NZITO ILIYOINGIA TANZANIA

Zama Mpya Pekee: Mbowe Ataka Wabunge Waape Kuwa Hawatakimbia CDM

Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Bw. Freeman Mbowe amewaagiza wabunge wote wa chama hicho kutoa kauli zao hadharani mara moja na kuahidi kutokiacha chama wakati huu ambapo kuna wimbi la wabunge na madiwani wa chama hicho kukikimbia.

Katika waraka alioutoa jana ambao Zama Mpya imepata nakala yake. Bw. Mbowe amesema kuwa “nawaagiza wabunge wote wa Chadema kujitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuelezea misimamo yao ya kutohama chama ili kuwajengea Imani wananchi kwa chama chetu” imesema barua hiyo fupi iliyotolewa jana na kusambazwa kuanzia usiku wa jana.

Pamoja na agizo hilo Mbowe alitumia waraka huo kuwapongeza wabunge na viongozi wengine mbalimbali ambao tayari wametoa misimamo yao ya kutokihama chama. Vilevile, Mbowe aliwahimiza wale ambao hawajafanya hivyo bado wafanye hivyo mara moja kwani kuchelewa kutekeleza agizo hilo kunaweza kusababisha hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi yao.

Barua hiyo ya Mbowe kwa wabunge imekuja siku moja tu baada ya aliyekuwa mgombea wa chama hicho Bw. Edward Lowassa kukutana na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar-es-Salaam jana ambapo alifanya naye mazungumzo na hatimaye kuzungumza na waandishi wa habari na kutoa kauli ambazo zilionekana kuiunga mkono serikali ya Magufuli. Kitendo cha Lowassa kumsifia Magufuli kilipokelewa kwa masikitiko na viongozi wa juu wa chama chake akiwemo Mwanasheria Mkuu wa chama hicho na Mnadhibu Mkuu wa Upinzani Tundu Lissu ambaye yuko kwenye matibabu huko Ubelgiji. Lisu alijeruhiwa katika shambulio la risasi miezi minne nyuma ambapo aliponea chupuchupu katika kile ambacho amekiita ni jaribio “la mauaji ya kisiasa” dhidi yake.

Lissu akiandika kutoka Ubelgiji alilaani vikali kitendo cha Lowassa kukutana na Magufuli wakati huu ambapo upinzani una malalamiko mengi dhidi ya Serikali na utendaji kazi wa Rais Magufuli. Akinukuliwa katika mtandao wa JamiiForum Lissu amesema “Katika mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, uamuzi wowote wa kufanya nae mazungumzo, hata kwa nia njema yoyote ile, bila kushauriana au kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama, ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.”

Mwenyekiti mwenyewe Mbowe alikataa kabisa kubariki kauli za Lowassa mbele ya Magufuli jana na kudai kuwa aliyoyasema jana hayakuwa msimamo wa chama na hakuwa na taarifa na mpango wa Lowassa kuzungumza na Magufuli jambo ambalo hata Lissu amelisema katika andiko lake fupi. Wote hawajafurahishwa na jinsi Lowassa amewavuka viongozi wenzie ndani ya chama na kwenda kufanya mazungumzo na mtu ambaye anadaiwa kuunyanyasa na kuuminya upinzani Tanzania. “Katika mazingira ambapo hata jumuiya ya kimataifa imeanza kuhoji mwenendo wa Rais Magufuli, kutoa kauli kwamba ‘anafanya kazi nzuri’ ni ‘kumtupia taulo’ la propaganda litakalomfichia madhambi mengi aliyowafanyia Watanzania katika miaka hii miwili” amesema Lissu.

Kiongozi mwingine ambaye ameonesha wazi kutokufurahishwa na uamuzi wa Lowassa kuzungumza na Magufuli ni Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema. Lema kama wengine wamechukulia kitendo hicho kama ni cha aina Fulani ya kusaliti harakati za upinzani nchini.

Barua ya Mbowe inakuja wakati ambapo wimbi la viongozi mbalimbali wa upinzani na hasa Chadema wakiamua kuweka manyanga chini na kuamua kujiunga na CCM katika kile walichodai kuwa ni “kuunga mkono” kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli. Hadi hivi sasa madiwani kadhaa wa Chadema pamoja na wabunge wengine wa upinzani wameachia nafasi zao. Hili limeleta hoja inawezekana mazungumzo ya Lowassa na Magufuli jana yamepalilia njia kwa Lowassa kuamua kurejea CCM ambako alikuwa ni mwanasiasa maarufu Zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

Kukatwa kwa jina lake miezi kama mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu ndiko kulikomsababisha kukimbilia Chadema ambako alipewa nafasi ya kugombea Urais tena bila ya kuwa na sifa zozote za maana za kukubalika kama mpinzani wa kweli kitu ambacho kilisababisha mgawanyiko ndani ya Chadema na ndani ya wafuasi wao ambao waliona kuwa Chadema imejiuza kwa mtu ambaye walikuwa wanamtuhumu kwa miaka nenda rudi kuwa ni fisadi nambari moja.

Barua ya Mbowe haijaeleza wabunge hao wana muda gani wa kutekeleza agizo hilo na wala kuelezea kiwango cha hatua za kinidhamu ambazo zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wale watakaokaidi agizo hilo.

(130)

About the author

bongoz

1 Comment

Click here to post a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  • I personally don’t have a problem with this. It’s just like a Shepherd who wants to ensure his flock is safe basi

OZ TV MAGUFULI ADAI TZ TUNAWEZA!

Bofya kutazama zaidi...

VIDEO YA LEO

KILICHOPOSTIWA PUNDE

PAYPAL

KUNDI LA HABARI

KINACHOENDELEA SASA

Waandishi Makala

No recent posts available