mwanza. Lakini tofauti na ilivyo ada ya misiba, usiku huo isingewezekana kuufikisha mwili wa Marehemu nyumbani kwao.

 

Nani angewaelewa ikiwa hakukuwa na maandalizi yoyote?

Wazee wakaitana, majadiliano yakafanyika na ikakubaliwa kuwa, alfajiri ya siku iliyofuata, Tegu na wazee wengine kadhaa waende kwanza nyumbani kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu na baada ya kuwekana sawa na kupima kile ambacho angewajibu ndipo sasa mwili upelekwe na msiba upate pa kufikia.

 

Walipitia tena mipango yao, wakachambua chambua na mila za kisukuma, wakauliza na kujibiana juu ya faini ambazo wangeweza kukabiliwa nazo ili mwili ule kupokelewa. Wakapigiwa simu wenyeji kadhaa na kuulizwa hili na lile. Baada ya masaa mawili ya kupanga na kupangua, mpango kamili ukawa umekamilika na ukakabidhiwa kwa wazee watano..

Upodo akiwa mwenyekiti, Tegu kama rafiki wa Masagida, Mzee Babudi, Makamba na Laswai kutoka Singida, na Mzee Urubani Ng’wanzalima aliyekuwa rafiki mkubwa wa Tegu na Masagida.

Wakakaa wakipiga soga na kunywa gahawa kuingoja alfajiri.

Mipango ikiwa barabara kabisa..

 

Hawakujua kuwa yooote waliyopanga yalikuwa ni kuteka maji kwenye kapu, waliyachota kisimani na kuyaweka kichwani, lakini walipofika nyumbani walikuwa wamelowa..

 

Walikuwa wakipanga na kupangua ujinga mtupu!!!

Ubatili mtupu na kujilisha upepo!!!

***

(153)

About the author

Paul Mpazi

Add Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available